Kuzaa Watoto—Je, Humfanya Mtu Awe Mwanamume?
Vijana Huuliza . . .
Kuzaa Watoto—Je, Humfanya Mtu Awe Mwanamume?
“Najua [jamaa] wachache ambao husema, ‘nina binti anayeishi hapa na mwana anayeishi kule,’ na namna wanavyosema, huonyesha kana kwamba hawajali.”—Harold.
KILA mwaka takriban wasichana matineja milioni moja hupata mimba huko Marekani. Watoto wengi wanaozaliwa na mama hao huzaliwa nje ya ndoa. Miongoni mwa mama hao matineja, 1 kati ya 4 ataishia kuwa na mtoto wa pili katika miaka miwili inayofuata. Gazeti la Atlantic Monthly lasema hivi: “Ikiwa mielekeo ya sasa itaendelea, zaidi ya nusu ya watoto wote waliozaliwa leo wataendelea kuishi pamoja na mama na baba zao utotoni. Watoto wengi Wamarekani wataishi kwa miaka kadhaa katika familia zilizo na mama peke yake.”
Ingawa Marekani ina kiwango cha juu zaidi cha matineja wanaopata mimba kuliko nchi nyingine zilizositawi, tatizo la watoto wanaozaliwa nje ya ndoa liko ulimwenguni kote. Katika nchi fulani za Ulaya, kama vile Ufaransa na Uingereza, viwango vya kuzaa nje ya ndoa vyalingana na vya Marekani. Katika nchi fulani za Afrika na Amerika Kusini, kiwango cha kuzaa miongoni mwa matineja ni takriban maradufu ya kile cha Marekani. Ni nini kinachosababisha tatizo hilo?
Kile Ambacho Huchangia Tatizo Hilo
Kwa kiwango kikubwa, hali hii ni tokeo la kuzorota kwa maadili ya “nyakati hatari” tunamoishi. (2 Timotheo 3:1-5) Katika miongo ya karibuni viwango vya talaka vimeongezeka kwa ghafula. Ugoni-jinsia-moja na mitindo ya maisha isiyo ya kawaida imekuwa mamboleo. Vijana wamekuwa shabaha ya propaganda nyingi ya vyombo vya habari—muziki wa kushawishi na vidio za muziki, makala na matangazo ya biashara yanayotisha kwenye magazeti, maonyesho ya televisheni na sinema zinazotukuza ngono ya kihobelahobela. Kupatikana kwa urahisi kwa huduma za kutoa mimba na kupanga uzazi kumechangia pia itikadi iliyoenea sana miongoni mwa vijana kwamba ngono haina madhara yoyote. Baba mmoja asiyefunga ndoa asema: “Nataka nifanye ngono bila kuwa na daraka.” Mwingine asema “ngono hufurahisha na ni mchezo.”
Huenda mitazamo hiyo imeenea sana miongoni mwa vijana maskini. Mtafiti Elijah Anderson alihoji vijana wengi sana wanaoishi kwenye sehemu ya jiji yenye watu wengi na
kusema hivi: “Kwa wavulana wengi, ngono ni ishara muhimu ya hadhi ya kijamii; kufanya ngono huonwa kuwa mafanikio.” Kwa hakika, baba mmoja asiyefunga ndoa aliliambia gazeti Amkeni! kwamba wengi huona kuvutiwa na ngono kuwa kama “vikombe vya ushindi unavyoweza kuweka kwenye rafu.” Ni nini ambacho huchangia mtazamo huo sugu? Anderson aeleza kwamba katika visa vingi watu wa maana zaidi maishani mwa kijana anayeishi kwenye sehemu ya jiji yenye watu wengi “ni marika wake. Wao humwekea viwango vya mwenendo, na linakuwa jambo la maana kwake kuishi kupatana na viwango hivyo.”Kwa hiyo, Anderson asema kwamba wanaume wengi vijana huona kufanya ngono kuwa mchezo tu, “lengo likiwa ni kumfanya yule mwingine aonekane mpumbavu, hasa mwanamke kijana.” Aongezea kwamba “mchezo huo watia ndani namna mvulana anavyojiendesha, kutia ndani mavazi yake, mapambo, sura, uwezo wa kucheza dansi, na maongezi.” Wavulana wengi wachanga wana ustadi wa kushinda “mchezo” huo. Lakini Anderson asema: “Msichana anapopata mimba, mvulana humwacha.”—Young Unwed Fathers—Changing Roles and Emerging Policies, kilichohaririwa na Robert Lerman na Theodora Ooms.
Maoni ya Mungu
Lakini je, kwa kweli kuzaa mtoto humfanya mtu awe mwanamume? Je, ngono ni mchezo tu? Maoni ya Muumba wetu Yehova Mungu ni tofauti. Katika Neno lake Biblia, Mungu huonyesha waziwazi kwamba ngono ina kusudi kuu. Baada ya kusema juu ya uumbaji wa mwanamume na mwanamke wa kwanza, Biblia husema: “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi.” (Mwanzo 1:27, 28) Halikuwa kusudi la Mungu kamwe kwamba watoto waachwe na baba zao. Aliwaunganisha mwanamume na mwanamke wa kwanza katika kifungo cha kudumu cha ndoa. (Mwanzo 2:24) Kwa hiyo kusudi lake lilikuwa kila mtoto awe na baba na mama.
Ingawa hivyo, baada ya muda mfupi, wanaume walianza kujitwalia wake wengi. (Mwanzo 4:19) Mwanzo 6:2 hutuambia kwamba malaika fulani “waliwaona binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri.” Baada ya kujitwalia miili ya kibinadamu, malaika hao ‘walijitwalia wake,’ wakichukua kwa pupa “wote waliowachagua.” (Italiki ni zetu.) Furiko la Noa liliwalazimisha roho waovu hao warejee kwenye makao ya roho. Hata hivyo, Biblia huonyesha kwamba sasa wamezuiliwa kwenye ujirani wa dunia. (Ufunuo 12:9-12) Kwa hiyo Shetani na roho waovu wake hutokeza uvutano mkubwa sana kwa watu leo. (Waefeso 2:2) Wanaume wachanga wanaathiriwa na uvutano huo mwovu wanapozaa watoto wasiotakikana na wasiopendwa.
Hivyo, kwa sababu nzuri Maandiko husema: “Haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kule kutakaswa kwenu, kwamba mjiepushe na uasherati; kwamba kila mmoja wenu apaswe kujua jinsi ya kupata umiliki wa chombo chake mwenyewe katika utakaso na heshima, si katika hamu yenye tamaa ya ngono kama ile waliyo nayo pia mataifa wale wasiomjua Mungu; kwamba yeyote asifikie hatua ya kudhuru na kuziingilia haki za ndugu yake katika jambo hilo, kwa sababu Yehova ndiye atozaye adhabu kwa ajili ya mambo yote haya.”—1 Wathesalonike 4:3-6.
‘Kujiepusha na uasherati’? Huenda wanaume wengi vijana wakadhihaki wazo hilo. Kwa vyovyote vile, wao ni vijana na tamaa zao ni zenye nguvu! Lakini ona kwamba uasherati wahusisha ‘kudhuru na kuingilia haki’ za wengine. Je, si wamdhuru msichana unapomzalisha mtoto bila mume wa kumtegemeza? Na vipi juu ya hatari za kumwambukiza maradhi yanayopitishwa kingono, kama vile ugonjwa wa malengelenge katika viungo vya uzazi, kaswende, kisonono, au UKIMWI? Ni kweli kwamba nyakati nyingine unaweza kuepuka matokeo hayo. Ijapokuwa hivyo, bado ngono kabla ya ndoa huingilia haki za msichana za kudumisha sifa njema na kuanza ndoa akiwa bikira. Hivyo, kujiepusha na uasherati ni jambo la kiakili na linalodhihirisha ukomavu. Ni kweli kwamba wahitaji kujidhibiti na kuazimia ‘kupata umiliki wa chombo chako mwenyewe’ na kujiepusha na ngono kabla ya ndoa. Lakini kama andiko la Isaya 48:17, 18 lituambiavyo, kupitia sheria zake, Mungu ‘anatufundisha ili tupate faida.’
“Endeleeni Kama Wanaume”
Ingawa hivyo, mwanamume kijana anaweza kujithibitishaje kuwa mwanamume halisi? Kwa hakika si kwa kuzaa watoto haramu. Biblia hutuhimiza hivi: “Kaeni macho, simameni imara katika imani, endeleeni kama wanaume, kueni mwe wenye uweza. Acheni mambo yenu yote yatendeke kwa upendo.”—1 Wakorintho 16:13, 14.
Ona kwamba ‘kuendelea kama wanaume’ kwahusisha kuwa macho, imara katika imani, moyo mkuu, na mwenye upendo. Bila shaka, kanuni hizi hutumika kwa uzito uleule kwa wanaume na wanawake. Lakini ukisitawisha sifa za kiroho kama hizi, watu watakuwa na sababu nzuri za kukuheshimu na kuvutiwa nawe kama mwanamume halisi! Na ujifunze somo kutokana na yule mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi—Yesu Kristo. Ebu fikiria tu jinsi alivyojiendesha kiume na kudhihirisha moyo mkuu alipokuwa anakabili mateso na hata kifo. Lakini Yesu alijiendeshaje alipokuwa na watu wa jinsia tofauti?
Kwa hakika Yesu alikuwa na fursa ya kufurahia ushirika wa wanawake. Alikuwa na wafuasi wanawake, ambao baadhi yao ‘walikuwa wakimhudumia [yeye na mitume wake] kutokana na mali zao.’ (Luka 8:3) Alikuwa na uhusiano wa karibu hasa na dada wawili wa Lazaro. Kwa hakika, Biblia husema kwamba “Yesu alimpenda Martha na dada yake.” (Yohana 11:5) Je, Yesu alitumia akili yake, haiba, au sura nzuri, ambayo bila shaka alikuwa nayo akiwa mwanadamu mkamilifu, kushawishi wanawake hao wajihusishe na ukosefu wa adili? Kinyume cha hilo, Biblia husema kuhusu Yesu kwamba “hakufanya dhambi.” (1 Petro 2:22) Hakujiendesha isivyofaa hata wakati mwanamke ambaye alijulikana sana kuwa mtenda-dhambi, labda kahaba, ‘alipotoa machozi na kuanza kulowesha miguu yake kwa machozi naye akawa akiyafuta kwa nywele za kichwa chake.’ (Luka 7:37, 38) Yesu hata hakufikiri kumtumia vibaya mwanamke huyo ambaye angeweza kudhuriwa kwa urahisi! Alidhihirisha uwezo wa kudhibiti hisia zake—ishara ya mwanamume halisi. Alitendea wanawake, si kama vitu vya kutumiwa kwa ajili ya ngono, bali kama watu wanaostahili staha na upendo.
Ikiwa wewe ni mwanamume Mkristo kijana, kufuata kielelezo cha Kristo—wala si cha marika wako—kutakuzuia ‘usidhuru na kuingilia haki’ za mtu fulani. Pia kutakulinda na huzuni kubwa ya kuzaa mtoto haramu. Ni kweli kwamba huenda wengine wakakutania kwa sababu ya kujiepusha na uasherati. Lakini mwishowe, utanufaika kupata kibali cha Mungu badala ya kupata kibali cha muda kutoka kwa marika wako.—Mithali 27:11.
Lakini, vipi ikiwa, kijana aliishi maisha yasiyo na adili zamani lakini tayari ameacha mwenendo wake usio wa adili na kutubu kikweli? Ikiwa ndivyo, kama Mfalme Daudi mwenye toba, aliyejihusisha na mwenendo usiofaa kingono, aweza kuwa na hakika juu ya msamaha wa Mungu. (2 Samweli 11:2-5; 12:13; Zaburi 51:1, 2) Lakini ikiwa mimba imepatikana nje ya ndoa, huenda mwanamume kijana akahitaji kufanya maamuzi mazito. Je, amwoe msichana huyo? Je, ana madaraka yoyote kuelekea mtoto wake? Makala ya wakati ujao itashughulikia maswali hayo.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Vijana wengi hukosea kwa kuamini kwamba ngono haina madhara yoyote