Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Maradhi ya Cystic Fibrosis Ningependa kuwashukuru sana kwa ajili ya makala “Kuishi na Maradhi ya Cystic Fibrosis.” (Oktoba 22, 1999) Mimi na mume wangu tuna umri unaokaribia wa Jimmy Garatziotis na mkewe, na inatia moyo sana kuona vijana wenye imani thabiti namna hiyo licha ya magumu.

S. D., Italia

Nimekuwa nikisubiri makala ya aina hiyo kwa miaka mingi. Mimi na mume wangu tuna binti mwenye umri wa miaka sita anayeugua cystic fibrosis. Kwa hiyo nilisoma makala hiyo mara moja. Inapendeza kuona Jimmy Garatziotis akihubiri kwa bidii licha ya ugonjwa. Na inasisimua kujua kwamba tunatumaini ulimwengu mpya ambao hautakuwa na magonjwa tena.

H. O., Marekani

Kielelezo cha Jimmy kinathibitisha kwamba tunaweza kutimiza mengi katika kumsifu Yehova tujapokuwa na afya mbaya.

P. C., Brazili

Dawa za Kulevya Asanteni kwa kuchapisha ule mfululizo “Je, Dawa za Kulevya Zinaudhibiti Ulimwengu?” (Novemba 8, 1999) Nilikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya—kokeini, marijuana, na bangi. Mbali na kuvuta zaidi ya sigareti 40 kwa siku nilikunywa pombe kupindukia. Ilikuwa vigumu kuacha mazoea hayo, lakini Mungu alinitia nguvu. Miaka tisa imepita tangu nilipoacha, nami nashukuru kwamba niliweza kujitenga kabisa na uchafu wa ulimwengu huu bila kuambukizwa maradhi hatari au kutiwa mbaroni. Kwa sababu ninajua matatizo ya kimwili, kihisia-moyo, na kiuchumi yanayosababishwa na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, ninatumaini kwamba makala hizo zitagusa mioyo ya vijana.

G. M., Italia

Nilitumia mfululizo huo kuandika insha shuleni, iliyoniwezesha kupokea maksi za juu na sifa ya mwalimu. Sikuzote mimi hufurahia kusoma Amkeni!, hasa makala zinazoshughulikia matukio ya karibuni. Hunisaidia kuona mambo kwa njia halisi.

I. M., Italia

Bustani za Michikichi Ile makala “Kuzuru Bustani ya Pekee” (Novemba 8, 1999) ni mojawapo ya makala zenye kuvutia zaidi nilizofurahia kusoma karibuni. Niliwazia kwamba niko katika Paradiso, nikipanga kwa uangalifu bustani hiyo maridadi. Moyo wangu uliguswa na upendo alio nao mtu huyo kuelekea mimea yake. Jinsi anavyothamini uumbaji maridadi wa Yehova, kama tupaswavyo kuuthamini sote!

L. C., Kanada

Kuwa Mwenye Urafiki Zaidi Ile makala “Vijana Huuliza . . . Naweza Kuwaje Mwenye Urafiki Zaidi?” (Novemba 22, 1999) ilinigusa moyo sana. Nina umri wa miaka 16 nami hushindwa kuwasiliana na wengine, hasa katika mikutano ya Kikristo. Asanteni kwa ajili ya kutufikiria sisi vijana tulio na tatizo hilo. Nitajaribu kutumia shauri zuri mlilotoa katika makala hiyo.

I. A., Ufaransa

Ndege Wanaoimba Asanteni kwa ajili ya makala “Waimbaji Wawili Wenye Muziki Mtamu.” (Desemba 8, 1999) Niliwazia ndege hao wakiporomosha muziki mtamu kutoka kwenye tawi la mti! Kila siku mimi humshukuru Yehova kwa kuumba wanyama wanaotutumbuiza.

Y. S., Japani

Ugonjwa wa Kisukari Wakati wa masomo yangu ya baada ya kupokea shahada, nilipewa mgawo wa kuongoza semina ya ugonjwa wa kisukari aina ya melittus. Maelezo sahili na ya moja kwa moja yaliyochapishwa katika makala “Binti Yenu Ana Ugonjwa wa Kisukari!” (Septemba 22, 1999) yalinisaidia sana. Simulizi la Sonya Herd lilifanya ning’amue jinsi mgonjwa anavyohitaji kuwa na habari sahihi.

T. K., Brazili