Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wewe Huathiriwa na Laktosi?

Je, Wewe Huathiriwa na Laktosi?

Je, Wewe Huathiriwa na Laktosi?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO

“Mimi na mume wangu tulikuwa tumewatembelea marafiki fulani katika jimbo la Puebla, nchini Mexico. Wenyeji wetu walikuwa na ng’ombe, kwa hiyo walitupa maziwa pamoja na kifungua-kinywa na chakula cha jioni.

“Tulihisi vibaya usiku wa kwanza, lakini siku ya pili hali ikawa mbaya hata zaidi. Tumbo langu lilivimba sana hivi kwamba nilionekana kana kwamba nina mimba ya miezi kadhaa. Kisha sote wawili tukaanza kuharisha sana.

“Baada ya miaka mingi kupita tuligundua kwamba tunaathiriwa na laktosi.”—Bertha.

KISA cha Bertha si cha kipekee, kwa kuwa watu fulani hukadiria kwamba kadiri ya asilimia 75 ya watu wazima ulimwenguni pote huenda wakaathiriwa na dalili kadhaa au dalili zote za laktosi. * Hali hiyo ni nini, nayo husababishwa na nini? Zaidi ya yote, ni nini kinachoweza kufanywa ili kukabiliana nayo?

Maneno “athari za laktosi” yarejezea kushindwa kwa mwili kumeng’enya laktosi, sukari yenye nguvu iliyo katika maziwa. Ili iweze kufyonzwa kwenye mfumo wa damu, lazima laktosi iyeyushwe na kuwa glukosi na galaktosi. Ili jambo hilo liwezekane, kimeng’enya kinachoitwa laktati chahitajiwa. Tatizo ni kwamba mwili hutokeza laktati kidogo zaidi kadiri tunavyoendelea kukua. Kwa kukosa laktati, watu wazima wengi huathiriwa na laktosi.

Mtu anapokula laktosi nyingi—kutoka kwa maziwa na bidhaa zinazotokana nayo—na kushindwa kuimeng’enya, bakteria kwenye utumbo mkubwa huigeuza kuwa asidi maziwa na kaboni dioksidi. Kwa muda mfupi wa dakika 30 hivi, dalili halisi hutokea, kutia ndani kichefuchefu, kubana kwa misuli, kuvimba, na kuharisha. Watu fulani wasiojua kwamba huathiriwa na laktosi huenda wakajaribu kutuliza tumbo kwa kunywa maziwa zaidi, na hivyo kuzidisha tatizo hilo.

Kiwango cha kustahimili athari za laktosi hutofautiana kwa watu mbalimbali. Watu fulani waweza kunywa glasi ya maziwa bila kupatwa na athari mbaya. Kwa wengine, hata kiasi hiki kidogo kitatokeza matatizo. Wengine hudokeza kwamba ili kujua ni kiasi gani unachoweza kustahimili, wapaswa kuanza kwa kiasi kidogo cha maziwa. Kisha uongeze kiasi hicho hatua kwa hatua katika pindi zinazofuata. Kwa habari hii, kumbuka kwamba ingawa dalili za athari za laktosi humfanya mtu akose kustarehe, huwa hatari kwa nadra sana.

Cha Kuliwa na cha Kuepukwa

Ikiwa wewe huathiriwa na laktosi, unapaswa kuamua unachoweza kula na usichoweza. Mengi yatategemea kiwango unachoweza kustahimili. Vyakula vyenye laktosi vyatia ndani maziwa, aiskrimu, mtindi, siagi, na jibini. Vyakula vingine vilivyotayarishwa, kama vile keki, chakula cha nafaka, na viungo vya saladi vyaweza kuwa na laktosi pia. Kwa hiyo, watu wanaoathiriwa na laktosi wapaswa kuangalia kibandiko cha lishe kwenye bidhaa hizo.

Bila shaka, maziwa ndiyo chanzo kikuu cha kalisi, na mtu anapokosa kula kalisi ya kutosha aweza kushikwa na ugonjwa wa mifupa. Hivyo, watu wanaoathiriwa na laktosi wapaswa kutafuta vyakula vingine vyenye kalisi. Mboga zilizotolewa shambani, kama vile brokoli, kabichi, na mchicha huwa na kalisi. Lozi, ufuta, na samaki wenye mifupa laini, kama vile sadini na salmoni vina kalisi pia.

Hata ikiwa unaathiriwa na laktosi, huenda isiwe lazima kuepuka kabisa maziwa na bidhaa zinazotengenezwa kwa maziwa. Badala yake, jaribu kujua ni kiasi gani unachoweza kustahimili, kisha usizidishe kiasi hicho. Inapowekezana, kula vyakula vingine pamoja na bidhaa zozote zenye laktosi. Pia, kumbuka kwamba jibini iliyokaa sana huwa na laktosi kidogo, na huenda isisababishe matatizo. Namna gani mtindi? Una kiwango cha laktosi kinachokaribia cha maziwa, lakini watu fulani wanaoathiriwa na laktosi wanaweza kuumeng’enya kwa urahisi. Kwa nini? Kwa sababu mtindi una vijiumbe ambavyo husanisi laktati, na hilo husaidia kumeng’enya laktosi.

Kwa hiyo, ikiwa unaathiriwa na laktosi, usifanye wasiwasi. Kama tulivyoona, unapoujua ugonjwa huu utaweza kuudhibiti kwa urahisi. Lakini kumbuka mambo yafuatayo:

(1) Tumia kiasi kidogo cha maziwa na bidhaa zinazotengenezwa kwa maziwa, pamoja na vyakula vingine, ili ujue ni kiasi gani unachoweza kustahimili.

(2) Kunywa mtindi na kula jibini iliyokaa, ambavyo kwa kawaida humeng’enywa kwa urahisi.

(3) Tumia bidhaa zozote zinazopatikana zisizo na laktosi au zilizo na laktati.

Kwa kufuata madokezo hayo, unaweza kukabiliana na athari za laktosi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Waasia huathiriwa zaidi na laktosi kuliko kikundi kingine chochote. Watu wa nasaba ya kaskazini mwa Ulaya hawaathiriwi sana.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26, 27]

Kupambanua Athari za Laktosi

Njia kadhaa hutumiwa kugundua athari za laktosi.

Majaribio ya kustahimili laktosi: Baada ya kufunga kula, mgonjwa hunywa umajimaji wenye laktosi. Sampuli za damu hupimwa ili kujua jinsi laktosi inavyomeng’enywa.

Jaribio la pumzi la hidrojeni: Laktosi ambayo haijameng’enywa hutokeza gesi mbalimbali, kutia ndani hidrojeni. Hizo hupita kutoka kwenye utumbo na kuingia kwenye mfumo wa damu kisha kwenye mapafu, na mwishowe hutolewa nje.

Majaribio ya kupima asidi kwenye kinyesi: Laktosi ambayo haijameng’enywa ndani ya utumbo mkubwa hutokeza asidi zinazoweza kugunduliwa kwenye kinyesi kinachopimwa.

Kwa kawaida upimaji huo hufanyiwa wagonjwa wanaotibiwa na kurudi nyumbani.