Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Mhalifu wa Zamani Lazima niandike kusema jinsi nilivyothamini simulizi la Enrique Torres, Jr., lenye kichwa “Simba Angurumaye Awa Kondoo Mpole.” (Agosti 8, 1999) Lilikazia upendo na rehema za Mungu wetu Yehova, na jinsi yeye alivyo mwenye subira kwetu. Pia lilionyesha kwamba tukiwa wazazi, hatupaswi kukata tamaa kuhusu watoto wetu, hata wawe mbali jinsi gani na viwango vya Mungu.
J. F., Uingereza
Nililelewa nikiwa Mkristo, lakini kwa sababu ya mashirika mabaya, nikajiingiza katika dawa za kulevya na jeuri. Nikiwa na umri wa miaka 18, nilihukumiwa kifungo cha miaka 25. Ijapokuwa nimerudishwa katika kutaniko la Kikristo, mara nyingi mimi huhisi kuwa sistahili. Hata hivyo, baada ya kusoma makala hiyo, niliweza kufahamu kwamba Yehova hayuko mbali na wale wanaomtafuta. Ijapokuwa ningali gerezani, simulizi hilo la maisha lilinitia moyo nisimame imara.
R. B., Marekani
Ndege-Mvumaji Makala “Ndege Ambaye Hubusu Maua” (Agosti 8, 1999) ilikuwa nzuri sana. Nimewachunguza ndege-wavumaji hapo awali, lakini sikutambua kwamba wangeweza kuwa wadogo hivyo. Kupitia kwa maneno na picha, mliamsha kupendezwa kwangu katika viumbe hawa wenye kuvutia sana.
R. H., Ujerumani
Nilivutiwa na habari na picha maridadi. Wakati wa kiangazi mara nyingi ndege-wavumaji huja kwenye bustani yangu. Ni shangwe sana kuwatazama ndege hao wa ajabu. Mara nyingi, kuwaona tu hunichangamsha.
C. S. S., Brazili
Usalama wa Ngazi Asanteni kwa makala “Kutumia Ngazi—Je, Wewe Hufanya Ukaguzi Huu wa Usalama?” (Agosti 8, 1999) Hivi majuzi nilianguka kutoka kwenye ngazi, na ikanibidi nipasuliwe goti. Nathamini madokezo kumi mliyotoa na nitayakumbuka wakati mwingine nitumiapo ngazi.
D. N., Mexico
Kituo cha Angani Nina umri wa miaka 16, na sikuzote nimekuwa nikipendezwa na uvumbuzi wa angani. Kwa hiyo, nataka kutoa shukrani zangu kwa makala “Kituo cha Angani cha Kimataifa—Maabara Inayozunguka.” (Agosti 22, 1999) Makala za aina hii hunipendeza sana!
K. E., Marekani
Mwakipa utukufu kituo hicho cha angani bila kukilaumu. Mungu hakutaja hicho kuwa sehemu ya mpango wake kwa mwanadamu. Na gharama ya kurusha chombo kimoja angani, huku mamilioni ya watu wakifa njaa, ni ya kufedhehesha. Mwampunguzia Mungu sifa mnapotukuza vitu kama hivyo.
P. N. M., Uingereza
Biblia husema kwamba ‘wanadamu wamepewa dunia.’ (Zaburi 115:16) Hata hivyo, hakuna msingi wa Maandiko wa kusema kwamba ni vibaya mwanadamu kupendezwa na anga. Kwa kweli, Biblia hutia moyo wanadamu wenye imani watazame mbingu kama njia ya kutazama hekima ya Mungu na uwezo wake wa uumbaji. (Zaburi 8:3, 4; 19:1) Kwa vyovyote vile, halikuwa kusudi letu kukitukuza kituo hicho cha angani kinachokusudiwa; tulikuwa tu tukiripoti mipango ya kukijenga. Iwe kituo hicho cha angani kitaandaa utafiti utakaostahili gharama yake kubwa, twangoja kuona.—Mhariri.
Kuokoka Mnyanyaso Nimemaliza tu kusoma makala “Kumtumikia Mungu Licha ya Kukabiliwa na Kifo.” (Agosti 22, 1999) Kwa sababu ya uvumilivu wa ndugu wa Angola kwa zaidi ya miaka 17, nchi ambayo ilionekana kuwa ukiwa kiroho sasa imebarikiwa na matokeo mengi sana!
R. Y., Japani