Siri Iliyofichwa Sana
Siri Iliyofichwa Sana
“Hakuna mtu atakayewekwa utumwani au kutumikishwa: utumwa na biashara ya utumwa itazuiwa katika namna zake zote.”-Azimio La Haki Za Kibinadamu Kwa Wote.
WAKATI mwingine utakapoweka sukari ndani ya kahawa, mfikirie Prevot, kutoka Haiti aliyeahidiwa kazi nzuri katika nchi nyingine ya Karibea. Badala yake, aliuzwa kwa dola nane.
Prevot alipatwa na mambo kama yale yanayowapata maelfu ya wananchi wenzake wanaotumikishwa ambao hulazimishwa kukata miwa kwa miezi sita au saba kwa mshahara mdogo sana au bila malipo. Mateka hao huwekwa kwenye mazingira yaliyojaa watu na yenye uchafu mwingi. Baada ya mali zao kutwaliwa, wanapewa panga. Lazima wafanye kazi ili kupata chakula. Wakijaribu kutoroka, huenda wakapigwa.
Fikiria kisa cha Lin-Lin, msichana kutoka Kusini-Mashariki ya Asia. Alikuwa na umri wa miaka 13 mama yake alipokufa. Shirika la kutafutia watu kazi lilimnunua kutoka kwa baba yake kwa dola 480 za Marekani, huku likimwahidi kazi nzuri. Bei iliyolipwa kwa ajili yake iliitwa “mapato yake ya kimbele”—njia ya kuhakikisha kwamba hatatoka kamwe kwa wamiliki wake wapya. Badala ya kupewa kazi inayofaa, Lin-Lin alipelekwa kwenye danguro, ambapo wateja humlipa mmiliki dola 4 za Marekani kwa saa. Lin-Lin anakaribia kuwa mtumwa, kwa sababu hawezi kuondoka hadi deni lake litakapolipwa. Hilo latia ndani gharama ya mmiliki wa danguro kwa kuongezea riba na gharama nyinginezo. Lin-Lin akikataa kukubaliana na mwajiri wake, huenda akapigwa au kuteswa. Jambo baya hata zaidi ni kwamba akijaribu kutoroka, huenda akauawa.
Je, Watu Wote Wako Huru?
Watu wengi wanafikiri kwamba utumwa haupo tena. Kwa kweli, baada ya mikusanyiko mingi, maazimio, na sheria, utumwa umezuiwa rasmi katika nchi nyingi. Utumwa unachukiwa kwa dhati kila mahali. Sheria za kitaifa hupiga marufuku utumwa, na umezuiwa na sheria za kimataifa—hasa Kifungu cha 4 cha Azimio la Haki za Kibinadamu kwa Wote la 1948, kilichotajwa hapo juu.
Hata hivyo, utumwa ungalipo na unanawiri—ijapokuwa kwa watu fulani ni siri iliyofichwa sana. Kutoka Phnom Penh hadi Paris, kutoka Mumbai hadi Brasília, mamilioni ya wanadamu wenzetu—wanaume, wanawake, na watoto—wanalazimishwa kuishi na kufanya kazi wakiwa watumwa au chini ya hali za utumwa. Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa la London, shirika la kale zaidi ulimwenguni linalochunguza kazi ya kulazimishwa, lataja idadi ya watu walio watumwa kuwa mamia ya mamilioni. Kwa kweli, huenda kukawa na watumwa wengi zaidi ulimwenguni leo kuliko wakati mwingine wowote!
Ni kweli kwamba pingu, mijeledi, na minada tunayojua si ishara ya utumwa wa siku ya kisasa. Kazi ya kulazimishwa, ndoa ya kiutumwa, kufungwa kwa ajili ya deni, kuajiriwa kwa watoto, na mara nyingi ukahaba ni baadhi tu ya njia zilizo wazi zaidi za utumwa wa wakati wetu. Huenda watumwa wakawa masuria, wapanda-ngamia, wakataji-miwa, wafumaji-mikeka, au wajenzi wa barabara. Ni kweli kwamba wengi wao hawauzwi kwenye minada ya umma, lakini kwa kweli wako sawa tu na watumwa wenzao wa kale. Katika visa fulani wao hupatwa na mambo yenye kuhuzunisha hata zaidi maishani.
Ni nani wanaokuwa watumwa? Wanakuwa watumwa jinsi gani? Ni nini kinachofanywa ili kuwasaidia? Je, utumwa utakomeshwa hivi karibuni?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
UTUMWA WA KISASA NI NINI?
Hili ni swali ambalo limekuwa gumu sana kujibiwa hata na Umoja wa Mataifa baada ya kujitahidi kwa miaka mingi. Fasiri moja ya utumwa ni ile iliyobuniwa na Mkusanyiko wa Utumwa wa mwaka wa 1962, iliyosema hivi: “Utumwa ni hali ya kutumia nguvu za kiasi au nguvu zote zinazohusu haki ya kumiliki mtu fulani.” Hata hivyo, neno hilo laweza kufasiriwa vinginevyo. Kulingana na mwandishi wa habari Barbara Crossette, “utumwa ni jina wanaloitwa wafanyakazi wa mshahara mdogo kwenye viwanda vya kutengenezea nguo na mavazi ya michezo huko ng’ambo na kwenye viwanda vya kutumikisha watu katika miji ya Marekani. Hutumiwa kushutumu biashara ya ngono na kazi ya jela.”
Mike Dottridge, mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa, aamini kwamba “kwa kuwa utumwa huwa wa namna tofauti-tofauti—au kadiri neno hilo litumiwavyo kurejezea hali nyingi—kuna hatari kwamba maana yake itapotea.” Aonelea kwamba “utumwa hutambulishwa na kumiliki au kudhibiti maisha ya mtu fulani.” Unatia ndani kushurutisha na kunyima uhuru wa kutembea—uhakika wa kwamba “mtu fulani hayuko huru kuondoka, wala kubadili mwajiri.”
A. M. Rosenthal, akiandika katika The New York Times, asema: “Watumwa huishi maisha ya utumwa—kazi ya kuumiza, kubakwa, njaa, kuteswa, kudhalilishwa kabisa.” Aliongezea hivi: “Waweza kununua mtumwa kwa dola hamsini, kwa hiyo [wamiliki] hawajali wataishi kwa muda gani kabla miili yao haijatupwa ndani ya mto fulani.”
[Hisani]
Ricardo Funari