Je, Macho Yako Yana Madoa?
Je, Macho Yako Yana Madoa?
Labda umewahi kuyaona—madoa madogo ya kijivujivu yasiyoonekana vizuri yakielea mbele ya macho yako. Waweza kuyaona unaposoma au unapotazama ukuta wenye rangi isiyokoza au anga lisilo na mawingu.
IKIWA umewahi kujaribu kukazia macho madoa hayo, unajua kwamba haiwezekani. Unapogeuza macho kidogo tu madoa hayo hutoweka kwa kasi, na hata ikiwa moja litapita mahali unapoliona, bado hutaweza kujua ni nini.
Madoa hayo ni nini? Je, yako juu ya mboni ya jicho lako, au yamo ndani? Pepesa kope zako bila kugeuza macho yako. Madoa hayo yakielekea upande mwingine au yakitoweka, basi yako juu na siyo tunayozungumzia katika makala hii.
Lakini ikiwa hakuna badiliko lolote au kuna badiliko dogo, basi yamo ndani, yanaelea katika ute unaong’aa, uowevu unaojaza sehemu ya ndani ya mboni ya jicho lako. Kwa kuwa yako nyuma ya lenzi za macho, hayaonekani waziwazi. Na kwa kuwa ute unaong’aa ni jeli iliyo nyepesi kuliko maji, yanaweza kujongea, yakielekea upande mwingine unapojaribu kukazia macho doa moja. Jina lake la kitiba latokana na hali hiyo—muscae volitantes, linalomaanisha “nzi wanaoruka.”
Hutoka Wapi?
Madoa hayo hutoka wapi? Baadhi yake yalitokana na ukuzi uliotukia kabla hujazaliwa. Mtoto mchanga anapoanza kukua, sehemu ya ndani ya jicho huwa na nyuzinyuzi. Wakati wa kuzaliwa, nyuzinyuzi hizo na chembe nyingine hubadilika na kuwa ute unaong’aa. Hata hivyo, chembe nyingine na nyuzinyuzi chache zaweza kubaki, nazo ndizo huelea. Pia kuna mfereji unaotoka kwenye neva ya macho hadi kwenye lenzi ulio na mshipa ambao hulisha lenzi kabla mtoto hajazaliwa. Kwa kawaida, kabla ya kuzaliwa, mshipa huo hunywea na kufyonzwa lakini sehemu zake ndogondogo zaweza kusalia.
Lakini kuna vyanzo vingine pia. Hata katika mtu mzima, ute wote unaong’aa si jeli. Umezingirwa na utando mwangavu ulio nyeti. Huo hutanda kwenye retina, kiwambo cha tishu zinazoathiriwa na nuru ambazo hulainisha sehemu kubwa ya ndani ya jicho lako na ambazo hunasa picha unazoona. Utando mwangavu hujishikiza kwenye retina kuzunguka sehemu yote ya mbele. Kutoka kwenye mkunjo huo nyuzinyuzi ndogo sana huelea kwenye ute unaong’aa.
Tunapozeeka, nyuzinyuzi hizo ndogo huanza kunywea. Nyingine hukatika. Ute unaong’aa pia huwa na uowevu zaidi, kwa hiyo vipande vilivyokatika vyaweza kuelea ndani yake kwa urahisi. Ute unaong’aa hupungua kwa kiasi kidogo na huanza kujivuta kutoka kwa retina, labda ukiacha mabaki ya chembe. Hivyo, umri unaposonga utaona “nzi [hao] wanaoruka” wengi zaidi wakielekea huku na huku machoni.
Chanzo kingine cha madoa madogo yanayoelea chaweza kuwa mishipa ya damu ya retina. Mshipa mdogo waweza kutokeza uzi wa chembe nyekundu za damu
unapopigwa ngumi kichwani au mboni ya jicho inaposongwa sana. Chembe nyekundu hunata, kwa hiyo hujikusanya pamoja au kufanyiza mnyororo. Chembe mojamoja au zikiwa vikundi zaweza kupenya ute unaong’aa, na zikibaki karibu na retina, zaweza kuonekana. Mwili huweza kufyonza tena chembe nyekundu, kwa hiyo hatimaye hutoweka. Hata hivyo, hizo si muscae volitantes, kwa kuwa hutokezwa na majeraha madogo.Je, kuwepo kwa muscae volitantes huonyesha kwamba kuna kasoro fulani? Kwa kawaida sivyo. Watu wasio na kasoro ya macho, hata vijana, huyaona, nao hujifunza kuyapuuza hatua kwa hatua. Lakini hali fulani zaweza kuashiria hatari.
Kunapokuwa na Hatari
Ikiwa kwa ghafula waanza kuona madoa mengi zaidi kuliko awali, huenda ikamaanisha kuna kasoro fulani. Ni kweli hasa ikiwa waona mimweko midogo ya nuru ndani ya jicho lako. Hali hii isiyo ya kawaida hutoka kwenye retina, ambapo nuru hugeuzwa kuwa mpwito. Manyunyu ya vitu vinavyoelea na mimweko ya nuru kwa kawaida husababishwa na kubanduka kwa retina. Hilo hutokeaje?
Retina ina uzito na unene unaotoshana na karatasi yenye unyevunyevu na huathirika kwa urahisi kama karatasi. Tabaka lake linaloathiriwa na nuru limeshikiliwa na tabaka lililo nyuma kwenye ute unaong’aa katika ncha yake ya mbele tu, na kwenye neva ya macho, kwa kujishikilia kidogo katika eneo la kutazamia. Ute unaong’aa husaidia kushikilia ipasavyo sehemu inayobaki ya retina. Jicho ni thabiti sana hivi kwamba kwa kawaida hata ngumi hazipasui retina au kuitenganisha na sehemu ya chini.
Hata hivyo, ngumi yaweza kusababisha madhara yanayodhoofisha retina katika sehemu fulani au yanayofanya ipasuke kidogo au itoboke. Shimo hilo laweza pia kusababishwa na mnato kati ya ute unaong’aa na retina: Kutikisika kwa ghafula au jeraha hufanya ute unaong’aa ujivute kwenye retina na kupasuka kidogo. Uowevu kutoka kwenye chemba ya ute unaong’aa waweza kuvuja nyuma ya retina, na kuiinua kutoka sehemu yake ya chini. Vurugu hilo husababisha chembe za neva zinazoathiriwa na nuru zing’ae, nazo huonekana kama mimweko ya nuru.
Nyakati fulani kuvuja damu, kiasi kidogo au kingi, huandamana na mtengano huo, kwa kuwa sehemu ya ndani ya retina ina mishipa yake ya damu. Chembe za damu hutumbukia kwenye ute unaong’aa, nazo huonekana kuwa vitu vinavyoelea kwa ghafula. Muda mfupi baada ya hilo, retina inapojibandua, shela, au pazia la upofu huziba mahali pa kutazamia.
Kwa hiyo, ukipata kuona idadi ya madoa ikiongezeka, hasa yakiandamana na mimweko, nenda kwa daktari wa macho au hospitalini mara moja! Huenda ikawa retina imebanduka. Huenda isiwezekane kurekebisha madhara baada ya retina kubanduka sana.
Je, macho yako yamekuwa na madoa yasiyo na mimweko ya nuru kwa miaka mingi? Labda hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Karibu kila mtu huona madoa hayo pia. Ukiyapuuza, hayatatoweka, lakini ubongo huweza kuficha picha hizo unapoendelea na shughuli zako za kila siku. Uhakika wa kwamba madoa yanaweza kuwapo bila kudhuru uwezo wa kuona ni ushuhuda wa jinsi jicho lilivyobuniwa kwa uthabiti na uwezo wa ubongo wa kujipatanisha na hali.
Hata hivyo, kabla ya kusema kwa uhakika kwamba hakuna haja ya kuwa na wasiwasi, mtu yeyote anayeona vitu vikielea apaswa kuchunguzwa na daktari wa macho.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]
Mwanzo wa Hatua ya Kisasa ya Kurekebisha Kasoro za Macho
Ikiwa wewe huvaa miwani ya kupimwa au lenzi zinazoambatanishwa na mboni, katika njia fulani ni kwa sababu ya muscae volitantes. Tabibu maarufu Mholanzi wa karne ya 19, Frans Cornelis Donders, alichochewa na udadisi kuanzisha uchunguzi wa kisayansi kuhusu maumbile na magonjwa ya macho. Mbali na kutambulisha vyanzo fulani vya muscae volitantes, aligundua kwamba uwezo wa kuona mbali husababishwa na kupungua ukubwa kwa mboni ya jicho na kwamba kutoona vizuri kunakosababishwa na dosari katika jicho huletwa na kutojilainisha vizuri kwa konea na lenzi. Uchunguzi wake uliwezesha kuanzishwa kwa miwani ya kupimwa.
[Picha]
Donders
[Hisani]
Courtesy National Library of Medicine
[Mchoro katika ukurasa wa 24]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Retina iliyobanduka
Chembe nyekundu
Mpasuko katika retina
Utando mwangavu
Lenzi
Mboni
Musuli-mboni
Misuli ya siliari
Ute unaong’aa
Mishipa ya damu
Neva-jicho inayoongoza kwenye ubongo