Kwa Nini Uache Kuvuta Sigareti?
Kwa Nini Uache Kuvuta Sigareti?
WATU wanaotaka kuishi muda mrefu kwa furaha hawatavuta sigareti. Uwezekano wa kwamba mvutaji-sigareti wa muda mrefu atakufa hatimaye kutokana na tumbaku ni 1 kwa 2. Mkurugenzi-mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) alisema hivi: “Sigareti ni . . . bidhaa iliyobuniwa kwa werevu ili kutokeza kiasi barabara cha nikotini cha kumfanya mvutaji awe mraibu maishani kabla ya kumwua.”
Kwa hiyo, sababu moja ya kuacha kuvuta sigareti ni kwamba inahatarisha afya na uhai. Kuvuta sigareti kumeshirikishwa na zaidi ya maradhi 25 yenye kuhatarisha uhai. Kwa mfano, kunachangia sana mshtuko wa moyo, kupooza ubongo, mkamba sugu, kuvimba mapafu, na kansa mbalimbali, hasa kansa ya mapafu.
Pasipo shaka, mtu aweza kuvuta sigareti kwa miaka mingi kabla hajashikwa na mojawapo ya maradhi hayo. Wakati huohuo, mvutaji-sigareti huwakera wengine. Matangazo ya biashara huonyesha wavutaji-sigareti wakiwa wenye kuvutia na wenye afya. Ukweli ni kwamba sivyo ilivyo. Kuvuta sigareti hutokeza pumzi yenye uvundo na hutia meno na vidole rangi ya kahawia-manjano. Huwafanya wanaume wawe mahanithi. Humfanya mvutaji-sigareti akohoe na kuhema-hema. Pia wavutaji-sigareti huelekea kuwa na makunyanzi usoni na matatizo mengine ya ngozi mapema.
Jinsi Kuvuta Sigareti Kunavyowaathiri Wengine
Biblia husema: “Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.” (Mathayo 22:39) Kuwapenda majirani wako—na washiriki wa familia yako wakiwa majirani wa karibu zaidi—ni sababu muhimu ya kuacha.
Kuvuta sigareti huumiza wengine. Zamani kidogo mvutaji angeweza kuvutia sigareti popote pale bila kipingamizi chochote. Lakini mitazamo
inabadilika kwa sababu watu wengi zaidi wanaelewa hatari za kuvuta moshi unaotokezwa na sigareti za wengine. Kwa mfano, mtu asiyevuta sigareti aliyefunga ndoa na mvutaji-sigareti yuko katika hatari ya kuugua kansa ya mapafu inayozidi kwa asilimia 30 hatari hiyo kama angekuwa amefunga ndoa na mtu asiyevuta sigareti. Watoto wanaoishi na wazazi wanaovuta sigareti wanaelekea sana kuugua nimonia au mkamba katika miaka miwili ya kwanza ya maisha yao kuliko watoto wanaoishi katika nyumba ambamo hamna mvutaji.Wanawake wajawazito wanaovuta sigareti huhatarisha watoto wao ambao hawajazaliwa. Nikotini, kaboni monoksaidi, na kemikali nyingine hatari zilizo katika moshi wa sigareti hufyonzwa na damu ya mama na kuingia moja kwa moja katika mwili wa mtoto aliye katika tumbo la uzazi. Matokeo yatia ndani hatari kubwa ya kuharibika kwa mimba, mtoto kufa katika tumbo la uzazi, na vifo vya watoto waliozaliwa karibuni. Isitoshe, hatari ya kifo cha ghafula cha kitoto ni mara tatu zaidi kwa watoto wachanga ambao mama zao walivuta sigareti walipokuwa wajawazito.
Gharama Ni Nyingi
Sababu nyingine ya kuacha kuvuta sigareti ni kwamba ni ghali mno. Uchunguzi uliofanywa na Benki ya Dunia ulikadiria kwamba gharama za kutunza afya zisababishwazo na uvutaji-sigareti hufikia takriban dola bilioni 200 za Marekani kila mwaka. Bila shaka, kiasi hicho, hakifunui mateso na maumivu yanayowakumba wale wanaoshikwa na maradhi yaletwayo na tumbaku.
Ni rahisi kupiga hesabu ya gharama ya sigareti ya kila mvutaji. Ikiwa wewe ni mvutaji-sigareti, zidisha kiasi cha fedha unazotumia kununulia sigareti kwa siku moja mara 365. Hesabu hiyo itakuonyesha kiasi cha fedha unachotumia kwa mwaka. Zidisha kiasi hicho mara kumi, na utaona gharama utakayopata ikiwa utavuta sigareti kwa miaka kumi zaidi. Jawabu laweza kukushangaza. Fikiria njia nyingine unayoweza kutumia fedha hizo zote.
Je, Ni Salama Kubadili Sigareti?
Makampuni ya tumbaku hutangaza sigareti zenye kiasi kidogo cha nikotini na lami—zinazoitwa sigareti zisizo kali—kama njia ya
kupunguza hatari za afya zinazoletwa na kuvuta sigareti. Hata hivyo, wale wanaovuta sigareti zenye kiasi kidogo cha nikotini na lami huwa na hamu sana ya kiasi kilekile cha nikotini kama awali. Hivyo basi, wavutaji wanaobadili sigareti kwa kawaida hujitosheleza kwa kuvuta sigareti zaidi, huvuta kwa nguvu na mara nyingi zaidi, au huvuta sigareti zaidi za namna zote mbili. Hata wale ambao hawabadili sigareti ili wajitosheleze, wanapata faida kidogo za afya ikilinganishwa na faida za kuacha kabisa.Vipi juu ya viko na biri? Ingawa kwa muda mrefu makampuni ya tumbaku yametumia viko na biri kuwa ishara za umashuhuri, moshi wake ni hatari sana kama wa sigareti. Hata ikiwa wavutaji hawavuti moshi wa biri au kiko, bado wako katika hatari ya kuugua kansa ya mdomo, kinywa, na ulimi.
Je, tumbaku zisizokuwa na moshi ni salama? Zinatumiwa kwa njia mbili: kunusa ugoro na kutafuna tumbaku. Ugoro ni tumbaku ya unga, kwa kawaida huuzwa makoponi au katika vifuko. Kwa kawaida, watumiaji huitia mdomoni. Tumbaku ya kutafunwa huuzwa katika nyuzi ndefu, kwa kawaida hupakiwa kifukoni. Kama jina lake linavyodokeza, inatafunwa haimumunywi. Kunusa na kutafuna tumbaku husababisha pumzi yenye uvundo kinywani, huchafua meno, kansa ya kinywa na koromeo, uraibu wa nikotini, vidonda vyeupe mdomoni vinavyoweza kutokeza kansa, kuharibika kwa ufizi na mfupa unaozingira meno. Kwa wazi, kumumunya au kutafuna tumbaku si jambo la hekima sawa na kuvuta sigareti.
Manufaa ya Kuacha
Tuseme wewe ni mvutaji-sigareti wa muda mrefu. Ni nini hutukia unapoacha? Dakika 20 baada ya kuvuta sigareti ya mwisho, msongo wako wa damu hushuka hadi kipimo cha kawaida. Baada ya juma moja mwili wako husafisha nikotini yote. Baada ya mwezi mmoja kikohozi, kuziba puani, uchovu, na kuhema-hema huanza kupungua. Baada ya miaka mitano hatari ya kufa kutokana na kansa ya mapafu hupungua kwa asilimia 50. Baada ya miaka 15 hatari ya kuugua maradhi ya mishipa ya moyo hupungua na
kufikia ile ya mtu ambaye hajawahi kuvuta sigareti kamwe.Utafurahia ladha tamu ya chakula. Pumzi, mwili, na mavazi yako hayatakuwa na uvundo. Hutahangaishwa na gharama ya kununua tumbaku. Utahisi kwamba umetimiza mradi fulani. Iwapo una watoto, kielelezo chako kitapunguza uwezekano wao wa kuwa wavutaji-sigareti. Yaelekea kwamba utaishi muda mrefu zaidi. Zaidi, utakuwa ukitenda kupatana na mapenzi ya Mungu, kwa kuwa Biblia husema: “Acheni tujisafishe wenyewe kila unajisi wa mwili na wa roho.” (2 Wakorintho 7:1) Usihisi kwamba ni kuchelewa mno kwako kuacha; itakuwa bora, ukiacha haraka iwezekanavyo.
Kinachofanya Iwe Vigumu Sana Kuacha
Ni vigumu kuacha kuvuta sigareti—hata kwa wale ambao wameazimia kabisa. Ugumu huo husababishwa hasa na nikotini iliyo katika tumbaku ambayo ni dawa ya kulevya yenye uwezo mkubwa wa kuleta uraibu. “Katika viwango vya uwezo wa kutokeza uraibu wa dawa za kulevya zinazoathiri akili, nikotini ilionwa kuwa na uwezo zaidi wa kutokeza uraibu kuliko heroini [na] kokeini,” lataarifu WHO. Tofauti na heroini na kokeini, nikotini haitokezi dalili za wazi za ulevi, kwa hiyo ni rahisi kupuuza uwezo wake. Lakini hisia nyepesi ya furaha inayotokezwa huwafanya watu wengi waendelee kuivuta ili wahisi hivyo tena na tena. Kwa kweli nikotini hubadili hali yako; hutuliza mahangaiko. Hata hivyo, mkazo unaopunguzwa na sigareti husababishwa kwa sehemu na hamu ya nikotini hiyo.
Ni vigumu pia kuacha kuvuta sigareti kwa sababu ni tabia inayozoewa. Mbali na kuwa waraibu wa nikotini, wavutaji-sigareti husitawisha mazoea yasiyokoma ya kuwasha na kuvuta. ‘Ni jambo unalofanya kwa mikono yako.’ ‘Hupitisha wakati,’ huenda wengine wakasema.
Jambo la tatu linalofanya iwe vigumu kuacha ni kuwa tumbaku imekuwa sehemu ya maisha. Makampuni ya tumbaku hutumia takriban dola bilioni sita za Marekani kila mwaka katika kampeni za matangazo ya biashara ambayo huwasifu wavutaji kuwa watu wenye kuvutia, wenye bidii, afya, na wenye akili. Kwa kawaida wao huonyeshwa wakiendesha farasi, wakiogelea, wakicheza tenisi, au wakishiriki utendaji mwingine wenye kuvutia. Sinema na vipindi vya televisheni huonyesha watu wakivuta sigareti—na mara nyingi si wahalifu. Tumbaku huuzwa kihalali na yaweza kupatikana kwa urahisi karibu kila mahali. Mara nyingi wengi wetu hukutana na mvutaji-sigareti. Huwezi kuepuka uvutano huo.
Kwa kusikitisha, hakuna tembe uwezayo kumeza ili uzuie hamu ya kuvuta sigareti kama vile aspirini iwezavyo kuponya maumivu ya kichwa. Lazima mtu aazimie endapo atafanikiwa katika kazi ngumu ya kuacha kuvuta. Sawa na kupunguza uzito, kunahitaji uwajibikaji mkubwa wa muda mrefu. Daraka la kufanikiwa lategemea mvutaji-sigareti.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Wamekuwa Waraibu Mapema
Uchunguzi mmoja huko Marekani ulionyesha kwamba kijana 1 kati ya 4 waliojaribu sigareti hatimaye alikuja kuwa mraibu. Viwango hivyo vya uraibu ni sawa na viwango vya watumiaji wa kokeini na heroini waliochunguzwa. Ingawa asilimia 70 hivi ya wabalehe wanaovuta sigareti hujuta, ni wachache wanaoweza kuacha.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Moshi wa Sigareti Una Nini?
Moshi wa sigareti una lami yenye kemikali zaidi ya 4,000. Kemikali 43 kati yake husababisha kansa. Miongoni mwake ni sianidi, benzini, methanoli, na asetilini (fueli inayotumiwa katika vitambulio). Moshi wa sigareti huwa pia na nitrojeni oksaidi na kaboni monoksaidi, gesi zenye sumu. Sehemu yake muhimu sana ni nikotini, dawa ya kulevya yenye uwezo mkubwa wa kutokeza uraibu.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Kumsaidia Mtu Umpendaye Aache
Ikiwa wewe huvuti sigareti na unajua hatari za kuvuta sigareti, yaelekea kwamba unavunjika moyo wakati marafiki na wapendwa wako wanapoendelea kuvuta. Utawasaidiaje waache? Kusumbua, kusihisihi, kushurutisha, na kudhihaki mara nyingi hakufanikiwi. Wala kuonya kila mara kwa ukali. Badala ya kuacha, mvutaji-sigareti aweza kuvuta sigareti ili apunguze maumivu ya kihisia-moyo yanayosababishwa na mbinu hizo. Hivyo jaribu kuelewa jinsi ilivyo vigumu kuacha na kwamba ni vigumu zaidi kwa watu fulani kuliko wengine.
Huwezi kumfanya mtu aache kuvuta sigareti. Ni lazima mvutaji mwenyewe aazimie moyoni na kwa usadikisho kuacha sigareti. Wahitaji kutumia njia za upendo za kumtia moyo na kumtegemeza mtu mwenye tamaa ya kuacha.
Unaweza kufanyaje hivyo? Katika wakati unaofaa, waweza kumwambia mtu huyo unampenda na kwamba unahangaishwa na zoea lake la kuvuta sigareti. Mweleze kwamba uko tayari kuunga mkono uamuzi wowote wa kuacha. Bila shaka, mfikio huu ukitumiwa kupita kiasi, utapoteza maana na kukosa matokeo.
Unaweza kufanya nini mpendwa wako akiamua kuacha? Kumbuka kwamba anaweza kuwa na dalili za kuacha, kutia ndani kusumbua-sumbua na kushuka moyo. Maumivu ya kichwa na shida ya kupata usingizi yaweza kutatiza pia. Mkumbushe mpendwa wako kwamba dalili hizo ni za muda tu na zinaonyesha kwamba mwili unajipatanisha na hali mpya ya afya. Uwe mchangamfu na utarajie kufaulu. Mweleze jinsi unavyofurahi kwamba yeye anaacha kuvuta sigareti. Katika muda wote wa kuacha, msaidie mpendwa wako aepuke hali zenye mkazo zinazoweza kumfanya arudie uvutaji-sigareti.
Namna gani ikiwa anarudia uvutaji? Usikasirike kupita kiasi. Uwe mwenye huruma. Ione hali hiyo kuwa somo kwenu nyote, linaloonyesha kwamba huenda atafaulu akijaribu tena.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Makampuni ya tumbaku hutumia takriban dola bilioni sita za Marekani kila mwaka katika matangazo ya biashara