Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Michezo Inayokufanya Mhusika-Mkuu Hivi majuzi nilipokea kompyuta mpya. Nilikusudia kucheza michezo michache tu lakini mwishowe nikacheza mfululizo kwa muda wa saa 16 hivi! Nilipogundua kilichotokea, nilifuta mara moja michezo yote katika kompyuta yangu. Ingawa hivyo, baadaye nilianza kufikiria kwamba labda nilikuwa nimepita kiasi kidogo. Lakini juma hilohilo, ikaja makala yenu “Vijana Huuliza . . . Je, Kuna Hatari Yoyote Katika Michezo Inayokufanya Uwe Mhusika-Mkuu?” (Agosti 22, 1999) Nilitambua madhara ambayo michezo hiyo ilikuwa ikiniletea. Namshukuru Yehova kwa kunitahadharisha kuhusu hatari hiyo.

L. H., Brazili

Kuna mchezo wa kadi ambao umependwa sana Japani. Nyingi za kadi hizo zina majina ya kishetani, kwa mfano, “Pazia ya Ibilisi Mweusi.” Nilicheza sana mchezo huo hivi kwamba hali yangu ya kiroho ikawa mbaya. Mwishowe mama yangu alipata kadi zangu na kuzitupa. Bado nilizipenda sana kadi hizo. Lakini baada ya kusoma makala hiyo, nilikoma kuzipenda. Makala hiyo ilinisaidia sana.

K. N., Japani

Tiba Bila Damu Nina umri wa miaka 11, na makala “Je, Kweli Ni Lazima Kutiwa Damu Mishipani?” ilikuwa ya pekee kwangu. (Agosti 22, 1999) Dada yangu alifanyiwa upasuaji wa moyo mara mbili. Wazazi wangu waliomba ufanywe bila damu. Nilifikiri kwamba angekufa, lakini miaka mitatu imepita sasa naye ni mzima!

C. S., Marekani

Farasi Asiye Sawa! Nilifurahia sana ile makala “Soko Linalofanywa Oktoba—‘Soko la Farasi la Kimataifa la Kale Zaidi Katika Ulaya.’” (Machi 22, 1999) Lakini nilishangaa kuona kwamba picha ya farasi aina ya skewbald akiitwa “farasi mfupi mnene mwenye rangi mbalimbali.”

S. P., Afrika Kusini

Msomaji wetu awajua farasi kwelikweli! Kulingana na British Skewbald and Piebald Association, farasi mfupi mnene mwenye rangi mbalimbali ana alama nyeusi na nyeupe tu—tofauti na “skewbald” aliyeonyeshwa kwenye picha yetu. Twaomba radhi kwa kosa hilo.—Mhariri.

Chembe za Urithi Nina umri wa miaka 16, nami napendezwa sana na biolojia ya molekuli. Ule mfululizo wa “Kufumbua Fumbo la Chembe Zako za Urithi” (Septemba 8, 1999) ulieleza mambo kwa njia barabara isiyo sahili sana wala ngumu sana. Nilisoma kitabu ambacho kilieleza fumbo la DNA kwa kina sana. Nilishangaa sana kwamba makala yenu iliongea juu ya habari hiyo yote lakini kwa uelewevu zaidi na kwa maneno rahisi.

S. R., Ufaransa

Kwa sababu ya makala hizo, niliweza kupata maksi za juu katika mtihani wangu wa biolojia. Ufafanuzi wenu wa jinsi nucleic acids zinavyohusiana na tabia za urithi ulikuwa sahili sana na kamili!

D.A.N., Brazili

Mimi ni mwalimu wa shule ya msingi, na sikuzote nimeshangaa jinsi ambavyo ningeweza kusaidia wanafunzi wangu waelewe muundo wa mwili wa binadamu. Niliona habari katika makala hizo kuwa sahili vya kutosha kwa wanafunzi wangu kuelewa, hata ingawa ilikuwa na maneno kadhaa magumu ya kisayansi. Amkeni! iliyafanya yaeleweke.

K. M., Lesotho

Hofu ya Kusafiri Angani Asanteni! Nitasafiri Jumatatu kwa ndege mara ya kwanza, nami nina wasiwasi sana. Nafikiri sababu ni kwamba siwezi kuwazia jinsi mashine kubwa mno hivyo inavyoweza kwenda kinyume cha nguvu za uvutano. Kwa hiyo nilifurahi kuona ile makala “Ni Nini Kinachohusika Ili Ziendelee Kusafiri Angani?” (Septemba 8, 1999) Kujua kwamba mashirika ya ndege hukagua na kuhakikisha kwamba ndege ziko salama—hata kuzifanyia eksirei—kumenisaidia kutokuwa na wasiwasi zaidi kuhusu kusafiri angani. Kwa hiyo, licha ya woga wangu, nitabeba makala hiyo nami nitapanda ndege hiyo!

T. T., Marekani