Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kampuni ya Tumbaku Yakiri Kwamba

Uvutaji-Sigareti Husababisha Kansa

Baada ya miongo mingi ya mabishano kuhusu matokeo ya uchunguzi wa wanatiba mashuhuri, Philip Morris, kampuni kubwa zaidi ya kutengeneza sigareti huko Marekani, sasa imekiri kwamba uvutaji-sigareti husababisha kansa ya mapafu na maradhi mengine ya kufisha. Habari za kampuni moja zilizochapishwa magazetini zasema: “Kuna muafaka mkubwa sana wa kitiba na wa kisayansi kwamba kuvuta sigareti husababisha kansa ya mapafu, ugonjwa wa kuvimba mapafu na maradhi mengine mabaya sana miongoni mwa wavutaji-sigareti.” Gazeti la The New York Times lasema kwamba “hapo awali, kampuni ilishikilia kauli . . . kwamba uvutaji-sigareti ‘uliongeza hatari’ au ‘ulichangia hatari’ ya maradhi kama vile kansa ya mapafu, na kwamba haukusababisha maradhi.” Hata hivyo, licha ya kukiri hivyo, kampuni hiyo yasema: “Tunajivunia sana sigareti zetu na kampeni za utangazaji ambazo zimeziunga mkono kwa miaka mingi.”

Majengo Muhimu Yanatoweka

Maghala ya nafaka yanatoweka polepole kutoka mbuga za nyasi za magharibi mwa Kanada. Kilele cha idadi ya maghala ya nafaka kilifikiwa mwaka wa 1933 kulipokuwa na maghala 5,758 kwenye sehemu za mashambani. Tangu wakati huo idadi hiyo imepunguka hadi 1,052. Kwa sababu gani? Mtu mmoja aliyeshuhudia kuharibiwa kwa ghala moja la nafaka aliomboleza hivi: “Nyakati zimebadilika sana. Sasa kilimo kimekuwa biashara ya vifaa vya kilimo. Hakuna mashamba ya familia tena. Ndivyo na maghala ya nafaka.” “Mbuga za nyasi zisizo na maghala ya nafaka ni sawa na Venice isiyo na mifereji, New York isiyo na majengo marefu au Uingereza isiyo na vilabu vya pombe,” laripoti gazeti la Harrowsmith Country Life. Vikundi vinavyoonyesha upendezi wa pekee vinafanya kazi ili kuhifadhi kile kinachoonwa kuwa ishara ya usanifu-majengo ya nyanda za Kanada. Ghala moja la nafaka lilibadilishwa kuwa jumba la makumbusho na jingine likafanywa kuwa mkahawa wa michezo ya kuigiza.

Hakuna Kabisa Wakati wa Kutosha

Kotekote Ulaya watu wengi zaidi wanahisi wakiwa mbioni, laripoti gazeti la Ujerumani Gießener Allgemeine. Hali ni namna moja iwe watu wanafanya kazi mbali na nyumbani, kazi ya nyumbani, au wanafurahia mapumziko. “Watu wanalala kwa muda mfupi zaidi, wanakula haraka zaidi, na kuhisi kana kwamba wanakimbizwa wanapokuwa kazini kuliko ilivyokuwa miaka 40 iliyopita,” asema mwanasaikolojia Manfred Garhammer, wa Chuo Kikuu cha Bamberg. Aliona kwamba maisha ya kila siku yamekuwa ya mbiombio katika mataifa yote ya Ulaya ambayo ameyachunguza. Vifaa vya nyumbani vya kupunguza kazi na kupunguzwa kwa saa za kufanya kazi havijatokeza “jamii iliyostarehe” au “kuongeza muda.” Badala yake, kwa wastani, wakati wa mlo umepunguzwa kwa dakika 20 na wakati wa kupumzika usiku kwa dakika 40.

Uraibu wa Kucheza Kamari Huko Australia

“Sasa kucheza kamari kumekuwa jambo linaloathiri sana afya katika Australia, kukiathiri moja kwa moja angalau wacheza-kamari sugu 330,000,” laripoti gazeti la The Australian. Kwa mujibu wa gazeti hilo, zaidi ya mashine 1 kati ya kila mashine 5 za kielektroni za kamari ulimwenguni pote iko Australia, ambapo asilimia 82 ya watu wazima hucheza kamari. Tume iliyokuwa ikichunguza uchezaji kamari huko Australia ilipata kwamba asilimia 2.3 ya watu wazima wa Australia wana tatizo kubwa sana la kucheza kamari. Kati ya hao, asilimia 37 walikuwa wamefikiria kujiua, zaidi ya asilimia 11 walikuwa wamejaribu kujiua, na asilimia 90 walisema kwamba walishuka moyo sana kwa sababu ya kucheza kamari. Tume hiyo iliomba uchezaji-kamari uchunguzwe kikamili na imedokeza kwamba ishara za kuonya zibandikwe kwenye majumba ya kuchezea kamari.

Kushinda Mkazo

Je, una mkazo? Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la El Universal, Taasisi ya Malipo ya Uzeeni ya Mexico yapendekeza madokezo yafuatayo ili kukabili mkazo. Lala kwa muda mrefu kadiri mwili wako utakavyo—kati ya saa sita na kumi kila siku. Kula kifungua-kinywa kamili, mlo wa mchana wa kiasi, na chakula chepesi cha jioni. Pia, katika sehemu nyingi watafiti wanapendekeza kwamba upunguze kula chakula chenye mafuta mengi, upunguze chumvi, baada ya kufikia umri wa miaka 40, punguza matumizi ya maziwa na sukari. Jaribu kutafuta wakati wa kutafakari kwa ukimya. Punguza mkazo zaidi kwa kutazama vitu vya asili.

Urembo Wenye Sumu

Njia ya urembo inayohusisha kudungwa sindano yenye sumu ya kufisha iitwayo botulin sasa inatumiwa kuondoa makunyanzi ya uso, laripoti gazeti la The Toronto Star. Sumu hiyo hufanya misuli hususa ya uso ipooze, na baada ya siku chache hupoteza nguvu, na kuondoa makunyanzi yote. Tiba hiyo hudumu kwa muda wa miezi minne hivi na kumfanya mtu aliyepewa tiba hiyo aonekane kuwa kijana zaidi. Hata hivyo, inaleta hasara. Ripoti hiyo yaonya kwamba “watumizi hupoteza makunyanzi yao, lakini pia hupoteza uwezo wa kuinua nyusi zao wanaposhangaa, kuonyesha tabasamu kwenye uso wote, [na] kukunja kipaji.” Utahitaji kuwa tayari “kufanya sehemu fulani za uso wako zipooze kwa ajili ya uzuri wa ujana,” lasema gazeti hilo.

“Mungu Yuko Upande Gani?”

“Sinuii kudharau itikadi za mtu yeyote,” aandika mwandishi wa habari za michezo Sam Smith, “lakini je, wonyesho huo wa hadharani wa uchaji haujapita kiasi michezoni? Kwa nini wachezaji-kandanda wanasali baada ya kufunga bao?” Wachezaji haohao ambao hujikusanya ili kusali baada ya mechi waweza kuonekana pia “wakilaani maripota” kwenye vyumba vya kubadilishia mavazi au “wakijaribu kuumiza wachezaji” mchezo unapopamba moto, asema Smith. Kufikiri kwamba Mungu hupendelea timu moja kuliko nyingine “ni kudharau itikadi katika Mungu,” asema. Hivyo, makala yake yamalizia: “Tusifanye michezo kuwa ibada ya kidini.”

Kazi Hatari

Ni kazi zipi kumi zilizo hatari zaidi? Kulingana na takwimu zilizokusanywa na shirika la U.S. Bureau of Labor Statistics, wakataji-miti waliongoza katika orodha hiyo kwa vifo 129 kwa kila wafanyakazi 100,000, huku wavuvi na wafanyakazi wa meli wakifuatia kwa ukaribu kwa vifo 123 na 94 kwa kila wafanyakazi 100,000. Orodha hiyo inayoanza na kazi zilizo hatari zaidi hadi zilizo afadhali, yataja kazi nyingine kama za marubani wa ndege, wafanyakazi wa vyuma, wachimba-migodi, vibarua wa kujenga, madereva wa teksi, madereva wa malori, na wafanyakazi wa shambani. Hata hivyo, “hatari ya ujumla inayosababishwa na kujeruhiwa kazini—asilimia 4.7 kwa kila wafanyakazi 100,000—imepungua kwa asilimia 10 hivi” katika miaka mitano iliyopita, laripoti gazeti la Scientific American.

Ndege Wenye Akili!

“Mbayuwayu katika Calcutta hujiepusha na malaria,” laripoti gazeti la Kifaransa la viumbe wa asili Terre Sauvage. Wataalamu wamegundua kwamba kwa sababu ya malaria kuongezeka, sasa mbayuwayu wanaruka mbali zaidi kutafuta majani ya mti unaojulikana kuwa na kwinini nyingi ya asili, ambayo ni dawa ya malaria. Pamoja na kutumia majani hayo kujengea upande wa ndani wa viota vyao, yaonekana ndege hao hula majani hayo. “Mbayuwayu wanaopenda maeneo ya mjini na wanaoogopa malaria, yaonekana wamepata njia ya kujilinda,” lasema gazeti hilo.

Pesa Chafu

Zaidi ya asilimia 99 ya noti za benki ya London zimechafuliwa na kokeini, laripoti gazeti la Guardian. Wataalamu walichunguza noti 500 za benki na kupata kwamba 496 zilikuwa na madoa ya dawa hiyo ya kulevya. Noti hizo huanza kuchafuka zinapokuwa mikononi mwa watumizi wa dawa za kulevya. Kisha noti hizo huchafua pesa nyingine wakati zinapotenganishwa na mashine za benki au zinapohifadhiwa pamoja. Huko Uingereza kokeini imekuwa dawa ya kulevya ya kujifurahisha inayozidi kupendwa na watu wenye umri wa miaka 20 hadi 24. Kwa mujibu wa shirika la London la Youth Awareness Project, matineja hutumia kokeini kwa sababu wanahisi kwamba huwafanya wajulikane zaidi na kuwaongezea nguvu.

“Ambukizo la Damu Lililo la Kawaida Zaidi”

“Angalau Wamarekani milioni 2.7 wana virusi vya Mchochota wa Ini C, jambo linaloufanya uwe ambukizo la damu la kawaida zaidi nchini Marekani,” yasema ripoti ya Shirika la Habari la Associated Press. Mchochota wa Ini C hupitishwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine hasa kwa kufanya ngono au kupitia damu iliyoambukizwa. Wale wanaokabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na maradhi hayo ni watumiaji wa dawa za kulevya zipitishwazo mishipani ambao hutumia sindano zilezile na watu wanaojihusisha na ngono isiyo salama. Hata hivyo, ambukizo hilo laweza kuenezwa na watu wanaochanja na wataalamu wa tiba ya kujitoboa ambao hawasafishi vifaa vyao ifaavyo. Watu ambao wametiwa damu mishipani wamo hatarini pia. Kila mwaka, takriban watu 1,000 hupandikizwa ini nchini Marekani kwa sababu maini yao hukosa kufanya kazi kwa sababu ya virusi hivyo.