Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Nimeze Aspirini Kila Siku?

Je, Nimeze Aspirini Kila Siku?

Je, Nimeze Aspirini Kila Siku?

Lifuatalo ni simulizi la kweli lililoelezwa na daktari. Kwa kusikitisha, linaonyesha tatizo linalotukia mara nyingi.

FAMILIA nzima ilikuwa na wasiwasi. Sasa hata daktari mwenyewe alikuwa na wasiwasi pia. “Asipoacha kuvuja damu karibuni,” akasema daktari, “huenda tukahitaji kumtia damu mishipani.”

Mtu huyo alikuwa akivuja damu polepole kwenye matumbo kwa majuma kadhaa, na tatizo lake lilikuwa limebainishwa kuwa uvimbe-tumbo. “Una hakika kwamba hutumii dawa zozote?” akauliza daktari aliyefadhaika.

“La. Ni dawa hizi za dukani tu kwa ajili ya ugonjwa wangu wa baridi-yabisi,” akasema mtu huyo.

Kwa ghafula daktari akaanza kusikiliza kwa makini zaidi. “Ebu nizione.” Alipotazama kibandiko kwa makini, alipata alichokuwa akitafuta. Asidi ya acetylsalicylic! Tatizo hilo lilikuwa karibu kutatuliwa. Mgonjwa alipoacha kutumia msombo uliokuwa na aspirini na kupewa dawa fulani za kuponyesha tumbo na madini ya chuma, aliacha kuvuja damu na polepole chembe za damu zikarudia hali ya kawaida.

Kuvuja Damu Kunakosababishwa na Dawa

Kuvuja damu tumboni kunakosababishwa na dawa ni tatizo kubwa la kitiba leo. Ingawa dawa nyingi zaweza kuhusika, matatizo mengi ya aina hiyo husababishwa na dawa zinazotumiwa kuzuia baridi-yabisi na maumivu. Hizo zatia ndani aina ya dawa zisizo na steroidi za kutibu uvimbe, au NSAIDS. Huenda majina yakatofautiana katika nchi mbalimbali.

Dawa nyingi za dukani huwa na aspirini, na katika nchi nyingi katika miaka ya karibuni watu wanaotumia aspirini kila siku wameongezeka. Kwa nini?

Kutamani Aspirini

Mwaka wa 1995 Harvard Health Letter liliripoti kwamba “kutumia aspirini kwa ukawaida huokoa uhai.” Wakinukuu uchunguzi uliofanywa ulimwenguni pote, ambao umerudiwa mara nyingi tangu wakati huo, watafiti walikata kauli: “Karibu kila mtu aliyepatwa na mshiko wa moyo au ugonjwa wa kupooza, aliye na angina au aliyewahi kufanyiwa upasuaji wa mishipa apaswa kutumia nusu tembe au tembe moja ya aspirini kila siku isipokuwa awe na mzio wa dawa hiyo.” *

Watafiti wengine hudai kwamba wanaume wenye umri unaozidi miaka 50 na vilevile wanawake wanaokabili hatari ya mshiko wa moyo hunufaika kwa kutumia aspirini kila siku. Zaidi ya hayo, kuna uchunguzi unaoonyesha kwamba kutumia aspirini kila siku kwaweza kupunguza hatari ya kansa ya utumbo mpana na kwamba inapotumiwa kwa wingi na kwa muda mrefu yaweza kusaidia kupunguza kiwango cha sukari kwa watu walio na ugonjwa wa kisukari.

Aspirini hufanyaje kazi ili kuandaa manufaa hayo yaliyotajwa? Ijapokuwa mambo yote hayajulikani, kuna uthibitisho kwamba aspirini hufanya vigandisha-damu visinate sana, na hivyo kuvuruga kuganda kwa damu. Inadhaniwa kuwa, hilo husaidia kuzuia mishipa midogo inayoelekea kwenye moyo na ubongo isijizibe, kwa njia hiyo kuepusha madhara kwa viungo muhimu.

Mbona kila mtu hatumii aspirini licha ya manufaa yote yaliyotajwa? Kwanza, bado kuna mambo mengi yasiyojulikana. Hata kiasi kinachofaa hakijulikani. Kuna mapendekezo yanayoanza na tembe moja ya kawaida mara mbili kwa siku hadi tembe moja ya watoto kila baada ya siku moja. Je, kiasi cha wanawake chapasa kutofautiana na cha wanaume? Madaktari hawana hakika. Ingawa aspirini iliyofunikwa ili isifunguke ndani ya tumbo yaweza kuonwa kuwa yenye mafaa, faida inayoletwa na aspirini isiyo na asidi ingali inabishaniwa.

Sababu za Kutahadhari

Ingawa kihalisi aspirini ni msombo wa asili—Wamarekani wa asili walipata misombo ya aspirini kwenye ganda la mti umeao karibu na maji—ina athari nyingi. Kwa kuongezea matatizo ya kuvuja damu kwa watu fulani, aspirini hutatanisha katika hali nyingi, kutia ndani mizio kwa watu wanaoathiriwa na aspirini. Ni wazi kwamba si kila mtu anayepaswa kutumia aspirini kila siku.

Hata hivyo, mtu anayekabili hatari ya mshiko wa moyo au ugonjwa wa kupooza au aliye na hatari zilizo dhahiri, huenda akataka kumwuliza daktari wake juu ya hatari na manufaa za kutumia aspirini kila siku. Bila shaka mgonjwa atataka kuhakikisha kwamba hana matatizo ya kuvuja damu, haathiriwi na aspirini, na hana matatizo yoyote ya tumbo. Matatizo mengine yanayoweza kutokea au utendeano wa dawa yapasa kuzungumziwa pamoja na tabibu kabla mtu hajaanza tiba.

Kama ilivyotajwa mbeleni, dawa za aspirini na zile zinazofanana na aspirini hutokeza hatari ya kuvuja damu. Na huenda kuvuja damu kusijulikane mara moja, na kuendelee kuongezeka polepole baada ya muda. Dawa nyingine pia zahitaji kufikiriwa kwa uangalifu, hasa dawa nyingine za kutibu uvimbe. Hakikisha umemwambia tabibu wako ikiwa unatumia mojawapo ya dawa hizo. Katika visa vingi lingekuwa jambo la busara kuacha kutumia dawa kabla ya upasuaji. Labda hata kupimwa kwa ukawaida kiwango cha damu kwenye maabara kwaweza kusaidia.

Ikiwa twataka kujilinda na matatizo ya wakati ujao, tutii mithali ya Biblia: “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; bali wajinga huendelea mbele wakaumia.” (Mithali 22:3) Kwa habari hii ya kitiba, na tuwe miongoni mwa wenye busara ili tusidhuru afya yetu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Gazeti la Amkeni! halipendekezi tiba fulani hususa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20, 21]

Watu Wawezao Kutumia Aspirini Kila Siku

Watu walio na maradhi ya moyo au kunywea kwa ateri za kichwa (mishipa mikuu ya damu shingoni).

Watu waliowahi kushikwa na ugonjwa wa kupooza unaosababishwa na kuganda kwa damu katika ateri au ugonjwa wa kuziba kwa mishipa ya moyo kwa muda mfupi.

Wanaume walio na umri unaozidi miaka 50 wanaokabili hatari mojawapo au zaidi ya maradhi ya moyo: kuvuta sigareti, msukumo mkubwa wa damu, ugonjwa wa kisukari, kuongezeka kwa kiwango cha kolesteroli, kupungua kwa kolesteroli ya HDL, kunenepa kupita kiasi, kutumia vileo kupita kiasi, historia ya familia ya kupatwa na maradhi ya moyo katika umri wa mapema (mshiko wa moyo kabla ya umri wa miaka 55) au ugonjwa wa kupooza, na mtindo wa maisha wa kukaa kitako.

Wanawake walio na umri unaozidi miaka 50 wanaokabili hatari mbili au zaidi zilizoonyeshwa.

Huenda ukataka kushauriana na tabibu wako kabla ya kufanya uamuzi wowote uhusuo habari hii.

[Hisani]

Kutoka kwa: Consumer Reports on Health