Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sasa Wakiri Kutovumiliana Kidini

Sasa Wakiri Kutovumiliana Kidini

Sasa Wakiri Kutovumiliana Kidini

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA

“MAASKOFU Wasikitikia ‘Uhalifu Mbaya’ wa Malkia Mary,” ndicho kilichokuwa kichwa cha habari cha gazeti la Catholic Herald la Uingereza la Desemba 11, 1998. Maaskofu wa Uingereza na Wales wa Katoliki ya Kiroma walikiri kwamba “uhalifu mbaya ulitendwa kwa jina la dini ya Katoliki, kwa mfano kuelekea Waprotestanti wakati wa Marekebisho Makubwa ya Kidini huko Uingereza.” Malkia Mary alikuwa nani? Alitenda uhalifu gani uliowasukuma maaskofu wakiri? Na kwa nini maaskofu wa Uingereza na Wales wakaamua kutoa taarifa yao wakati huu?

Mary Tudor alizaliwa katika Uingereza ya Kikatoliki mnamo mwaka wa 1516. Akiwa mtoto pekee aliye hai wa Catherine wa Aragon, mke wa kwanza wa Mfalme Henry wa Nane, Mary alilelewa na mamaye akawa Mkatoliki mtendaji. Babaye alitaka mrithi wa kiume, lakini Catherine hakuzaa yeyote. Henry alichukua hatua kwa kuwa papa alikataa kuvunja ndoa yake na Catherine, na hivyo akaanzisha Mabadiliko Makubwa ya Waprotestanti huko Uingereza. Alimwoa Anne Boleyn mwaka wa 1533, miezi minne kabla Askofu Mkuu wa Canterbury, Thomas Cranmer, hajaharamisha rasmi ndoa ya kwanza ya Henry.

Mwaka uliofuata Henry mkaidi alikatisha uhusiano wote na Kanisa Katoliki na akapewa cheo cha kuwa msimamizi mkuu wa Kanisa la Anglikana. Mary, ambaye sasa alionwa kuwa mtoto-haramu, hakumwona mamaye tena, kwa kuwa ilimbidi Catherine aishi miaka iliyosalia akiwa amejitenga na watu.

Kutovumiliana kwa Waprotestanti

Kwa miaka 13 iliyofuata, watu waliokataa kumtambua Henry kuwa kiongozi wa kanisa au wale walioendelea kujitiisha chini ya mamlaka ya papa waliuawa. Henry alikufa mwaka wa 1547 na Edward mwenye umri wa miaka tisa akarithi cheo chake, mwanaye pekee aliye halali, wa mke wa tatu kati ya wake zake sita. Edward na washauri wake walijaribu kufanya Uingereza iwe ya Kiprotestanti. Wakatoliki walinyanyaswa kwa kufuata dini yao, sanamu na madhabahu yakaondolewa makanisani.

Baada ya muda vizuizi vya kuchapisha na kusoma Biblia katika Kiingereza viliondolewa, na ibada ya kanisa iliyohusisha kusoma Biblia ilipasa kufanywa kwa Kiingereza badala ya Kilatini. Lakini mwaka wa 1553, Edward alikufa kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu akiwa na umri wa miaka 15 tu. Mary alionwa kuwa mrithi halali naye akawa malkia wa Uingereza.

Kutovumiliana kwa Wakatoliki

Mwanzoni, watu walimkaribisha Mary mwenye umri wa miaka 37, lakini punde si punde wakamchukia. Raia zake walikuwa wamezoea Uprotestanti, na sasa Mary aliazimia kurudisha Ukatoliki nchini. Muda si muda, sheria zote za kidini zilizotungwa na Edward zikafutwa. Mary alimwomba msamaha papa kwa niaba ya taifa lote. Mara nyingine tena, Uingereza ikawa ya Kikatoliki.

Mapatano hayo na Kanisa Katoliki yalizusha mnyanyaso mpya dhidi ya Waprotestanti. Walifananishwa na jipu hatari lililohitaji kuondolewa kabla halijaathiri mwili mzima. Wengi waliokataa mafundisho ya Kanisa Katoliki walichomwa wangali hai mtini.

Kuwaadhibu Waasi

John Rogers alikuwa wa kwanza kuuawa wakati wa utawala wa Mary. Alikuwa ametunga ile inayoitwa Matthew’s Bible, iliyokuwa msingi wa King James Version. Baada ya kutoa hotuba iliyopinga Kanisa Katoliki na kuonya dhidi ya “Upapa wenye kuumiza, ibada ya sanamu, na ushirikina,” alifungwa gerezani kwa mwaka mmoja, na katika Februari 1555 alichomwa hadi kifo kwa sababu ya uasi.

John Hooper, askofu wa Gloucester na Worcester, aliitwa pia mzushi. Alitangaza rasmi kwamba ilikuwa halali kwa makasisi kuoa na kwamba kutaliki kwa sababu ya uzinzi kuliruhusiwa. Pia alikana kwamba Kristo alikuwepo kimwili wakati wa Misa. Hooper alichomwa akiwa hai, kifo chake chenye maumivu makali kilidumu kwa takriban dakika 45. Ilipofika zamu ya kumchoma mhubiri Mprotestanti Hugh Latimer mwenye umri wa miaka 70, alimtia moyo Nicholas Ridley, Mwanaharakati mwenzake ambaye pia alikuwa ametundikwa mtini kwa kumwambia: “Jifariji, Bwana Ridley, na ujikaze kiume. Siku ya leo tutatokeza mabadiliko Uingereza kwa fadhili za Mungu, kwa kuwa ninatumaini kwamba hayatakomeshwa kamwe.”

Thomas Cranmer, Askofu wa kwanza Mprotestanti wa Canterbury, pia alihukumiwa kifo kwa shtaka la uasi wakati wa utawala wa Henry na Edward. Licha ya kukana itikadi zake za Kiprotestanti, mwishowe alibadili msimamo wake hadharani, akamshutumu papa kuwa adui wa Kristo, na kutia mkono wake wa kulia motoni ili uchomeke kwanza, kwa kuwa ulikuwa na hatia ya kutia sahihi hati za kukana itikadi zake.

Ijapokuwa Waprotestanti matajiri wapatao 800 walikimbilia nchi za ng’ambo ili kupata usalama, angalau watu 277 walichomwa moto mtini huko Uingereza katika muda wa miaka mitatu na miezi tisa iliyofuata hadi kifo cha Mary. Wahasiriwa wengi walikuwa watu wa kawaida ambao hawakujua kabisa waitikadi nini. Vijana waliokua na kuzoea kusikia papa akishutumiwa sasa walikuwa wanaadhibiwa kwa sababu ya kumkashifu. Wengine walikuwa wamejifunza kujisomea Biblia wenyewe na walikuwa wamebuni maoni tofauti ya kidini.

Vifo vya polepole vyenye maumivu makali vya wanaume, wanawake, na watoto waliochomwa moto mtini vilifadhaisha wengi. Mwanahistoria Carolly Erickson asimulia kisa kimoja: “Kwa kawaida kuni za moto zilikuwa mbichi, au majani yalilowa sana kiasi cha kutoweza kuchomeka upesi. Mifuko yenye baruti iliyofungiliwa kwenye miili ya wahasiriwa ili kupunguza maumivu yao ilikosa kuwaka, au iliwaumiza vibaya sana pasipo kuwaua.” Wahasiriwa hawakutiwa kitambaa mdomoni, na kwa hiyo “vilio vyao na sala zilisikiwa mara nyingi hadi walipokufa.”

Watu wengi zaidi wakaanza kutilia shaka dini iliyowashurutisha watu kufuata mafundisho yake kwa kuwachoma moto mtini. Hali ya kuwasikitikia wahasiriwa iliwachochea watumbuizaji watunge nyimbo kuhusu wafia-imani Waprotestanti. John Foxe alianza kuandika kitabu chake cha Book of Martyrs, ambacho kiliwaathiri sana Wanaharakati Waprotestanti kama Biblia. Watu wengi waliokuwa Wakatoliki mwanzoni mwa utawala wa Mary wakawa Waprotestanti mwishowe.

Urithi wa Mary

Baada ya kuwa malkia, Mary alisema kwamba angefunga ndoa na Philip binamu yake, mrithi wa kiti cha ufalme cha Hispania. Alikuwa mfalme mgeni na Mkatoliki mwenye juhudi, jambo lililowachukiza sana Waingereza. Maasi ya Waprotestanti yaliyopangwa kwa nia ya kupinga ndoa hiyo hayakufua dafu, na waasi 100 wakauawa. Philip alifunga ndoa na Mary Julai 25, 1554, ingawa Philip hakutawazwa kamwe. Hata hivyo, Mary aliyetaka mrithi Mkatoliki alisononeka sana kwa sababu ya kukosa mtoto.

Afya ya Mary ilizorota, hatimaye akafa akiwa na umri wa miaka 42 baada ya kutawala kwa muda mfupi wa miaka mitano. Alikufa kwa majonzi. Mumewe alikuwa amechoshwa naye, na raia wengi walimchukia. Wakazi wengi wa London walifanya karamu barabarani alipokufa. Badala ya kujenga upya Ukatoliki, aliendeleza Uprotestanti kwa ushupavu wake. Sifa yake yaonyeshwa na jina ambalo amebandikwa—Mary Mwuaji.

Dhamiri Iliyozoezwa Vibaya

Kwa nini Mary aliamuru watu wengi sana wauawe kwa kuchomwa moto? Alikuwa amefunzwa kwamba Mungu aliwaona waasi wa kidini kuwa wahaini, naye akajitwalia daraka la kuwakomesha kabla hawajaathiri taifa zima. Alifuata dhamiri yake lakini akapuuza haki za wengine ambao walidhamiria kuwa na maoni tofauti.

Hata hivyo, Waprotestanti pia hawakuvumilia dini nyingine. Wakati wa utawala wa Henry na Edward, watu walichomwa pia kwa sababu ya itikadi zao za kidini. Mwandamizi Mprotestanti wa Mary, Elizabeth wa Kwanza, alitangaza kufuata Ukatoliki kuwa kosa la uhaini, na wakati wa utawala wake zaidi ya Wakatoliki Waingereza 180 waliuawa. Katika karne iliyofuata, mamia zaidi waliuawa kwa sababu ya itikadi zao za kidini.

Mbona Wanaomba Radhi Sasa?

Desemba 10, 1998, ilikuwa siku ya ukumbusho wa miaka 50 ya kuidhinishwa kwa Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa. Kifungu cha 18 chatambua “uhuru wa kuwaza, dhamiri na dini,” pamoja na uhuru wa kubadili dini, kuifuata na kuifundisha. Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Uingereza na Wales waliteua ukumbusho wa miaka 50 kuwa “wakati unaofaa wa Wakatoliki kuchunguza dhamiri zao kwa habari hii” na kukiri “uhalifu mbaya” uliotendwa, hasa wakati wa Mary Tudor.

Ijapokuwa matendo ya kutovumiliana kwa kidini ya miaka ipatayo 450 iliyopita yanasikitikiwa, je, kweli hali imebadilika? Ingawa watu hawachomwi moto mtini, lakini wengi wanaoitwa eti Wakristo wanaendelea kubaka na kuua wafuasi wa dini nyingine. Kutovumiliana huko hakumpendezi Mungu. Kwa kweli, Yesu Kristo, yule anayedhihirisha kikamili sifa za Mungu, alisema hivi: “Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.”—Yohana 13:35.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Malkia Mary

[Hisani]

From the book A Short History of the English People

[Picha katika ukurasa wa 13]

Latimer na Ridley walichomwa moto mtini

[Hisani]

From the book Foxe’s Book of Martyrs

[Picha katika ukurasa wa 13]

Cranmer ahakikisha kwamba mkono wake wa kulia unachomeka kwanza

[Hisani]

From the book The History of England (Vol. 1)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Pambizoni: 200 Decorative Title-Pages/Alexander Nesbitt/Dover Publications, Inc.