Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Lesi Inayoshabihi Utando wa Buibui”-Ufumaji wa Paraguai Unaovutia

“Lesi Inayoshabihi Utando wa Buibui”-Ufumaji wa Paraguai Unaovutia

“Lesi Inayoshabihi Utando wa Buibui”-Ufumaji wa Paraguai Unaovutia

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA PARAGUAI

ASUNCIÓN, PARAGUAI. Tuna dakika chache za kuweza kutalii kwenye uwanja wa ndege huku mizigo yetu ikipakuliwa. Ghafula mke wangu anielekeza kwenye ukuta wenye bidhaa fulani. “Ni vitu maridadi kama nini!” asema kwa mshangao, huku akiashiria kitambaa cha mezani chenye lesi maridadi na mshono tata. Mara astaajabia jinsi kilivyoshonwa.

Lesi inayoshabihi utando wa buibui ilibuniwa Arabia. Kulingana na kitabu cha Paraguay, Touristic and General Information, “ilipelekwa katika Visiwa vya Canary na Hispania, na kati ya karne ya 17 na 18, ikaletwa Paraguai, ambako lesi aina ya sun kutoka Tenerife iliitwa lesi ya Paraguai, au nanduti.” Katika Paraguai lesi hii maridadi ilitegemea mtindo wa fundi wa lesi, na sifa za mimea na wanyama wa mahali alipo, zilionyeshwa katika ufumaji. Ingawa lesi hiyo ilibuniwa nchi nyingine, Waparaguai waliboresha lesi yao kwa mishono mipya. Ufumaji wa lesi umekuwa kazi inayowaruzuku wenyeji wengi.

Wao hufumaje lesi hii tata inayoshabihi utando wa buibui? Ili kutusaidia kupata jibu, kiongozi wetu alitupeleka umbali wa kilometa 30 mashariki ya Asunción kwenye mji mdogo wa Itauguá. Alitueleza kwamba nyingi za lesi zinazoshabihi utando wa buibui za Paraguai hufumwa katika eneo hilo. Kwa kweli, bidhaa nyingi zinazofumwa huonyeshwa kwenye maduka mengi pambizoni mwa barabara kuu.

Mmiliki wa duka moja alituamkua kwa uchangamfu na kutuonyesha bidhaa zenye kuvutia. Akaeleza hivi: “Lesi iliyofumwa kwa mikono huainishwa kulingana na namna ilivyofanyizwa. Lesi inayoshabihi utando wa buibui imeshonwa kwa sindano. Washonaji-lesi wengi Waparaguai hutumia ubuni wao, japo wengine hutumia bombwe. Wote hutumia kitambaa cha pamba kilichowambwa kwenye fremu ya mbao kisha hufuma lesi kwa sindano na uzi. Wao hufunzwa ustadi huu na mama zao wanapokuwa na umri mdogo nao huwafunza watoto wao.”

Buibui aina ya orb weaver hujenga utando kwa saa mbili au tatu tu. “Inachukua muda wa miezi miwili hadi mitatu kushona kitambaa cha meza ya watu wanane uzi usio laini unapotumiwa. Kushona kitambaa hicho-hicho kwa uzi laini huchukua miezi sita hadi minane,” alisema mwenyeji wetu wa kike. “Uzi laini zaidi, hutokeza umaridadi zaidi.”

Ashikapo kitambaa cheupe cha kukalia sahani, yeye asema: “Kina mchoro wa ua la mpera katikati, na nyuzi hizi huhesabiwa kinaposhonwa. Mchoro huu ni mgumu zaidi kushona, nao hushonwa kwa muda wa majuma mawili kwa uzi laini. Mwanzoni washonaji-lesi walitumia tu uzi laini na lesi zote zilikuwa ghali mno. Kwa hiyo, washonaji-lesi wengi wakaanza kutumia uzi usio laini ili kupunguza muda na gharama yake.”

Mikeka, vitambaa vya mezani na vya kuwekea sahani, vikalio vya glasi na sinia, na vifaa vingine vya nyumbani vyeupe na vya rangi mbalimbali vilionyeshwa waziwazi. Tulipoulizia nguo, mwenyeji wetu wa kike alileta haraka vazi la kawaida, la bintiye, na pasipo shaka alilionea fahari. Lilikuwa vazi pana maridadi la rangi za upindemvua. Katika maduka mengine, tuliona postikadi maridadi zenye lesi laini. Si ajabu kwamba lesi inayoshabihi utando wa buibui huonwa kuwa ufumaji mashuhuri sana wa Paraguai.

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 18]