Petra Jiji Lililochongwa Kutoka Kwenye Mwamba
Petra Jiji Lililochongwa Kutoka Kwenye Mwamba
MAJIJI mengi ya kale yalizingirwa na mito muhimu, iliyokuwa na maji mengi ambayo yaliyategemeza na kuyalinda. Lakini kulikuwa na jiji moja kwenye mpaka wa kaskazini-magharibi wa Jangwa la Arabuni ambalo lilikuwa mashuhuri kwa sababu ya uhaba wa maji. Jiji hilo liliitwa Petra.
Katika nchi za jangwa zinazopakana na Mediterania, njia za msafara ziliunganisha miji ya mbali kama vile barabara za kisasa huvuka kontinenti. Lakini kama vile magari huhitaji vituo vya petroli, ndivyo na ngamia—licha ya kusimuliwa kuwa wavumilivu katika hekaya—huhitaji vituo vya maji. Petra lilikuwa mojawapo ya vituo vya maji vilivyo mashuhuri zaidi katika Mashariki ya Kati, miaka 2,000 iliyopita.
Petra lilikuwa kwenye kivuko cha njia mbili muhimu za biashara. Moja iliunganisha Bahari Nyekundu na Dameski, kisha nyingine, Ghuba ya Uajemi na Gaza, kwenye kingo za Mediterania. Misafara kutoka Ghuba, ikiwa na mizigo mingi ya vikolezo vyenye thamani, ilihitaji kuvumilia hali ngumu za Jangwa la Arabuni kwa majuma kadhaa kabla ya kuwasili hatimaye kwenye korongo kuu, nyembamba na tulivu—Siq—mwingilio wenye kupendeza wa Petra. Huko Petra mtu angeweza kupata chakula na mahali pa kulala, na zaidi ya yote, maji baridi yenye kuburudisha.
Bila shaka, raia wa Petra hawakutoa huduma
hizo bila malipo. Mwanahistoria Mroma Pliny aripoti kwamba walinzi, walinda-lango, makuhani, na watumishi wa mfalme walihitaji kupewa zawadi—mbali na malipo ya chakula cha mifugo na makao. Lakini bei ghali mno za vikolezo na marashi katika miji yenye fanaka ya Ulaya zilifanya misafara izidi kuja na kutajirisha Petra.Kuhifadhi Maji na Kushinda Mawe
Petra hupokea mvua ya kiasi cha sentimeta 15 tu kila mwaka, na vijito ni nadra sana. Watu wa Petra walipataje maji yenye thamani ili kuendeleza jiji hilo? Walichonga milangobahari, mabwawa, na matangi ya maji kutoka kwenye mwamba mgumu. Baada ya muda, karibu kila tone la mvua lililoanguka kandokando ya Petra lilikusanywa na kuhifadhiwa. Ustadi wao wa kukusanya na kuhifadhi maji uliwezesha watu wa Petra kulimia mazao, kufuga ngamia, na kujenga kituo cha biashara ambacho wanabiashara wake walitajirishwa na ubani na manemane walizouza. Hata leo, mlangobahari wa mawe wenye kujipinda-pinda husafirisha maji kupitia Siq yote.
Ikiwa raia wa Petra walijua namna ya kutumia maji, pia walikuwa waashi stadi. Jina lenyewe Petra, linalomaanisha “Tungamo-Mwamba,” humfanya mtu afikiri juu ya jiwe. Na kwa kweli Petra lilikuwa jiji la mawe—tofauti na jiji jingine lolote katika Roma. Wakazi wa Nabataea, wajenzi wa jiji hilo, walichonga kwa saburi nyumba zao, maziara, na mahekalu kutoka kwenye mwamba mgumu. Milima ya mawe-mchanga mekundu ambayo Petra ilichongwa kutoka kwake ilifaa sana, na kufikia karne ya kwanza W.K., jiji kubwa sana lilikuwa limejengwa katikati ya jangwa.
Biashara Hadi Utalii
Petra lilitajirishwa na biashara milenia mbili zilizopita. Lakini wakati Waroma walipogundua njia za baharini zinazoelekea Mashariki, biashara ya vikolezo iliyofanywa kwenye bara ilididimia na hatua kwa hatua Petra likabaki jangwa. Lakini kazi ya waashi wa jangwa haikutoweka. Leo, takriban watalii nusu milioni huzuru Jordan kila mwaka ili kutazama jiji la Petra la rangi ya waridi nyekundu, ambalo majengo yake yangali yanashuhudia umaarufu wa kale.
Baada ya mgeni kutembea kupitia Siq yenye baridi, iliyo na urefu wa kilometa moja, akigeuka kwenye kuta za korongo kuu kwa ghafula ataona Treasury, jengo lenye kuvutia kwa sababu ya ukubwa wake na ambalo sehemu yake ya mbele ilichongwa kutoka kwenye jabali kubwa sana. Watu wengi watakumbuka sura yake, ni mojawapo ya majengo bora zaidi yaliyohifadhiwa ya karne ya kwanza. Jumba hilo lilipewa jina la buli la jiwe kubwa lililo juu ya jengo na ambalo ladhaniwa kuwa lilihifadhi dhahabu na mawe ya thamani.
Mahali ambapo korongo kuu ni pana, mtalii huingia eneo la asili lenye mteremko na kuta za mawe-mchanga lililo na mapango mengi. Lakini uangalifu wake huelekezwa hasa kwa maziara—maziara yaliyochongwa kutoka kwenye miamba, maziara marefu sana hivi kwamba hufanya wageni wanaoingia sehemu za ndani zenye giza waonekane kuwa wadogo mno. Safu ya nguzo na ukumbi wa michezo huthibitisha kuwepo kwa Waroma katika jiji hilo katika karne ya kwanza na ya pili.
Mabedui wa siku za kisasa, wazao wa Nabataea, hujitolea kubeba watalii walio dhaifu kwa ngamia, huuza hedaya, au kuwapa mifugo yao maji kwenye mabubujiko ya Petra, ambayo huburudisha mwanadamu na mnyama. Barabara za kale za mawe za jiji la Petra zingali zimetengwa kwa ajili ya ngamia, farasi, na punda peke yao. Hivyo, leo jiji hilo lina sauti zilezile zilizosikika siku za kale, wakati ambapo ngamia walikuwa mashuhuri na Petra lilitawala jangwa.
Jua lituapo kwenye jiji hilo, na kuongeza rangi nyekundu kwenye sehemu za mbele za majengo hayo makubwa, mgeni mwenye kufikiri aweza kutafakari masomo tunayojifunza kutokana na Petra. Bila shaka jiji hilo lathibitisha ubunifu wa mwanadamu wa kuhifadhi maliasili chache, hata katika mazingira yasiyofaa. Lakini pia latumika kuwa kikumbusha cha kuelimisha cha kwamba mali za kimwili zaweza ‘kuruka mbinguni’ upesi sana.—Mithali 23:4, 5.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Picha ndogo: Garo Nalbandian