Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mabomu ya Ardhini—Kuchunguza Athari Zake

Mabomu ya Ardhini—Kuchunguza Athari Zake

Mabomu ya Ardhini​Kuchunguza Athari Zake

Katika Desemba 26, 1993, Augusto mwenye umri wa miaka sita alikuwa akitembea katika sehemu iliyo wazi karibu na Luanda, mji mkuu wa Angola. Kwa ghafula aliona kitu chenye kung’aa ardhini. Kilimvutia sana, akaamua kukiokota. Bomu hilo la ardhini lililipuka alipoligusa.

Ilibidi Augusto akatwe mguu wake wa kulia kwa sababu ya mlipuko huo. Sasa akiwa na umri wa miaka 12, anatembea kwa kiti cha magurudumu, naye ni kipofu.

AUGUSTO alilemazwa na bomu la ardhini linalokusudiwa kujeruhi watu, kwa sababu lengo lake ni watu wala si vifaru au magari mengine ya vita. Inakadiriwa kwamba kufikia sasa, zaidi ya aina 350 za mabomu ya ardhini yanayokusudiwa kujeruhi watu yametengenezwa angalau katika nchi 50. Mengi yake yamekusudiwa kujeruhi pasipo kuua. Kwa nini? Kwa sababu wanajeshi waliojeruhiwa huhitaji msaada, na mwanajeshi aliyejeruhiwa hupunguza utendaji wa kijeshi—fursa nzuri kwa maadui. Isitoshe, kilio cha kuomba msaada cha mwanajeshi aliyejeruhiwa chaweza kuwatia woga wanajeshi wenzake. Hivyo, kwa kawaida wahasiriwa wanapoponea chupuchupu ndipo mabomu ya ardhini yaonwapo kuwa na matokeo sana.

Hata hivyo, kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, wahasiriwa wengi wa mabomu ya ardhini huwa raia, si wanajeshi. Haitukii tu kwa nasibu sikuzote. Kulingana na kitabu Landmines—A Deadly Legacy, baadhi ya mabomu ya ardhini “hutegwa kimakusudi ili kuwafukuza raia kutoka kwenye maeneo, kuharibu maeneo yanayotoa chakula, kutokeza wakimbizi, au kueneza hofu tu.”

Kwa mfano, katika pambano moja huko Kambodia, mabomu ya ardhini yalitegwa kuzunguka vijiji vya maadui, kisha vijiji hivyo vikashambuliwa kwa mizinga. Raia walipojaribu kutoroka waliingia moja kwa moja katika maeneo yenye mabomu yaliyotegwa ardhini. Wakati huohuo, wanamgambo wa Khmer Rouge walitega mabomu katika mashamba ya mpunga huku wakijaribu kuilazimisha serikali ikubali majadiliano, hatua hiyo iliwatia hofu kubwa wakulima na kukomesha kilimo.

Jambo lililotukia Somalia mwaka wa 1988 huenda lilikuwa bovu zaidi. Mji wa Hargeysa ulipolipuliwa kwa mabomu, wakazi walilazimika kukimbia. Kisha wanajeshi wakatega mabomu ya ardhini katika nyumba zilizoachwa. Wakimbizi waliporejea baada ya mapigano kukoma, walilemazwa au kuuawa na mabomu yaliyofichwa.

Mbali na kuua na kulipua viungo vya mwili, mabomu ya ardhini hutokeza madhara zaidi. Fikiria baadhi ya athari nyingine za silaha hizi hatari.

Athari za Kiuchumi na Kijamii

Katibu-mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan asema hivi: “Kuwapo—au hata hofu ya kuwapo kwa bomu moja la ardhini kwaweza kuzuia shamba zima lisilimwe, kusababisha njaa kijijini, kuzuia kujenga upya na maendeleo nchini.” Hivyo, katika Afghanistan na Kambodia, zaidi ya asilimia 35 hivi ya ardhi ingelimwa endapo wakulima hawangehofu kukanyaga udongo. Baadhi yao hujihatarisha. “Naogopa sana mabomu ya ardhini,” asema mkulima mmoja wa Kambodia. “Lakini nisipoenda kufyeka nyasi na mianzi, tutakufa.”

Mara nyingi, manusura wa mabomu ya ardhini hulipia gharama kubwa sana. Kwa mfano, katika nchi inayositawi, mtoto anayepoteza mguu akiwa na umri wa miaka kumi huenda akahitaji viungo bandia 15 hivi maishani mwake, kila kiungo kikigharimu dola 125 za Marekani kwa wastani. Ni kweli kwamba huenda wengine wanaweza kumudu gharama hizo. Lakini kwa wakazi wengi wa Angola, dola 125 za Marekani ni mshahara wa zaidi ya miezi mitatu!

Fikiria pia athari mbaya za kijamii. Kwa mfano, raia wa nchi moja ya Asia huepuka kushirikiana na watu waliokatwa viungo, kwa sababu ya kuhofia “bahati mbaya.” Mtu aliyekatwa kiungo cha mwili aweza kukosa tumaini la kufunga ndoa. “Mimi sipangi kuoa,” asikitika mwanamume mmoja wa Angola ambaye alikatwa mguu baada ya kujeruhiwa na mlipuko wa bomu la ardhini. “Mwanamke hutaka mwanamume anayeweza kufanya kazi.”

Kwa wazi, wahasiriwa wengi hukumbwa na hisia za kutojistahi. “Siwezi tena kulisha familia yangu,” asema mwanamume mmoja wa Kambodia, “na hilo huniaibisha.” Nyakati nyingine hisia hizo zaweza kumdhoofisha mtu hata kuliko kupoteza kiungo. “Naamini kwamba niliumia zaidi kihisia-moyo,” asema Artur, mhasiriwa wa Msumbiji. “Mara nyingi nilikasirika kwa sababu tu ya kuangaliwa na mtu. Nilidhani kwamba hakuna mtu aliyenistahi tena na kwamba sitawahi kuishi maisha ya kawaida tena.” *

Vipi Juu ya Kuondoa Mabomu ya Ardhini?

Katika miaka ya majuzi mataifa yametiwa moyo sana yapige marufuku utumiaji wa mabomu ya ardhini. Pia, serikali fulani zimeanza kazi hatari ya kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini. Lakini kuna vizuizi kadhaa. Kizuizi cha kwanza ni wakati. Kuondoa mabomu ya ardhini ni kazi inayofanywa miaka nenda miaka rudi. Kwa hakika, wateguaji wa mabomu hayo hukadiria kwamba kwa wastani, muda unaohitajiwa kuondoa bomu lililotegwa ardhini ni mara 100 zaidi ya muda unaotumiwa kulitega. Kizuizi kingine ni gharama. Bomu moja hugharimu kati ya dola 3 hadi 15 za Marekani, lakini kuliondoa kwaweza kugharimu dola zipatazo 1,000.

Kwa hiyo, yaonekana kuondoa mabomu yote yaliyotegwa ni jambo lisilowezekana. Kwa mfano, kuondoa mabomu yote ya ardhini huko Kambodia, kutamaanisha kwamba kila mtu nchini humo atoe mshahara wake wote kwa miaka kadhaa kwa ajili ya kazi hiyo. Inakadiriwa kwamba hata fedha zikiwapo, kuondoa mabomu yote ya ardhini yaliyotegwa huko kungechukua muda wa karne moja. Hali ya ulimwenguni pote ni yenye kusikitisha hata zaidi. Inakadiriwa kwamba kuondoa mabomu yote duniani kwa kutumia tekinolojia ya kisasa, kungegharimu dola bilioni 33 za Marekani na kungechukua muda wa zaidi ya miaka 1,000!

Ni kweli kwamba mbinu mpya za kuondoa mabomu ya ardhini zimependekezwa—kutoka kutumia nzi-tunda ambao wametiwa chembe za kuwasaidia kugundua mabomu hadi kutumia magari makubwa yenye kuelekezwa kwa mawimbi ya redio ambayo yangeondoa mabomu kwenye eneo la ekari tano kwa kila saa moja. Lakini, itahitaji muda fulani kabla ya mbinu hizo kuweza kutumiwa kila mahali, na yaelekea zitatumiwa katika nchi tajiri tu.

Hivyo, nchi nyingi hutumia mbinu za kale za kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini. Mtu hujikokota kwa tumbo huku akichimba-chimba mbele kwa kijiti, sentimeta kwa sentimeta, eneo la meta 20 hadi 50 za mraba kwa siku. Ni hatari, sivyo? Ndivyo! Kwa kila mabomu 5,000 yanayoondolewa, mteguaji mmoja hufa na wawili hujeruhiwa.

Waungana Kukomesha Mabomu ya Ardhini

Mnamo Desemba 1997, wawakilishi kutoka nchi kadhaa walitia sahihi Mkataba wa Kupiga Marufuku Utumiaji, Urundikaji, Utengenezaji na Uuzaji wa Mabomu ya Ardhini na wa Kuharibu mabomu hayo, pia huitwa mkataba wa Ottawa. “Hayo ni mafanikio yasiyo na kifani katika sheria ya kimataifa ya upunguzaji wa silaha au sheria ya kimataifa inayotetea haki za binadamu,” asema Jean Chrétien, waziri mkuu wa Kanada. * Hata hivyo, nchi zipatazo 60—kutia ndani baadhi ya watengenezaji mashuhuri wa mabomu ya ardhini ulimwenguni—hazijatia sahihi mkataba huo.

Je, mkataba wa Ottawa utafaulu kukomesha kabisa tatizo la mabomu ya ardhini? Labda kwa kiasi fulani. Lakini wengi wana shaka. “Hata nchi zote ulimwenguni zikifuata mkataba wa Ottawa,” asema Claude Simonnot, mkurugenzi-msaidizi wa Shirika la Handicap International, katika Ufaransa, “hiyo itakuwa hatua moja tu katika kukomesha hatari ya mabomu ya ardhini duniani.” Kwa nini? “Mamilioni ya mabomu yangali yametegwa ardhini, yakisubiri kuwalipua watu,” asema Simonnot.

Mwanahistoria wa kijeshi John Keegan ataja sababu nyingine. Yeye asema kwamba vita “huathiri hisia-moyo za mwanadamu, . . . ambazo ni chimbuko la fahari, hisia zenye nguvu, na tabia za kiasili zilizojificha.” Mikataba haiwezi kubadili tabia za binadamu zilizokita mizizi kama vile chuki na pupa. Lakini je, hilo lamaanisha kwamba wanadamu wataendelea kuwa wahasiriwa wa mabomu ya ardhini daima?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kwa habari zaidi juu ya kushughulikia kupoteza kiungo cha mwili, ona makala kuu ya mfululizo yenye kichwa “Tumaini kwa Walemavu,” katika ukurasa wa 3-10 wa toleo la Amkeni! la Juni 8, 1999.

^ fu. 20 Mkataba huo ulianza rasmi Machi 1, 1999. Kufikia Januari 6, 2000, ulikuwa umetiwa sahihi na nchi 137 na kuidhinishwa na nchi 90 kati yake.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Je, Wanachuma Fedha Maradufu?

Kanuni ya msingi ya biashara ni kwamba makampuni yanapasa kushtakiwa bidhaa zao zinapodhuru watu. Hivyo, Lou McGrath, wa shirika la Mines Advisory Group, asema kwamba makampuni ambayo yamefaidika kutokana na utengenezaji wa mabomu ya ardhini yapasa kushurutishwa kulipia hasara. Lakini, jambo la kushangaza ni kwamba watengenezaji wengi ndio wanaochuma fedha kwa kuondoa mabomu hayo. Kwa mfano, imeripotiwa kwamba kampuni moja ya Ujerumani iliyokuwa ikitengeneza mabomu ya ardhini ilipata kandarasi ya dola milioni 100 za Marekani ili kuondoa mabomu ya ardhini huko Kuwait. Na huko Msumbiji, shirika lenye makampuni matatu—mawili kati yake yalikuwa yametengeneza mabomu ya ardhini—lilipata kandarasi ya dola milioni 7.5 ya kuondoa mabomu kwenye barabara zilizoteuliwa.

Baadhi ya watu wanahisi kwamba ni ukosefu mkubwa wa adili kwa makampuni yanayotengeneza mabomu ya ardhini kuchuma fedha kwa kuondoa mabomu hayo. Wanadai kwamba kwa njia fulani watengenezaji wa mabomu ya ardhini huchuma fedha maradufu. Kwa vyovyote vile, kutengeneza na kuondoa mabomu ya ardhini bado ni biashara zinazositawi.

[Mchoro katika ukurasa wa 5]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Idadi ya wastani ya mabomu ya ardhini kwenye eneo la kilometa 2.5 za mraba katika nchi tisa zenye mabomu mengi yaliyotegwa

BOSNIA na HERZEGOVINA 152

KAMBODIA 143

KROATIA 137

MISRI 60

IRAKI 59

AFGHANISTAN 40

ANGOLA 31

IRAN 25

RWANDA 25

[Hisani]

Kutoka kwa: United Nations Department of Humanitarian Affairs, 1996

[Picha katika ukurasa wa 7]

Huko Kambodia, mabango na ishara kubwa huonya juu ya mabomu ya ardhini

Kwa kila mabomu 5,000 yanayoondolewa, mteguaji mmoja hufa na wawili hujeruhiwa

[Hisani]

Mandhari nyuma: © ICRC/Paul Grabhorn

© ICRC/Till Mayer

© ICRC/Philippe Dutoit