Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Somo Muhimu Kutoka kwa Kisiwa Kidogo Sana

Somo Muhimu Kutoka kwa Kisiwa Kidogo Sana

Somo Muhimu Kutoka kwa Kisiwa Kidogo Sana

RAPA NUI, ardhi yenye eneo la kilometa 170 za mraba iliyotokana na volkano na isiyo na miti ndiyo nchi yenye wakazi iliyojitenga zaidi ulimwenguni. * Kisiwa chote sasa ni kumbukumbu la kihistoria, kwa kiasi fulani ni kwa sababu ya sanamu zake za miamba ziitwazo moai. Zilitokana na ustaarabu wa kale uliokuwa na ufanisi mno.

Baadhi ya sanamu za moai zilizochongwa kutoka kwa mwamba wa volkano zimefukiwa chini sana hivi kwamba ni vichwa vyake vikubwa tu vinavyoonekana. Pingiti za sanamu nyingine ndizo zinazoibuka ardhini, na moai nyingine bado zimerembwa kichwa kwa shungi la jiwe liitwalo pukao. Lakini sanamu nyingi zisizokamilishwa ziko machimboni au zimetawanyika kwenye barabara za kale, ni kana kwamba wachongaji walitupilia mbali vifaa vyao na kwenda bila kukamilisha kazi. Kuna sanamu mojamoja zilizo wima au zilizopangwa kwa safu zenye sanamu 15 hivi, ambazo huelekeza migongo baharini. Kwa wazi, watalii wengi wamestaajabia mno sanamu za moai.

Katika miaka ya majuzi sayansi imeanza kuelewa si tu fumbo la moai bali pia fumbo la kiini cha kuporomoka kwa ustaarabu wenye ufanisi uliozibuni. Muhimu ni kwamba mambo hakika yanayofunuliwa si yenye manufaa kihistoria tu. Kulingana na Encyclopædia Britannica, yanafunza “ulimwengu wa kisasa somo muhimu.”

Somo hilo lahusu utunzaji wa dunia, hususan mali yake ya asili. Bila shaka, dunia ni tata zaidi na ina mifumo mingi ya kibiolojia kuliko kisiwa kidogo, lakini hilo halimaanishi kwamba twapaswa kupuuza somo la Rapa Nui. Basi acheni tupitie kifupi mambo muhimu katika historia ya Rapa Nui. Simulizi letu laanza mwaka wa 400 W. K. wakati familia za kwanza zilipowasili kwa mitumbwi ya baharini. Kisiwa hicho kilikuwa tu na mamia ya ndege wa baharini wakizunguka angani.

Kisiwa cha Paradiso

Ingawa kisiwa hicho hakikuwa na jamii nyingi za mimea, kilikuwa na misitu ya michikichi, hauhau, na miti ya toromiro, mbali na vichaka, mimea ya misimu, kangaga, na manyasi. Eneo hilo lililojitenga lilikuwa na angalau jamii sita za ndege, kutia ndani bundi, kulastara, rail, na kasuku wengi. Rapa Nui kilikuwa pia “eneo bora la viota vya ndege wa baharini katika Polinesia na labda katika Pasifiki yote,” lasema gazeti Discover.

Huenda wakoloni walileta kisiwani kuku na panya wanaolika, mlo ambao waliuona kuwa mtamu mno. Pia walileta mimea ya mazao: myugwa, kiazi kikuu, kiazi kitamu, ndizi, na miwa. Udongo ulikuwa na rutuba, kwa hiyo walianza kufyeka vichaka na kupanda mara moja—kazi iliyoongezeka kadiri watu walivyoongezeka. Licha ya kwamba Rapa Nui kilikuwa na misitu, eneo lilikuwa dogo na miti ilikuwa michache.

Historia ya Rapa Nui

Twaweza kupata historia ya Rapa Nui kutokana hasa na nyanja tatu: kuchunguza chavuo, elimu-kale, na elimu ya visikuku. Uchunguzi wa chavuo huhusisha kutwaa sampuli za chavuo kutoka kwa masimbi ya vidimbwi na maeneo ya topetope. Sampuli hizo hufunua jamii za mimea na wingi wake kwa mamia mengi ya miaka. Kadiri sampuli ya chavuo ilivyo chini kabisa kwenye masimbi, ndivyo ilivyo ya kale zaidi.

Elimu-kale na elimu ya visikuku hukazia mno mambo kama vile makao, vyombo vya nyumbani, moai, na mabaki ya wanyama ambao waliliwa. Tarehe za kabla ya kuwasili kwa Wazungu zimekadiriwa tu, na makisio mengi hayawezi kuthibitishwa kwa kuwa wakazi wa Rapa Nui waliandika rekodi zao kwa maandiko ya kale ya picha ambayo hayaeleweki kwa urahisi. Kwa kuongezea, matukio fulani yaliyoorodheshwa chini huenda yalitukia katika vipindi tofauti vya wakati. Tarehe zote zilizoandikwa kwa herufi nzito, ni za Wakati wa Kawaida.

400 Masetla Wapolinesia wapatao 20 hadi 50 wawasili, labda kwa mitumbwi yenye urefu wa meta 15 hivi huku kila mtumbwi ukiweza kubeba uzito wa kilogramu 8,000.

800 Chavuo ya miti katika masimbi yapungua, ikidokeza kwamba ukataji-miti waendelea. Chavuo ya nyasi yaongezeka huku nyasi ikisambaa kwenye maeneo yaliyofyekwa vichaka.

900-1300 Takriban theluthi ya mifupa ya wanyama walionaswa kwa ajili ya kuliwa wakati huo ni mifupa ya pomboo. Wakazi wa kisiwani wasafirisha pomboo kutoka baharini kwa mitumbwi mikubwa iliyotengenezwa kwa mashina ya michikichi mikubwa. Miti pia hutumiwa kutengenezea vifaa vya kusafirisha na kuinulia moai, uchongaji wa sanamu hizo umepamba moto. Kuenea kwa kilimo na uhitaji wa kuni unazidi kuharibu misitu hatua kwa hatua.

1200-1500 Uchongaji wa sanamu wafikia kilele. Wakazi wa Rapa Nui walitumia mali, nishati na ustadi mwingi katika uchongaji wa moai na majukwaa yake ya kisherehe. Mtaalamu wa elimu-kale Jo Anne Van Tilburg aandika: “Mfumo wa kijamii wa Rapa Nui ulikazia kwa dhati uchongaji wa sanamu nyingi na kubwa zaidi.” Yeye aongezea kwamba “takriban sanamu 1,000 zilichongwa katika muda wa miaka 800 hadi 1,300 . . . , sanamu moja kwa kila watu saba hadi tisa inapokadiriwa wakati wa kilele cha idadi ya watu.”

Yaonekana sanamu za moai hazikuabudiwa, ingawa zilitumiwa katika sherehe za ibada za mazishi na kilimo. Huenda zilionwa kuwa makao ya viumbe wa roho. Yaonekana kwamba ziliwakilisha pia nguvu, hadhi na kizazi cha mchongaji.

1400-1600 Idadi ya watu yafikia kilele cha kati ya 7,000 na 9,000. Sehemu zilizobaki za misitu zatokomea, kwanza kwa sababu ya kutoweka kwa ndege wa asili, ambao walichavusha miti na kutawanya mbegu zake. “Aina zote za ndege wa asili wa barani walitoweka kabisa,” lasema gazeti Discover. Panya walichangia pia uharibifu wa misitu; uthibitisho waonyesha kwamba walitafuna mbegu za michikichi.

Punde si punde mmomonyoko wa udongo waanza, vijito vyaanza kukauka, na maji yawa haba. Mifupa ya pomboo yatoweka karibu mwaka wa 1500, labda kwa sababu ya ukosefu wa miti mikubwa vya kutosha kuweza kutengenezea mitumbwi. Sasa hakuna njia ya kutoroka kisiwani. Ndege wa baharini wanaliwa wote kwa sababu ya uhaba mkubwa wa chakula. Kuku zaidi wanaliwa.

1600-1722 Kuharibiwa kwa miti, kutumia ardhi kupita kiasi, na udongo kukosa rutuba kwachangia uharibifu mkubwa wa mazao. Njaa kuu inaenea. Wakazi wa Rapa Nui wagawanyika katika vyama viwili vinavyopingana. Dalili za kwanza za machafuko ya kijamii zazuka, labda hata za ulaji wa nyama ya mwanadamu. Ni enzi ya ubarobaro. Watu wahamia mapangoni ili kupata ulinzi. Idadi ya watu yashuka ghafula na kufikia takriban watu 2,000 yapata mwaka wa 1700.

1722 Mvumbuzi Mholanzi Jacob Roggeveen ndiye Mzungu wa kwanza kuvumbua kisiwa hicho. Alikivumbua siku ya Ista, kwa hiyo akiita Kisiwa cha Ista. Aandika alivyoona mwanzoni: “Hali mbaya ya [Kisiwa cha Ista] yaonyesha tu ufukara na ukame usio wa kawaida.”

1770 Wakati huo ukoo mbalimbali wenye uhasama wa wakazi waliosalia wa Rapa Nui waanza kubwaga chini sanamu za maadui wao. Mvumbuzi Mwingereza Kapteni James Cook azurupo kisiwa hicho mnamo 1774, yeye aona sanamu nyingi zilizoangushwa.

1804-1863 Mawasiliano pamoja na ustaarabu mwingine yanawiri. Utumwa, ulioenea mno katika Pasifiki, na maradhi zasababisha hasara kubwa. Utamaduni wa kale wa Rapa Nui waporomoka kabisa.

1864 Kufikia sasa sanamu zote za moai zabwagwa chini, nyingi zikiwa zimekatwa vichwa.

1872 Wenyeji wa asili wapatao 111 tu ndio wanaosalia kisiwani.

Kisiwa cha Rapa Nui kikawa jimbo la Chile mwaka wa 1888. Katika miaka ya karibuni idadi ya watu wa jamii mbalimbali walio Rapa Nui ilifikia 2,100 hivi. Chile ilitangaza kisiwa chote kuwa kumbukumbu la kihistoria. Sanamu nyingi zilisimamishwa tena ili kuhifadhi utamaduni na historia ya pekee ya Rapa Nui.

Somo Kwetu Leo

Mbona wakazi wa Rapa Nui hawakutambua hatari iliyowakabili na kujaribu kuepuka msiba? Fikiria maoni ya watafiti mbalimbali kuhusu hali hiyo.

“Msitu . . . haukutoweka tu siku moja—ulitoweka polepole, kwa miongo mingi. . . . Mkazi yeyote wa kisiwa hicho ambaye angejaribu kuonya watu kuhusu hatari za kuendelea kukata miti angepuuzwa na wachongaji, warasimu, na viongozi wenye ubinafsi.”—Discover.

“Hasara waliyopata kwa sababu ya kuzingatia mawazo yao ya kiroho na kisiasa ilibadili kabisa kisiwa hicho na umbo lake la kiasili.”—Easter Island—Archaeology, Ecology, and Culture.

“Hali iliyopata Rapa Nui yaonyesha kwamba tamaa isiyodhibitiwa ya kuharibu mazingira kupita kiasi haikutokezwa tu na nchi zinazositawi; ilisababishwa na mtazamo wa mwanadamu.”—National Geographic.

Matokeo yatakuwa nini leo endapo mwanadamu hatabadili ule unaoitwa eti mtazamo wake? Hali itakuwaje mwanadamu akiendelea kuangamiza mfumo wa mazingira wa dunia yetu—kito kilicho angani? Mwandikaji mmoja alisema kwamba ni heri sisi kuliko watu wa Rapa Nui. Tunaonywa na mifano ya “historia ya jamii nyingine zilizoangamia.”

Lakini, huenda tukauliza, Je, wanadamu wanatilia maanani historia hiyo? Uharibifu mkubwa mno wa misitu na kutoweka kasi kwa viumbe duniani kwaonyesha kwamba hawafanyi hivyo. Linda Koebner asema hivi katika kitabu Zoo Book: “Kutoweka kwa jamii moja, mbili au hamsini kutatokeza athari tusizoweza kubashiri. Kutoweka kwa viumbe kunaleta mabadiliko kabla hatujaelewa madhara yake.”

Mtu mharibifu anayeng’oa msumari mmoja-mmoja kutoka kwenye ndege hajui ni upi utakaoifanya ianguke; lakini msumari huo muhimu ung’olewapo, ndege haina budi kuanguka, japo huenda isianguke katika safari ifuatayo. Hali kadhalika, wanadamu wanaharibu “misumari” hai ya dunia kwa kiwango cha zaidi ya jamii 20,000 kila mwaka, bila dalili za kukoma! Ni nani ajuaye itakapokuwa kuchelewa mno? Na je, kujua hivyo mapema kutawasaidia kweli watu wabadilike?

Kitabu Easter Island—Earth Island kilitoa maelezo haya muhimu: “Mtu aliyekata mti wa mwisho [katika Rapa Nui] angeweza kuona kwamba ulikuwa mti wa mwisho. Lakini bado akaukata.”

“Hatuna Budi Kubadili Dini Yetu”

“Iwapo kutakuwa na tumaini lolote,” chaongezea kitabu Easter Island—Earth Island, “ni wazo muhimu la kwamba hatuna budi kubadili dini yetu. Miungu yetu ya sasa ya usitawi wa kiuchumi, sayansi na tekinolojia, kupanda daima kwa kiwango cha maisha, na mashindano tunayopenda—ndiyo mambo tunayoona kuwa muhimu zaidi—ni kama sanamu kubwa kwenye majukwaa katika Kisiwa cha Ista. Kila kijiji kilishindana na vijiji jirani kuchonga sanamu kubwa zaidi. . . . Walitia jitihada zaidi na kutumia mali nyingi . . . , lakini ilikuwa kazi bure kuchonga, kusafirisha na kusimamisha sanamu hizo.”

Mtu mmoja mwenye hekima alisema hivi wakati mmoja: “Njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Muumba wetu ndiye pekee anayeweza kutuonyesha jinsi ya ‘kuelekeza hatua zetu.’ Ndiye pekee anayeweza kutuokoa kutokana na hali yetu ya kuhuzunisha. Anaahidi kufanya hivyo katika Neno lake, Biblia—kitabu ambacho pia kinarekodi mifano mingi mizuri na mibaya ya ustaarabu wa kale. Kwa kweli, kitabu hicho chaweza kuwa ‘mwanga wa njia yetu’ katika nyakati hizi zenye giza.—Zaburi 119:105.

Hatimaye, njia hiyo itawaongoza wanadamu watiifu kwenye paradiso ya amani na usitawi—ulimwengu mpya utakaotia ndani kisiwa kidogo katika Pasifiki Kusini kinachoitwa Rapa Nui.—2 Petro 3:13.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Ijapokuwa wenyeji hujiita na kuita kisiwa chao Rapa Nui, kwa kawaida huitwa Kisiwa cha Ista, na wenyeji huitwa Wakazi wa Kisiwa cha Ista.

[Ramani katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kisiwa cha Ista

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 23]

“Walichonga takriban sanamu 1,000”

[Picha katika ukurasa wa 25]

Dunia nzima, kutia ndani visiwa vilivyo mbali sana, itakuwa paradiso