Kurekebisha Saa—Je, Ni Wazo Lililotolewa Mapema Mno?
Kurekebisha Saa—Je, Ni Wazo Lililotolewa Mapema Mno?
Kwa nini watu walio wengi wahitaji kurekebisha saa zao mara mbili kwa mwaka? Baadhi ya watu wanaona ni tatizo kubwa wakati saa zao zinapohitaji kurekebishwa kwenda ama mbele ama nyuma. Nazo zapasa kusogezwa mbele lini na kurudishwa nyuma lini? Jambo hilo lilitokana na nini? Ni nani aliyeanzisha wazo la kurekebisha saa?
Kichapo Encyclopædia Britannica chasema kwamba Benjamin Franklin alipendekeza wazo hilo la kurekebisha saa, ili watu waweze kutumia kipindi cha mwangaza wa mchana kwa manufaa zaidi, mnamo 1784. Zaidi ya karne moja baadaye, Mwingereza aitwaye William Willett alilifanyia jambo hilo kampeni. Hata hivyo, Willett akafa kabla ya Bunge kulifanya kuwa sheria.
Mwandishi Mwingereza Tony Francis anasema kwamba Willet, mjenzi stadi wa Chislehurst, Kent, aligundua umuhimu wa kurekebisha saa, alipokuwa akimwendesha farasi wake asubuhi moja mapema majira ya kiangazi huko Petts Wood. Aliona kwamba madirisha ya nyumba nyingi yalikuwa yamefungwa. Lazima alikuwa akifikiri ‘Watu hupoteza mwangaza wa mchana kama nini!’ Alianza kufanya kampeni katika Bunge la Uingereza ili kuwe na sheria ya kurekebisha saa. Ikiwa wangesogeza saa zao dakika 80, yaani kuzisongeza saa zao dakika 20 mara nne wakati wa miezi ya masika na ya kiangazi na kuzirudisha nyuma wakati wa kupukutika kwa majani, wangekuwa na wakati zaidi wenye mwangaza jioni.
Francis ataarifu kwamba Willett aliandika hivi katika mojawapo ya vikaratasi vyake: “Mwangaza ni mojawapo ya zawadi kubwa zaidi ambayo Muumba amewapa wanadamu. Huku tukiwa na mwangaza wa mchana, uchangamfu upo, mahangaiko si mazito sana, nao ujasiri wa kupambana na maisha unaongezeka.”
Mfalme Edward wa Saba hakungoja sheria ipitishwe na Bunge. Alitangaza kwamba Sandringham, jumba lake la kifalme lililo katika shamba lake la ekari 19,500, kuwa sehemu ya kuokoa mwangaza wa mchana. Alifanya vivyo hivyo katika mashamba ya kifalme ya Windsor na Balmoral.
Ni nini kilichowashawishi mwishowe wanasiasa kukubali rasmi jambo hilo la kurekebisha saa? Walitaka kuhifadhi mafuta wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza kwa kupunguza uhitaji wa kuwasha taa! Watu katika nchi nyingine walifanya vivyo hivyo kwa sababu kama hizo. Uingereza ilirekebisha saa zake maradufu wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Jambo hilo lilitokeza tofauti ya muda wa saa mbili wakati wa majira ya kiangazi na muda wa saa moja wakati wa majira ya baridi kali.
Kuna nguzo ya ukumbusho kwa heshima ya William Willett huko Petts Wood, ona picha iliyopo upande wa kulia. Nguzo hiyo ni kwa heshima ya “mpiganaji asiyechoka wa ‘wakati wa kiangazi’.” Maandishi yaliyoandikwa chini ya saa ya kivuli yasema hivi: “Horas non numero nisi aestivas,” yanayomaanisha “sihesabu saa, ila saa za majira ya kiangazi.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
With thanks to the National Trust