Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Ndugu Mdogo” Arejeapo Nyumbani

“Ndugu Mdogo” Arejeapo Nyumbani

“Ndugu Mdogo” Arejeapo Nyumbani

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA

KILA majira ya masika, puffin hurejea kwenye makao yake katika Aktiki baada ya kuhamia baharini muda wa miezi saba au minane. Ni msimu wa kujamiiana, na puffin aonekana maridadi sana tayari kwa kipindi hicho. Kwa kweli, miguu yake imebadilika na kuwa ya rangi nyangavu ya machungwa, na mdomo wake una gamba lenye kuvutia, ambalo huambuka baadaye. Manyoya yake meusi na meupe yenye kung’aa hudumu mwaka wote, nayo humfanya puffin ashabihi kasisi. Huenda hilo likafunua kiini cha jina la kisayansi la puffin wa Atlantiki Fratercula arctica, limaanishalo “mtawa mdogo, au ndugu wa kaskazini.” *

Vikundi vidogo vya puffin vinavyoitwa raft ambavyo huwa na ndege 20 au 30 hivi huelekea kwenye mashimo yao yaliyo kwenye magenge. Puffin hupata mwenzi ama wakati wa safari ama wafikapo shimoni. Ajabu ni kwamba puffin wengi huishi kwenye shimo lilelile—na kuwa na mwenzi yuleyule miaka nenda miaka rudi.

Puffin wanaweza kuruka, lakini kwa wazi si “warukaji” stadi miongoni mwa ndege wote. Kwa kweli, wao hutua kwa kishindo ufuoni! Isitoshe, puffin hupaa kwa shida, na nyakati nyingine huonekana kana kwamba mabawa yake hayawezi kuubeba mwili wake mnene. Baadhi ya puffin hata hushindwa kutoka majini. Lakini mara mabawa yanapopigapiga—na yaweza kupigapiga mara 400 kwa dakika—puffin anaweza kuruka kwa mwendo wa taratibu wa kilometa 80 kwa saa.

Bila shaka puffin wamezoea kuishi baharini kuliko barani. Lakini hawana budi kuja kwenye bara kwa sababu puffin wa kiume na wa kike sharti watayarishe shimo la vifaranga wao. Wafikapo barani, wao husafisha shimo hilo lenye urefu wa meta 0.5 hadi meta 2 hivi. Wao hutandika nyasi, vitawi, na manyoya shimoni. Puffin wengine hutaga mayai kwenye mianya chini ya miamba au kwenye nyufa miambani. Puffin huchimba-chimba udongoni kwa mdomo wake kisha huondoa udongo kwa miguu yake yenye utando.

Puffin wawili huchumbiana majini. Wakati wa sherehe hiyo puffin wa kiume hutikisa-tikisa vichwa, huvimbisha kidari, hupigapiga mabawa, na wenzi hao hugongana-gongana midomo. Kugongana huko huendelea hata baada ya kujamiiana. Yaonekana ndivyo wenzi hao wanavyoimarisha uhusiano wao.

Yai lililotagwa hutunzwa na wazazi wote—baba na mama hushiriki wajibu huo. Kazi ngumu huanza kinda linapoanguliwa majuma sita baadaye. Kinda hilo la rangi ya kijivu-nyeusi lililofichwa huatamiwa kwa muda wa juma moja ili kudumisha halijoto ya mwili wake. Wazazi wa puffin huenda baharini mara nyingi ili kukusanya chakula cha kutosha kinda lao. Safari za uvuvi si hatari sana, kwa kuwa kuna puffin wengi sana wanaoenda baharini na kurudi mashimoni. Yaonekana kwamba kwa sababu ya hekaheka hizo shakwe na adui wengine hushindwa kuwashambulia.

Puffin ni waogeleaji na wapiga-mbizi hodari. Wakitumia miguu yao yenye utando kama usukani na mabawa yao kujisogeza mbele, wanaweza kukaa majini kwa zaidi ya sekunde 30, katika kina cha meta 30 hivi. Puffin aweza kurejea nyumbani akiwa amebeba mdomoni samaki mmoja au wawili wadogo—labda capelin au sand lance. Bila shaka, kadiri samaki alivyo mdogo ndivyo puffin awezavyo kubeba wengi mdomoni. Puffin mmoja alionekana akiwa amebeba zaidi ya samaki 60! Mdomo wa puffin huwa na miiba iliyoinama nyuma ambayo humwezesha kushikilia samaki kwa nguvu huku akiendelea kuvua wengine. Kuvua samaki wengi kwafaa kwa sababu kinda la puffin laweza kula samaki 50 kwa siku.

Baada ya majuma sita hivi, wazazi wa puffin hurudi tena baharini. Kinda la puffin lililoachwa peke yake hujitayarisha kutoka shimoni. Wakati wa jioni hufanya mazoezi ya kupigapiga mabawa. Hatimaye, giza liingiapo puffin huyo hukimbia baharini na kuogelea kwa kasi.

Miaka miwili hadi mitatu hupita kabla puffin huyo mchanga hajarejea alikozaliwa, na miaka minne au mitano hupita kabla ya kujamiiana. Puffin huyo mkomavu aweza kuwa na uzito wa zaidi ya kilogramu 0.49 na kimo cha meta 0.3 tu. Ingawa puffin mwenye afya ni mdogo kwa kadiri fulani, anaweza kuishi kwa muda wa miaka 25 hivi. Puffin mmoja wa Atlantiki aliishi sana na kuzeeka akiwa na umri wa miaka 39!

Wataalamu hukadiria idadi ya puffin wa Atlantiki kuwa milioni 20. Inavutia sana kutazama ndege hao. “Puffin hutumbuiza hata katika mambo ya kawaida,” wakaandika David Boag na Mike Alexander katika kitabu chao The Atlantic Puffin. Na endapo unaishi karibu na fuo za kaskazini za bahari ya Atlantiki au ya Pasifiki, huenda ukawaona. Kwa vyovyote vile, jambo moja ni hakika—kila majira ya masika, “ndugu mdogo wa kaskazini” hurejea nyumbani, na kizazi kipya cha ndege wa baharini wenye manyoya meusi kitazaliwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Jina hilo pia laweza kuelekezea zoea la puffin la kufumbata pamoja miguu yake yenye utando wa ngozi baada ya kuibuka majini, kana kwamba anasali.

[Picha katika ukurasa wa 15]

“Puffin” katika Ghuba ya Witless, Newfoundland

[Hisani]

Kwa hisani ya: Tourism, Newfoundland and Labrador; mpiga-picha: Barrett and Mackay

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Kwa hisani ya: Tourism, Newfoundland and Labrador

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Tom Veso/Cornell Laboratory of Ornithology