Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Maadili Ni Mabaya Zaidi Kuliko Awali?

Je, Maadili Ni Mabaya Zaidi Kuliko Awali?

Je, Maadili Ni Mabaya Zaidi Kuliko Awali?

IKIWA ungewauliza wanahistoria, “Je, maadili ya watu leo ni bora au ni mabaya zaidi kuliko awali?” huenda wengine wakajibu kwamba ni vigumu kulinganisha maadili ya vipindi tofauti-tofauti. Huenda wakawa na maoni kwamba kila kizazi chapasa kuonwa kulingana na jinsi kilivyo.

Kwa mfano, fikiria kutokea kwa uhalifu wenye jeuri katika Ulaya tangu karne ya 16. Miaka 400 iliyopita visa vya uuaji-kimakusudi vilikuwa jambo la kawaida. Mara nyingi watu walichukua sheria mikononi, na uhasama kati ya watu wa ukoo ulikuwa jambo la kawaida.

Hata hivyo, wanahistoria Arne Jarrick na Johan Söderberg waandika katika kitabu Människovärdet och makten (Adhama na Uwezo wa Binadamu) kwamba kipindi cha kati ya mwaka wa 1600 na wa 1850 “kilitofautishwa kwa ustaarabu wa kweli katika maisha ya jamii” katika sehemu fulani. Watu walikuwa bora kwa kuzingatia mahitaji ya wengine—walikuwa wenye hisia-mwenzi zaidi. Kwa mfano, wanahistoria wengine wanasema kwamba wivi na uhalifu dhidi ya mali haukuwa wa kawaida sana katika karne ya 16 kama leo. Magenge ya wezi yaliyopangwa yalikuwa nadra, hasa miongoni mwa watu wa mashambani.

Bila shaka, utumwa ulikuwa umeanzishwa na ulitokeza uhalifu mbaya zaidi katika historia—kutekwa nyara kwa Waafrika na wafanya-biashara wa Ulaya na kutendwa kinyama kwa mamilioni ya watumwa hao wakiwa katika nchi walizopelekwa.

Hivyo, tukumbukapo karne zilizopita, kwa kuchunguza historia, huenda tukaona kwamba hali nyingine zilikuwa bora, ilhali nyingine zilikuwa mbaya zaidi. Hata hivyo, jambo fulani tofauti kabisa na baya sana—kwa kweli lisilo na kifani—lilitukia katika karne ya 20 na lingali linatukia.

Karne ya 20—Wakati wa Badiliko

Wanahistoria Jarrick na Söderberg wasema: “Katika miaka ya 1930 visa vya uuaji-kimakusudi na uuaji wa binadamu viliongezeka tena, na, kwa kusikitisha, tangu wakati huo mwelekeo huu umeendelea kwa zaidi ya nusu karne.”

Kulingana na watoaji-maoni wengi, maadili yalizorota sana katika karne ya 20. Insha moja inayohusu falsafa za maadili yasema hivi: “Mtu aweza kuona waziwazi kwamba maoni ya jamii kuhusu ngono na mambo yanayokubalika kiadili yamebadilika sana katika miaka 30 hadi 40 iliyopita—zamani jamii ilionyesha waziwazi mambo yanayofaa kiadili, kupitia sheria kali, siku hizi kuna maoni ya kibinafsi na ya uhuru.”

Hii yamaanisha kwamba mwenendo wa kingono na mambo mengine yahusuyo maadili ni mambo ambayo watu wengi sasa huhisi kwamba wanaweza kujiamulia. Kwa kielelezo, insha hiyo yataja takwimu zinazoonyesha kwamba katika mwaka wa 1960 ni asilimia 5.3 tu ya watoto wote Marekani waliozaliwa nje ya ndoa. Katika mwaka wa 1990 tarakimu hiyo ilikuwa asilimia 28.

Katika mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha Notre Dame, Seneta wa Marekani Joe Lieberman alifafanua maadili ya wakati wetu kuwa “kipindi kisicho na kanuni zozote, . . . ambapo mawazo ya kidesturi ya linalofaa na lisilofaa yamepuuzwa hatua kwa hatua.” Kulingana na Lieberman, “hali hiyo imekuwako kwa vizazi viwili.”

Kupuuza Dini

Wanahistoria na wachanganuzi wengine hutoa sababu gani kwa tukio hili kubwa sana katika karne ya 20? “Mojawapo ya mabadiliko ya maana zaidi katika jamii katika karne mbili zilizopita ni kupuuza dini,” chasema kitabu Människovärdet och makten. Kupuuza dini kulimaanisha kwamba “watu wangepewa fursa ya kuchukua msimamo wa maoni tofauti-tofauti kwa kujitegemea. Wazo hilo . . . lilitokana na wanafalsafa wa karne ya 18 wa chama cha Enlightenment, waliokuwa wa kwanza . . . kukataa Biblia kuwa chanzo pekee cha kweli.” Hivyo, dini, hasa zile za Jumuiya ya Wakristo, hazitegemewi kuandaa mwongozo wa kiadili kama zilivyotegemewa sana zamani.

Lakini ni kwa nini falsafa iliyoanzishwa karne ya 18 ilichukua zaidi ya miaka 200 ili kupendwa? “Mawazo hayo hayakuenezwa kwa urahisi kwa umma,” chasema kitabu kilichotajwa juu. “Harakati ya kupuuza dini ilikuwa ya polepole.”

Hata ikiwa mwelekeo wa kuacha viwango vya kiadili vya zamani na kanuni za Kikristo ulichukua muda katika kipindi kirefu cha miaka 200 iliyopita, uliongezeka sana katika karne ya 20. Imekuwa hivyo hasa katika miongo michache iliyopita. Kwa nini iwe hivyo?

Ubinafsi na Pupa

Jambo kuu linalochangia ni maendeleo ya haraka ya kitekinolojia na kiuchumi katika jamii mnamo karne ya 20. Makala moja katika gazeti la Kijerumani Die Zeit yalisema kwamba tunaishi katika “kipindi maalumu cha mabadiliko na si kama ilivyokuwa katika karne zilizopita, katika ulimwengu uliokuwa tuli.” Makala hayo yalieleza kwamba hiyo imeongoza kwenye mfumo wa soko huru, unaotegemea mashindano na kuchochewa na ubinafsi.

Makala hiyo iliendelea kusema “ubinafsi huu, hauwezi kukomeshwa na chochote. Tokeo limekuwa kuongezeka kwa unyama unaotendeka kila siku, na vilevile ufisadi, ambao katika nchi nyingi umehusisha hata serikali. Watu hujifikiria wenyewe na kutosheleza tamaa zao kwa kiwango kikubwa zaidi.”

Mwanasosholojia Robert Wuthnow, wa Chuo Kikuu cha Princeton, kupitia kura ya maoni aliyofanya kikamili alipata kwamba leo Wamarekani huhangaikia pesa zaidi kuliko walivyofanya kizazi kimoja kilichopita. Kulingana na uchunguzi huo “Wamarekani wengi huhofu kwamba tamaa ya pesa imetangulizwa kuliko maadili mengine kama vile watu kustahiana, ufuatiaji wa haki kazini na kushiriki katika jumuiya zao.”

Pupa katika jamii imeongezeka zaidi kwa sababu wasimamizi wengi wa biashara wamejiongezea mishahara mikubwa na marupurupu mengi ya kustaafu huku wakiwahimiza wafanyakazi wao wadai mishahara ya kiasi. “Tatizo linalohusu ufuatiaji wa faida miongoni mwa wasimamizi wa biashara ni kwamba mtazamo wao huathiri wengine na kupunguza kiwango cha maadili miongoni mwa watu kwa ujumla,” asema Kjell Ove Nilsson, profesa mwandamizi wa maadili na mkurugenzi wa theolojia kwenye Baraza la Kikristo la Sweden. “Bila shaka, jambo hili huathiri sana maadili—katika jamii na vilevile ya mtu mmoja-mmoja.”

Utamaduni wa Vyombo vya Habari

Jambo jingine kuu linalochangia kuzorota haraka kwa maadili mwishoni mwa karne ya 20 ni utamaduni wa vyombo vya habari. “Vyombo vipya vya kusambaza maadili ni watayarishaji wa vipindi vya televisheni, watu mashuhuri katika sinema, watangazaji-mitindo, waimbaji wa rapu ya magenge ya mitaani, na wengine wengi katika utamaduni tata wa vyombo vya habari vya elektroni,” asema Seneta Lieberman. “Watu hao wanaoanzisha mitindo huathiri sana utamaduni wetu na watoto wetu hasa, na mara nyingi hawakubali kulaumiwa kwa kueneza maadili yenye kudhuru.”

Kwa mfano, Lieberman ataja wimbo uliotungwa na bendi ya muziki wenye mdundo mzito iliyoitwa Cannibal Corpse. Waimbaji wafafanua kwa undani kubakwa kwa mwanamke mmoja huku akiwa ameelekezewa kisu. Yeye pamoja na mfanyakazi mwenzi waliomba kampuni ya kurekodi iondoe rekodi hiyo. Lakini kama asimuliavyo Lieberman, hawakufanikiwa.

Kwa hiyo, leo wazazi wanaochukua madaraka kwa uzito wanapambana vikali na utamaduni wa vyombo vya habari ili kubainisha ni nani atakayelea watoto wao na kuwa na uvutano juu yao. Lakini vipi juu ya familia ambazo wazazi si waangalifu? “Katika visa hivyo,” asema Lieberman, “utamaduni huo haupingwi bali huonwa kuwa kiwango, na uwezo wa mtoto wa kutofautisha mema na mabaya na mambo anayotanguliza maishani huathiriwa hasa na kile anachojifunza kwenye televisheni, sinema, na redio yenye CD.” Na hivi karibuni zaidi, twaweza kuongezea Internet kwenye orodha hiyo.

Kurudia “Maadili ya Enzi ya Vyombo vya Mawe”

Athari za mavutano hayo yasiyofaa zinaonekanaje miongoni mwa vijana? Kwanza, katika miaka ya karibuni watoto na matineja wengi zaidi wamefanya vitendo vikatili vya jeuri dhidi ya watoto wengine na vilevile dhidi ya watu wazima.

Kisa chenye kushtua kilitukia huko Sweden mwaka wa 1998. Wavulana wawili, wenye umri wa miaka mitano na saba, walimkaba koo mwenzao mwenye umri wa miaka minne waliyekuwa wakicheza naye hadi akafa! Wengi walijiuliza swali hili: Je, watoto hawana uwezo wa kujizuia kabla ya kufanya jambo linalopita kiasi? Daktari wa magonjwa ya akili ya watoto alitoa maelezo haya yenye uzito: “Kujizuia kufanya jambo linalopita kiasi, ni jambo ambalo lazima watu wajifunze,” alisema. “Kungehusu . . . vielelezo ambavyo watoto huona na kile wanachojifunza kutoka kwa watu wazima walio karibu nao.”

Tukio linalofanana na hilo laweza kuonwa miongoni mwa wahalifu wenye jeuri. Kulingana na Sten Levander, profesa wa magonjwa ya akili katika Sweden, kati ya asilimia 15 hadi 20 ya wafungwa wote leo ni wagonjwa wa akili—watu ambao wanajifikiria sana, wasio na hisia-mwenzi, na wasioweza au wasiotaka kuelewa dhana ya jema na baya. Hata miongoni mwa watoto na vijana wanaoonekana kuwa wa kawaida, watazamaji wameona maadili yakipuuzwa. “Tumerudia maadili ya Enzi ya Vyombo vya Mawe,” adai Christina Hoff Sommers, profesa wa falsafa. Alisema kwamba wanafunzi wake wachanga wanapokabili suala lihusulo jambo linalofaa na lisilofaa, wengi wao hawajihisi salama kabisa. Kisha hujibu kwamba hakuna kitu kama jambo linalofaa au lisilofaa. Wanaamini kwamba kila mtu apaswa kufikiria kile kinachomfaa.

Katika nyakati za karibuni, wengi wa wanafunzi wake wamepinga kanuni ya adhama ya pekee na thamani ya uhai wa kibinadamu. Kwa mfano, walipoulizwa wangefanya nini ikiwa wangekabili uamuzi kati ya kuokoa uhai wa mnyama kipenzi wao au uhai wa mwanadamu mwenzao wasiyemjua, wengi walisema wangechagua mnyama huyo.

“Tatizo si kwamba vijana hawana ujuzi, hawaaminiki, ni wakatili, au ni wahaini,” asema Profesa Sommers. “Kusema waziwazi, hawajui jema na baya.” Adai kwamba vijana wengi leo kwa kweli hutilia shaka kama kuna jema au baya, anaona kwamba mtazamo huo hutokeza mojawapo ya tisho kubwa zaidi kwa jamii.

Kwa hiyo, kupuuza maadili katika nyakati zetu ni jambo halisi. Wengi huhofu kwamba kungeweza kuwa na matokeo hatari. Makala katika gazeti la Die Zeit lililorejezewa mapema yasema kwamba uchumi wa soko huru la leo ungeweza ‘kudhoofika hatua kwa hatua na labda siku fulani kuporomoka kama ilivyotukia kwa mfumo wa kisoshalisti hivi karibuni.’

Kwa kweli haya yote yanamaanisha nini? Na twapaswa kutazamia wakati ujao wa namna gani?

[Picha katika ukurasa wa 6, 7]

“Vyombo vipya vya kusambaza maadili ni watayarishaji wa vipindi vya televisheni, watu mashuhuri katika sinema, watangazaji-mitindo, waimbaji wa rapu ya magenge ya mitaani . . .”