Je, Uhai Unakosa Kuthaminiwa kwa Vyovyote?
Je, Uhai Unakosa Kuthaminiwa kwa Vyovyote?
“Ulimwengu hauthamini uhai. Uuaji waweza kutekelezwa kwa mamia machache ya pauni [za Uingereza] na kuna watu chungu nzima walio tayari kukodiwa ili kuua.”—The Scotsman.
Mnamo mwezi wa Aprili 1999, kisa kilichoshtua ulimwengu mzima kilitukia huko Littleton, Colorado, Marekani, wakati vijana wawili waliposhambulia kwa jeuri Shule ya Sekondari ya Columbine na kuwaua watu 15. Uchunguzi ulionyesha kwamba mmojawapo wa washambuliaji hao alikuwa na Web site kwenye Internet ambamo alikuwa ameandika: “WAFU HAWAJADILIANI!” Washambuliaji wote wawili walikufa katika msiba huo.
UUAJI-KIMAKUSUDI umeenea ulimwenguni pote, kila siku idadi isiyohesabika ya watu huuawa kinyama. Mwaka wa 1995, nchi ya Afrika Kusini iliongoza ulimwenguni ikiwa na kiwango cha mauaji cha 75 kwa kila wakazi 100,000. Uhai hauthaminiwi hususan katika nchi moja ya Amerika Kusini, ambako zaidi ya watu 6,000 waliuawa kwa sababu za kisiasa mwaka wa 1997. Mauaji yanayotekelezwa na wauaji wa kukodiwa yamekuwa jambo la kawaida. Ripoti moja juu ya nchi hiyo yasema: “Jambo linalotisha ni kwamba uuaji-kimakusudi wa watoto umeongezeka sana: Mnamo mwaka wa 1996, watoto 4,322 waliuawa, ongezeko la asilimia 40 kwa muda wa miaka miwili tu.” Hata watoto pia wameanza kuwa wauaji—wanaua watoto wengine na wazazi wao wenyewe. Kwa kweli uhai hauthaminiwi kwa vyovyote.
Mbona Kuna “Utamaduni wa Mauaji”?
Mambo hakika na takwimu hizo zaonyesha nini? Ongezeko la kutostahi uhai. Watu wenye tamaa ya uongozi na ya fedha huua bila wasiwasi wowote. Mabwanyenye wa ulanguzi wa dawa za kulevya huagiza mauaji ya familia nzima-nzima. Wao hupunguza uzito wa uuaji wanaotekeleza kwa kutumia misemo kama “kipigo,” “kufutilia mbali,” “kuondosha,” au “kukomesha” wahasiriwa wanaolengwa. Maangamizi ya jamii nzima-nzima na
uuaji-kimakusudi wa kikabila yameongeza idadi ya wanaouawa na hivyo kudunisha uhai wa binadamu. Tokeo ni kwamba visa vya mauaji vimekuwa habari za kawaida kwenye televisheni kotekote ulimwenguni.Zingatia pia jeuri na machafuko yanayotukuzwa kwenye televisheni na sinema, inaonekana kwamba jamii yetu imezingirwa na utamaduni wenye kuchukiza unaokazia mauaji. Kichapo Encyclopædia Britannica chasema hivi kuhusiana na jambo hilo: “Katika nusu ya mwisho ya karne ya 20, habari za mauaji zimekuja kupendwa mno isivyo kawaida. Jambo la kushangaza ni kwamba, hapo awali, habari za mauaji ziliepukwa kabisa katika utafiti wa kina wa kisayansi, na kwa kadiri fulani katika makisio ya kifalsafa.” Josep Fericgla, profesa Mkataloni wa elimu ya utamaduni wa binadamu asema, “mauaji yamekuwa uamuzi wa mwisho katika jamii zetu, na hivyo yamekuwa mojawapo ya vyombo muhimu sana vya kudhibiti mawazo leo.”
Huenda sifa kuu ya “utamaduni [huu] wa mauaji” ikawa dhana inayopendwa sana ya kwamba nguvu, mamlaka, fedha, na raha ni muhimu zaidi kuliko uhai wa binadamu na viwango vya adili.
“Utamaduni [huu] wa mauaji” huenezwaje? Wazazi wanaweza kufanya nini ili kuzuia athari hii yenye kufisidi iliyoenea na ambayo inawaathiri watoto wao? Hayo ni baadhi ya maswali yatakayojibiwa katika makala zifuatazo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
Uhai Una Thamani Gani?
▪ “Washiriki wachanga wa magenge [huko Mumbai, India] wanahitaji fedha sana, waweza kuua kwa kulipwa kiasi kidogo mno cha rupia 5,000 [dola 115 za Marekani].”—Far Eastern Economic Review.
▪ “Alimwua Mpita-Njia Aliyemnyima Sigareti.”—Kichwa cha Habari kwenye gazeti La Tercera, Santiago, Chile.
▪ “Mkataba wa kumwua mtu huko Urusi [mwaka wa 1995] uligharimu dola 7,000 za Marekani kwa wastani . . . Mauaji ya mpango yameongezeka sana sambamba na mabadiliko makubwa ya kiuchumi yaliyotukia Urusi baada ya kuporomoka kwa ukomunisti.”—Shirika la habari la Reuters, yatokana na ripoti moja katika gazeti Moscow News.
▪ “Wakala mmoja wa mali isiyohamishika huko Brooklyn alikamatwa . . . na kushtakiwa kwa kosa la kumlipa kijana mmoja sehemu ya malipo ya dola 1,500 za Marekani ili aweze kumwua mke wake mjamzito na mama mkwe wake.”—The New York Times.
▪ ‘Malipo ya kumwua mtu katika Uingereza yanapungua. Malipo ya kumwua mtu yameshuka toka pauni 30,000 miaka mitano iliyopita hadi kiasi ambacho wengi wanaweza kumudu cha pauni 5,000 hadi pauni 10,000.’—The Guardian.
▪ ‘Mafia waonekana kuwa si kitu walinganishwapo na magenge katili ya eneo la Balkani. Huyu ni mhalifu mpya, mwenye sheria mpya na silaha mpya. Ana mabomu na bunduki mimina-risasi naye hakawii kuzitumia.’—The Guardian Weekly.