Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ulimwengu Ulio na Uraibu wa Sigareti

Ulimwengu Ulio na Uraibu wa Sigareti

Ulimwengu Ulio na Uraibu wa Sigareti

BILL alikuwa mwanamume mwenye fadhili, mwenye akili, na mkakamavu. Aliipenda familia yake. Hata hivyo, alianza kuvuta sigareti akiwa bado kijana. Baadaye maishani alichukia zoea hilo. Hata alipokuwa akivuta sigareti, aliwaonya sana wanawe wasivute sigareti, huku akieleza jinsi lilivyo tendo la kipumbavu. Nyakati nyingine angekunjakunja paketi ya sigareti kwa mikono yake yenye nguvu na kuitupa mbali chumbani, huku akiapa kwamba hatavuta sigareti nyingine. Hata hivyo, punde si punde alianza kuvuta sigareti tena—kwanza kwa kujificha, kisha waziwazi.

Bill alikufa kutokana na kansa miaka 15 iliyopita, baada ya kuteseka sana kwa miezi mingi. Kama hangelikuwa mvutaji-sigareti, labda angelikuwa hai leo. Bado mkewe angelikuwa na mume; na wanawe wangelikuwa na baba.

Japo kifo cha Bill kiliihuzunisha familia yake, lakini hakishangazi. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), magonjwa yasababishwayo na uvutaji wa tumbaku huua takriban watu milioni nne kila mwaka, au mtu mmoja kila sekunde nane. Uvutaji-tumbaku ni kisababishi kikuu kinachoweza kuzuiwa cha maradhi ulimwenguni kote. Hali ya sasa ikiendelea, baada ya miaka 20 uvutaji-sigareti utakuwa kisababishi kikuu cha kifo na ulemavu ulimwenguni kote, utaua watu wengi zaidi ya UKIMWI, kifua kikuu, vifo vya ujauzito, aksidenti za magari, kujiua, na machinjo ya binadamu kwa pamoja.

Sigareti huua. Lakini wavutaji ni wengi mno. Shirika la WHO lataarifu kwamba ulimwenguni pote angalau watu bilioni 1.1 ni wavutaji-sigareti. Hilo lamaanisha kwamba takriban thuluthi ya watu wazima ulimwenguni huvuta sigareti.

Wachunguzi wanakadiria kwamba ingawa kampuni za tumbaku hulipa mamia ya mamilioni ya dola sasa kwa sababu ya mashtaka ya kisheria, kiasi hicho ni kidogo sana kikilinganishwa na faida za mabilioni ya dola wanazochuma. Katika Marekani pekee, viwanda vya tumbaku hutengeneza sigareti bilioni 1.5 hivi kila siku. Ulimwenguni kote, kampuni za tumbaku na mashirika ya kiserikali huuza zaidi ya sigareti trilioni tano kila mwaka!

Kwa nini watu wengi sana huendelea na zoea hili lenye kufisha? Ikiwa wewe ni mvutaji-sigareti, unaweza kuachaje zoea hilo? Maswali haya yatajibiwa katika makala zinazofuata.