Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Watoto na Ibada za Kidini

“Je, watoto wanahudhuria ibada za kidini?” lauliza toleo la karibuni la kichapo Canadian Social Trends. Lajibu kwamba uchunguzi wa shirika la Statistics Canada waonyesha kwamba, “zaidi ya theluthi, asilimia 36 ya watoto wa Kanada wenye umri unaopungua miaka 12 walihudhuria ibada za kidini angalau mara moja kwa mwezi, na wengi wao walihudhuria kila juma. Asilimia 22 zaidi hawakuhudhuria kwa ukawaida, lakini walihudhuria angalau mara moja kwa mwaka.” Hata hivyo, makala hiyo ilionyesha pia kwamba “mashirika mbalimbali ya kidini yalisababisha tofauti kubwa ya uhudhuriaji wa kawaida wa watoto katika ibada za kidini. . . . Zile zinazoonwa na wengi kuwa dini zenye wafuasi wengi, kama vile Kanisa la Anglikana na United Church, zilikuwa na hudhurio la chini sana la watoto kila juma (asilimia 18).” Watoto Wakatoliki walifanya vyema kidogo, asilimia 22 walihudhuria kila juma. Asilimia 44 ya watoto Waislamu ndio waliohudhuria ibada ya dini ya Kiislamu kila juma, “dini hiyo ilikuwa pia na idadi kubwa zaidi ya wasiohudhuria (asilimia 39) mwaka uliotangulia uchunguzi huo.”

Onyo Kuhusu Kigari cha Watoto cha Matembezi

Kutumia kigari cha watoto cha matembezi kunaweza kuathiri ukuzi wa kimwili na kiakili wa watoto wachanga, laripoti gazeti Independent la London. Watafiti katika Chuo Kikuu cha State huko New York waligundua kwamba vigari vya matembezi vyenye trei kubwa ya mbele huzuia watoto kuona miguu yao na kuweza kutambaa na kushika vitu vinavyowazunguka. Uchunguzi ulionyesha kwamba watoto wachanga wanaotumia vigari vya matembezi huketi wima, hutambaa, na kutembea baada ya zaidi ya majuma matano kuliko watoto ambao hawakuwahi kutumia kigari cha matembezi. Pia, uchunguzi ulifunua kwamba kila mwaka asilimia 50 ya watoto wachanga wanaotumia vigari vya matembezi hujeruhiwa wanapoanguka ngazini, motoni, au sakafuni. Dakt. Denise Kendrick, wa Kitivo cha Kitiba katika Chuo Kikuu cha Nottingham, Uingereza, asema hivi: “Vigari vya matembezi si salama. Yaonekana vinapunguzia wazazi usumbufu wa watoto badala ya kuwanufaisha watoto.”

Vikolezo Huua Bakteria

Msiba mbaya zaidi ulimwenguni wa kusumishwa kwa chakula ulitukia Uingereza mnamo 1996, na uliua watu 18. Sumu hiyo ilisababishwa na nyama iliyosumishwa na bakteria ya E. coli O157. Hivi majuzi, watafiti waligundua kwamba kutia dalasini ndani ya maji ya tofaa yenye vijidudu kuliua asilimia 99.5 ya bakteria zote katika muda wa siku tatu, lasema gazeti The Independent la London. Katika pindi nyingine, wanasayansi hao waliongeza vikolezo kwenye nyama mbichi ya ng’ombe na soseji na kugundua kwamba dalasini, karafuu, na kitunguu saumu viliua bakteria ya E. coli O157 kabisa. Watafiti wanafikiri kwamba vikolezo hivyo vinaweza kutumiwa kuua bakteria nyingine, kutia ndani salmonella na campylobacter.

Madeni ya Kibinafsi ya Waingereza

Waingereza wanadaiwa dola bilioni 170 za Marekani kutokana na mikopo midogo, kadi za mikopo, na malipo ya polepole nao hulipa riba ya dola bilioni 5.5 kila mwaka, kulingana na takwimu zilizochapishwa na People’s Bank na kuripotiwa na gazeti The Times la London. Zaidi ya theluthi ya watu wote wana deni fulani lisilo na rehani, wastani wa dola 10,400 za Marekani kwa kila mtu. Gharama za kadi za mkopo katika Uingereza zilirudufika katika muda wa miaka mitatu, na kufikia dola bilioni 115 mnamo 1998. Uchunguzi huo ulifunua pia kwamba ni asilimia 13 tu ya watu ndio wanaohangaikia uwezekano wa kurundamana kwa madeni yao. Na mtu 1 kati ya 5 alikiri kuwa yeye hukopa “ili adumishe mtindo wake wa maisha,” yasema People’s Bank.

Kinyume cha Mapenzi Yake

Karibu robo ya wanawake vijana 304 waliohojiwa katika uchunguzi ulioripotiwa na gazeti Psychologie Heute la Ujerumani, walisema kwamba walikuwa wameshurutishwa kushiriki utendaji fulani wa kingono kinyume cha mapenzi yao. Pia, ripoti hiyo yasema kwamba zaidi ya robo ya wanawake hao waliripoti kwamba wanaume walijaribu kutumia dawa za kulevya na pombe ili kuwashawishi wafanye ngono pasipo hiari. Yaongezea hivi: “Ukizingatia majaribio ya wanaume vijana ya kuwafanya wanawake wawe hoi kwa kuwashawishi kwa maneno, dawa za kulevya, au pombe, uwezekano wa mwanamke kijana mwenye umri wa kati ya miaka 17 na 20 kushurutishwa kufanya ngono kinyume cha mapenzi yake utaongezeka kwa zaidi ya asilimia 50.”

Hifadhi ya Kwanza Ulimwenguni ya Anga la Giza

“Anga maridadi la mahameli wakati wa usiku halionwi na wengi leo kwa kuwa limefichwa na mwangaza wa taa za mijini, na kufunikwa na utusitusi wa hewa iliyochafuliwa,” lasema gazeti The Globe and Mail la Kanada. Mwandikaji wa astronomia Terence Dickinson alalamika hivi: “Inawezekana watu kukua, hata kufikia utu uzima, bila kuona kamwe umaridadi wa anga la usiku.” Mathalani, yeye asema, baada ya tetemeko la ardhi kukata umeme katika sehemu nyingi huko California miaka michache iliyopita, wakazi fulani waliwapigia simu polisi na kuwaeleza “kuhusu sura ajabu ya nyota na ukanda wenye ukungu” angani. Ardhi ya umma yenye ukubwa wa ekari 4,900 katika jimbo la Muskoka Lakes kaskazini ya Toronto imetengwa kuwa “hifadhi ya anga la giza,” ili wapenzi wa nyota huko Kanada waweze kuona anga la usiku lenye kung’aa pasipo uchafuzi wa mwangaza. Hifadhi hiyo yaitwa Torrance Barrens Conservation Reserve, na yaaminika kuwa ni hifadhi ya kwanza ya anga la giza ulimwenguni.

Akina Baba na Binti

Ripoti ya majuzi ya kichapo cha Health Canada inayotegemea uchunguzi wa vijana 2,500 yafunua kwamba kuna ukosefu wa uwasiliano kati ya baba na watoto wao, hasa binti, laripoti gazeti Globe and Mail la Kanada. Ni asilimia 33 tu ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 16 “wanaowasiliana kwa urahisi na baba zao kuhusu mambo yanayowasumbua sana,” ikilinganishwa na asilimia 51 ya wavulana. Na bado, “wasichana huelekea kuthamini sana baba zao na wanahitaji msaada wao,” yasema ripoti hiyo. Profesa Alan King wa Chuo Kikuu cha Queen akiri kwamba “ni vigumu kwa akina baba kuwasiliana na watoto wao, hasa wakati wa magumu wanapoanza kubalehe,” wakati huo akina baba wengi hupuuza masuala ya kingono na mwenendo hatari wa watoto. Lakini yeye awashauri akina baba wajitahidi kuwasiliana, hasa kwa kuwa akina mama wengi sasa hawana wakati wa kuwa na watoto wao kama awali.

‘Haiwezekani Kumudu Hali Bila Televisheni!’

Ungechukua nini kama ungelazimika kuishi kwa muda katika kisiwa kilichojitenga? Vijana 2,000 huko Ujerumani waliulizwa swali hilo. Kwa wengi wao, kifaa muhimu zaidi kingekuwa televisheni na redio, CD na kanda zenye mirekodio, laripoti gazeti Westfälische Rundschau. Kisha chakula na vinywaji vikawa vya pili, huku washiriki wa familia na marafiki wakichukua nafasi ya tatu. Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 13 alieleza chaguo lake: “Siwezi kumudu hali bila televisheni.” Ni theluthi tu ya wale waliohojiwa waliosema kwamba wangechukua vifaa muhimu kama vile visu, majembe, na misumeno. Ni asilimia 0.3 tu waliosema wangechukua Biblia. Mshiriki mchanga zaidi, msichana mwenye umri wa miaka saba, alisema: “Ningeambatana tu na mama yangu. Awapo nami, mambo huwa shwari.”

Mababe ya Mieleka ya Sumo

Wapigaji-mieleka ya sumo, walio maarufu ulimwenguni kwa sababu ya viuno vyao vinene, wanaongeza uzito zaidi kushinda uwezo wa miguu yao, wasema wataalamu wa utendaji wa mwili katika Japani. Gazeti New Scientist laripoti kwamba visa vya kujeruhiwa katika vikundi vya kwanza viwili vya sumo viliongezeka maradufu katika miaka mitano iliyopita, na kulazimu jopo la wataalamu wa utendaji wa mwili kulinganisha mafuta ya mwili na uwezo wa miguu wa wapigaji-mieleka 50. “Robo kati yao hawakuwa na misuli yenye nguvu vyakutosha kutegemeza miili yao ifaavyo,” yasema ripoti hiyo. Uzito wa mwili wa wastani wa wapigaji-mieleka ya sumo walio mashuhuri uliongezeka toka kilogramu 126 mwaka wa 1974 hadi kilogramu 156 mnamo 1999. “Kwa sehemu inahusiana na ongezeko la ukubwa wa wastani wa Wajapani wote kwa ujumla,” asema mtangazaji wa sumo Doreen Simmonds. Lakini ushindi hautegemei hasa uzito mkubwa wa mwili. “Umbo linalofaa katika sumo ni umbo la pea,” asema Simmonds. “Nyonga fupi, mapaja manene na mashavu ya miguu yanayoshabihi mwaloni.”

Watoto Wamo Hatarini

Angola, Sierra Leone, na Afghanistan ndizo nchi hatari zaidi ulimwenguni kwa watoto, na ‘uwezekano wa mtoto kufikia umri wa miaka 18 ni mdogo sana,’ yasema ripoti moja ya Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF). Kwa sababu ya vita, ufukara usiokoma, na kuenea kwa virusi vya UKIMWI, watoto wanakabili hatari zaidi kuliko ile waliyokabili mwongo mmoja uliopita. Likitumia “kipimo cha hatari inayokabili watoto” kwa uwiano wa 1 kwa 100, shirika la UNICEF lapiga hesabu kipimo cha 96 huko Angola, 95 huko Sierra Leone, na 94 huko Afghanistan. Tofauti na nchi hizo, kipimo cha wastani cha hatari inayokabili watoto katika Ulaya ni 6, laripoti gazeti The Times la London.