Chakula Kilichobadilishwa Maumbile—Je, Ni Salama Kwako?
Chakula Kilichobadilishwa Maumbile—Je, Ni Salama Kwako?
IKITEGEMEA mahali unakoishi, huenda leo umekula chakula kilichobadilishwa maumbile wakati wa kifungua-kinywa, chakula cha mchana, au cha jioni. Labda ni viazi ambavyo dawa ya kuua wadudu imetiwa katika chembe zake au labda ni nyanya ambazo haziozi haraka baada ya kuchumwa. Huenda chakula au kiambato hicho kilichobadilishwa maumbile hakina maelezo hayo, na ulimi wako hauwezi kukitofautisha na kile cha kawaida.
Hata sasa hivi, mimea hiyo iliyobadilishwa maumbile kama vile maharagwe, mahindi, mbegu za rapa, na viazi yaendelea kukua huko Argentina, Brazili, China, Kanada, Marekani, na Mexico. Ripoti moja yasema kwamba “kufikia mwaka wa 1998, asilimia 25 ya mahindi, asilimia 38 ya maharagwe, na asilimia 45 ya pamba zinazokuzwa huko Marekani zilikuwa zimebadilishwa maumbile, ili kufanya mimea hiyo istahimili dawa ya kuua magugu au itengeneze dawa yake binafsi ya kuua wadudu.” Kufikia mwishoni mwa mwaka wa 1999, ekari zipatazo milioni 100 ulimwenguni kote zilipandwa mazao ya kuuza yaliyobadilishwa maumbile, ingawa baadhi ya mimea hiyo si ya chakula.
Je, vyakula vilivyobadilishwa maumbile ni salama kwako? Je, mbinu za kisayansi zinazotumiwa kuzalisha mimea iliyobadilishwa maumbile zina hatari yoyote kwa mazingira? Huko Ulaya, mjadala juu ya vyakula vilivyobadilishwa maumbile unapamba moto. Mlalamikaji mmoja huko Uingereza alisema hivi: “Sababu pekee inayofanya nipinge vyakula vilivyobadilishwa maumbile ni kwamba hivyo si salama, havihitajiki na si vya lazima.”
Chakula Hubadilishwaje Maumbile?
Sayansi inayotumiwa kubadilisha maumbile ya chakula huitwa biotekinolojia ya chakula, yaani, kutumia mbinu za kisasa za elimu ya chembe ili kuboresha mimea, wanyama, na viumbe vidogo ili kuzalisha chakula. Bila shaka, mbinu ya kubadili
chembe za viumbe-hai ni ya zamani kama kilimo chenyewe. Mkulima wa kwanza aliyemfanya fahali bora ampande ng’ombe jike bora ili kuboresha mifugo yake, badala ya kuwaachilia wanyama wapandane ovyoovyo, alikuwa anatumia biotekinolojia ya kikale. Mwokaji wa kwanza aliyetumia chachu katika uokaji wa mikate vilevile alikuwa anatumia kiumbe-hai ili kutengeneza chakula bora. Jambo moja ambalo lipo katika mbinu hizo zote za kale ni utumizi wa taratibu za asili ili kubadilisha chakula.Vivyo hivyo, biotekinolojia ya kisasa hutumia viumbe ili kutengeneza au kubadili mazao. Lakini kinyume cha mbinu za kikale, biotekinolojia ya kisasa huwezesha kubadili moja kwa moja chembe za urithi za viumbe kwa usahihi. Hiyo huwezesha viumbe wasiohusiana kimaumbile wabadilishane chembe za urithi, na kufanyiza michanganyo isiyoweza kutokea kiasili. Sasa wazalishaji waweza kuchukua tabia za viumbe fulani kisha waziweke katika chembe za urithi za mmea—kwa mfano, chembe ya samaki yenye uwezo wa kustahimili baridi, kustahimili magonjwa kutoka kwa virusi, na chembe yenye uwezo wa kuua wadudu kutoka katika bakteria za udongoni.
Labda mkulima hataki viazi au matofaa yake yageuke rangi yanapokatwa au kukwaruzwa. Watafiti hutatua tatizo hilo kwa kuondoa chembe za urithi zinazosababisha rangi kugeuka na badala yake huweka aina ya chembe zilizobadilishwa ambazo huzuia rangi kugeuka. Au labda mkulima wa viazisukari ataka kupanda mapema ili apate mavuno bora. Kwa kawaida hawezi kupanda mapema kwa sababu viazisukari vingeharibiwa na baridi. Ndipo biotekinolojia hutumiwa ili kuweka chembe za urithi za samaki wanaostahimili maji baridi katika chembe za viazisukari. Matokeo ni kwamba viazisukari vinavyoweza kustahimili baridi kali inayofikia digrii -6.5 Selsiasi, ambayo ni baridi mara mbili kuliko kiwango ambacho kwa kawaida viazisukari vyaweza kustahimili.
Hata hivyo, tabia hizo zinazotokana na
kuhamishwa kwa chembe mojamoja za urithi zina mipaka. Lingekuwa jambo tofauti sana kubadili tabia tata zaidi, kama vile muda wa ukuzi au kustahimili ukame. Sayansi ya kisasa bado haiwezi kubadili vikundi vizima-vizima vya chembe za urithi. Kwani, hata nyingi za chembe hizo za urithi hazijagunduliwa bado.Je, Ni Mabadiliko Mapya ya Kilimo?
Hata mabadiliko madogo katika maumbile ya mimea hufanya wanaounga mkono biotekinolojia wajawe na matumaini. Wanasema kwamba mimea iliyobadilishwa maumbile italeta mabadiliko mapya ya kilimo. Kiongozi mmoja wa kampuni ya biotekinolojia asema kwamba sayansi ya kubadilisha maumbile ni “chombo bora katika jitihada ya kuzalisha chakula kingi zaidi” ili kulisha idadi ya watu duniani inayoongezeka kwa karibu 230,000 kila siku.
Mimea hiyo tayari imesaidia kupunguza gharama za kuzalisha chakula. Mimea ya chakula imeimarishwa kupitia chembe ya urithi inayofanya kazi kama dawa ya asili ya kuua wadudu, ikiondoa uhitaji wa kunyunyiza dawa kwenye maeneo makubwa ya mimea. Mimea iliyobadilishwa maumbile inayokuzwa hutia ndani maharagwe na nafaka zenye protini nyingi zaidi—zinazonufaisha sana maeneo yenye umaskini ulimwenguni. “Mimea bora” kama hiyo yaweza kupitisha chembe za urithi na tabia zake mpya kwa vizazi vinavyofuata, ikitokeza mazao mengi zaidi katika maeneo yenye ukame ya nchi maskini na zenye watu wengi mno.
“Bila shaka yafaa kuboresha hali ya wakulima ulimwenguni,” akasema msimamizi wa kampuni moja maarufu ya biotekinolojia. “Nasi tutafanya hivyo—kwa kutumia biotekinolojia katika chembe mojamoja za urithi ili kutimiza mambo ambayo wazalishaji wamekuwa wakifanya kwa ‘mimea mizima-mizima’ kwa karne nyingi. Tutatokeza mazao bora yanayotosheleza mahitaji hususa nasi tutafanya hivyo haraka kuliko zamani.”
Hata hivyo, wanasayansi wa kilimo wanasema kuwa harakati za kuendeleza ubadilishaji wa maumbile kama suluhisho kwa upungufu wa chakula ulimwenguni zinadhoofisha utafiti wa sasa wa mimea. Ingawa utafiti huu si wa pekee sana, una manufaa zaidi nao waweza kuyafaidi maeneo yenye umaskini ulimwenguni. “Hatupaswi kuongozwa na tekinolojia hii ambayo haijathibitishwa wakati tuna masuluhisho mengi mazuri kwa matatizo ya chakula,” asema Hans Herren, mtaalamu wa kupambana na magonjwa ya mimea.
Wasiwasi wa Maadili
Mbali na hatari za afya na mazingira ziwezazo kutokea, wengine huonelea kwamba kubadilisha maumbile ya mimea na viumbe wengine huleta matatizo ya maadili. Mwanasayansi Douglas Parr aliye pia mhamasishaji alisema: “Kubadilisha maumbile huvuka mpaka muhimu katika hali ya mwanadamu ya kuisimamia dunia, kukibadilisha hali ya asili ya uhai.” Naye Jeremy Rifkin, mwandikaji wa kitabu cha The Biotech Century, akasema hivi: “Unapovuka mipaka yote ya maumbile ya asili, unaanza kuwaona viumbe fulani kuwa tu vifaa vya kisayansi viwezavyo kubadilishwa. Hilo hutufanya tuuelewe kwa njia mpya kabisa uhusiano wetu na viumbe, na pia jinsi tunavyowatumia.” Basi akauliza: “Je, uhai una thamani ya asili au una thamani ya kutumiwa tu? Je, tuna wajibu gani kwa vizazi vya baadaye? Tuna wajibu gani kwa viumbe tunaoishi nao?”
Wengine, akiwemo Prince Charles wa Uingereza, hubisha kwamba kubadilishana chembe za urithi kati ya viumbe mbalimbali wasio na uhusiano wa kimaumbile “hutuingiza katika maeneo ambayo ni haki ya Mungu peke yake.” Wanafunzi wa Biblia huamini kabisa kwamba Mungu ndiye “chemchemi ya uzima.” (Zaburi 36:9) Hata hivyo, hakuna uthibitisho hakika kwamba Mungu hukataza uzalishaji wa wanyama na mimea kwa utaratibu wa kuteua, mbinu ambayo imefanya dunia yetu iwalishe mabilioni ya watu waliomo. Baada ya muda kupita, ndipo tu tutakapoweza kujua iwapo biotekinolojia inadhuru wanadamu na mazingira. Iwapo kweli biotekinolojia inaingilia “maeneo ambayo ni haki ya Mungu,” ndipo—kwa kuchochewa na upendo na hangaiko kwa wanadamu—aweza kuyabatilisha madhara hayo.
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Hatari Yaweza Kutokea?
Sayansi ya biotekinolojia imesitawi haraka sana hivi kwamba sheria na mashirika yanayoidhibiti hayawezi kwenda sambamba nayo. Utafiti hauwezi kuzuia matokeo yasiyoonekana kimbele. Watu wengi wanaozidi kupinga mbinu hiyo huonya juu ya matokeo yasiyotarajiwa, kama vile kuharibika kabisa kwa mfumo wa kiuchumi wa wakulima ulimwenguni hadi kuharibiwa kwa mazingira na matisho kwa afya ya mwanadamu. Watafiti huonya kwamba hakuna uchunguzi wa muda mrefu, ulio kamili wa kuthibitisha usalama wa chakula kilichobadilishwa maumbile. Wao hutaja hatari kadhaa ziwezazo kutokea.
● Mizio. Kwa mfano, iwapo chembe ya urithi inayotokeza protini yenye kusababisha mizio ingeingia katika mahindi, hiyo ingekuwa hatari kubwa kwa watu wenye mizio ya chakula. Licha ya uhakika wa kwamba mashirika yanayosimamia usalama wa chakula huzitaka kampuni zitoe ripoti zinazoonyesha iwapo chakula kilichobadilishwa maumbile kina protini zozote zenye madhara, watafiti fulani wana wasiwasi kwamba vizio visivyojulikana vyaweza kupenya pasipo kutambuliwa na vyombo vya kupima.
● Sumu nyingi. Wataalamu fulani huamini kwamba kubadilisha maumbile kwaweza kuongeza sumu za asili katika mimea kwa njia zisizotarajiwa. Wakati chembe ya urithi inapowekwa katika mmea, mbali na kuwa na matokeo yanayotafutwa, huenda ikaanzisha utengenezaji wa sumu za asili.
● Kustahimili viuavijasumu. Wanasayansi hutumia chembe-tambulishi ili kutambua iwapo chembe ya urithi inayotakikana imepandikizwa kwa mafanikio. Kwa kuwa chembe-tambulishi nyingi hustahimili viuavijasumu, wapinzani wana wasiwasi kwamba hilo lingeweza kuendeleza tatizo sugu la kustahimili viuavijasumu. Hata hivyo, wanasayansi wengine hubisha wakisema kwamba tabia za urithi za chembe-tambulishi hubadilishwa kabla ya kutumiwa, hivyo hatari hiyo huondolewa.
● Kusambaa kwa “magugu sugu.” Mojawapo ya wasiwasi mkubwa ni kwamba mara mimea iliyobadilishwa maumbile inapopandwa, chembe za urithi zitasambaa kupitia mbegu na chavua na kuingia katika magugu yenye uhusiano wa karibu kimaumbile na kutokeza “magugu sugu” yanayoweza kustahimili dawa za kuua magugu.
● Madhara kwa viumbe wengine. Mwezi wa Mei 1999, watafiti wa Chuo Kikuu cha Cornell waliripoti kwamba viwavi wa kipepeo-maliki waliokula majani yenye chavua kutoka kwa mahindi yaliyobadilishwa maumbile walipata ugonjwa wakafa. Ingawa wengine hutilia shaka uhalali wa uchunguzi huo, kungali wasiwasi fulani kwamba viumbe wasionuiwa waweza kudhuriwa.
● Kutokomea kwa dawa salama za kuua wadudu. Baadhi ya mimea iliyobadilishwa maumbile inayositawi sana ina chembe ya urithi inayozalisha protini fulani ambayo ni sumu kwa wadudu. Hata hivyo, wanabiolojia huonya kwamba wadudu wakiizoea sumu ambayo chembe hiyo ya urithi hutokeza, itafanya wadudu hao wakuze ustahimilivu na hivyo kufanya dawa za wadudu zisifae kitu.