Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Dunia Ni Sayari ya Pekee Sana

Waastronomia wanasema kwamba sayari mpya zaendelea kugunduliwa huku wanasayansi wakipima mtikisiko mdogo—unaosababishwa na nguvu za uvutano za sayari—wa nyota ya mbali inayozungukwa na sayari. Kufikia mwaka wa 1999, yadaiwa kwamba kuna sayari 28 kama hizo nje ya mfumo wetu wa jua. Sayari mpya ambazo zasemekana zimegunduliwa zatoshana na sayari iitwayo Jupita au hata ni kubwa zaidi. Ukubwa wa Jupita wazidi ukubwa wa Dunia mara 318. Yadhaniwa kwamba sayari hizo, sawa na Jupita, zimefanyizwa na heliamu na hidrojeni. Kwa sababu ya umbali wa mizunguko ya sayari hizo, yasemekana haielekei hata kidogo kwamba sayari zozote zinazotoshana na dunia zingeweza kudumu huko. Isitoshe, tofauti na mzunguko-duara wa Dunia ulio umbali wa kilometa milioni 150, sayari hizo huzunguka nyota zake kwa mizunguko ya umbo la yai. Umbali wa mzunguko mmoja kutoka kwa nyota yake waongezeka tokea kilometa milioni 58 hadi kilometa milioni 344. “Imeanza kuwa dhahiri kwamba mizunguko ya duara barabara kama ile tunayoiona kwenye mfumo wetu wa jua ni nadra sana,” asema mwastronomia mmoja.

Kuwasiliana kwa Kupiga Mbinja

Watoto wa shule Wahispania kwenye kisiwa cha Gomera, mojawapo ya Visiwa vya Canary, wanatakiwa wajifunze lugha ya kupiga mbinja iliyotumiwa kwa karne nyingi na wachungaji katika visiwa hivyo, laripoti gazeti The Times la London. Lugha ya mbinja ya Gomera hutumia sauti ili kuiga silabi za usemi, nayo ilibuniwa kwa madhumuni ya kuwasiliana ng’ambo ya mabonde kwenye maeneo yenye milima-milima. Wapiga-mbinja hutia vidole vinywani mwao ili kutokeza sauti mbalimbali, nao hukunja mikono yao iwe na umbo la kikombe ili sauti hiyo iweze kufika umbali wa kilometa tatu hivi. Lugha ya mbinja iliyokaribia kutokomea katika miaka ya 1960, imeibuka tena, na kila mwaka kisiwa hicho huwa na siku ya kupiga mbinja. Hata hivyo kuna mipaka. “Mwaweza kuwasiliana lakini si katika kila jambo,” asema Juan Evaristo, mkurugenzi wa elimu kisiwani humo.

Watoto na Usingizi

Gazeti Parents lasema, “lazima wazazi waweke mipaka si tu kuhusu wakati wa watoto wao kulala, bali pia kuhusu mambo wanayopaswa kufanya kabla ya kulala.” “Kutazama televisheni, kucheza michezo ya kompyuta na vidio, na kuvinjari kwenye Internet ni mambo yenye kusisimua ambayo watoto hujihusisha nayo kupita kiasi. Utendaji chungu nzima wa baada ya shule huwazuia watoto kumaliza kazi yao ya shule kwa wakati unaofaa.” Utafiti huonyesha kwamba kukosa kulala vya kutosha huwaathiri watoto wadogo kwa njia tofauti—wanakuwa machachari na wasioweza kudhibitiwa, ilhali watu wazima wanatulia na kusinzia-sinzia. Tokeo ni kwamba watoto wanaokosa kulala vya kutosha, hushindwa kuwa makini, kusikiliza, kushika wanayofundishwa, na kufanya hesabu wanapokuwa shuleni. Wataalamu wasema kwamba wazazi wapaswa kuweka wakati wa watoto wao kulala na kuliona kuwa jambo muhimu—si jambo la kufanywa kwa sababu tu wamechoka au hawana la kufanya.

UKIMWI Ulimwenguni Pote

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa yasema kwamba “watu zaidi ya milioni 50 [ulimwenguni pote] wameambukizwa virusi vya UKIMWI—idadi inayolingana na idadi ya watu huko Uingereza—na watu milioni 16 wamekufa,” lasema gazeti The Globe and Mail la Kanada. “Utafiti katika nchi tisa za Afrika waonyesha kwamba asilimia 20 ya wanawake zaidi ya wanaume sasa wameambukizwa ugonjwa huo” na kwamba “wasichana huelekea kuambukizwa virusi vya UKIMWI mara tano zaidi ya wavulana.” Peter Piot, mkurugenzi mkuu wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa HIV/AIDS, asema kwamba ugonjwa huo “unaenea kasi” katika Ulaya Mashariki. Ripoti hiyo yasema kwamba “maambukizo ya virusi vya UKIMWI katika uliokuwa Muungano wa Sovieti ni zaidi ya maradufu ya ilivyokuwa miaka miwili iliyopita, ndilo ongezeko kubwa zaidi ulimwenguni.” Wataalamu wanasema kwamba hilo latokana na ongezeko la kutia dawa za kulevya mishipani katika eneo hilo. Zaidi ya nusu ya wale walioambukizwa virusi vya UKIMWI ulimwenguni pote, “huambukizwa ugonjwa huo wakiwa na umri wa miaka 25 nao hufa kabla ya kufikia miaka 35.”

Kansa na Losheni za Kukinga Miale ya Jua

“Kujipaka losheni zenye uwezo mkubwa wa kukinga miale ya jua huwafanya watu wadhani wako salama na kwaweza kuzidisha hatari ya kupata kansa ya ngozi,” laripoti The Times la London. “Wao hufyonza mnururisho zaidi kwa sababu ya kukaa Juani kwa muda mrefu.” Watafiti wa Taasisi ya Ulaya ya Tiba ya Uvimbe huko Milan, Italia, waligundua kwamba wale wanaojipaka losheni yenye kipimo cha 30 cha kukinga miale ya jua walikaa juani kwa asilimia 25 zaidi ya muda unaotumiwa na wale wanaotumia ile yenye kipimo cha 10. Mwanzilishi wa uchunguzi huo, Phillipe Autier asema hivi: “Uwezo wa losheni hizo wa kuzuia kansa ya ngozi, hasa uvimbe mweusi hatari, haujathibitishwa miongoni mwa umma, lakini kuna habari yenye kusadikisha inayoonyesha uhusiano mahususi baina ya muda wa kuota jua na kansa ya ngozi.” Sasa wataalamu wa afya wanaonya dhidi ya kuota jua kwa muda mrefu, haidhuru uwezo wa losheni wa kukinga miale ya jua. Christopher New, meneja wa kampeni ya kupambana na kansa ya Shirika la Uingereza la Elimu ya Afya, ashauri hivi: “Usiache kutumia losheni za kukinga miale ya jua, lakini kumbuka kwamba hilo halimaanishi uote jua kwa muda mrefu zaidi.”

Je, Ni Njia Bora ya Usafiri?

Magari-baiskeli, ambayo huitwa pia riksho, yametumiwa India kwa miongo mingi. Hata hivyo, gazeti Outlook, lasema kwamba hayajabadilika, yangali “na mbao nzito, kiunzi kikubwa cha chuma, viti vinavyoinama kiholela na hayana gia.” Katika miaka ya majuzi, watu wengi hawataki magari hayo yatumiwe kwa sababu ya mkazo unaowapata madereva wake, ambao mara nyingi huwa wazee ambao hawali chakula kinachofaa. Leo, magari-baiskeli hayo yamepata fursa mpya kwa sababu ya uchafuzi mbaya sana wa hewa katika India. Kampuni moja jijini Delhi imebuni magari-baiskeli yaliyo mepesi na laini ili kupunguza ukinzani wa upepo, yenye mfumo wa gia unaorahisisha uendeshaji, kiti cha dereva chenye starehe, usukani mwepesi kwa mikono, na viti vyenye starehe na nafasi tosha kwa abiria. T. Vineet, kiongozi wa mradi huo asema kwamba “yanafaana na hali ya sasa ya kisiasa na kijamii inayokazia mno haki za binadamu na mazingira yasiyo na uchafuzi.” Gazeti Outlook lasema: “Gari-baiskeli linalopuuzwa laweza kuibuka kuwa njia bora ya usafiri katika karne ya 21.”

Fungu la Barua Haliwezi Kubadilishwa

Hadi sasa, “tekinolojia haijafaulu kubuni njia inayoweza kuchukua fungu la barua,” lasema gazeti la Le Figaro. Mnamo 1999 huduma ya posta ya Ufaransa iliwasilisha barua zipatazo bilioni 25. Asilimia 90 ya barua hizo zilikuwa barua za kibiashara, na ni asilimia 10 tu zilizokuwa za kibinafsi. Takriban nusu ya barua zote zilizotumwa zilikuwa na matangazo fulani ya kibiashara, na asilimia 98 ya watu waliohojiwa walikiri kwamba walikuwa wamezisoma kwa uangalifu. Kila siku, wafanyakazi 90,000 wanaopeleka barua sehemu mbalimbali nchini Ufaransa, asilimia 40 wakiwa wanawake, husafiri zaidi ya mara 72,000 ili kupeleka barua milioni 60 zinazotumwa kila siku.

Wenye Kampuni za Bima Wahangaika

Gazeti la Ufaransa Le Monde liliripoti kwamba mwaka wa 1999 ulikuwa “mwaka mbaya kwa bima.” Misiba ya kiasili mnamo 1998 ilisababisha hasara ya dola bilioni 90 za Marekani, dola bilioni 15 kati yake zililipwa na kampuni za bima. Hata hivyo, mwaka wa 1999—uliokumbwa na matetemeko ya ardhi huko Uturuki na Taiwan, vimbunga katika Japani, mafuriko katika India na Vietnam, na misiba mingine—huenda ukagharimu kampuni za bima kiasi kikubwa hata zaidi. Wenye kampuni za bima wanahangaishwa na uwezekano wa kwamba huenda misiba mikubwa itakumba maeneo yenye watu wengi. Mwenye kampuni kubwa zaidi ya bima ulimwenguni aonya juu ya “athari mbaya sana” za kuongezeka kwa joto duniani na “athari za utendaji wa wanadamu kwa tabia ya nchi.”

Mlima Everest Sasa Ni Mrefu Hata Zaidi

“Mlima Everest, mlima mrefu zaidi ulimwenguni, ni mrefu hata zaidi ya walivyofikiri wanasayansi, na bado unarefuka,” yasema ripoti moja ya shirika la habari la Reuters. “Wakitumia mifumo tata ya setilaiti, wakweaji walipima urefu wa Everest kuwa futi 29,035—maili tano na nusu hivi . . . Urefu huo unazidi kwa futi saba ule urefu rasmi wa awali wa futi 29,028, uliopimwa mapema mwaka wa 1954.” Urefu huo mpya ni kimo cha kilele chenye theluji. Kimo halisi cha kilele cha mwamba ulio chini bado hakijulikani. Shirika la National Geographic Society linatumia kipimo hicho kipya kwenye ramani zake. Mbali na kurefuka, mlima huo—hususan safu yote ya milima ya Himalaya—inasonga upande wa kaskazini-mashariki, kuelekea China, kwa milimeta 1.5 hadi milimeta 6 kila mwaka.