Tai za Zamani na za Sasa
Tai za Zamani na za Sasa
KWA milenia nyingi wanaume wamependezwa kuremba koo na shingo zao. Mathalani, yapata mwaka wa 1737 K.W.K., Farao wa Misri alimpa Yosefu mkufu wa dhahabu.—Mwanzo 41:42.
Leo katika sehemu nyingi ulimwenguni, wanaume huvalia tai. Kulingana na vyanzo mbalimbali, watu walitumia mavazi fulani kabla tai hazijaanza kutumiwa katika Uingereza na Ufaransa mwishoni mwa karne ya 16. Wanaume walivalia jaketi lililoitwa jaketi la kubana. Walivalia kitambaa cha shingoni ili kujirembesha. Katika visa vingi kitambaa cha shingoni, ambacho kingeweza kuwa na unene wa sentimeta kadhaa, kilikuwa utepe wenye umbo la kisahani uliozingira shingo. Kilishonwa kwa kitambaa cheupe na kufanywa kiwe kigumu ili kidumishe umbo lake.
Hatimaye, kola inayoning’inia ikaanza kutumiwa badala ya kitambaa cha shingoni. Hii ilikuwa kola nyeupe iliyofunika bega zima na ilining’inia juu ya mkono. Kola hizo ziliitwa pia Vandykes. Miongoni mwa wengine, zilivaliwa na Wapiuriti.
Katika karne ya 17, koti refu la ndani lililoitwa kizibao lilivaliwa ndani ya koti refu la kawaida. Mwenye kulivaa alifunika shingo yake kwa vitambaa vilivyoshabihi shali, au skafu. Kitambaa hiki kilizungushwa kwenye shingo zaidi ya mara moja. Ncha zake zilining’inia mbele ya shati. Michoro ya mwishoni mwa karne ya 17 huonyesha kwamba skafu zilipendwa sana wakati huo.
Skafu zilishonwa kwa kitambaa cha pamba, bafta, na hata gidamu. Zile zilizoshonwa kwa gidamu zilikuwa ghali. Yasemekana James wa Pili wa Uingereza alilipa pauni 36 na shilingi 10 kwa ajili ya skafu moja siku ya kutawazwa kwake, bei ghali mno nyakati hizo. Skafu nyingine za gidamu zilikuwa kubwa. Kinyago cha Charles wa Pili katika Makao ya Watawa ya Westminster chaonyesha skafu yake ilikuwa na upana wa sentimeta 15 na urefu wa sentimeta 86.
Mafundo ya aina nyingi yalitumiwa kufunga skafu hizo. Katika visa fulani utepe wa hariri uliwekwa juu ya skafu ili kuishikilia kisha ikafungwa katika fundo kubwa chini ya kidevu. Mtindo huu wa tai uliitwa solitaire. Fundo hilo lilishabihi bow tie ya kisasa. Yasemekana kwamba kulikuwa na angalau njia mia moja za kufunga skafu. Yasemekana kwamba Mwingereza Beau Brummell, aliyechangia sana mitindo ya mavazi ya wanaume, alitumia asubuhi nzima kufunga skafu moja ili kuhakikisha iko sawa kabisa.
Kufikia miaka ya 1860, skafu yenye ncha ndefu ilianza kushabihi tai za mtindo wa kisasa na ikaitwa tai. Pia iliitwa tai yenye fundo la kitanzi. Jina hilo lilitokana na fundo lililotumiwa na madereva wa gari lililokokotwa na farasi wanne. Shati zenye kola zikawa ndio mtindo. Tai ilifungwa chini ya kidevu, na ncha zake ndefu zilining’inia mbele ya shati. Wakati huo ndipo tai za kisasa zilipotokea. Aina nyingine ya tai, bow tie, ilianza kupendwa katika miaka ya 1890.
Leo wengi huiona tai kuwa muhimu kwa sura ya mtu. Watu fulani waweza kuwa na maoni hususa kuelekea mtu wasiyemjua ikitegemea aina ya tai anayovalia. Hivyo, ni jambo la hekima kuvalia tai safi zenye vigezo au rangi zinazofaana na shati, suruali, au jaketi lako.
Wapaswa kufunga fundo unalochagua kwa njia nadhifu. Labda fundo la kitanzi ndilo linalopendwa sana. (Ona mchoro kwenye ukurasa wa 14.) Ni nadhifu na la kiasi nalo hukubaliwa katika sehemu nyingi kunapokuwa na sherehe rasmi. Fundo jingine linalopendwa ni fundo pana isivyo kawaida, ambalo ni kubwa kwa kadiri fulani. Kwa kawaida kibonyeo kidogo hufanyizwa kwenye tai chini tu ya fundo.
Wanaume wengi hawapendi kufunga tai. Hawapendi kusongwa kwenye shingo zao. Hata hivyo, wengi ambao wamepatwa na tatizo hilo wamegundua kwamba saizi ya shati ndiyo humkosesha mtu starehe. Ikiwa una tatizo hilo, hakikisha kwamba kola ya shati yako si ndogo sana. Inapokuwa ya saizi inayofaa, huenda hata usitambue kwamba umefunga tai.
Katika nchi nyingi tai huonwa kuwa sehemu muhimu ya mavazi rasmi au ya kazi. Kwa sababu hiyo wanaume wengi Wakristo huvalia tai wanapojihusisha na sehemu mbalimbali zilizo rasmi za huduma yao. Naam, tai yaweza kumwongezea mwanamume adhama na kumfanya aheshimike.
[Mchoro katika ukurasa wa 14]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Jinsi ya kufunga tai kwa fundo la kitanzi *
1 Anza na ncha ya tai iliyo pana karibu sentimeta 30 chini ya ncha nyembamba, na kuizungusha kwenye upande mwembamba, ukiirudisha upande wa chini.
2 Izungushe tena ncha pana, na kuipitisha kwenye pindo.
3 Ukiwa umeshikilia sehemu ya mbele ya fundo bila kuikaza kwa kidole cha shahada, vuta upande mpana ndani ya pindo kuelekea mbele.
4 Kaza fundo polepole, ukishikilia upande mwembamba na kutelezesha fundo kwenye kola.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 15 Kutoka katika kitabu Shirt and Tie
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mitindo ya tai kuanzia karne ya 17 hadi wakati wa sasa