“Mzoga” Warudia Uhai
“Mzoga” Warudia Uhai
Na mleta-habari wa Amkeni! katika INDONESIA
MNAMO JULAI 17, 1997, habari za jioni za taifa nchini Indonesia zilikuwa na tangazo lisilo la kawaida. Mmojawapo wa mimea mikubwa zaidi ulimwenguni ulikuwa umechanua maua. Kwa nini kuchanua maua tu kwa mmea kulionwa kuwa muhimu, hata kutangazwe katika habari za jioni? Ni kwa sababu mmea huu ni tofauti—huenda ukachanua maua kwa siku mbili au tatu, mara tatu au nne tu kwa maisha yake ya miaka 40. Baada ya tangazo hilo wageni waliotembelea Bustani ya Mimea ya Bogor, mahali ulipo mmea huo, waliongezeka kwa asilimia 50. Kwa kweli, katika siku moja tu watu zaidi ya 20,000 walikuja kuona mmea huo!
Jina kamili la kisayansi la mmea huo ni Amorphophallus titanum. Wengi wanauita mmea huo kwa kifupi, titan arum, lakini kwa kawaida Waindonesia wanauita ua-mzoga kwa sababu uchanuapo maua huvunda kama mzoga wa samaki au panya uozapo. Uvundo huo wenye kuchukiza huwajulisha nyuki wanaochavusha kwamba mmea umechanua maua.
Mbali na uvundo wake wa pekee, hata ukubwa wake hufanya titan arum kuwa mmea usio na kifani. Ni watu wachache sana walio warefu kuliko mmea uliokomaa wa titan arum. Mmea mmoja katika Bustani ya Mimea ya Bogor ulikuwa na urefu wa meta 2.5 nao ulikuwa na shina pana lenye umbo la tunguu lililopindika-pindika na lenye kipenyo cha meta 2.6. Mmea huu mkubwa wenye maua ulimea kutokana na shina-kiazi lenye uzito wa kilogramu 100 hivi!
Ingawa ua la titan arum ni kubwa sana, ua lake si kubwa kushinda maua ya mimea mingine ulimwenguni, kwa kuwa limefanyizwa kwa maua mengi madogo-madogo.
Titan arum ni mfano mwingine tu uonyeshao ukweli wa maneno ya mtunga-zaburi: “Ee BWANA, Mungu wangu, umefanya kwa wingi miujiza yako . . . Hakuna awezaye kufananishwa nawe.”—Zaburi 40:5.