Ulaya Iliyoungana—Kwa Nini Ni Jambo Linalopasa Kufikiriwa?
Ulaya Iliyoungana—Kwa Nini Ni Jambo Linalopasa Kufikiriwa?
VIZIBO vya shampeni viliruka kwa kelele. Fataki zikaangaza anga. Ni nini kilichokuwa kikisherehekewa? Je, ni milenia mpya? La, kwa wazi tukio hili lilikuwa la maana zaidi ya kubadili kalenda kutoka mwaka wa 1999 hadi mwaka wa 2000. Ilikuwa Januari 1, 1999. Fedha mpya ya pamoja ya Muungano wa Ulaya (EU)—fedha inayoitwa euro—ilikuwa imeanzishwa rasmi siku hiyo.
Wazungu wengi wanaona kuanzishwa kwa fedha ya pamoja kuwa hatua ya kihistoria katika jitihada ya muda mrefu ya kuunganisha Ulaya. Gazeti la Uholanzi la De Telegraaf lilisifu kuanzishwa kwa euro kuwa “heshima ya kuunganishwa kwa Ulaya.” Kwa kweli, baada ya miongo mingi ya mradi uliotamaniwa, diplomasia, na kuchelewa, sasa muungano wa Ulaya waelekea kufikiwa kuliko wakati mwingine wowote.
Ni kweli kwamba watu wasioishi Ulaya huenda wakajiuliza ni nini hiki kinachowasisimua watu. Kuanzishwa kwa euro na jitihada za kuunganisha Ulaya huenda zisiathiri kwa vyovyote maisha yao ya kila siku. Hata hivyo, kuunganishwa kwa Ulaya kungetokeza mojawapo ya jumuiya zenye uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi ulimwenguni. Kwa hiyo bila kujali unaishi wapi—hungekosa kutambua Ulaya iliyoungana.
Kwa mfano, hivi karibuni Waziri Msaidizi wa Mashauri ya Nchi za Kigeni wa Marekani Marc Grossman aliwaambia hivi wasikilizaji wa Amerika Kaskazini: “Ufanisi wetu unahusiana na Ulaya.” Kwa nini? Baadhi ya sababu alizotaja ni kwamba “1 kati ya wafanyakazi wa viwandani 12 wa Marekani, hufanya kazi katika mojawapo ya viwanda 4,000 vinavyomilikiwa na Wanaulaya huko Marekani.” Pia inaripotiwa kwamba huenda fedha mpya ya Ulaya ikaathiri bei za bidhaa zinazoingizwa nchini—na hata viwango vya rehani—katika nchi zilizo mbali na Ulaya.
Huenda nchi zinazositawi zikanufaika. Jinsi gani? Uchunguzi mmoja wasema hivi: “Kuondolewa kwa fedha mbalimbali za Ulaya na kuwepo kwa euro kutarahisisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi zinazositawi na EU.” Kwa kuongezea, watu fulani wanatabiri kwamba mashirika ya biashara ya Japani na Marekani yanayofanya biashara Ulaya yatanufaika. Baada ya euro kuimarika, hakutakuwa na kubadilika-badilika kwa viwango vya ubadilishaji wa fedha kati ya nchi za Ulaya. Huenda kukawa na faida kubwa kufanya biashara Ulaya.
Ikiwa unapanga kusafiri Ulaya, huenda vilevile ukaona manufaa ya kuunganishwa kwa Ulaya. Karibuni utaweza kununua bidhaa katika nchi tofauti-tofauti za Ulaya kwa kutumia fedha ileile, euro, ambayo thamani yake inakaribia dola ya Marekani. Watalii hawatatatanika tena kushughulika na gulden, faranga, lira, maki, na mashine za mfukoni za kupigia hesabu.
Hata hivyo, jitihada za Ulaya za kuwa na bara lililoungana hutokeza jambo fulani lenye kuvutia hata zaidi—tumaini. Ebu fikiria, miongo michache tu iliyopita Ulaya ilikuwa imekumbwa na vita vingi sana. Kwa kufikiria maoni hayo, kuunganishwa kwa Ulaya ni tukio la kushangaza. Watu wanatambua jambo hilo ulimwenguni pote.
Wengi wanajiuliza ikiwa muungano wa ulimwenguni pote waweza kupatikana kwa vyovyote vile. Kwa kweli hili ni tazamio lenye kutamanisha bure! Je, hatua za Ulaya za kuungana zitafanya wanadamu wakaribie kuwa na ulimwengu ulioungana? Kabla ya kushughulikia suala hilo, twahitaji kuchunguza waziwazi kuungana kwa Ulaya. Ni vizuizi gani vinavyozuia muungano huo ambavyo bado vyahitaji kuondolewa?
[Sanduku/Chati katika ukurasa wa 4]
JE, MUUNGANO UNAFANYIZWA?
Wazo la muungano wa Ulaya si jipya kabisa. Kulikuwa na muungano wa kadiri fulani wakati wa Milki ya Roma, iliyokuwa ikitawaliwa na Charlemagne, kisha baadaye na Napoléon wa Kwanza. Katika visa hivyo, muungano ulitegemea nguvu na ushindi. Hata hivyo, baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, nchi nyingi zilizokumbwa na vita ziliona uhitaji wa muungano unaotegemea ushirikiano. Nchi hizi zilitumaini kwamba ushirikiano huo ungezisaidia zijiimarishe kiuchumi tena na pia kupiga vita marufuku. Zifuatazo ni hatua za kihistoria zilizoongoza kwenye hali ya kisasa:
• 1948 Mamia ya viongozi wa kisiasa wa Ulaya wakutana pamoja Hague, Uholanzi, na kuweka nadhiri kwamba: “Hatutawahi kupigana tena sisi kwa sisi.”
• 1950 Ufaransa na Ujerumani zaanza kushirikiana ili kulinda viwanda vyao vya makaa-mawe na feleji. Nchi nyingine zajiunga nao na kuongoza kwenye kubuniwa kwa Jumuiya ya Ulaya ya Makaa-Mawe na Feleji (ECSC). Jumuiya ya ECSC yaanza kufanya kazi mwaka wa 1952 na yatia ndani Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Luxembourg, Uholanzi, na Ujerumani Magharibi.
• 1957 Wanachama sita wa ECSC waanzisha mashirika mengine mawili: Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya (EEC) na Jumuiya ya Nguvu za Atomi ya Ulaya (Euratom).
• 1967 EEC yaungana na ECSC na Euratom kufanyiza Jumuiya ya Ulaya, (EC).
• 1973 Denmark, Ireland na Uingereza zajiunga na EC.
• 1981 Ugiriki yajiunga na EC.
• 1986 Hispania na Ureno zajiunga na EC.
• 1990 EC yapanuka hata zaidi wakati Ujerumani Magharibi na Mashariki ziunganapo, na kuingiza ile iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwenye shirika hilo.
• 1993 Jitihada kubwa zaidi za kiuchumi na kisiasa za washiriki wa EC zaongoza kwenye kubuniwa kwa Muungano wa Ulaya, (EU).
• 2000 EU yatia ndani nchi wanachama 15—Austria, Denmark, Finland, Hispania, Ireland, Italia, Luxembourg, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, na Ureno.
[Picha katika ukurasa wa 1]
Euro itachukua mahali pa fedha nyingi za Ulaya
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Euro na ishara za euro kwenye ukurasa wa 3, 5-6, na 8: © European Monetary Institute