Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Anaconda Je, Wanafunua Siri Fulani?

Anaconda Je, Wanafunua Siri Fulani?

Anaconda Je, Wanafunua Siri Fulani?

Na Mwandishi-habari Wa Amkeni!

SIJUI kama una maoni kama yangu, lakini nyoka wakubwa hunivutia sana kuliko wanyama wengine. Na tuzungumziapo nyoka wakubwa, twamaanisha chatu aina ya anaconda, wa jamii ya wanyama inayoitwa Boidae. Ajabu ni kwamba licha ya ukubwa wao, tabia yao imejulikana hivi majuzi tu.

Mnamo 1992, mwanabiolojia Jesús A. Rivas na watafiti wa Shirika la Kuhifadhi Wanyama wa Porini (WCS) lenye makao yake huko New York walianza kuchunguza majitu haya kwa mara ya kwanza yakiwa porini. * Niliposoma kwamba ripoti ya uchunguzi wao wa porini wa miaka sita, uliofanyiwa sehemu yenye majimaji huko Venezuela, ilifunua mambo mapya, nilitaka kujua mambo hayo. Nitajaribu kuyachunguza leo.

Majina na Jamii za Anaconda

Alasiri moja yenye jua, naondoka ofisini mwangu huko Brooklyn na kuelekea kwenye makao makuu ya WCS yaliyoko katika Bustani ya Wanyama ya Bronx, New York City. Tayari nilikuwa nimefanya utafiti wa kutosha kuhusu anaconda.

Inashangaza kwamba jina anaconda labda halikubuniwa Amerika Kusini anakopatikana mnyama huyo. Baadhi ya watu husema kwamba latokana na neno la Kitamil anai, limaanishalo “tembo,” na kolra, limaanishalo “mwuaji.” Wengine hufikiri kwamba linatokana na neno la Kisinhala henakandayā (hena, limaanishalo “radi,” na kanda, limaanishalo “chimbuko”). Yaelekea kwamba maneno hayo ya Kisinhala—yaliyotumiwa kwanza Sri Lanka kurejezea chatu—yaliletwa Amerika Kusini kutoka Asia na wafanyabiashara Wareno.

Kuhusu matumizi mabaya ya majina, hata jina la kisayansi linalofaa la anaconda, Eunectes murinus, si sahihi kabisa. Eunectes humaanisha “mwogeleaji stadi”—na kwa kweli ndivyo alivyo. Lakini murinus humaanisha “mwenye rangi ya panya.” Jina hilo “yaonekana halifai kwa kweli,” kwa nyoka mwenye ngozi ya zeituni ya kijani-kibichi, chasema kichapo kimoja.

Tunaweza kutaja jambo jingine zaidi kuhusu majina ya kisayansi na jamii za nyoka huyo. Vichapo vinavyozungumzia anaconda kwa kawaida hutaja jamii mbili za anaconda. Makala hii inataja jamii moja—anaconda wa kijani-kibichi, au chatu wa majini, hunyiririka hasa katika vinamasi vya bonde la Amazon na Orinoco huko Guiana. Jamii ile nyingine ni ya anaconda wadogo wa manjano (E. notaeus), wanaopatikana Paraguai, kusini mwa Brazili, na kaskazini mwa Argentina.

Kutana na Mtaalamu

Nimewasili katika Bustani ya Wanyama ya Bronx. Jamii zaidi ya 4,000 za wanyama, kutia ndani jamii 12 hivi za chatu aina ya anaconda huishi katika hifadhi hiyo yenye eneo la ekari 265 lililojaa miti. William Holmstrom wa Idara ya Utafiti wa Wanyama-Watambaazi katika WCS aliyevalia mavazi ya kaki ananisubiri katika lango la bustani hiyo ya wanyama. Bw. Holmstrom—mkazi wa New York mwenye umri wa miaka 51 akiwa na miwani, masharubu, na ni mwenye tabasamu—ni msimamizi wa ukusanyaji wa wanyama-watambaazi katika hifadhi hiyo na ameshiriki pia katika uchunguzi huo wa porini wa chatu hao huko Venezuela. Yeye asema kwamba sasa wanasayansi wamegundua jamii ya tatu ya anaconda (E. deschauenseei), wanaopatikana kaskazini-mashariki mwa Brazili na pwani ya Guiana ya Ufaransa. * Alasiri ya leo nitatembezwa na Bw. Holmstrom ambaye ni mtaalamu.

Hainichukui muda mrefu kugundua kwamba mtembezaji wangu anapenda nyoka jinsi wengine wanavyopenda mbwa au kasuku. Aniambia kwamba tangu alipokuwa mtoto, wazazi wake walifuga mijusi aina ya salamanda, chura, na wanyama wengineo. “Baba aliwapenda. Mama hakujali.” Ni wazi kwamba Bw. Holmstrom alimwiga babaye.

Ukubwa Wenye Kustaajabisha na Tofauti Kubwa Mno

Katika makao hayo ya wanyama-watambaazi yaliyojengwa miaka 100 iliyopita, twasimama mbele ya boma lenye anaconda. Napigwa na bumbuazi nimwonapo mnyama huyo, hata ingawa nilikuwa nikitamani kumwona. Nastaajabishwa na ukubwa na unono wake usio wa kawaida. Kichwa chake chenye umbo la pua, kilicho kikubwa kupita mkono wa mwanadamu, ni kidogo sana kikilinganishwa na mwili wake mkubwa. Mtembezaji wangu aniambia kwamba nyoka huyo maridadi mwenye urefu wa meta 5 na uzito wa kilogramu 80 ni wa kike. Ingawa mwili wake ni mnene kama mlingoti wa simu, naelezwa kwamba yeye ni mdogo sana akilinganishwa na chatu mkubwa zaidi ulimwenguni—chatu mfupi mnono wa kike aina ya anaconda aliyenaswa mnamo 1960, alikadiriwa kuwa na uzito wa kilogramu 227 hivi!

Hakuna anaconda yeyote wa kiume awezaye kuwa na ukubwa na unono wa kustaajabisha jinsi hiyo. Japo wataalamu wa wanyama-watambaazi walijua kwamba anaconda wa kiume huwa wadogo kuliko wa kike, uchunguzi wao ulionyesha kwamba chatu wa kiume ni wadogo mno hivi kwamba wanashabihi anaconda wadogo wa kike. Kwa kweli, uchunguzi huo ulionyesha kwamba kwa wastani chatu wa kike huwa wakubwa mara tano zaidi ya wa kiume. Mwanabiolojia Jesús Rivas aligundua kwamba tofauti ya umbo baina ya anaconda wa kiume na wa kike yaweza kukanganya. Alikuwa amefuga anaconda mdogo kama mnyama-kipenzi lakini hakujua kwa nini chatu huyo mdogo alikuwa akimwuma. Ni wakati tu wa uchunguzi wa porini ndipo alipogundua kwamba kumbe alikuwa nyoka wa kiume mkomavu mwenye hasira!

Watafutwa!—Kuna Tuzo

Mbali na sifa yake ya kuwa mkubwa, urefu wake unavutia pia. Kwa kweli, anaconda si wakubwa kupita kiasi kama vile ambavyo Shirika la Marekani la Filamu linavyoonyesha—sinema moja ilionyesha anaconda mwenye urefu wa meta 12—lakini urefu wao wa meta tisa hivi hustaajabisha sana isivyowazika.

Kuna anaconda wachache mno wanaofikia urefu huo. Anaconda wakubwa zaidi wa kike walionaswa wakati wa uchunguzi huo walikuwa na uzito wa kilogramu 90 na urefu wa meta 5. Ni vigumu sana kupata anaconda wakubwa zaidi kwani tuzo la dola 1,000 za Marekani, lililotolewa miaka 90 iliyopita na Shirika la Huduma za Wanyama wa Porini la New York (lililotangulia WCS), kwa mtu atakayenasa nyoka yeyote mwenye urefu unaozidi meta 9.2 halijatwaliwa hadi leo. “Sisi hupigiwa simu mara mbili au tatu kwa mwaka na watu kutoka Amerika Kusini wanaodai tuzo hilo,” asema Bw. Holmstrom, “lakini tunapowaomba walete uthibitisho kabla ya sisi kufunga safari ya kuwaona nyoka hao, hawaleti uthibitisho.” Kwa sasa, tuzo la kumpata nyoka aliye hai mwenye urefu wa meta 9.2 ni dola 50,000 za Marekani!

Kuwachunguza kwa Ukaribu

Namfuata mtembezaji wangu kwenye orofa ya pili ya jengo la wanyama-watambaazi, humo ndimo wanamohifadhiwa na kuatamia mayai. Sehemu hiyo ina joto na unyevunyevu. Bw. Holmstrom afungua mlango wa kizimba chenye anaconda wa kike mkubwa ajabu ili niweze kumwona kwa ukaribu.

Tuko umbali wa meta mbili tu kutoka kwa nyoka huyo. Kisha, anaconda huyo ainua kichwa chake taratibu kutuelekea. Kufikia sasa kuna umbali wa meta moja tu kati ya kichwa chake na vichwa vyetu.

“Ni heri twende,” asema Bw. Holmstrom kwa kusisitiza, “yaonekana anatafuta mlo.” Nakubali mara moja. Afunga mlango wa kizimba, naye anaconda huyo arudisha nyuma kichwa chake hadi kinapotulia katikati ya mwili wake ulioviringika.

Ukifaulu kupuuza macho makali ya anaconda kisha utazame kwa makini kichwa chake chenye milia myekundu, utaona kwamba kina sehemu nyingi za kuvutia. Kwa mfano, macho na pua ya anaconda zimeinuka kichwani. Hilo humwezesha nyoka huyo atumbukie majini huku macho na pua zikiwa juu ya maji—kama aligeta wanavyofanya. Ndiyo sababu nyoka huyo huweza kukaribia windo pasipo kuonekana.

Miviringo Yenye Nguvu na Taya Zinazolegea

Anaconda hana sumu. Yeye huua kwa kujizungusha kwa nguvu kwenye kiwiliwili cha windo lake. Havunji mifupa ya windo lake, lakini kila mara mnyama aliyenaswa anapopumua, nyoka huyo humbana zaidi hadi anapokuwa hoi na kufa kwa kukosa pumzi. Yeye hushambulia kiumbe yeyote—kuanzia bata hadi kulungu. Lakini ripoti zenye kuaminika za watu walioliwa na anaconda ni nadra sana.

Chatu aina ya anaconda humeza mnyama mfu akiwa mzima-mzima kwa kuwa nyoka hawatafuni au kunyofoa mnofu—hata mnyama akiwa mkubwa kuliko nyoka mwenyewe. Kwa hakika, kama ungekula mlo njia ya anaconda, ungehitaji kubugia nazi na kuimeza nzima-nzima bila shida kana kwamba ni njugu. Anaconda hufanyaje hivyo?

“Humeza windo lake taratibu,” asema Bw. Holmstrom. Aeleza kwamba taya za anaconda huwa legelege. Kabla hajakamata windo lake kwa meno, taya lake la chini hulegea na kupanuka. Kisha anaconda husogeza mbele upande mmoja wa taya lake na kushika windo kwa meno yake yaliyojipinda, halafu huvuta windo mdomoni kwa upande huo wa taya. Kisha, hufanya vivyo hivyo kwa upande ule mwingine wa taya la chini. Taya la juu laweza kusogea vivyo hivyo kwa kadiri fulani. Mnyama huyo huweza kumeza windo lake taratibu kwa kusogeza taya lake mbele na nyuma. Mara baada ya kumeza windo, labda baada ya saa kadhaa, nyoka huyo hupiga miayo mara kadhaa, na sehemu mbalimbali za kichwa chake kinachonyumbulika hurudia hali yake ya kawaida.

Ni nini kinachomzuia anaconda kusongwa? Kuna koromeo chini ya mdomo wake linaloweza kurefuka. Anapomeza mlo wake, anaconda husukuma nje koromeo lake kuelekea sehemu ya mbele mdomoni. Hivyo, koromeo hilo linaloshabihi mrija wa hewa wa mzamiaji humwezesha anaconda apumue anapokula.

Utabainishaje Kila Anaconda?

Mtembezaji wangu anaondoa kifuniko kwenye kizimba kimoja, ndani twaona anaconda wawili wachanga. Wanafanana sana hivi kwamba nashindwa kujua namna ambavyo watafiti waliweza kubainisha mamia ya anaconda wa porini waliochunguzwa katika mradi wa Venezuela.

Bw. Holmstrom aeleza kwamba walijaribu kutatua tatizo la kuwatambulisha kwa kutengeneza vyuma vidogo vya kutia alama kutokana na vishikizo. Walitia “vyuma” hivyo motoni na kuchapa nambari ndogo kwenye vichwa vya anaconda hao. Njia hiyo ilikuwa na matokeo hadi nyoka hao walipoambua ngozi zao zenye nambari! Ingawa hivyo, watafiti waligundua kwamba tayari kila anaconda ana alama ya kumtambulisha. Kila nyoka ana mpangilio wa madoa meusi chini ya mkia wake—mpangilio huo hutofautiana kwa kila nyoka kama alama za vidole vya wanadamu zinavyotofautiana. “Tulihitaji tu kuchora mpangilio wa alama iliyo kwenye magamba 15, na tulipata tofauti kubwa mno ya kubainisha nyoka 800 tuliochunguza.”

Je, Ni Mwepesi Zaidi, Mwenye Uwezo Zaidi wa Kiume, au Mwenye Nguvu Zaidi?

Tukamilishapo mahoji kwenye ofisi ya Bw. Holmstrom, yeye anionyesha picha aliyopiga huko Venezuela ya anaconda wa kiume wakiwa wamefungamana. Picha hiyo inaduwaza mno. Asema kwamba huo ni mfungamano wa kujamiiana wa anaconda. (Ona picha kwenye ukurasa wa 26.) “Anaconda wa kike yumo ndani ya mfungamano huo. Pindi moja tulikuta anaconda mmoja wa kike akiwa amezingirwa na anaconda 13 wa kiume—jambo la pekee kabisa.”

Je, hao wa kiume wanapigana? Kwa kweli, ni shindano la polepole la mieleka. Kila anaconda wa kiume anajaribu kumsukumia mbali mwingine angalau apate fursa ya kujamiiana na wa kike. Shindano hilo huendelea kwa majuma mawili hadi manne hivi. Ni yupi anayeshinda? Je, ni yule mwepesi (anayepata wa kike kwanza), mwenye uwezo zaidi wa kiume (anayetokeza shahawa zaidi), au mwenye nguvu (mume anayewapiga wengine mieleka)? Watafiti wanatarajia kupata jawabu karibuni.

Alasiri hiyo iishapo, namshukuru sana mtembezaji wangu kwa sababu ya matembezi hayo yenye kufana. Nirejeapo ofisini mwangu, natafakari mambo niliyojifunza. Bado sikubaliani na mwanabiolojia Jesús Rivas, aliyesema kwamba “anaconda hufurahisha,” lakini nakiri kwamba kwa kweli anaconda walinivutia. Huku watafiti wakiendelea kusaka anaconda porini, tutapendezwa kujua endapo tutajifunza mambo mapya yenye kuvutia kuhusu nyoka hao wakubwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Idara ya Wanyama wa Porini ya Venezuela na wanachama wa Shirika la Kimataifa la Kuzuia Biashara ya Wanyama na Mimea ya Porini Iliyohatarishwa yalidhamini uchunguzi huo.

^ fu. 11 Kichapo cha Journal of Herpetology, kilichochapishwa na Shirika la Utafiti wa Amfibia na Wanyama-Watambaazi, juzuu la 4, 1997, ukurasa wa 607-609.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Uchunguzi wa porini wa “anaconda” huko Venezuela

[Picha katika ukurasa wa 25]

William Holmstrom

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mfungamano wa kujamiiana wa “anaconda”