Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nini Kilichompata Peter Mdogo?

Ni Nini Kilichompata Peter Mdogo?

Ni Nini Kilichompata Peter Mdogo?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA EKUADO

GAZETI la Amkeni! la Agosti 22, 1970, la Kiingereza lilikuwa na makala yenye kichwa “Upasuaji wa Moyo Bila Utiaji-Damu Mishipani.” Lilisimulia kisa cha mvulana mwenye umri wa miaka saba kutoka Kanada anayeitwa Peter, aliyehitaji kupasuliwa ili kuokoa uhai wake mnamo mwaka wa 1963.

Tabibu mkuu wa Peter alisema kwamba kulikuwa na njia ya kurekebisha mshipa wake wa moyo uliokuwa na kasoro. Lakini wakati wazazi wa Peter walipompeleka mwanao kwa mtaalamu na kuuliza ikiwa upasuaji huo ungefanywa bila damu, daktari huyo alijibu: “La. Haiwezekani kabisa. Naweza kuwahakikishia hilo.”

Pasipo kuvunjika moyo, wazazi wa Peter waliendelea kutafuta na hatimaye wakapata daktari-mpasuaji aliyekubali kufanya upasuaji bila damu. Ikawaje? Ijapokuwa Peter hakufa wakati wa upasuaji huo, wazazi wake waliambiwa kwamba mafanikio ya upasuaji huo yangejulikana tu baada ya muda fulani. Kwa hiyo, ni nini kilichompata Peter mdogo?

Alipokuwa na umri wa miaka 13, Peter na familia yao walihamia Ekuado, Amerika Kusini, kutumikia mahali ambapo kulikuwa na uhitaji mkubwa zaidi wa wahubiri wa habari njema za Ufalme wa Mungu. (Mathayo 24:14) Peter alibatizwa akiwa na umri wa miaka 15 na kuwa painia wa kawaida (mweneza-evanjeli wa wakati wote) akiwa na umri wa miaka 18. Akiwa na umri wa miaka 26 akawa painia wa pekee, akitumikia katika kijiji kimoja kilicho kwenye mwinuko wa meta 3,000 juu ya usawa wa bahari katika Andes. Mnamo mwaka wa 1988, akiwa na umri wa miaka 31, Peter pamoja na mke wake, Isabel, walianza kutumikia wakiwa wawakilishi wasafirio wa Watch Tower Society. Anaendelea kutumikia katika wadhifa huo leo, akizuru kutaniko tofauti-tofauti kila juma ili kulitia moyo.

Kwa kweli, Peter ni mtendaji sana maishani, na hahitaji upasuaji wowote wa ziada. Yeye pamoja na maelfu ya Mashahidi wengine wanashukuru kama nini kwa ajili ya ushirikiano wa madaktari-wapasuaji stadi ambao wamestahi haki za wagonjwa wao!

[Picha katika ukurasa wa 23]

Peter akiwa na umri wa miaka saba, muda mfupi tu baada ya kufanyiwa upasuaji

[Picha katika ukurasa wa 23]

Peter na Isabel Johnston leo