Ni Nani Walio Watumwa Leo?
Ni Nani Walio Watumwa Leo?
HEBU wazia idadi yao. Inakadiriwa kwamba kati ya watoto milioni 200 na 250 wenye umri unaopungua miaka 15 hutumia muda mwingi wakati wa asubuhi kazini. Watoto robo milioni, wengine wakiwa na umri mchanga wa miaka saba, waliingizwa vitani mnamo mwaka wa 1995 na 1996 pekee, hivyo wengine wao wakawa watumwa wa vita. Idadi ya watoto na wanawake wanaouzwa wakiwa watumwa kila mwaka inakadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja.
Lakini tarakimu haziwezi kufunua hali ya kukatisha tamaa ya watu hao. Kwa mfano katika nchi moja iliyoko kaskazini mwa Afrika, mwandishi Elinor Burkett alikutana na Fatma, mwanamke kijana aliyefaulu kumtoroka bwana wake mkatili. Hata hivyo, baada ya kuzungumza naye, Burkett aling’amua kwamba Fatma “atakuwa mtumwa milele kulingana na maoni yake.” Je, Fatma aweza kuwazia wakati ujao ulio bora? “Hawezi kufanya mipango yoyote kunapopambazuka sembuse ya wakati ujao,” asema Burkett. “Wakati ujao ni mojawapo ya mambo mengi ya kuwaziwa tu asiyokuwa nayo.”
Ndiyo, katika pindi hii, mamilioni ya wanadamu wenzetu ni watumwa wasio na tumaini. Ni kwa nini na jinsi gani watu hawa wote huwa watumwa? Wako katika utumwa wa aina gani?
Wauzaji wa Binadamu
Broshua ya watalii inayoenezwa Marekani ilisema hivi kinagaubaga: “Safari za ngono hadi Thailand. Wasichana halisi. Ngono halisi. Bei rahisi kweli. . . . Je, ulijua kwamba unaweza kununua msichana bikira kwa dola za Marekani 200 peke yake?” Jambo ambalo halikutajwa na broshua hiyo ni kwamba “bikira” hao yaelekea wametekwa nyara au kuuzwa kwa lazima kwenye madanguro, ambapo wanahudumia kwa wastani wateja 10 hadi 20 kwa siku. Wakikataa kutoa huduma za ngono, wanapigwa. Moto ulipozuka kwenye danguro moja katika Kisiwa cha Phuket, mahali pa kutalii huko kusini mwa Thailand, makahaba watano walichomeka hadi wakafa. Kwa nini? Kwa sababu wamiliki wao
walikuwa wamewafungia vitandani kwa minyororo ili wasitoroke kutoka utumwani.Wanawake hawa wachanga hutoka wapi? Inaripotiwa kwamba, sekta hii ya biashara ya ngono imejaa mamilioni ya wasichana na wanawake kutoka ulimwenguni pote ambao wametekwa nyara, wametishwa, na kuuzwa kwenye ukahaba. Biashara ya kimataifa ya ngono inanawiri kwa sababu ya umaskini katika nchi zinazositawi, utajiri katika nchi zenye ufanisi, na sheria zinazopuuza ulanguzi wa kimataifa na mikataba ya kuwa utumwani.
Mashirika ya wanawake katika Kusini-Mashariki ya Asia yamekadiria kwamba kuanzia miaka ya katikati ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, wanawake milioni 30 waliuzwa ulimwenguni pote. Walanguzi wa kibinadamu hutembea-tembea kwenye stesheni za gari-moshi, vijiji maskini, na barabara za mjini wakitafuta wasichana na wanawake wachanga wanaoweza kushambuliwa kwa urahisi. Kwa kawaida wahasiriwa huwa hawajaelimika, mayatima, walioachwa, au mafukara. Hupewa ahadi bandia za kazi, husafirishwa na kuvushwa mipakani, kisha huuzwa kwenye madanguro.
Tangu kuporomoka kwa muungano wa nchi za Kikomunisti mwaka wa 1991, kumekuwa na wanawake na wasichana wengi sana mafukara. Kuondoa vizuizi, ubinafsishaji, na kuongezeka kwa pengo kati ya matabaka kumeongeza uhalifu, umaskini, na ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Wanawake na wasichana wengi Warusi na wa Ulaya-Mashariki wamekuwa wakitumiwa vibaya ili kufaidi mashirika ya kimataifa ya kikahaba yaliyopangwa. “Kulangua wanadamu si hatari sana kuliko kulangua dawa za kulevya,” akasema aliyekuwa Mjumbe wa Haki wa Ulaya Anita Gradin.
Hali ya Utotoni Iliyoharibiwa
Katika kiwanda kimoja kidogo cha mikeka huko Asia, watoto wenye umri mdogo wa miaka mitano wanafanya kazi kuanzia saa kumi usiku hadi saa tano usiku bila malipo. Katika visa vingi watoto hao walioajiriwa hukabili hatari kubwa za kiafya: mashine zisizo salama, *
saa nyingi katika mazingira yasiyo na nuru na hewa ya kutosha, na kemikali hatari zinazotumiwa kutengeneza vitu.Kwa nini watoto hutafutwa kwa bidii ili wawe wafanyakazi? Kwa sababu ni rahisi kulipa watoto na kwa sababu kwa asili watoto hufundishika, ni rahisi kuwatia nidhamu, na huogopa kulalamika. Umbo lao dogo na vidole vyepesi huonwa na waajiri wasiozingatia kanuni zozote kuwa rasilimali ya kufanya aina fulani za kazi kama vile, kufuma mikeka. Mara nyingi watoto hao huajiriwa, huku wazazi wao wakikaa nyumbani, bila kazi ya kuajiriwa.
Jambo linalofanya hali ya watoto walioajiriwa kufanya kazi ya nyumbani iwe mbaya zaidi, hasa ni uwezekano wa kutendwa vibaya kingono na kimwili. Watoto wengi hutekwa nyara, huzuiwa kwenye kambi za mbali, na kufungiwa usiku ili kuwazuia wasitoroke. Huenda wakafanya kazi ya kujenga barabara na kuchimba mawe wakati wa mchana.
Njia nyingine ambayo hali ya utotoni huharibiwa ni kupitia ndoa ya kiutumwa. Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa laeleza kisa kimoja cha mfano: “Msichana mwenye umri wa miaka 12 aambiwa kwamba familia yake imepanga afunge ndoa na mwanamume mwenye umri wa miaka 60. Ni wazi kwamba ana haki ya kukataa, lakini kihalisi hana fursa ya kudhihirisha haki hiyo na hana habari kwamba anaweza kufanya hivyo.”
Watumwa wa Deni
Mamia ya maelfu ya wafanyakazi hufungwa kwa waajiri wao na mahali walipoajiriwa kwa sababu ya mikopo ambayo wao au wazazi wao wamepewa. Kidesturi, ufungwa wa kikazi hutokea hasa katika maeneo ya kilimo, ambapo wafanyakazi hufanya kazi wakiwa watumishi wa kawaida au wakulima. Katika visa fulani, deni hupokezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, na kuhakikisha kwamba washiriki wa familia wanabaki katika ufungwa huo daima. Katika visa vingine, wanaowiwa pesa, huuza deni hilo kwa mwajiri mpya. Katika visa visivyo vya kawaida, wafanyakazi waliofungwa hawalipwi chochote kwa kazi yote wanayofanya. Au huenda wakafungwa na pesa chache wanazolipwa kimbele za mshahara wao, jambo linalorudiwa bila kikomo, ili wafungwe kwa mwajiri wao.
Utumwa wa Kidesturi
Binti, kutoka Afrika Magharibi, ana umri wa miaka 12 na ni mmojawapo kati ya maelfu ya wasichana wanaotumikia wakiwa trocosi, linalomaanisha katika lugha ya Ewe “watumwa wa miungu.” Amelazimishwa kuishi maisha
ya utumwa ili kulipia uhalifu ambao hakuwa ameufanya—kubakwa ambako kulifanya azaliwe! Kwa sasa wajibu wake unatia ndani tu kufanya kazi nyumbani mwa kasisi wa hapo mwenye sanamu inayoabudiwa. Baadaye kazi za Binti zitaongezeka na kutia ndani kumhudumia kingono kasisi anayemmiliki. Kisha afikapo umri wa makamo, mahali pa Binti patachukuliwa na mwingine—kasisi huyo atatafuta wasichana wengine wanaovutia ili kumhudumia wakiwa trocosi.Kama vile Binti, maelfu ya wasichana ambao ni watumwa wa kidesturi hutolewa na familia zao wafanye kazi wakiwa watumwa katika jitihada za kulipia tendo ambalo huonwa kuwa dhambi au kosa dhidi ya agizo takatifu. Katika sehemu kadhaa za ulimwengu, inawabidi wasichana au wanawake watekeleze wajibu wa kidini na kuwahudumia kingono makasisi au wengineo—kwa kisingizio cha kwamba wanawake hao wameolewa na mungu. Katika visa vingi wanawake hao huandaa huduma nyingine bila kulipwa. Hawaruhusiwi kuhama wanapoishi au kufanya kazi tofauti na mara nyingi hubaki utumwani kwa miaka mingi.
Utumwa wa Kawaida
Ijapokuwa nchi nyingi zinadai kwamba zimepiga marufuku utumwa kisheria, hivi karibuni katika maeneo fulani kumetokea utumwa wa kawaida. Mara nyingi huo hutokea mahali palipo na mapambano ya kiraia au ya kivita. “Sheria imepuuzwa katika maeneo yenye mapambano,” laripoti Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa, “na askari au wanamgambo wenye silaha wanaweza kuwalazimisha watu wawafanyie kazi bila malipo . . . bila kuogopa adhabu; mazoea hayo yameripotiwa hasa katika maeneo yanayodhibitiwa na vikundi vyenye silaha ambavyo havijatambuliwa ulimwenguni pote.” Hata hivyo, kulingana na shirika hilohilo, “hivi karibuni kumekuwako pia na ripoti za askari wa serikali wanaowalazimisha raia kufanya kazi kama watumwa, bila kufuata sheria yoyote. Imeripotiwa kwamba askari pamoja na wanamgambo huhusika katika biashara ya watumwa, wakiuza wale waliowateka ili wawafanyie kazi wengine.”
Kwa kusikitisha, laana ya utumwa ingali inasumbua wanadamu katika njia nyingi na mbinu zisizo wazi. Tua na kufikiri tena juu ya idadi ya watu wanaohusika—mamilioni ya watu wanaoteseka wakiwa watumwa tufeni pote. Kisha fikiri juu ya watumwa wa kisasa mmoja au wawili ambao umesoma masimulizi yao katika kurasa hizi—labda Lin-Lin au Binti. Je, ungependa kuona zoea la utumwa wa kisasa likikomeshwa? Je, kukomeshwa kwa utumwa kutapata kuwa jambo halisi? Kabla hakujawa hivyo, lazima mabadiliko makubwa sana yatukie. Tafadhali soma juu yake katika makala yanayofuata.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 11 Ona “Kuajiriwa kwa Watoto—Mwisho Wake Wakaribia!” katika toleo la Amkeni! la Mei 22, 1999.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
KUTAFUTA UTATUZI
Mashirika rasmi mbalimbali, kama vile Shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya Watoto na Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni, yanafanya kazi kwa bidii kubuni na kutekeleza mbinu za kuondoa utumwa wa kisasa. Kwa kuongezea, mashirika mengine mengi yasiyo ya kiserikali, kama vile Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa na shirika la Human Rights Watch, yamejitahidi kuelimisha umma kuhusu utumwa wa kisasa na kuweka huru wale wanaohusika. Baadhi ya mashirika hayo yanataka vibandiko vya pekee vianzishwe vitakavyoonyesha kwamba bidhaa hazikutengenezwa na watumwa au na watoto walioajiriwa. Ili kwamba watu wanaofanya ngono na watoto washtakiwe wanaporudi katika nchi ya kwao, mashirika fulani yanatoa mwito sheria itungwe katika nchi ambamo “safari za ngono” huanzia. Watetezi fulani wa haki za kibinadamu hata wamefikia hatua ya kulipa wafanya-biashara wa utumwa na wakubwa wao kiasi kikubwa cha fedha kusudi wakomboe watumwa wengi kadiri wawezavyo. Jambo hilo limetokeza ubishi fulani, kwa kuwa mazoea hayo yaweza kutokeza fursa ya kuuza watumwa kwa faida na kuongeza bei yao kwa kiasi kikubwa.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wasichana wengi wachanga hulazimishwa kufunga ndoa
[Hisani]
UNITED NATIONS/J.P. LAFFONT
[Picha katika ukurasa wa 8]
Foleni za chakula za watumwa waliofungwa
[Hisani]
Ricardo Funari
[Picha katika ukurasa wa 8]
Nyakati fulani watoto wachanga hulazimishwa kuingia katika utumishi wa jeshi
[Hisani]
UNITED NATIONS/J.P. LAFFONT