Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vipi Juu ya Kutoboa Mwili?

Vipi Juu ya Kutoboa Mwili?

Vijana Huuliza . . .

Vipi Juu ya Kutoboa Mwili?

‘Mara ya kwanza nilipoona watu waliotoboa midomo na sehemu nyingine za mwili, nilidhani “Loo! Ni jambo la pekee.”’—Lisa.

LISA hayuko peke yake. Idadi inayoongezeka ya vijana wanavaa vipuli na hazama katika sehemu mbalimbali za mwili wao, hata katika nyusi zao, kwenye ulimi, midomoni, na kitovuni. Zoea hilo linaitwa kutoboa mwili. *

Heather mwenye umri wa miaka 16 anataka sana kutoboa mwili. Anaamini kwamba kipuli kilicho kitovuni “kitavutia sana.” Hata hivyo, Joe mwenye umri wa miaka 19, tayari ametia kipuli cha dhahabu kwenye ulimi wake. Na msichana mwingine mchanga aliamua kutoboa nyusi zake kwa sababu alitaka mtindo “wenye kutokeza sana” ambao “ungewashangaza watu.”

Wazo la kutia vito mwilini si jambo geni. Hapo awali katika nyakati za Biblia, mwanamke mcha-Mungu aitwaye Rebeka alivalia hazama puani mwake. (Mwanzo 24:22, 47) Waisraeli walipotoka Misri walivalia pete masikioni. (Kutoka 32:2) Hata hivyo, haijulikani iwapo vito hivyo vilishikizwa tu au viliwekwa kwa kutoboa masikio na pua. Hata hivyo, watumwa waaminifu walitobolewa masikio ikiwa ishara ya uaminifu wao kwa mabwana-wakubwa wao. (Kutoka 21:6) Kutoboa mwili kulipendwa sana katika tamaduni nyingine za kale pia. Waazteki na Wamaya walitoboa ndimi zao kwa sababu za kiroho. Kutoboa mdomo kumeenea sana katika Afrika na miongoni mwa Wahindi wa Amerika Kusini. Kutia mapambo puani ni jambo la kawaida miongoni mwa Wamelanesia na wakazi wa India na Pakistan.

Hadi miaka ya majuzi, kwa kawaida wanawake katika nchi za Magharibi walitoboa ndewe za masikio yao pekee. Lakini sasa vijana chipukizi na watu wazima wanaume kwa wanawake wanavalia vito karibu kila sehemu ya mwili.

Sababu Inayofanya Watobolewe

Wengi hutobolewa kwa sababu wanahisi kwamba ni jambo la kimtindo—la kisasa. Wengine hufikiri kwamba kutoboa kutaboresha sura yao. Kwa kweli, mtindo huu umesambazwa na wanamitindo mashuhuri, wachezaji hodari, na wanamuziki maarufu. Vijana wengine hufikiri kwamba kutoboa mwili huonyesha pia kwamba wako huru, wanataka kujitegemea, ni njia ya kuonyesha kwamba wao ni tofauti na kila mtu. Mwandikaji-habari John Leo asema: “Nia kuu ya kutoboa mwili mara nyingi yaonekana ni tamaa ya kuwaudhi wazazi na kushangaza watu wa kawaida.” Kutoridhika, kutoridhiana, ufidhuli, na uasi yaonekana kuwa unasababisha hali hii ya kujionyesha.

Hata kuna wale wanaotobolewa ili watimize mahitaji ya moyoni ya kisaikolojia au ya kihisia. Kwa mfano, vijana wengine hudhani kwamba kutazidisha kujistahi. Wahasiriwa wengine waliotendwa vibaya wakiwa watoto wameona kutobolewa mwili kuwa njia ya kuonyesha wanadhibiti miili yao.

Hatari za Kiafya

Lakini je, kutoboa mwili kwa njia yoyote ni salama? Wanatiba wengi wanasema kwamba njia nyingine si salama. Kwa kweli, kujitoboa mwili ni hatari sana. Na kuwaendea wale wanaoitwa eti wataalamu wa kutoboa mwili kwaweza kuwa na hatari zake. Wengi hawajazoezwa vya kutosha, kwa kuwa walijifunza kazi hiyo kutoka kwa marafiki, magazeti, au vidio. Tokeo ni kwamba huenda wakakosa kutumia mbinu zinazozingatia usafi wa kiafya au hata wakawa hawaelewi hatari za kutoboa mwili. Isitoshe, watu wengi wanaotoboa mwili hawaelewi mwili na viungo vyake. Hili ni jambo zito sana, kwa kuwa kutoboa shimo mahali pasipofaa kwaweza kusababisha kuvuja damu nyingi. Kutoboa neva kwaweza kuleta madhara ya kudumu.

Hatari nyingine kubwa ni maambukizo. Vifaa vyenye vijidudu vyaweza kueneza maradhi hatari kama vile mchochota wa ini, UKIMWI, kifua-kikuu, na pepo-punda. Uangalifu wahitajiwa hata baada ya kutumia mbinu za kufisha vijidudu. Kwa mfano, kutoboa kitovu huelekea kuumiza kwa sababu husuguliwa kila mara na mavazi. Chaweza kuchukua muda wa miezi tisa hivi kupona.

Madaktari wanasema kwamba kutoboa tishu za pua au sikio ni hatari zaidi kuliko kutoboa ndewe. Kijarida kilichoandikwa na shirika la American Academy of Facial Plastic and Reconstructive Surgery chaeleza hivi: “Kutoboa mashimo mengi ya vipuli hasa juu ya sikio kunatia hofu—maambukizo mabaya yaweza kusababisha kupoteza sehemu yote ya juu ya sikio. Hazama za puani ni hatari pia—kuambukizwa kwa pua kwaweza kuathiri mishipa ya damu ya karibu na kusambaa kwenye ubongo.” Kijarida hicho chamalizia hivi: “Kwa wazi, ni ndewe tu zinazopasa [kutobolewa].”

Hatari nyingine ni makovu mabaya na maitikio ya mizio kwa vito vyenye kudunga. Endapo vipuli vilivyo katika sehemu nyeti, kama vile matiti, vinashikwa au kuvutwa na mavazi, mashimo yaliyotobolewa yaweza kupasuka kwa urahisi. Kovu kwenye tishu za matiti ya msichana mdogo laweza kuziba vifereji vya maziwa, na asipotibiwa, huenda akashindwa kumnyonyesha mtoto wakati ujao.

Hivi karibuni, Shirika la American Dental Association lilisema kwamba kutoboa mdomo ni zoea hatari kwa afya ya umma. Hatari zaidi za kutoboa mdomo zatia ndani kusongwa na vito baada ya kuvimeza, ulimi kufa ganzi na kutoonja ladha, kuvuja damu mfululizo, meno yaliyomeguka au kuvunjika, mate mengi mdomoni, kumwaga mate ovyoovyo, jeraha kwenye fizi, tatizo la kuongea, kupumua, kutafuna na kumeza. Mwanamke kijana aitwaye Kendra alipotobolewa ulimi, “ulivimba kama kibofu.” Jambo baya hata zaidi ni kwamba mtoboaji alitumia hazama ya kidevu, nayo ikapasua ulimi na kurarua tishu ndani ya ulimi wa Kendra. Nusura apoteze kabisa uwezo wa kuongea.

Mungu aliwafundisha watu wake Waisraeli kustahi na kuepuka kuumiza miili yao. (Mambo ya Walawi 19:28; 21:5; Kumbukumbu la Torati 14:1) Na ingawa Wakristo leo hawako chini ya Sheria ya Musa, bado wanatiwa moyo wastahi miili yao. (Waroma 12:1) Hivyo basi, je, haipatani na akili kuepuka hatari za kiafya zisizo za lazima? Hata hivyo, kuna mambo mengine upaswayo kufikiria mbali na afya.

Kutoboa Mwili Kunatoa Wazo Gani?

Biblia haitoi amri yoyote hususa kuhusu kutoboa mwili. Lakini hututia moyo tujirembe kwa “kiasi na utimamu wa akili.” (1 Timotheo 2:9) Ingawa jambo fulani laweza kuonwa kuwa la kiasi katika sehemu fulani ya ulimwengu, suala muhimu ni jinsi ambavyo linaonwa unapoishi. Kwa mfano, zoea la wanawake kutoboa ndewe laweza kukubalika katika sehemu moja ya ulimwengu. Lakini katika nchi au tamaduni nyingine, jambo hilo laweza kuwachukiza baadhi ya watu.

Licha ya kupendwa na watu mashuhuri, zoea la kutoboa mwili na la wanaume kuvaa vipuli halikubaliwi kwa kawaida katika nchi za Magharibi. Sababu moja yaweza kuwa kwamba hayo yamekuwa mazoea ya wafungwa hasa, magenge yanayotumia pikipiki, waimbaji wa roki, wagoni-jinsia-moja na watu wakatili. Kwa wengi, kutoboa mwili hudokeza ufidhuli na uasi. Baadhi ya watu huliona kuwa zoea lenye kushangaza na kuchukiza. Msichana Mkristo aitwaye Ashley asema hivi: “Kijana mmoja katika darasa letu ametoboa pua yake. Yeye anadhani inapendeza. Mimi nafikiri ni jambo lenye kuchukiza sana!”

Hivyo, si ajabu kwamba duka moja maarufu la Marekani lina sheria ya kwamba wafanyakazi wanaoshughulika moja kwa moja na wateja wanaruhusiwa kuvaa kipuli kimoja tu katika kila sikio na kwamba kutoboa sehemu nyingine zilizo wazi kumepigwa marufuku. “Hujui jinsi ambavyo wateja wataitikia,” aeleza msemaji mmoja mwanamke wa kampuni hiyo. Vivyo hivyo, washauri wa kazi-maisha huwashauri wanafunzi wanaume wa vyuo wanaotafuta kazi wasivae “vipuli au vito vingine mwilini; wanawake hawapaswi kuvaa . . . hazama puani.”

Vijana Wakristo hasa wapaswa kuhangaikia wazo la kuonwa ifaavyo na wengine, hata wanaposhiriki kazi ya kueneza-evanjeli. Hawataki ‘kuwa sababu ya kukwaza katika njia yoyote, ili huduma yao isitafutiwe kosa.’ (2 Wakorintho 6:3, 4) Bila kujali maoni yako binafsi juu ya kutoboa mwili, sura yako inafunua mengi kuhusu mitazamo na mtindo wako wa maisha. Je, ungependa watu wawe na maoni gani kukuhusu?

Hatimaye, wewe—na bila shaka, wazazi wako, lazima mwamue mtakachofanya kuhusu jambo hilo. “Usiruhusu ulimwengu unaokuzunguka ukufinyange kulingana na mtindo wake,” ndilo shauri linalofaa la Biblia. (Waroma 12:2, Phillips) Kwa vyovyote vile, matokeo yataathiri maisha yako.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Haturejezei kutoboa kuliko kwa kawaida katika nchi nyingi. Badala yake, twarejezea mazoea yenye kupita kiasi yanayopendwa leo.—Ona Mnara wa Mlinzi, Mei 15, 1974, ukurasa wa 318-319, Kiingereza.)

[Picha katika ukurasa wa 12]

Vijana wengi wanapenda sana kutoboa mwili