Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Je, Dubu wa Kikahawia wa Ulaya Wanatoweka?

Dubu wa kikahawia katika Ulaya Magharibi wamo hatarini, kulingana na Hazina ya Ulimwenguni Pote ya Maliasili (WWF). Idadi yao imepungua hadi kufikia sehemu ndogo sita tu. “Walio hatarini zaidi ya dubu hao wa kikahawia hupatikana Ufaransa, Hispania, na Italia, ambako wahifadhi-mazingira wanaonya kwamba huenda wakatoweka ikiwa dubu hawataletwa kutoka mahali pengine,” lasema gazeti la The Daily Telegraph la London. “Katika Italia, kuna dubu wanne tu kusini mwa Alp,” laongezea gazeti hilo. Katika Ugiriki, kuna tatizo zito la uwindaji haramu unaofanywa na wakulima na wafugaji-nyuki, waliokasirishwa na kuharibiwa kwa mifugo au mizinga. Tofauti na hilo, sehemu fulani za Ulaya Mashariki zinaripoti idadi inayoongezeka ya dubu. Hatua madhubuti za ulinzi huko Rumania na miradi ya kuleta dubu kutoka sehemu nyingine zimewezesha idadi yao iimarike na kuongezeka. Na katika Urusi, ambako dubu hulindwa, kuna dubu wapatao 36,000. “Hatua ya hima ni muhimu ili kuokoa dubu waliobaki Ulaya Magharibi,” asema Callum Rankine, wa Kampeni ya Ulaya ya Kuhifadhi Wala-Nyama ya shirika la WWF. “Hatua isipochukuliwa mara moja, dubu hawa watatoweka kabisa.”

Msaada Ghali

Mamilioni ya watu wamenufaika na dawa zilizochangwa katika nyakati zenye taabu. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) wafunua kwamba dawa zilizochangwa mara nyingi hazitambulishwi ifaavyo au huharibika baada ya muda mfupi. Ingawa zinatolewa kwa nia njema, dawa nyingi “hushindwa kutosheleza mahitaji halisi ya kiafya ya haraka na, zinapoingia nchini, hurundamana kwenye ghala za ugawanyaji ambazo tayari zimejaa kupita kiasi na huwa vigumu kuziharibu,” asema ofisa wa WHO Dakt. Jonathan Quick. Zaidi ya nusu ya dawa zilizochangwa Bosnia hazikufaa. Tanuri za pekee zilihitaji kupelekwa Armenia na Mostar, Bosnia na Herzegovina, ili kuharibu dawa zisizofaa. Inakadiriwa kwamba gharama ya kusafirisha tani 1,000 za dawa zisizofaa kutoka Kroatia hadi mahali penginepo ili kuharibiwa kwa njia inayofaa ni kati ya dola za Marekani milioni mbili na nne.

Sauti Yatumiwa Kuwa Chambo

Ingawa mimea mingi huvutia vichavushaji kwa rangi au harufu, mmea wa kitropiki unaoitwa Mucuna holtoni hufanya kazi hiyo kwa kuakisi sauti, laripoti gazeti la Ujerumani la Das Tier. Popo hutua kwenye mmea huo unaotambaa, ambao hutokeza mfano wa mazingira yao kwa kutoa ishara za sauti isiyosikika kwa sikio la binadamu. Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Erlangen waligundua kwamba nekta ya mmea huo hutenda kama “kiakisi sauti,” kwa kuakisi ishara za sauti isiyosikika kwa sikio la binadamu na kuirudisha moja kwa moja hadi kwenye popo. “Katika njia hii mmea huo hufanya iwe rahisi zaidi kwa popo kuona maua,” lasema gazeti hilo.

Hatari za Kuvu

“Katika Ulaya Mashariki na kaskazini mwa Italia, ambako kuna zoea la kuokota viyoga, watu wengi hufa na kusumishwa kila mwaka,” laripoti gazeti The Times la London. Kwa sababu kumekuwa na zoea la kupika kwa kutumia kuvu za mwituni, wataalamu wanaonya kuhusu hatari za kula mojawapo ya aina zipatazo 250 zenye sumu zinazokua katika sehemu za mashambani huko Uingereza. Uyoga unaoitwa death cap na destroying angel zaweza kufisha zinapoliwa. Ili kujilinda wenyewe, waokotaji wa viyoga wanahimizwa wajiunge na vikundi vinavyoongozwa na wataalamu wa kutafuta viyoga. “Hakuna sheria sahili za kuonyesha ikiwa kuvu fulani hudhuru au haidhuru, kwa hiyo ni kosa mtu kujiokotea mwenyewe bila mtaalamu,” aonya mshiriki mmoja wa ngazi ya juu wa Chama cha Taaluma ya Kuvu cha Uingereza.

Athari za Kiuchumi Ziletwazo na UKIMWI

Mbali na kutokeza msiba kwa afya ya umma, UKIMWI unaelekea kwa haraka kuwa msiba wa kiuchumi barani Afrika, laripoti gazeti la Le Monde. Kukiwa na watu wapatao milioni 23 wenye HIV na milioni 2 wanaokufa kila mwaka kutokana na virusi hivyo, “karibuni ugonjwa wa kuenea wa UKIMWI utabatilisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Afrika.” Makampuni ya Afrika yanapambana na tatizo la wafanyakazi wengi wasiofika kazini au vifo vinavyosababishwa na maradhi hayo. Kampuni moja ya kitaifa ya reli imepoteza asilimia 10 ya wafanyakazi wake. Kwenye shirika jingine kubwa, wafanyakazi 3,400 kati ya 11,500 wana virusi vya HIV. Kilimo kinadidimia huku wakulima wakiangamizwa na UKIMWI. Kwa kuongezea, kiwango cha elimu kinapungua, na watu wasiojua kusoma na kuandika wanaongezeka, kwa kuwa familia hazina wala fedha wala wakati wa kupeleka watoto shuleni na mamia ya walimu wamekufa kwa UKIMWI.

Waastronomia Waomba Kuwe na Hali ya Ukimya

Waastronomia wa redio, wanaosikiliza ishara zinazoonyesha kuzaliwa kwa galaksi na nyota za kwanza, wanazidi kufadhaika kwa sababu ya “kuwepo kwa vifaa vingi vya elektroni vya ustaarabu wa kisasa,” laripoti gazeti la International Herald Tribune. Vituo vya televisheni, transmita za redio, setilaiti za mawasiliano, na simu za mkononi zinafanya sauti ya chinichini kutoka angani isisikiwe na wanasayansi wanaojaribu kuisikia. Ili kufanya utafiti wao, waastronomia wanatafuta mahali palipo na utulivu “ambapo mawasiliano yote ya redio yatapigwa marufuku.” Wakiwa huko wanakusudia kujenga virushia-sauti vingi vya redio vitakavyosambaa mamia ya kilometa ambavyo vitakuwa “na nguvu mara 100 zaidi kuliko vifaa vinavyotumika leo.” Wanasayansi wanatumaini kwamba habari itakayopatikana itasaidia kujibu maswali yahusuyo mwanzo wa wakati, anga, na mata.

Idadi ya Ndege Yaongezeka Sana Katika Mexico City

Idadi ya ndege haiwezi kudhibitiwa tena katika Mexico City. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la Reforma, takriban njiwa 1,335,000 sasa wanaishi katika jiji hilo. Ndege hao hupenda kupumzika kwenye nguzo za ukumbusho na sanamu. Wataalamu wa kudhibiti ndege wameripoti kwamba “ndege ambao wamefaana na mazingira ya jijini hugawanya safari zao za kila siku mara tatu,” lasema gazeti hilo. “Wanachagua mahali pamoja pa kulala, pengine pa kutafuta chakula, na pengine pa kupumzikia, lakini katika [kila sehemu] huacha alama ya kinyesi chao.” Pia husababisha magonjwa mbalimbali kuanzia yale ya mizio hadi ya bakteria, maambukizo yanayoletwa na kuvu, na virusi. Shirika la International Association for the Ecological Protection and Peaceful Relocation of Urban Doves “limependekeza kubuniwa kwa sheria inayokataza kulisha ndege hao mahali pa umma.” Hata hivyo, lapendekeza pia “kuadhibu mtu yeyote anayeua ndege hao ikiwa ni hatua ya kudhibiti idadi yao.”

“Wakumbatiwa Hadi Kufa”

‘Mojawapo ya miti ya kale mikubwa zaidi ulimwenguni inakumbatiwa hadi kufa,’ laripoti gazeti la The Australian. Mti huo wa jamii ya msunobari, ulioko kaskazini ya Auckland, New Zealand, hutembelewa kila mwaka na maelfu ya watalii ambao kwa kufuata desturi huunganisha mikono yao kuzunguka ukubwa wake, na kukanyaga-kanyaga shina lake. “Mti huo una urefu unaozidi meta 50 lakini si mojawapo ya miti mirefu zaidi ulimwenguni,” lasema gazeti hilo. “Hata hivyo, kuhusu kiasi cha mbao unachotokeza, ni miongoni mwa miti mikubwa zaidi.” Unajulikana kuwa “mzee wa msitu,” kirasmi una miaka 2,000 lakini unaaminiwa kuwa na miaka maradufu ya hiyo. Baada ya kuokoka miaka mingi ya misiba ya asili, visumbufu, na vitisho vya kukatwa, yaelekea sasa utakumbatiwa hadi kufa. Ofisa mmoja wa kuhifadhi mazingira asema hivi: “Labda unakufa lakini hatujui kama hatua hiyo yaweza kurekebishwa au la.”

Je, Kunyonyesha Hudhibiti Uzito?

Watafiti wanasema kwamba wamegundua manufaa nyingine ya kunyonyesha: Huenda kukasaidia kuzuia mtoto asiwe mzito kupita kiasi baadaye maishani. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la Ujerumani la Focus, kikundi cha watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Munich walifikia mkataa kuhusu uzito wa watoto 9,357 wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi sita na kuchunguza chakula ambacho kila mmoja alilishwa akiwa kitoto kichanga. Matokeo yalionyesha kwamba watoto walionyonyeshwa kwa miezi mitatu hadi mitano walikabili mwelekeo unaopungua asilimia 35 wa kuwa wazito kupita kiasi walipoanza kwenda shuleni kuliko wale ambao hawakupata kunyonyeshwa. Kwa kweli, kadiri mtoto anavyonyonyeshwa kwa muda mrefu zaidi ndivyo hukabili uwezekano mdogo zaidi wa kuwa mzito kupita kiasi. Mtafiti mmoja asifu maziwa ya mama kuwa ndiyo yanayotokeza manufaa hayo, ambayo husaidia kuyeyusha chakula.

Watoto Wanahitaji Maji Kiasi Gani?

Watoto wenye umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka minne mara nyingi hunywa maji kidogo sana. Hayo yalifunuliwa katika uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Uchunguzi wa Lishe ya Watoto, huko Dortmund, Ujerumani, na kuripotiwa katika gazeti la uuzaji-bidhaa la Test. Watoto wenye umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka minne huweza kuathiriwa hasa na kuishiwa maji mwilini na wapaswa kunywa takriban lita moja ya maji, mbali na maji yaliyo katika chakula. Kwa wastani, wao hunywa kiasi kinachopungua kwa thuluthi moja—mara nyingi si kwa hiari yao. Watafiti waligundua kwamba katika kisa 1 kati ya visa 5, mzazi alimnyima mtoto kinywaji alipokiomba. Kinywaji bora zaidi ni gani? Mahali ambapo maji ni salama, ndiyo kinywaji bora, lasema gazeti la Test.