Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kukadiria Umashuhuri kwa Kutegemea Vitabu

“Ikiwa umashuhuri ungetegemea kitabu kilichoandikwa kukuhusu, . . . Yesu Kristo bado ndiye mtu mashuhuri zaidi katika ulimwengu wa kisasa,” lasema gazeti la Uingereza The Guardian. Utafiti kuhusu vitabu vilivyo katika Maktaba ya Congress, huko Washington, D.C., ulionyesha kuna vitabu 17,239 kuhusu Yesu. Vitabu hivyo ni karibu maradufu ya vile vilivyoandikwa kuhusu William Shakespeare, aliyechukua nafasi ya pili kwa vitabu 9,801. Vladimir Lenin alichukua nafasi ya tatu kwa vitabu 4,492, akifuatwa na Abraham Lincoln, aliyekuwa na vitabu 4,378 vilivyoandikwa kumhusu, na Napoléon wa Kwanza akiwa na vitabu 4,007. Maria, mama ya Yesu, alichukua nafasi ya saba, akiwa na vitabu 3,595, naye ndiye mwanamke pekee aliyekuwa katika mojawapo ya nafasi za kwanza 30. Joan wa Arc, mwanamke aliyemfuata kwa ukaribu, alikuwa na vitabu 545 vilivyoandikwa kumhusu. Kuhusu waimbaji, Richard Wagner ndiye aliyeongoza, akifuatwa na Mozart, Beethoven, na Bach. Picasso ndiye wa kwanza kwa wachoraji, na amewashinda Leonardo da Vinci na Michelangelo. Hata hivyo, Leonardo ndiye anayeongoza miongoni mwa wanasayansi na wavumbuzi, akimshinda Charles Darwin, Albert Einstein, na Galileo Galilei. “Hakuna mtu aliye hai ambaye anashikilia mojawapo ya nafasi za kwanza 30,” lasema gazeti The Guardian.

Je, Paradiso Imepotezwa?

Katika mkutano maalumu wa Baraza la Umoja wa Mataifa, mataifa madogo 43 ya visiwani yalitangaza wasiwasi wao kuhusu vitisho dhidi ya mazingira, laripoti gazeti la Ufaransa Le Monde. Vingi vya visiwa hivi vya kiparadiso vinazidi kukumbwa na vimbunga, tufani, mafuriko, na ukosefu wa maji. Kwa mujibu wa ripoti moja ya habari ya UM, inakadiriwa kwamba Kimbunga Mitch kilisababisha vifo vipatavyo 11,000 katika Karibea. Shelisheli na Mauritius zimekumbwa na ukame mkubwa sana katika miaka miwili iliyopita. Halijoto za kiwango cha juu na uchafuzi vinafanya matumbawe yawe meupe, na kupunguza viumbe mbalimbali. Wakazi wa visiwani pia wanahofu athari za kupanda kwa viwango vya bahari kutokana na ongezeko la joto la ulimwenguni pote. Inakadiriwa kwamba asilimia 80 ya visiwa vyenye matumbawe katika Maldives vingeweza kutoweka baharini.

Ulingano Kati ya Madereva Wenye Usingizi na Madereva Walevi

“Kutolala vya kutosha kwaweza kuwa na matokeo sawa na kunywa kupita kiasi,” lasema gazeti The New York Times. Uchunguzi katika Chuo Kikuu cha Stanford ulichunguza muda wa itikio la mwili kwa watu 113 wanaokosa hewa ya kutosha wanapolala—hali ambayo huvuruga usingizi usiku na kusababisha usingizi mchana—la kikundi chenye kudhibiti usingizi cha wajitoleaji 80. Baada ya muda wa itikio la mwili kujulikana, kikundi cha pili walianza kunywa kileo chenye nguvu asilimia 80. “Katika majaribio matatu kati ya saba ya muda wa itikio la mwili, watu waliojulikana kuwa hukosa hewa ya kutosha wanapolala walikuwa na itikio la muda mrefu kuliko wale ambao kiwango cha kileo katika damu kilikuwa asilimia [0.8], na kuwafanya wawe walevi hivi kwamba hawangeweza kuendesha gari katika majimbo 16,” likaripoti gazeti Times. Kulingana na Dakt. Nelson B. Powell kiongozi wa utafiti huo, matokeo hayo yakazia hatari za kuendesha gari unapokuwa na usingizi.

Karibu Thuluthi ya Watu Ulimwenguni Wameambukizwa Kifua Kikuu

Karibu thuluthi ya watu ulimwenguni—watu bilioni 1.86—waliambukizwa kifua kikuu mwaka wa 1997, chasema kikundi cha wataalamu wa afya 86 kutoka mataifa zaidi ya 40. Kikundi hicho, kilichoteuliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, pia kilikadiria kwamba watu milioni 1.87 walikufa kwa maradhi hayo mwaka huo, huku kukiwa na visa vipya vya maambukizo milioni 7.96. Uchunguzi huo uliochapishwa katika The Journal of American Medical Association ulisema kwamba “asilimia themanini ya visa vyote vya kifua kikuu vilikuwa katika nchi 22, huku zaidi ya nusu ya visa vyote vikitukia katika nchi 5 za Kusini-Mashariki ya Asia.” Kulingana na uchunguzi huo, “nchi tisa kati ya 10 zenye viwango vya juu zaidi kwa kila mtu zilikuwa Afrika.” Katika nchi fulani zenye viwango vya juu vya maambukizo ya HIV, vifo vilizidi asilimia 50. Kifua kikuu kinazidi kuongezeka kwa sababu ya “udhibiti mbaya” wa maradhi hayo katika nchi hizo. Waandishi wa uchunguzi huo wanatabiri kwamba kutakuwa na visa vipya vya kifua kikuu milioni 8.4 mwaka huu. Wengi wa wale wanaoambukizwa hawaugui ugonjwa huo. Hata hivyo, bakteria iliyo bwete, inaweza kuanza kutenda mgonjwa anapopatwa na utapiamlo au mfumo wa kinga unapodhoofika, yasema ripoti hiyo.

Watoto Wanaovuta Moshi wa Sigareti

“Karibu nusu ya watoto ulimwenguni huishi na mvutaji-sigareti,” chasema kichapo University of California Berkeley Wellness Letter, kikieleza kuhusu ripoti ya karibuni kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni. “Ni zaidi ya watoto milioni 700.” Kwa kuwa idadi ya watu wazima wanaovuta sigareti inatarajiwa kuongezeka na kufikia bilioni 1.6 katika miaka 20 ijayo, watoto wengi zaidi watalazimika kuvuta moshi wa sigareti unaotoka kwa wavutaji. Watoto hao wako katika hatari kubwa ya kupatwa na matatizo ya afya kama vile maambukizo ya sikio na magonjwa ya kupumua.

Kitabu Kinachouzwa Zaidi, Wasomaji Wachache

“Ndicho kitabu kinachouzwa zaidi katika historia ya sayari hii,” lasema gazeti Star-Telegram la Fort Worth, Texas. “Ikionwa kuwa sanamu ya kitamaduni na kiwango cha kiroho, Biblia hustahiwa na dini tatu kubwa ulimwenguni zenye mabilioni ya waumini. Uhakika wa kwamba Biblia hustahiwa na mabilioni ya watu na kusomwa na watu wachache sana unashangaza hivi kwamba hata ingekuwa vigumu kwa mfalme Solomoni mwenye hekima kueleza jambo hilo.” Hata hivyo, mauzo ya Biblia yanavunja rekodi mpya, na Wamarekani wengi—zaidi ya asilimia 90—wanasemekana kuwa wana tafsiri tatu kwa wastani, kulingana na shirika fulani la utafiti. Hata hivyo, uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba thuluthi mbili za watu hao hawasomi Biblia kwa ukawaida. Wengi wao hawawezi hata kutaja zile Gospeli nne au kutaja amri tano kati ya Amri Kumi. “Na wengi wao wanasema kwamba huiona Biblia kuwa haiwahusu,” lasema gazeti hilo.

Nyimbo za Dini kwa Ajili ya Milenia

Waingereza ambao huenda kanisani “hivi karibuni watakuwa wakiimba nyimbo za soka wakati wa ibada” iwapo wataamua kutumia kitabu kipya cha ibada Songs for the New Millennium, laripoti gazeti The Times la London. Kitabu hiki ambacho kimechapishwa kwa ushirikiano wa Kanisa la Anglikana na kanisa la Methodisti, kina nyimbo fulani zinazoelekezwa kwa “mpendwa mama Mungu.” Mmojawapo huomba “upendo wa mama” na kumrejezea Mungu kuwa wa jinsia ya kike katika sehemu zote. Katika wimbo mwingine, Yesu anaonyeshwa akiwa “mchezaji-meneja” wa timu ya soka, na korasi yake ni wimbo wa soka unaojulikana sana. Baadhi ya nyimbo hizo zinatoka kwa watoto, kutia ndani kikundi cha mayatima ambao wazazi wao walikufa kwa UKIMWI. Dave Hardman, mmojawapo wa wadhamini wa mradi huo, alisema: “Ni kitabu cha nyimbo kinachotia ndani mapokeo yote. Tulitaka waandishi wa nyimbo wakabiliane na uhalisi wa maisha kupitia imani.”

Je, Kumekuwa na Maiti Nyingi Sana Zilizotiwa Dawa ya Kuzihifadhi?

Tatizo la Misri ni la kipekee—ina vitu vingi sana vya kale. Ugunduzi mpya hutangazwa daima: kaburi lililorembwa la mtunzaji wa Tutankhamen huko Saqqâra, jiwe kuu la piramidi huko Dahshûr, eneo kubwa sana la hekalu huko Akhmīm, jengo kubwa sana la mazishi lililo chini ya ardhi lenye vyumba zaidi ya 200 huko Luxor, sanamu za kuchongwa na vitu vingine vilivyotengenezwa kwa mkono kutoka bandari na majumba ya wafalme yaliyozama karibu na Alexandria, tukitaja vichache. Jumba la Makumbusho la Misri huko Cairo lina zaidi ya vitu vya kale 120,000 vinavyoonyeshwa na vingine zaidi vimewekwa katika bohari. “Kila juma kunakuwa na ugunduzi mpya wenye kusisimua, ukitokeza msongo zaidi kwenye mabohari yaliyojaa, na vilevile kwa wakati na fedha za wale wanaochanganua, kuorodhesha na kuhifadhi vitu vya kale,” lasema gazeti The Economist. Kugunduliwa kwa eneo la makaburi lililo jangwani linaloweza kuwa na makaburi 10,000 kulimfanya mwakiolojia mmoja aseme: “Hatuhitaji tena maiti zilizotiwa dawa ya kuzihifadhi.” Ni chache tu kati ya zile zenye kutokeza zitakazowekwa kwenye maonyesho. Nyingine zitazikwa tena.

Mitego ya Kufisha

Angola ndiyo nchi yenye mabomu ya ardhini mengi zaidi ulimwenguni. Lakini watu wanaojaribu kutegua mabomu ya ardhini wanakabili tatizo jipya: mitego iliyoelekezwa dhidi yao. Kulingana na The Sunday Times la London, “wataalamu wa kutegua mabomu wamegundua aina mbili za swichi zilizo kwenye mabomu ya ardhini. Mojawapo hufanya yalipuke yanapopata mwangaza na hutegemea nishati ya betri zinazodumu kwa miezi 12. Ile nyingine ina koili yenye sumaku iliyobuniwa kutokeza mlipuko wakati kifaa cha kuondoa mabomu ya ardhini kinapoikaribia,” ambacho chaweza kuwa umbali wa meta 20. “Yaani, hili ni ‘bomu la ardhini lililoelekezwa kwa watu wanaotegua mabomu ya ardhini,’” akasema Tim Carstairs wa Kikundi cha Washauri wa Mabomu ya Ardhini. “Limekusudiwa kuua hasa watu kama vile wajitoleaji wetu wanaojaribu kusaidia jumuiya kwa kuondoa mabomu ya ardhini.” Sasa Angola ina watu wanaokadiriwa kuwa 70,000 waliokatwa viungo na mabomu ya ardhini—idadi kubwa zaidi ulimwenguni—na madaktari huwakata viungo watu 35 kwa wastani kila mwezi. Kadiri mabomu ya ardhini yanavyozidi kutegwa na vikundi vinavyopigana katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Angola, wakulima huacha mashamba yao na miji hukosa vyakula. Katibu-Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan aonya kwamba “mamia ya maelfu ya raia wa Angola wanakabili utapiamlo mbaya sana, maradhi na kifo.”