Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
“Tungenufaika Kuwabuni”
Profesa Anatoly P. Zilber, mwenyekiti wa Idara ya Wagonjwa Mahututi na Unusukaputi, kwenye Chuo Kikuu cha Petrozavodsk na Hospitali ya Republican huko Karelia, Urusi, awapongeza Mashahidi wa Yehova, akisema: “Hawatumii vileo isivyofaa, hawavuti sigareti, hawana pupa ya pesa, hawavunji ahadi zao, wala kutoa ushahidi wa uwongo . . . Si farakano la kifumbo, bali ni raia wanaotii sheria.” Aongezea: “[Wao] ni watu wanaostahili heshima, wenye furaha, wanaopendezwa na historia, fasihi, sanaa, na mambo yote yahusuyo maisha.” Kisha, baada ya kuorodhesha mabadiliko yanayofaa yaliyoletwa na Mashahidi kuhusu upasuaji bila damu, profesa huyo asema: “Kwa kubadili maneno ya Voltaire, tungeweza kusema kwamba ikiwa hakukuwa na Mashahidi wa Yehova, tungenufaika kuwabuni.”
Je, Ni Mtindo wa Kiwango cha Juu Zaidi?
Viatu vyenye visigino virefu, “kitu muhimu kwa vijana wanaopendezwa na mitindo,” hujeruhi watu wapatao 1,000 kwa mwaka huko Uingereza, lasema gazeti The Times la London. Steve Tyler, msemaji wa Taasisi ya Viwango ya Uingereza, asema: “Majeraha ya kawaida zaidi ni kuteguka tindi za miguu na kuvunjika miguu, lakini viatu hivyo vyaweza pia kusababisha matatizo ya mgongo, hasa kwa wasichana wachanga ambao miili yao ingali inakua.” Katika Japani viatu vyenye visigino virefu vimesababisha vifo vya wanawake wawili katika miezi ya majuzi. Katika kisa kimoja mfanyakazi mmoja wa shule ya nasari mwenye umri wa miaka 25 aliyekuwa amevalia malapa yenye visigino vya urefu wa sentimeta 12.5 alijikwaa, akavunjika fuvu la kichwa, na kufa. Mwanamke mwingine kijana alikufa baada ya gari alimokuwa akisafiria kugonga pao ya saruji kwa sababu dereva hangeweza kufunga breki sawasawa akiwa amevalia buti zenye kisigino cha sentimeta 15. Watengenezaji fulani wameanza kuweka vibandiko vyenye onyo katika viatu vyao, ili wasishtakiwe.
Kazi za Nyumbani za Kila Siku kwa Ajili ya Watoto
“Wazazi wa leo wenye shughuli nyingi huwa walegevu kuhusu kusaidiwa kazi za nyumbani na watoto wao,” laripoti The Toronto Star. Ijapokuwa kazi za kila siku “hazitawahi kuwa jambo la kutangulizwa na watoto,” asema Jane Nelsen, mwandishi wa Positive Discipline, kazi hizo “huwafanya watu wajitegemee na kujistahi.” Kulingana na uchunguzi katika gazeti Child, kazi fulani halisi za kila siku katika nyumba kwa ajili ya watoto wenye umri wa kati ya miaka miwili hadi mitatu zingeweza kutia ndani kuokota vichezeo na vilevile kuweka nguo chafu ndani ya kikapu. Watoto walio na umri wa kati ya miaka mitatu hadi mitano wanaweza kupanga meza, kupeleka vyombo kwenye beseni ya kuoshea vyombo, na kusafisha mahali wanapochezea. Wale walio na umri wa kati ya miaka 5 hadi 9 wanaweza kujitandikia vitanda vyao, kuokota majani, na kung’oa magugu, ilhali walio na umri wa kati ya miaka 9 hadi 12 wanaweza kufanya kazi kama vile kuosha na kukausha vyombo, kutupa takataka, kukata nyasi, na kufagia mkeka. Nelsen aongezea kwamba “kunakuwa na matokeo mazuri unapowawekea muda wa kumaliza kazi hizo.”
Vijana na Uhalifu
Uchunguzi Mkuu huko Scotland wafunua kwamba nchini Scotland asilimia 85 ya wavulana na asilimia 67 ya wasichana walio na umri wa kati ya miaka 14 na 15 walisema kwamba walihusika na uhalifu mwaka uliopita. Gazeti The Herald la Glasgow laripoti kwamba kati ya wanafunzi 1,000 waliofanyiwa uchunguzi kutoka shule sita, ni asilimia 12 tu waliosema kwamba hawakuwahi kufanya kosa lolote. Asilimia 69 ya wavulana na asilimia 56 ya wasichana walikuwa wameharibu mali katika visa hivyo vya uhalifu. Asilimia 66 ya wavulana na asilimia 53 ya wasichana walikuwa wameiba madukani, na karibu nusu walikuwa wameiba shuleni. Uhalifu mwingine ulitia ndani kuchoma mali na kujeruhi kwa kutumia silaha. Vijana wa rika hilo walidai kwamba kisababishi kikuu cha uhalifu waliofanya kilikuwa msongo wa marika, ilhali kwa wale walio na umri unaozidi miaka 15, kisababishi kikuu kilikuwa kutafuta pesa za kuendeleza zoea la kutumia dawa za kulevya.
Wanafunzi Wenye Fujo
Kwa kawaida, Japani haijawa na tatizo kubwa la uasi miongoni mwa matineja. Lakini sasa walimu wa shule kotekote katika Japani wanaripoti kwamba inazidi kuwa vigumu kudumisha utengamano darasani kwa sababu ya wanafunzi wasiotulia na wenye fujo.
Baraza la mji wa Tokyo lilihoji wanafunzi wenye umri wa miaka 9, 11, na 14 ili kujua maoni yao kuelekea watu wengine. Kulingana na The Daily Yomiuri, asilimia 65 walisema kwamba hukerwa na kuchoshwa na rafiki zao, asilimia 60 na wazazi wao, na asilimia 50 na walimu wao. Asilimia 40 walisema kwamba hushindwa kudhibiti hasira yao au huidhibiti kwa kiwango kidogo sana. Mwanafunzi 1 kati ya 5 asema kwamba yeye huondoa hasira kwa kuvunja vitu.“Virusi Visivyoeleweka”
“Damu inaambukizwa virusi visivyoeleweka ulimwenguni pote,” laripoti gazeti New Scientist. “Hakuna ajuaye ikiwa virusi hivyo viitwavyo ‘TT’ ni hatari, lakini watu wanahofu kwamba vyaweza kusababisha maradhi ya ini.” Virusi hivyo, vilivyoitwa TT herufi zinazowakilisha jina la mgonjwa Mjapani aliyekuwa mtu wa kwanza kupatikana na virusi hivyo katika damu, vimepatikana “katika watu wanaotoa damu na katika wagonjwa walio na maradhi ya ini wanaotiwa damu mishipani.” Kwa kweli, uchunguzi ulifunua kuwa watu 8 kati ya 102 kutoka California waliotoa damu ambayo haikuwa na virusi, kutia ndani virusi vya UKIMWI na mchochota wa ini B na C wana virusi hivyo. Inakadiriwa kwamba kiwango cha ambukizo ni asilimia 2 katika Uingereza, asilimia 4 hadi 6 katika Ufaransa, asilimia 8 hadi 10 katika Marekani, na asilimia 13 katika Japani. Wanasayansi “wanaochunguza virusi vya TT ulimwenguni pote wanajitahidi wasisababishe hofu,” yasema makala hiyo, lakini wanatafuta “kujua ikiwa virusi hivyo hutokeza hatari yoyote kwa afya.”
Kola ya Kuokoa Uhai
Wafugaji katika sehemu fulani za Afrika Kusini walikaribia kupoteza asilimia 40 ya mifugo waliozaliwa kila msimu kwa sababu ya kuliwa na mbweha. Jambo hilo halikuwataabisha tu kifedha bali pia lilisababisha ongezeko kubwa sana la mbweha. Jitihada za kuondoa mbweha hazikufua dafu na hata ziliathiri wanyama wengine wa mwitu. Hata hivyo, mbinu ya werevu imebuniwa na kutumiwa katika miaka ya karibuni. Ni kola ya kondoo iliyo ngumu kiasi, inayoweza kurekebishwa na kutumiwa tena, na ambayo haimzuii kondoo kutembea wala haiwadhuru mbweha. Humzuia tu mbweha asiume na kuua kondoo. Kulingana na gazeti Natal Witness, wakulima ambao wamekuwa wakitumia kola hizo “wameripoti kwamba visa vya mauaji yanayosababishwa na mbweha vimekoma kabisa.” Na kwa sababu mbweha wanalazimika kula tu wadudu, wagugunaji, na mizoga, idadi yao inapungua.
Nyigu Ambao ni Seremala
Nyigu aina ya ichneumon hutaga mayai mahali ambapo “hufanywa pagumu na manganisi au zinki iliyobadilishwa kuwa ioni,” laripoti gazeti National Geographic. Nyigu hutumia kifaa chake cha chuma kutoboa sehemu ya ndani kabisa ya mti ili kutaga mayai ndani ya mti huo au katika miili ya vimelea funza wanaopatikana ndani ya mti huo. “Wengine wanaweza kutoboa shimo lenye kina cha sentimeta 7.5 ndani ya mti mgumu,” asema Donald Quicke wa British Imperial College. Nyigu wanapoangua, hula funza wanaotoboa mti kisha wanatafuna mti kwa kutumia midomo yao iliyofanywa kuwa migumu na madini yanayotokana na funza waliowala.
“Hali ya Dharura Isiyo ya Kawaida” Katika India
“Licha ya kuboreshwa kwa afya na hali njema katika miaka michache iliyopita, bado utapiamlo ni ‘hali ya dharura isiyo ya kawaida’ katika India,” laripoti gazeti The Times of India. Utapiamlo hugharimu India zaidi ya dola milioni 230 za Marekani katika utunzaji-afya na kuharibika kwa kiwango cha uzalishaji. Kulingana na ripoti hiyo, zaidi ya asilimia 50 ya watoto Wahindi walio na umri unaopungua miaka minne wana utapiamlo, asilimia 30 ya watoto wanaozaliwa “wana uzito wa chini sana,” na asilimia 60 ya wanawake wana ugonjwa wa kupungukiwa na damu. Mtaalamu mkuu wa maendeleo ya kijamii katika Benki ya Dunia, Meera Chatterjee, asema kwamba “utapiamlo hauharibu tu maisha ya watu na familia bali pia hupunguza matokeo yaletwayo na elimu na huzuia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”
Je, Makasisi Hawana Furaha?
Mara tatu katika miaka sita iliyopita, uchunguzi umefanywa kuhusu mtazamo wa makasisi katika Ufaransa. Kama ulivyochapishwa katika gazeti la Kikatoliki La Croix, uchunguzi wa karibuni zaidi wafunua kwamba asilimia 45 ya Wafaransa hawawaoni makasisi kuwa watu wenye furaha au walioridhika. Kwa kawaida bado watu humwona kasisi kuwa mtu mwenye urafiki kwa wengine na ambaye husikiliza. Hata hivyo, gazeti hilo lasema kwamba “idadi inayozidi kupungua ya Wafaransa humwona kuwa mtu muhimu katika jamii” na kwamba ni asilimia 56 pekee ambao humwona kuwa “shahidi wa Mungu duniani.” Watu wanaopungua 1 kati ya 3 miongoni mwa umma na asilimia 51 ya wanaoenda kanisani kwa ukawaida ndio wanaoweza kumtia moyo mwana au mtu wao wa jamaa awe kasisi.