Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Utakufa!”

“Utakufa!”

“Utakufa!”

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA LEANNE KARLINSKY

Jitihada yangu ya kutafuta matibabu bora bila damu huko Hispania

KAMA ungekuwa na fursa ya kusafiri popote ulimwenguni, ungechagua kwenda wapi? Jibu langu lilikuwa rahisi. Mimi hufunza Kihispania shuleni, na pamoja na mume wangu, Jay, na mwanangu Joel, sisi huhudhuria kutaniko la Mashahidi wa Yehova la lugha ya Kihispania katika Galax, Virginia, Marekani. Wakati huo nilitaka sana kuzuru Hispania. Kwa hiyo, waweza kuwazia jinsi nilivyosisimuka wazazi wangu walipojitolea kunipeleka huko! Ijapokuwa mume na mwanangu hawangeweza kuambatana nami, hamu yangu ilikaribia kutimizwa tuliposafiri kwa ndege moja kwa moja hadi Madrid. Tulipowasili Aprili 21, tulikodi gari la kutupeleka Estella, mji mdogo huko Navarre, kaskazini mwa Hispania. Nilistarehe kwenye kiti cha nyuma na nikasinzia mara moja.

Ninakumbuka tu nikiwa nimelala kwenye nyasi, huku jua likinimulika machoni. ‘Niko wapi? Nilifikaje hapo? Je, ninaota ndoto?’ Niliwaza na kuwazua, kisha nikashtuka nilipozinduka. Kulikuwa na kasoro, haikuwa ndoto. Mkono wangu wa kushoto wa shati ulibaki matambara, na singeweza kusogeza wala mikono wala miguu yangu. Baadaye, niling’amua kwamba gari letu lilibomoa uzio wa barabarani nami nikarushwa nje lilipoporomoka kwenye mtaro wenye kina cha meta 20. Kwa uzuri, wala mimi wala wazazi wangu hatukumbuki aksidenti ilivyotukia.

Niliomba msaada kwa sauti kubwa, na dereva mmoja wa lori akaja hima-hima mahali nilipokuwa. Kisha akateremka mtaroni lilipokuwa gari, ambamo wazazi wangu walikwama. “Julisha gari la kubeba wagonjwa lije haraka!” akamwambia mwenzake kwa sauti kubwa. “Watu waliomo garini ni mahututi!” Halafu akarudi mahali nilipokuwa nimelala nikiwa nimelemaa, na kwa nia njema, alijaribu kuunyosha mguu wangu. Nililia kwa maumivu makali, ndipo nilipogundua kwamba nilikuwa nimejeruhiwa vibaya.

Punde si punde nilikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali moja huko Logroño. Kwa fadhili polisi waliwajulisha Mashahidi wa Yehova walio karibu kilichotukia. Punde si punde, wengi kutoka kutaniko la Estella na Logroño walikuwa kando ya kitanda changu, pamoja na Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali ya eneo hilo. Kwa kweli, muda wote niliolazwa hospitalini, Wakristo wenzangu wapendwa ambao sikuwa nimepata kukutana nao walikuwa tayari kushughulikia mahitaji yangu usiku na mchana. Pia, waliwatunza wazazi wangu kwa upendo hadi walipopata nafuu na kuruhusiwa kurejea nyumbani juma moja hivi baada ya aksidenti hiyo.

Siku ya Jumatano mwendo wa saa saba usiku, madaktari walikuja kuipasua nyonga yangu iliyovunjika. Nilimwambia daktari kwamba sikutaka kutiwa damu. * Kwa kusitasita alikubali kustahi ombi langu, ingawa aliniambia ilielekea kwamba ningekufa. Upasuaji ulifaulu, lakini nilishangaa kuona vidonda vyangu havikuoshwa, wala bendeji kubadilishwa.

Kufikia Ijumaa kiwango changu cha damu kilishuka kufikia 4.7, nikaanza kunyong’onyea. Daktari alikubali kutumia tiba ya badala—kunidunga sindano za erythropoietin (EPO), ambazo pamoja na madini ya chuma na dawa nyingine huongeza kiwango cha damu, na kuchochea kufanyizwa kwa chembe nyekundu za damu. * Jay na Joel walikuwa wamewasili wakati huo. Lilikuwa jambo zuri kama nini kumwona mume wangu na mwanangu!

Mwendo wa saa saba na nusu hivi usiku, daktari alimwambia Jay kwamba tayari hospitali ilikuwa imepokea kibali cha mahakama cha kunitia damu endapo hali yangu itazorota. Jay alimwambia kwamba sikutaka kutiwa damu mishipani kwa heri wala kwa shari. “Basi atakufa!” daktari akamjibu.

Jay alizungumza na Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali kuhusu kunihamishia hospitali nyingine—ambayo ingestahi msimamo wangu. Si matabibu wote waliokuwa na uhasama katika hospitali hiyo. Kwa mfano, daktari mmoja alinihakikishia kwamba angejitahidi sana kuhakikisha kwamba nimeshughulikiwa kwa staha niliyostahili. Lakini baada ya muda madaktari wengine walinibana sana. “Je, wataka kufa na kuacha familia yako?” wakaniuliza. Niliwahakikishia kwamba nilitaka matibabu bora bila kutiwa damu. Madaktari hao hawakuguswa moyo kunisaidia. “Utakufa!” mmoja wao akasema waziwazi.

Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali ilipata hospitali moja huko Barcelona ambayo ilikubali kunitibu bila kunitia damu. Kulikuwa na tofauti kubwa jinsi gani baina ya hospitali hizo mbili! Katika Barcelona wauguzi wawili waliniosha taratibu na kunistarehesha. Walipokuwa wakinibadili bendeji, muuguzi mmoja aliona kwamba zilikuwa kijani-kibichi na zilikuwa na damu iliyokauka. Alisema kwamba aliaibika kwa sababu wananchi wenzake walikuwa wamenitendea hivyo.

Muda si muda nilikuwa nikipokea matibabu ambayo nilihitaji kupokea katika ile hospitali katika Logroño. Yalikuwa na matokeo sana. Baada ya siku chache viungo vyangu muhimu vilikuwa salama, na kiwango changu cha hemoglobini kilikuwa kimepanda hadi 7.3. Nilipokuwa nikitoka hospitalini, kiwango hicho kilikuwa kimepanda hadi 10.7. Nilipohitaji kufanyiwa upasuaji zaidi katika hospitali moja huko Marekani, kilikuwa kimefikia 11.9.

Ninawashukuru sana madaktari na wauguzi walio tayari kustahi msimamo wa wagonjwa wao, iwe wanakubaliana nao au la. Wafanyakazi wa hospitali wanapostahi itikadi za mgonjwa, wanamtibu mgonjwa kikamili—na hivyo wanatoa matibabu bora kabisa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Mashahidi wa Yehova hukataa kutiwa damu mishipani kwa sababu za Kibiblia.—Ona Mwanzo 9:4; Mambo ya Walawi 7:26, 27; 17:10-14; Kumbukumbu la Torati 12:23-25; 15:23; Matendo 15:20, 28, 29; 21:25.

^ fu. 9 Iwe Mkristo atakubali EPO au la ni uamuzi wa binafsi.—Ona Mnara wa Mlinzi, Oktoba 1, 1994, ukurasa wa 31.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Nikiwa na mume wangu na mwanangu

[Picha katika kurasa za 13]

Washiriki wawili wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali