Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maadili Yakoje Leo?

Maadili Yakoje Leo?

Maadili Yakoje Leo?

Asubuhi moja katika Aprili 1999, hali ya utulivu ilivurugwa katika mji wa Littleton, karibu na Denver, Colorado, Marekani. Vijana wawili waliokuwa wamevalia makoti meusi ya mvua waliingia katika shule moja ya sekondari na kuanza kuwafyatulia risasi wanafunzi na walimu. Pia walilipua mabomu. Wanafunzi 12 na mwalimu mmoja waliuawa, na zaidi ya 20 wakajeruhiwa. Wavamizi hao walijiua hatimaye. Walikuwa na umri wa miaka 17 na 18 peke yake nao walichukia sana vikundi fulani.

KWA kusikitisha, mfano uliotajwa juu ni kisa cha kawaida. Magazeti, redio, na televisheni huripoti matukio kama hayo ulimwenguni pote. Kulingana na Kituo cha Kitaifa cha Takwimu za Elimu, mnamo mwaka wa 1997 kulikuwa na visa vya kijeuri takriban 11,000 vinavyohusisha silaha katika shule za Marekani. Katika Hamburg, Ujerumani, ripoti za vitendo vya kijeuri ziliongezeka kwa asilimia 10 mnamo 1997, na asilimia 44 ya washukiwa walikuwa ni vijana walio na umri unaopungua miaka 21.

Ufisadi miongoni mwa wanasiasa na maofisa wa serikali ni jambo la kawaida. Ripoti moja ya mjumbe wa Muungano wa Ulaya (EU) Anita Gradin katika mwaka wa 1998 ilifunua kwamba gharama ya ufisadi miongoni mwa Muungano wa Ulaya mnamo mwaka wa 1997 ilikadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 1.4. Ulihusisha kila kitu kuanzia kupuuzwa kwa maonyo ya kuegesha hadi kupokea mikopo ya kilimo au pesa nyinginezo za Muungano wa Ulaya kwa njia ya udanganyifu. Kubadili kiasi kikubwa cha fedha haramu na magendo ya silaha na mihadarati kuliruhusiwa, na wafanyakazi wa Muungano wa Ulaya walikuwa wamehongwa na mashirika ya wahalifu ili wanyamaze. Tume nzima ya Muungano wa Ulaya ilijiuzulu mnamo mwaka wa 1999.

Hata hivyo, udanganyifu hauhusishi tu wale wenye cheo cha juu katika jamii. Ripoti moja kutoka Tume ya Muungano wa Ulaya inayohusu wafanyakazi haramu ilifunua kwamba asilimia 16 ya pato kuu la kitaifa la Muungano wa Ulaya hutia ndani mapato yanayotoka kwa biashara ambazo hazijasajiliwa wala kulipiwa kodi. Katika Urusi mapato haramu yanaripotiwa kuwa asilimia 50 ya mapato yote kwa ujumla. Isitoshe, katika Marekani, Shirika Lenye Kibali cha Kuchunguza Upunjaji lilisema kwamba makampuni mengi ya Amerika hupoteza zaidi ya dola bilioni 400 kila mwaka kwa sababu ya wafanyakazi kuyaibia fedha au mali.

Watu wengi wanaovutiwa kingono na watoto wametumia Internet ili kushawishi watoto wajihusishe na vitendo vya ngono haramu. Msemaji wa shirika la Save the Children huko Sweden alisema kwamba kuna hangaiko kubwa kuhusu ponografia ya watoto kwenye Internet. Katika Norway mnamo mwaka wa 1997, shirika hilo lilipokea vidokezi 1,883 kuhusu Website katika Internet zenye ponografia ya watoto. Mwaka uliofuata idadi ya vidokezi hivyo iliongezeka sana kufikia 5,000 hivi. Nyingi ya habari hii hutokezwa katika nchi ambazo serikali au serikali za mitaa haziwezi kudhibiti utendaji huu wenye kudharaulika.

Je, Ilikuwa Afadhali Zamani?

Watu wengi wanaotishwa na hali mbaya ya maadili katika ulimwengu leo, huenda wakakumbuka siku za wazazi au za babu na nyanya zao ambapo kulikuwa na ushirikiano wa jamii. Labda walikuwa wamesikia kwamba watu waliishi maisha ya utulivu wakati huo na kwamba ufuatiaji wa haki na sifa nyingine za kiadili zilithaminiwa na watu wote katika jamii. Watu wenye umri mkubwa zaidi huenda walizungumza kuhusu wakati ambapo watu wenye kufanya kazi kwa bidii walivyosaidiana, vifungo vya familia vilikuwa imara, na vijana walikuwa salama na kusaidia kwenye mashamba na karakana za wazazi wao.

Hilo laongoza kwenye maswali haya: Je, kwa kweli maadili ya watu yalikuwa bora hapo zamani? Au je, kuna hisia tu ya mambo yaliyozoewa ambayo huvuruga kumbukumbu letu la wakati uliopita? Acheni tuone jinsi wanahistoria na wachanganuzi wengine wa kijamii wanavyotoa jibu.

[Sanduku katika ukurasa wa 3]

Maadili Yafasiliwa

Katika makala hizi neno “maadili” linatumiwa kuhusu kanuni za mema na mabaya katika tabia ya binadamu. Hiyo yatia ndani ufuatiaji wa haki, ukweli, na viwango vya juu vya mwenendo wa kingono na mambo mengineyo.