Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Biashara ya Tufeni Pote Ningependa kuwashukuru sana kwa ajili ya habari iliyo wazi iliyotolewa kwenye makala “Biashara ya Tufeni Pote—Jinsi Inavyokuathiri.” (Septemba 8, 1999) Sasa naelewa zaidi kinachosababisha pengo kati ya mataifa tajiri na maskini.
M. Z., Italia
Najifunza somo la uchumi chuoni na ndipo tu nimemaliza kusoma habari za biashara ya kimataifa. Makala yenu ilikuwa na mambo ambayo hatukusoma darasani. Nitayatumia nifanyapo mtihani mwezi ujao.
H. N., Zimbabwe
Je, Ni Leza Isiyofaa? Ile habari katika “Kuutazama Ulimwengu” yenye kichwa “Je, Ni Tiba ya Meno Isiyo na Maumivu?” (Oktoba 22, 1999) ilizungumzia matumizi ya “erbi: leza ya YAG kwa ajili ya upasuaji wa meno.” Je, haingepasa kuwa “neodimi: YAG”?
D. B., Kanada
Ingawa Chuo cha Tiba ya Meno kwa Kutumia Leza husema kuwa neodimi: leza ya YAG ndilo “wimbi linalotumiwa kwa kawaida katika tiba ya meno,” makala moja katika jarida “The Journal of the American Dental Association” (Agosti 1997, Buku la 128, ukurasa wa 1080-1087) husema kuwa matumizi ya erbi: leza ya YAG yanapendekezwa na gazeti “FDA Consumer.”—Mhariri.
Je, Wajua? Kuhusiana na maswali ya je, wajua?, mbona msichapishe majibu yake kwenye toleo linalofuata? Sikuzote mimi husoma gazeti lote kwanza kisha hujibu maswali hayo baadaye, na ni vigumu sana kusoma ukurasa wenye majibu hayo bila kuyatupia jicho.
J. L., Marekani
Twathamini dokezo hilo. Hata hivyo, kwa kuwa “Amkeni!” hugawanywa mlango kwa mlango, wasomaji wetu wengi hawapati matoleo yote yanavyofuatana. Kwa hiyo twaona kwamba inafaa kuweka majibu kwenye toleo hilohilo. Jitahidi kutoangalia majibu kabla ya kujibu maswali!—Mhariri.
Uchawi Nina umri wa miaka 13, na nilikutana na msichana mmoja shuleni anayeitikadi uchawi. Siku moja aliniuliza maoni yangu kuhusu uchawi. Nikamwambia kuwa mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova na kwamba siitikadi kutumia uwezo wa kimafumbo. Alikasirika sana na mara nyingi yeye huzusha swali hilo tena. Nilimwomba Yehova msaada, nami nikaupata kupitia makala “Maoni ya Biblia: Ni Nini Husababisha Uchawi?” (Novemba 8, 1999) Nilimpa makala hiyo, na tangu aisome, hajaniuliza tena maoni yangu juu ya uchawi.
K. E., Marekani
Mlo Mtamu Wenye Uvundo Asanteni kwa ajili ya makala “Surströmming—Mlo Mtamu Wenye Uvundo.” (Julai 8, 1999) Hatukuwa tumewahi kuusikia, kwa hiyo tukazungumza na mwamini mwenzetu anayetoka Sweden. Aliueleza mlo huo mtamu kwa shauku sana kisha akatushangaza baadaye kwa kutupa makopo mawili ya mlo huo. Tulikaribisha watu kadhaa kutoka kutaniko letu ili wale nasi mlo huo. Tulitii onyo lililotolewa kwenye makala hiyo kwa kufunua makopo hayo tukiwa nje bustanini. Ni vema kwamba tulifanya hivyo. Mlo huo ulivunda kupindukia tusivyotarajia! Hatungeweza kubaini ladha yake! Lakini kama haingelikuwa makala hiyo, hatungelikuwa kamwe na tukio hilo lisilosahaulika.
C. B., Ujerumani
RSD Imenichukua muda wa miaka miwili kabla ya kuwaandikia ili kuwashukuru kwa ajili ya makala “RSD—Ugonjwa wa Kukoroweza na Wenye Maumivu.” (Septemba 8, 1997) Sikuwa nimewahi kujua ugonjwa huo hadi nilipogundua kwamba mkono wangu wa kushoto ulikuwa umeambukizwa. Daktari wangu wa maungo alisema kwamba alijifunza mengi kutokana na makala hiyo kuliko alivyojifunza chuoni. Hata hivyo, asanteni kwa makala hiyo. Imenisaidia sana kustahimili hali.
L. M. K., Marekani