Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutumia Televisheni kwa Uangalifu

Kutumia Televisheni kwa Uangalifu

Kutumia Televisheni kwa Uangalifu

TELEVISHENI huwa kama “mhadithiaji mkuu, mlezi wa watoto na kifaa kinachoathiri maoni ya umma,” yasema ripoti ya Not in the Public Interest—Local TV News in America, iliyokusanywa na shirika moja linalochunguza habari huko Marekani. “Televisheni iko kila mahali . . . Imeenea sana kama moshi wa sigareti hewani.” Kutazama vipindi vya televisheni kwa muda mrefu bila kuwa mteuzi hudhuru kama kuvuta moshi wa sigareti ulio hewani—hasa watoto.

Kuhusu uhalifu na jeuri kwenye televisheni, ripoti hiyohiyo yasema kwamba “uchunguzi chungu nzima umeonyesha kwamba kutazama picha za jeuri huathiri sana kusoma, ukuzi na hisia-mwenzi za watoto.” Shirika la Kitiba la Marekani lilisema mnamo 1992 kwamba “jeuri kwenye televisheni ni jambo hatari linalotisha afya ya vijana.”

Unaweza kudhibitije uvutano wa vipindi visivyofaa vya televisheni kwa watoto wako? Ripoti hiyo yaorodhesha madokezo fulani, yaliyopendekezwa na mashirika kadhaa ya afya ya umma, kuhusu namna ya kutumia televisheni kwa uangalifu zaidi. Yafuatayo ni baadhi ya madokezo yaliyotolewa.

▪ Panga na uweke mipaka ya kutazama televisheni. Weka mipaka ya wakati wa watoto kutazama. Usiweke televisheni kwenye vyumba vya watoto.

▪ Weka ramani karibu na televisheni ili watoto waweze kutafuta sehemu zinazoonyeshwa kwenye televisheni.

▪ Tazama televisheni na watoto wako ili uweze kueleza tofauti iliyopo baina ya mambo ya kuwaziwa na mambo halisi. Watoto wengi wenye umri unaopungua miaka kumi hushindwa kutofautisha mambo hayo.

▪ Iweke televisheni mbali na sehemu iliyo wazi nyumbani mwenu. Ifungie televisheni kabatini. Haitakuwa rahisi kuiwasha na kubadili-badili vituo.