Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Historia Yenye Kuvutia ya “Nchi Iliyo na Utofautiano”

Historia Yenye Kuvutia ya “Nchi Iliyo na Utofautiano”

Historia Yenye Kuvutia ya “Nchi Iliyo na Utofautiano”

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI

IMEITWA “nchi iliyo na utofautiano”—kwa sababu nzuri. Ingawa Brazili ni nchi ya kitropiki hasa, tabia yake ya nchi hukaribia kuwa ya kitropiki upande wa kusini na hukaribia kuwa ya ikweta kwenye eneo la Amazon. Pia historia ya Brazili imejaa mambo yenye utofautiano. Kwa miaka mingi, nchi hiyo kubwa—yenye eneo la kilometa mraba 8,511,999 na pwani ya kilometa 7,400—imekuwa makao ya watu wenye tamaduni tofauti-tofauti.

Wareno walipofika Brazili miaka 500 iliyopita sifa waliyogundua kwanza ilikuwa ya ukarimu. Kwa kweli, alipokuwa akimwandikia Mfalme wa Ureno Manuel wa Kwanza mwaka wa 1500, Pero Vaz de Caminha alieleza wenyeji wa Brazili wakichangamana kwa uhuru na wageni wao Wareno na kuwakumbatia. Lakini Wareno walikuwa wakifanya nini huko Brazili?

Katika Machi 9, 1500, Pedro Álvares Cabral aling’oa nanga kutoka Ureno akiwa na msafara wa meli. Alinuia kuanzisha kituo cha biashara katika Calicut, India. Hata hivyo, kabla ya kufika mwisho wa safari yake, Cabral alifika kwenye pwani ambayo sasa ni jimbo la Brazili la Bahia. Ilikuwa Aprili 23, 1500.

Watafiti fulani husema kwamba tayari Wareno walijua kwamba Wabrazili walikuwepo na kwamba Cabral hakusimama hapo kwa nasibu. * Kwa vyovyote vile, ilionekana kwamba bidhaa pekee ambayo Wabrazili wangelazimika kutoa ilikuwa brazilwood, mti unaotoa rangi nyekundu. Ingawa mti huo kwa wazi ulikuwa na manufaa, vikolezo vya India vilikuwa na thamani zaidi.

Kwa hiyo, kwa miaka kumi Ureno ilikodisha Brazili kwa Fernando de Noronha wa Ureno, aliyekusanya brazilwood na kulipa Serikali ya Ureno kodi. Lakini nchi nyingine za Ulaya zilitaka pia kupanua biashara yao na Mabara Mapya, na Naronha hakuwa na uwezo wa kuzuia biashara haramu iliyokuwa ikiongezeka iliyofanywa na mabaharia Wafaransa, Waingereza, na Wahispania. Wakihofu kwamba huenda wakapoteza Brazili, Wareno walianzisha ukoloni mwaka wa 1532. Uzalishaji Sukari ukawa biashara ya kwanza inayoletea Brazili faida.

Kuchimba dhahabu na almasi kukawa biashara yenye kusitawi katika karne ya 18. Mwanzoni mwa karne ya 19, utomvu kutoka kwenye mpira ulikuwa biashara muhimu katika eneo la Amazon. * Baadaye, kilimo cha kahawa kilichangia kusitawisha miji ya Brazili, kutegemeza kifedha ujenzi wa reli na kufanya bandari za Santos na Rio de Janeiro ziwe za kisasa. Mwishoni mwa karne ya 19, nusu ya kahawa inayokuzwa ulimwenguni ilikuwa ikivunwa Brazili, nao mji wa São Paulo ulikuwa kituo kikuu cha biashara cha Brazili.

Kwa kusikitisha, historia ya Brazili ilitia ndani utumwa. Hapo kwanza, masetla Wareno walitumia Wahindi kukata na kusafirisha brazilwood. Baadaye, Wahindi walipelekwa kufanya kazi kwenye mashamba ya miwa. Kwa kusikitisha, idadi kubwa ya wazaliwa wa Brazili walishikwa na magonjwa ya Ulaya na kufa. Ureno ilileta watumwa kutoka Afrika ili kuchukua mahali pa wafanyakazi hao.

Kwa miaka mingi mamilioni ya Waafrika walipelekwa Brazili wakiwa watumwa, nao wakaja na urithi wao wa kitamaduni na kinasaba. Uvutano huo waweza kuonekana katika muziki unaopendwa kama vile samba na “capoeira” (namna ya kupigana) na vilevile katika vyakula kama vile feijoada, kinachopikwa kwa maharagwe meusi na nyama ya nguruwe, soseji, na nyama iliyokaushwa juani. Hatimaye, mwaka wa 1888, utumwa ulipigwa marufuku nchini Brazili. Takriban watu 750,000—ambao wengi wao walifanya kazi mashambani—waliachiliwa huru.

Kuanzia karne ya 19 na kuendelea, mamilioni ya wageni walimiminika Brazili, kutia ndani Wahispania, Waitalia, Wajerumani, na Wapoland na vilevile wale walio na nasaba ya Switzerland, Siria na Lebanoni. Brazili ni mahali pazuri pa kuishi. Ina mimea na wanyama wengi sana. Kwa kawaida, Brazili haipatwi na misiba ya asili. Hakuna vita, matetemeko ya dunia, volkeno, vimbunga, au mawimbi yenye nguvu. Kwa hiyo, mbona usiifahamu Brazili kwa kuzuru baadhi ya sehemu zake zenye kuvutia zinazojulikana? Utafurahia ukarimu uleule na uzuri wa asili uliowavutia Wareno miaka 500 iliyopita.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Wareno na Wahispania walipotia sahihi Mkataba wa Tordesillas mwaka wa 1494, waligawanya nchi hiyo kuelekea magharibi ya Atlantiki Kusini. Kwa hiyo, wengine husema kwamba Cabral alifunga safari ili kutwaa nchi ambayo tayari ilikuwa ya Ureno.

^ fu. 8 Ona Amkeni!, Mei 22, 1997, ukurasa wa 14-17.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

ENEO LA AMAZON

JIMBO LA BAHIA

Brasília

Rio de Janeiro

São Paulo

Santos

Maporomoko ya Iguaçú

[Picha]

1. Pedro Álvares Cabral

2. Mkataba wa Tordesillas, 1494

3. Wabebaji kahawa

4. Maporomoko ya Iguaçú, kama yaonekanavyo kutoka upande wa Brazili

5. Mhindi wa Ipixuna

[Hisani]

Culver Pictures

Courtesy of Archivo General de Indias, Sevilla, Spain

From the book Brazil and the Brazilians, 1857

FOTO: MOURA

[Picha katika ukurasa wa 18]

1. Kuna puma wengi Brazili

2. Okidi katika msitu wa Amazon

3. Vazi la kitamaduni la Salvador, Bahia

4. Kasuku

5. Ufuo wa Copacabana, Rio de Janeiro. Brazili ina pwani maridadi yenye urefu wa kilometa zaidi ya 7,000

[Hisani]

Courtesy Sáo Paulo Zoo

[Picha katika ukurasa wa 19]

Brasília—jiji kuu la Brazili tangu 1960

[Picha katika kurasa za 19]

São Paulo—kituo cha biashara cha Brazili

[Hisani]

FOTO: MOURA

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

© 1996 Visual Language