Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Watoto Wadogo na Televisheni

Chuo cha Marekani cha Maradhi ya Watoto chapendekeza kwamba watoto walio na umri unaopungua miaka miwili wasitazame televisheni, laripoti gazeti la The Toronto Star. Utafiti unaohusu ukuzi wa mapema wa ubongo waonyesha kwamba vitoto vichanga na watoto wadogo wanahitaji kuwasiliana moja kwa moja na wazazi na watunzaji wengine. Huenda kutazama televisheni “kukaathiri utendeano unaosaidia kukuza stadi zao za kijamii, kihisia-moyo na ufahamu.” Hata hivyo wataalamu wote hawakubaliani kuhusu suala hili. Kwa mfano, Chama cha Maradhi ya Watoto cha Kanada chasema kwamba kutazama vipindi bora chini ya uangalizi wa mzazi kwa muda usiozidi dakika 30 kwa siku humpa mtoto “fursa ya kufundishwa na mzazi.” Hata hivyo, mashirika yote mawili yanakubaliana kwamba watoto wachanga hawapaswi kuwa na televisheni au kompyuta kwenye vyumba vyao vya kulala na kwamba televisheni haipasi kutumiwa kuwa yaya wa muda. Kwa kuwa kutazama televisheni kwaweza kuathiri afya ya vijana, inapendekezwa kwamba “watoto watiwe moyo kucheza nje, kusoma vitabu au kujihusisha na fumbo la maneno au michezo.”

Kufadhaika Kazini

Kwa nini watu fulani hupandwa na hamaki au hata kuwa wenye jeuri kazini? Kulingana na mwanasaikolojia wa Toronto, Sam Klarreich, huenda sababu isiwe mkazo tu bali kufadhaika kwa kiasi fulani. Aamini hali hii huwapata wafanyakazi fulani wanaoona kwamba “wanaombwa wafanye kazi kupita kiasi halafu wanagundua kuwa mshahara haulingani na kazi waliyofanya,” laripoti gazeti la Globe and Mail. Klarreich aonya kwamba hasira ya muda mrefu “ni hisia-moyo yenye kudhuru sana afya” inayoweza kusababisha kupooza kwa ubongo au mshiko wa moyo. Anawatia moyo waajiriwa wajifunze kukubali mfadhaiko na kuketi na kuzungumza kwa utulivu pamoja na waajiri wao kuhusu kiasi cha kazi wanayoweza kufanya. Kwa upande mwingine, Klarreich awashauri waajiri wawe macho kuelekea waajiriwa wanaoonekana kuwa wamechoka kabisa na kuwapa msaada wa ziada, kuwapunguzia kazi, au kupendekeza kwamba wachukue likizo ya siku moja.

Kuimba Huuburudisha Moyo

Wanasayansi wamejifunza kwamba kuimba hutokeza kemikali katika ubongo ambazo hukufanya ustarehe na ufurahi, laripoti gazeti la Ujerumani la Stuttgarter Nachrichten. Watafiti wasema kwamba kuimba hufanya “molekuli za hisia-moyo” katika ubongo zisonge huku na huku. Hivyo, “inasemekana kwamba kuimba hakudhihirishi tu hisia-moyo bali pia huchochea hisia-moyo,” yasema ripoti hiyo. Walimu wa muziki wasema kuwa leo watu wengi huhisi kwamba kuimba ni “jambo la kikale” au kwamba sauti zao si nzuri, kwa hiyo wanasikiliza muziki na nyimbo kwenye vyombo vya habari. Hata hivyo, utafiti huo waonyesha kwamba watu hunufaika wanapoimba wenyewe.

Wizi wa Mazao

Katika majimbo kadhaa ya Ujerumani, wakulima wanalalamika kuhusu ongezeko la wizi wa mazao, laripoti gazeti la Siegener Zeitung. Wezi huiba ndoo zilizojaa matango na kujaza rundo la asparaga (aina fulani ya mboga) kwenye magari madogo ya kubebea mizigo. Katika kisa kimoja waliiba mimea 7,000 ya zabibubua. Ijapokuwa huenda watu fulani wakaiba chakula kwa sababu ya kuzorota kwa hali ya uchumi, wengine wanaliona kuwa zoea. Wakulima wanaripoti kwamba waliona “magari ya kila aina” karibu na mashamba yaliyoibiwa. Mara nyingi mashamba yanakuwa mbali na nyumba za wamiliki, na kwenye mashamba hayo wezi huwa wajasiri hata zaidi. Mshauri mmoja alipendekeza wakulima wafunike mazao yao na mbolea ili kuwavunja moyo wezi.

Wanaojihusisha na Utendaji wa Jamii Huenda Wakaishi Muda Mrefu Zaidi

Kwa mujibu wa uchunguzi mpya uliofanywa na Chuo Kikuu cha Harvard, wazee-wazee wanaojihusisha na utendaji wa jamii, kama vile kwenda kanisani, mikahawani, michezoni, na kwenye sinema, kwa wastani huishi miaka miwili na nusu zaidi ya wale wasiofanya chochote. Imedhaniwa kwa muda mrefu kwamba utendaji huo wa kimwili ulisaidia watu, akasema Thomas Glass wa Harvard, aliyeongoza uchunguzi huo. Hata hivyo, aliongezea kwamba uchunguzi huo waandaa “labda ushahidi mkubwa zaidi usiothibitishwa tulio nao kufikia sasa kwamba kuwa na kusudi uzeeni hurefusha maisha.” Glass alisema kwamba kufanya mengi zaidi, bila kujali utendaji, kulirefusha maisha karibu katika kila kisa.

Mivunjiko-Meli ya Kale Zaidi Ulimwenguni

Wanaelimu wa baharini wamegundua mabaki ya meli mbili za Foinike za mwaka wa 750 K.W.K. hivi, laripoti gazeti la Kifaransa la Sciences et avenir. Mashua hizo za meta 15 na 18, zilizo kando ya pwani ya Israel kwenye kina cha meta 500, ndizo meli za kale zaidi kuwahi kupatikana baharini. Mashua hizo zilianza safari kutoka bandari ya Tiro zikiwa zimebeba gudulia la udongo lenye divai, labda zikielekea Misri au kwenye jiji la Carthage huko Afrika Kaskazini. Kama ilivyonukuliwa kwenye kichapo cha International Herald Tribune, mgunduzi wa meli hizo, Robert Ballard, alisema: “Vina virefu vilivyoko baharini, kukosekana kwa nuru ya jua, kanieneo kubwa, huhifadhi vyombo vya kihistoria kwa muda mrefu zaidi ya vile tulivyofikiri.” Watafiti walisema kwamba ugunduzi huo “ungeweza kusaidia kufungua somo jipya kabisa katika utafiti wa utamaduni huu wa kale wa baharini.”

Chaguo la Kwanza la Kujiburudisha

Katika uchunguzi wa hivi majuzi, watu 1,000 kutoka nchi 30 waliulizwa ni utendaji gani waliopendelea ili kupunguza au kuondoa mkazo. Ulimwenguni pote, asilimia 56 ya waliohojiwa walisema kwamba chaguo lao la kwanza ni muziki, laripoti shirika la habari la Reuters. Katika Amerika Kaskazini, asilimia 64 waliupa muziki nafasi ya kwanza, kwa kulinganishwa na asilimia 46 katika nchi zilizositawi za Asia. Kwa ujumla, kutazama televisheni kulichukua nafasi ya pili, kukafuatiwa na kuoga. “Unapofikiria gharama na kupatikana kwa muziki kupitia redio, televisheni, redio za CD, Internet na njia nyingine mpya nyingi,” akasema Tom Miller, mkurugenzi wa uchunguzi uliofanywa na shirika la Roper Starch Worldwide, “haishangazi kwamba zaidi ya nusu ya watu ulimwenguni husikiliza muziki ili kujiburudisha.”

Umaskini—Tatizo la Ulimwenguni Pote

Msimamizi wa Benki ya Dunia James D. Wolfensohn, hivi majuzi alieleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa umaskini ulimwenguni. Wolfensohn alisema kwamba thuluthi ya watu bilioni sita ulimwenguni wangali wanaishi katika ufukara, laripoti gazeti la Mexico City la La Jornada. Aliongezea kwamba nusu ya wakazi wa dunia hujikimu kwa dola mbili hivi kwa siku; na watu bilioni moja, kwa dola moja hivi. Ijapokuwa anajivunia maendeleo yaliyofanywa na Benki ya Dunia kupigana na umaskini, Wolfensohn alitoa tarakimu zilizoonyesha kwamba tatizo hilo limeenea pote na halijakaribia kutatuliwa. Alisema hivi: “Lazima tutambue kwamba umaskini ni tatizo la ulimwenguni pote.”

Ukiwa na Shaka, Itupe

Kuvu fulani, kama zile zilizoko kwenye jibini ya buluu, ni salama kula. Lakini nyingine zaweza kuwa hatari hasa kwa watu walio na afya dhaifu, chaonya kijarida cha UC Berkeley Wellness Letter. Kuvu zilizo katika mkate na kwenye nafaka ni miongoni mwa zile zilizo na sumu zaidi. Mara nyingi kuvu zinazoonekana huwa na nyuzinyuzi kama mizizi ambayo hupenya chakula. Isitoshe, sumu inayotokezwa na kuvu haiwezi kuondolewa kwa kupika. Kijarida cha Wellness Letter chapendekeza:

▪ Weka chakula ndani ya friji ikiwezekana, na kitumie kabla kuvu haijakua.

▪ Tupa matunda madogo kama vile zabibu zenye kuvu. Osha tunda unapokuwa tayari tu kulila, kwa kuwa unyevu huchochea kuvu.

▪ Sehemu ndogo zenye kuvu za matunda makubwa na magumu, kutia ndani mboga, kama vile matofaa, viazi, koliflawa, au vitunguu, zaweza kukatwa kwa njia salama. Matunda mororo yenye kuvu, kama vile mapichi na matikiti, yapasa kutupwa.

▪ Jibini ngumu yenye kuvu yaweza kuokolewa kwa sehemu kwa kukata sehemu ya upande wa nje angalau sentimeta tatu hivi kutoka kwenye kuvu. Lakini tupa jibini nyororo na mtindi wenye kuvu, pamoja na mkate, nyama, makombo, kokwa, siagi ya njugu, shira, na vihifadhi vyenye kuvu.

Nyama Choma Iliyo Salama Zaidi

“Sikuzote kumekuwa na hangaiko la usalama wa chakula kuhusu nyama ambayo haijaiva, lakini katika miaka ya majuzi, kupika kupita kiasi—hasa kuchoma na kuunguza nyama, kuku na samaki kwenye jiko la kuchomea nyama katika ua—kunahusianishwa na tisho la afya la muda mrefu zaidi,” lasema gazeti la Kanada la National Post. Nyama inapopikwa kwa moto mwingi, misombo inayosababisha kansa inayoitwa heterocyclic amine (HCAs) hufanyizwa. Ripoti hiyo yapendekeza kwamba kutumia marinadi sahili yenye “kikolezo chenye asidi, kama vile maji ya limau, maji ya machungwa, au siki,” kwaweza kufanya kuchoma nyama kuwe salama zaidi. Katika majaribio mengine mengi, watafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Kansa ya Amerika “walipata kwamba chakula kilichotiwa marinadi kilikuwa na HCA inayopungua asilimia 92 hadi asilimia 99 kuliko vyakula ambavyo havikutiwa marinadi—na hakukuwa na tofauti yoyote iwe vilitiwa marinadi kwa muda wa dakika 40 au siku mbili.”