Uenezaji-habari Waweza Kufisha
Uenezaji-habari Waweza Kufisha
“Uwongo huenea upesi sana.”—Yadaiwa ni msemo wa MARK TWAIN.
“EWE Myahudi duni!” akafoka mwalimu wa shule, huku akimzaba kofi mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka saba. Kisha akasihi darasa limkaribie na kumtemea mate usoni.
Mwalimu na mwanafunzi huyo—aliyekuwa mpwa wake wa kiume—walifahamu vyema kabisa kwamba mvulana huyo na wazazi wake hawakuwa wa uzao wa Kiyahudi. Wala dini yao haikuwa ya Kiyahudi. Badala yake, walikuwa Mashahidi wa Yehova. Kwa kutumia kwa faida habari zenye chuki na zilizoenea dhidi ya Wayahudi, mwalimu huyo alikuwa akiendeleza chuki kuelekea mwanafunzi wake. Kwa miaka mingi mwalimu huyo na wanafunzi wake walikuwa wameambiwa na kasisi wao kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa watu wa kudharaulika. Ilisemekana kwamba wazazi wa mvulana huyo walikuwa Wakomunisti na pia maajenti wa CIA (Shirika la Ujasusi la Marekani). Kwa hiyo wanadarasa wa mwanafunzi huyo walikuwa na hamu ya kumkaribia ili kumtemea mate usoni “Myahudi duni.”
Kijana huyo alivumilia yote hayo. Hali ilikuwa tofauti kuhusu Wayahudi milioni sita waliokuwa wakiishi Ujerumani na nchi jirani yapata miaka 60 iliyopita. Uenezaji mwovu wa habari ndio uliochangia kuangamizwa kwa Wayahudi katika vyumba vya gesi ya sumu vya Nazi na kambi za mateso. Maoni mabaya sana yaliyoenea pote, yasiyochunguzwa, na uhasama mwovu dhidi ya Wayahudi ulifanya wengi wawaone kuwa maadui ambao ilikuwa lazima na pia haki kuwaangamiza. Katika kisa hicho, uenezaji-habari potovu ukawa silaha ya kuangamiza umati wa watu.
Naam, uenezaji-habari waweza kuonyeshwa waziwazi kwa kutumia mifano yenye chuki kama vile swastika au kwa njia ya hila kupitia mzaha usiopendeza. Mbinu zake zenye kushawishi hutumiwa kwa ukawaida na madikteta, wanasiasa, makasisi, watangazaji, wauzaji, waandishi-habari, watu mashuhuri katika redio na televisheni, maajenti wa habari, na wengine wanaopenda kuathiri mawazo na tabia.
Bila shaka, ujumbe unaopitishwa kwa uenezaji-habari waweza kutumiwa kutimiza mambo yanayofaidi jamii, kama vile katika kampeni za kupunguza madereva walevi. Lakini uenezaji-habari waweza kutumiwa pia kuendeleza chuki dhidi ya makabila au dini ndogo-ndogo au kushawishi watu wanunue sigareti. “Kila siku twashambuliwa na ujumbe mwingi wenye kushawishi,” wasema watafiti Anthony Pratkanis na Elliot Aronson. “Huo hushawishi mtu si kupitia mazungumzo na majadiliano, bali hutumia kwa faida mambo yenye kusisimua na hisia zetu za msingi za kibinadamu. Kizazi chetu ni cha uenezaji-habari uwe utaleta faida au hasara.”
Uenezaji-habari umetumiwaje kuathiri fikira na matendo ya wanadamu katika karne zote? Unaweza kufanya nini ili kujilinda na uenezaji-habari hatari? Je, kuna chanzo cha habari chenye kutegemeka? Maswali hayo na mengineyo yatazungumziwa katika makala zifuatazo.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Uenezaji-habari ulitumiwa kuwadhuru Wayahudi wakati wa yale Maangamizi Makubwa