Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Ulaya Itaungana Kweli?

Je, Ulaya Itaungana Kweli?

Je, Ulaya Itaungana Kweli?

IKIWA waona vigumu kuamini kwamba Ulaya inataka kuungana kwa kweli, unahitaji tu kuvuka mipaka yake michache ya ndani. Sasa watu husafiri kwa uhuru katika nchi za Muungano wa Ulaya (EU). Sasa watu hawasubiri kwenye mipaka. Bila shaka, wasafiri wanafurahi—lakini si wao peke yao wanaonufaika. Sasa raia wa nchi za EU wanaweza kwenda masomoni, kufanya kazi, na kuanzisha biashara popote katika EU. Hivyo kumekuwa na maendeleo ya kiuchumi katika maeneo maskini zaidi ya Muungano huo.

Bila shaka kuvuka mipaka kwa urahisi ni badiliko kubwa. Ingawa hivyo, je tufikie mkataa kwamba tayari Ulaya imeungana na kwamba hakuna vizuizi kuelekea muungano huo? Kinyume cha hilo, kungali na vizuizi, vingine ni vyenye kufadhaisha sana. Lakini kabla hatujavizungumzia, acheni tuchunguze mojawapo ya hatua kubwa zaidi ambayo imepigwa sasa kuelekea muungano. Na hivyo huenda tukaelewa kwa njia bora zaidi kwa nini watu wanatumaini kuwa na muungano.

Hatua Kuelekea Muungano wa Kifedha

Kudumisha mipaka kwaweza kuwa ghali sana. Utaratibu wa forodha miongoni mwa nchi 15 wanachama wa EU wakati mmoja uligharimu mataifa hayo euro bilioni 12 hivi kwa mwaka. Haishangazi kwamba hali mpya katika mipaka ya Ulaya imechochea ukuzi wa kiuchumi. Unapofikiri juu ya wakazi milioni 370 wa EU wakisafiri kwa uhuru kutoka nchi moja hadi nyingine katika soko moja la pamoja, ni wazi kwamba kuna uwezekano mkubwa wa ukuzi wa kiuchumi. Ni nini kilichowezesha maendeleo hayo?

Huko nyuma katika Februari 1992, viongozi wa serikali walipiga hatua kubwa kuelekea muungano kwa kutia sahihi Mkataba wa Muungano wa Ulaya, au Mkataba wa Maastricht. Mkataba huo uliweka msingi wa kuanzishwa kwa soko la pamoja katika Ulaya, benki kuu, na fedha ya aina moja. Hata hivyo, hatua nyingine ya maana ilipasa kufuata: kukomesha kupanda na kushuka kwa viwango vya ubadilishaji wa fedha. Kwani, biashara iliyofanywa leo huenda isiwe na faida siku itakayofuata kwa sababu ya badiliko la viwango vya ubadilishaji.

Kizuizi hiki kuelekea muungano kiliondolewa wakati Muungano wa Kiuchumi na Kifedha wa Ulaya (EMU) ulipoanzishwa na euro kuwa fedha ya pamoja. Sasa hakuna gharama ya ubadilishaji, na biashara hazihitaji kujilinda tena dhidi ya hatari za viwango vya ubadilishaji. Tokeo ni kwamba biashara zimekuwa na gharama za chini na biashara ya kimataifa imeongezeka. Hilo laweza kutokeza kazi zaidi za kuajiriwa na kuongeza uwezo wa kununua vitu—ambao ungefaidi kila mtu.

Kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Ulaya mwaka wa 1998 kuliashiria hatua nyingine ya maana kuelekea matumizi ya fedha moja. Benki hii inayojitegemea, iliyo katika jiji la Ujerumani la Frankfurt, hudhibiti fedha za serikali zinazohusika. Inajitahidi kudhibiti kupanda kwa gharama katika lile linaloitwa eneo la euro, linalotia ndani nchi 11, * na kuimarisha kushuka na kupanda kwa viwango vya ubadilishaji kati ya euro, dola, na yen.

Kwa hiyo kuhusu suala la fedha, maendeleo makubwa sana kuelekea muungano yamefanywa. Hata hivyo, mambo ya kifedha pia huonyesha ukosefu mkubwa wa muungano uliopo bado kati ya mataifa ya Ulaya.

Mambo Zaidi ya Kifedha

Mataifa maskini zaidi ya EU yana malalamishi yao. Yanahisi kwamba mataifa wanachama yaliyo tajiri zaidi hayashiriki utajiri wao vya kutosha pamoja nao. Hakuna mataifa wanachama yanayokataa uhitaji wa kutoa msaada zaidi wa kifedha kwa washiriki wenzao wa Ulaya walio maskini zaidi. Hata hivyo, mataifa tajiri zaidi yanahisi kwamba yana sababu halali za kutotoa msaada.

Kwa mfano ifikirie Ujerumani. Shauku ambayo nchi hii ilikuwa nayo ya kulipia gharama za kuunganishwa kwa Ulaya kwa wazi imefifia kwa vile mzigo wake wa madeni umeongezeka. Gharama ya kuunganisha Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi peke yake imekuwa kubwa sana—takriban dola za Marekani bilioni mia moja kwa mwaka. Kiasi hicho chawakilisha robo ya bajeti ya taifa! Mambo hayo yameongeza deni la taifa la Ujerumani kiasi cha kwamba Ujerumani ilihitaji kujitahidi sana ili kutimiza matakwa ya kuwa mwanachama wa EMU.

Washiriki Wapya Waomba Wasajiliwe Kwenye EU

Kwa muda mfupi uliopo, watetezi wa aina moja ya fedha wanatumaini kwamba nchi za EU ambazo bado si washiriki wa EMU zitashinda vizuizi vyao kabla ya mwaka wa 2002, wakati sarafu na noti za euro zitakapochukua mahali pa sarafu za sasa za Ulaya. Ikiwa Denmark, Sweden, na Uingereza, zitaacha kusitasita, hata watu katika nchi hizo huenda wakaona euro ikichukua mahali pa pauni, kroner, na kronor zao.

Kwa sasa, nchi nyingine sita za Ulaya zinaomba zisajiliwe kwenye EU. Hizo ni Cyprus, Estonia, Hungaria, Jamhuri ya Cheki, Poland, na Slovenia. Nchi nyingine tano zaidi zinasubiri zamu yake, yaani, Bulgaria, Latvia, Lithuania, Rumania, na Slovakia. Itazigharimu kiasi kikubwa kuwa wanachama. Makadirio yanaonyesha kwamba kati ya mwaka wa 2000 na 2006, EU italazimika kutoa euro bilioni 80 ili kusaidia nchi mpya kumi kutoka Ulaya Mashariki.

Hata hivyo, fedha ambazo nchi mpya zitahitaji kulipia ili kukubaliwa kuwa washiriki wa EU ni nyingi zaidi kuliko msaada zitakaopokea kutoka EU. Kwa mfano, Hungaria itahitaji kutumia euro bilioni 12 kuboresha reli na barabara zake. Jamhuri ya Cheki itahitaji kutumia zaidi ya euro bilioni 3.4 kutia maji dawa peke yake, na Poland itahitaji kutumia euro bilioni 3 kupunguza moshi wa salfa. Ijapokuwa hivyo, nchi zinazoomba kusajiliwa zinaona kwamba manufaa ni mengi kuliko gharama inayohusika. Kwanza, biashara yao na nchi za EU itaongezeka. Hata hivyo, nchi zinazoomba kusajiliwa zitahitaji kusubiri kwa muda fulani. Kulingana na maoni ya sasa ya umma, mataifa mapya wanachama yapasa kukubaliwa tu baada ya EU kurekebisha mambo yake ya kifedha.

Uchungu wa Moyo, Utukuzo wa Taifa, na Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa

Licha ya jitihada zote ambazo zimefanywa kuwa na muungano mkubwa zaidi, kuna hangaiko linalotoka ndani na nje ya Ulaya kuhusu maendeleo ya Bara hilo. Pia kuna mashaka kuhusu namna ya kushughulika na mapambano ya kikabila, kama yale yaliyo katika eneo linalosambaratika la Balkan—kwanza vita iliyo Bosnia kisha mapambano katika Kosovo. Mara nyingi washiriki wa EU hukosa kukubaliana kuhusu namna ya kushughulikia mapambano hayo katika Ulaya na kwingineko. Kwa kuwa EU si ushirika wa mataifa na haina sera moja ya kigeni, mara nyingi mapendezi ya kitaifa ndiyo hutawala. Kwa wazi, mapendezi ya kitaifa yanazuia kwa kadiri kubwa kuwapo kwa ‘Serikali za Muungano za Ulaya.’

Pia Ulaya ina tatizo jingine hatari—kiwango kikubwa cha ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Kwa wastani, asilimia 10 ya watu wawezao kufanya kazi hawajaajiriwa. Hii yamaanisha kwamba zaidi ya watu milioni 16 hawana kazi ya kuajiriwa. Katika nchi nyingi vijana, ambao ni takriban robo ya watu wa EU, wamejitahidi sana kutafuta kazi pasipo kufanikiwa. Si ajabu kwamba watu wengi wanahisi kuwa kupambana na ukosefu mkubwa sana wa kazi ya kuajiriwa ndilo tatizo kubwa zaidi la Ulaya! Kufikia sasa, jitihada za kutokeza nafasi za kazi za kuajiriwa hazijafua dafu.

Hata hivyo, kungali na kizuizi kikubwa zaidi cha muungano.

Ni Nani Anayesimamia?

Utawala ungali kizuizi kikubwa zaidi cha kuunganisha Ulaya. Lazima mataifa wanachama yakubali kuachilia utawala wao wa kitaifa kwa kadiri fulani. Mradi wa EU ni kuwa na utawala wa kimataifa. Mradi huo usipotimizwa, lasema gazeti la Le Monde, kuanzishwa kwa euro kutakuwa “ushindi wa muda” tu. Ingawa hivyo, mataifa mengine washiriki, huona ugumu kukubali wazo la kuachilia mamlaka. Kwa mfano, kiongozi wa taifa moja la EU alisema kwamba nchi yake “ilizaliwa iwe kiongozi wa mataifa, si mfuasi.”

Inaeleweka kwamba mataifa madogo zaidi yanahofu kuwa baada ya muda mrefu, mataifa makubwa zaidi yataanza kudhibiti na kukataa maamuzi ambayo yangeweza kuathiri mapendezi yao. Kwa mfano, mataifa madogo zaidi yanashindwa itaamuliwaje ni nchi zipi zitakazokuwa na makao makuu ya mashirika mbalimbali ya EU. Huo ni uamuzi muhimu kwa sababu mashirika ya namna hiyo huongeza nafasi za kazi za kuajiriwa katika nchi wenyeji.

Kwa sababu ya vizuizi hivi vya muungano—tofauti za kiuchumi, vita, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, na utukuzo wa taifa—huenda mtu akatamaushwa kwa urahisi na suala la kuunganishwa kwa Ulaya. Ingawa hivyo, uhakika ni kwamba maendeleo makubwa yamefanywa. Haijulikani ni maendeleo makubwa kadiri gani yatakayofanywa wakati ujao. Matatizo yanayokumba wale wanaojaribu kuunganisha Ulaya, hasa ni sawa na matatizo yanayokumba serikali zote za wanadamu.

Je, itawezekana wakati wowote kuleta serikali itakayotatua matatizo kama vile zogo la kikabila, ukosefu mkubwa wa kazi ya kuajiriwa, umaskini, na vita? Je, ni jambo halisi kufikiri juu ya ulimwengu ambamo watu huishi katika muungano wa kweli? Makala ifuatayo itatoa jibu ambalo huenda likakushangaza.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Nchi hizo ni Austria, Finland, Hispania, Ireland, Italia, Luxembourg, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, na Ureno. Kwa sababu mbalimbali, Denmark, Ugiriki, Uingereza, na Sweden hazijatiwa ndani bado.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Euro Yajitokeza!

Ijapokuwa sarafu na noti za kitaifa za washiriki wa Muungano wa Ulaya hazitatoweka hadi ufikapo mwaka wa 2002, mapatano ya biashara yasiyohusisha pesa taslimu tayari yanafanywa kwa euro. Badiliko hilo la kifedha limekuwa shughuli kubwa sana kwa mabenki. Hata hivyo, viwango vya ubadilishaji kati ya fedha za kitaifa za nchi wanachama na euro sasa vimeimarishwa. Pia ubadilishaji katika masoko ya hisa huonyesha bei kwa euro. Sasa maduka na biashara nyingi huonyesha bei za bidhaa zake kwa euro na fedha za nchi inayohusika.

Biashara za namna hiyo hutaka mabadiliko makubwa—hasa kwa watu wengi wazee-wazee, ambao hawataweza tena kutumia maki, faranga, au lira wanazozijua. Hata daftari-pesa na mashine za kielektroni za kuweka na kutoa pesa kwenye benki zahitaji kurekebishwa. Ili kufanya badiliko hilo liwe bila matatizo kwa kadiri iwezekanavyo, kampeni rasmi zimepangwa za kupasha umma habari kuhusu kuanzishwa kwa euro na matumizi yake.

Euro itakuja licha ya vizuizi vyovyote vinavyobakia. Kwa hakika, sarafu na noti za euro tayari zimeanza kutengenezwa. Na ni kazi nyingi kweli. Hata katika nchi ndogo kama vile Uholanzi, yenye watu milioni 15, matbaa na mashine za kutengeneza sarafu zitakuwa zikifanya kazi kwa miaka mitatu mfululizo ili kutokeza sarafu bilioni 2.8 na noti milioni 380 ifikapo Januari 1, 2002. Ikiwa noti hizi mpya zingewekwa katika rundo, zingefanyiza kitita chenye urefu wa kilometa zipatazo 20!

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

“Je, Euro Italeta Uharibifu Kamili”?

Mapema mwaka wa 1999 Tume ya Ulaya, baraza kuu la Muungano wa Ulaya (EU), iliponea chupuchupu kuchukuliwa hatua kali. Tume hiyo ilishtakiwa kwa upunjaji, ufisadi, na upendeleo. Kamati iliundwa ili kuchunguza madai hayo. Baada ya uchunguzi wa muda wa majuma sita, kamati hiyo ilipata kwamba Tume ya Ulaya ilihusika na ufisadi na kutumia fedha vibaya. Hata hivyo, kamati ya uchunguzi haikupata uthibitisho wowote kwamba wajumbe walikuwa wamejitajirisha.

Baada ya ripoti ya kamati hiyo kuchapishwa, Tume nzima ya Ulaya ilijiuzulu mnamo Machi 1999—hatua isiyo na kifani. Ilisababisha tatizo kubwa sana kwa EU. Gazeti Time liliita hatua hii “Uharibifu Kamili Uletwao na Euro.” Baada ya muda itajulikana kadiri tatizo hilo litakavyoathiri kuunganishwa kwa Ulaya.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Tayari imekuwa rahisi zaidi kuvuka mipaka katika Ulaya

[Picha katika ukurasa wa 7]

Benki Kuu ya Ulaya, iliyo Frankfurt, Ujerumani, ilianzishwa mwaka wa 1998