Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Matatizo ya Chombo cha Angani cha Mihiri

Mnamo Desemba, NASA ilishindwa kurudisha mawasiliano kati yake na chombo chake cha angani kiitwacho Mars Polar Lander kilipoingia katika angahewa ya Mihiri. Tatizo hilo lilitokea miezi miwili tu baada ya kushindwa kwa chombo cha Mars Climate Orbiter, kilichokusudiwa kusaidia kupasha habari kutoka Mars Polar Lander hadi dunia. Sababu ya kushindwa kwa Mars Polar Lander haijulikani. Hata hivyo, sababu moja ya kutofaulu kwa Mars Climate Orbiter ni kwamba maelekezo ya uendeshaji wa chombo hicho yaliandikwa kwa vipimo vya Uingereza badala ya vipimo vya mfumo wa meta utumiwao kwa kawaida! Tofauti hiyo ilizuia kupashana habari za uendeshaji. Ijapokuwa wamevunjika moyo kwa sababu ya hasara hiyo, wanasayansi wa NASA wanakusudia kuendelea kutimiza miradi yao, lasema shirika la habari la CNN. Miradi hiyo ni ya “kujifunza kuhusu hali-hewa na jiolojia ya sayari hiyo nyekundu; kutafuta ishara za uhai; na kufanya matayarisho kwa ajili ya kupeleka watu huko ili wafanye uvumbuzi.”

Maandishi ya Kichina Yanayoelekea Kutoweka

Nu Shu ni mfumo wa maandishi usio na kifani, ambao umetumiwa na wanawake pekee, kwa karne nyingi katika vijiji vidogo Mkoani Hunan, kusini mwa China. Maandishi hayo yaliundwa na wanawake wakulima wakati wasichana walipokatazwa kupata elimu. Zile herufi 700 za mfumo huo ni za kutamkwa; tofauti na maelfu ya herufi za lugha ya ishara ya Kichina. Maandishi ya Nu Shu huandikwa kwa mistari myembamba iliyopindika na kuegama ambayo, Yang Yueqing aliyetayarisha sinema kuhusu Nu Shu, asema kuwa “ni mazuri na ni wazi kwamba wanawake ndio walioyabuni, . . . na pia ni ya kisanaa kwelikweli kwa sababu hufumwa katika kitambaa na kushonwa kwa mapambo,” laripoti gazeti la The Sunday Times la London. Wanawake hao walieleza mapokeo yao na habari zao za maisha katika nyimbo na mashairi yaliyoandikwa kwa maandishi ya Nu Shu. Baada ya mwaka wa 1949 wanawake walipopata usawa, maandishi ya Nu Shu hayakutumiwa sana tena. Leo kuna watu watatu tu wajulikanao, wanaojua kuandika lugha hiyo, nao ni wanawake wazee.

Michezo ya Vidio Yenye Jeuri

Uchunguzi wa vijana 600 waliozoea kucheza michezo ya vidio unaonyesha kwamba, michezo mingi “inafundisha watoto wetu kufurahia jeuri,” aonya mtafiti Brent Stafford wa Chuo Kikuu cha Simon Fraser huko British Columbia, Kanada. Gazeti la Maclean’s laripoti hivi: “Wachezaji sugu wanaopenda michezo yenye jeuri nyingi ‘huwaua’ ‘wahusika wa michezo’ 1,000 katika jioni moja tu, nao uuaji huo mara nyingi huonekana kuwa halisi sana.” Uchunguzi huo ulionyesha jinsi ambavyo michezo ya vidio imebuniwa ili kuchochea hisia za mchezaji na “kufanya vijana kuwa sugu kuelekea jeuri, na hata uuaji.” Biashara ya kutengeneza michezo ya vidio huchuma dola bilioni 17 za Marekani kila mwaka, nayo “huchuma fedha nyingi kuliko biashara ya kutengeneza filamu na programu za televisheni.” Stafford awasihi wazazi wachunguze michezo ya watoto wao na kuwa macho kuona wakianza kuwa na mwelekeo wowote wa kufanya jambo lisilopatana na akili.

Habari za Vita

“Kwa wakati huu kuna vita 27 vinavyoendelea ulimwenguni,” laripoti gazeti la Psychology Today. Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm yatoa habari kwamba zaidi ya Waliberia 150,000 waliangamizwa katika vita yao ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa miaka 7, nao watu 500,000 wameuawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 15 vya Angola. Watu zaidi ya 37,000 wameuawa katika mapigano nchini Uturuki tangu 1984, nao watu zaidi ya 60,000 wameuawa vitani nchini Sri Lanka tangu 1983. “Kwa ujumla, zaidi ya watu milioni 20—wengi wao raia—wameuawa katika vita tangu Vita ya Ulimwengu ya Pili,” lasema gazeti hilo. “Huenda ikawa vita havitaepukika . . . kwa sababu ya uchumi. Vita ni mojawapo ya biashara kubwa zaidi duniani, huku vifaa vya vita vya dola bilioni 800 za Marekani vikitumiwa kila mwaka, nayo inaleta mapato makubwa pia.” Makala hiyo ya mhariri yasema: “Sisi ni viumbe wa ajabu kama nini hivi kwamba twaumiza wanadamu wenzetu kwa ukatili hivyo.” Shirika la Umoja wa Mataifa limetangaza mwaka huu kuwa mwaka wa amani wa kimataifa.

Uhusiano Kati ya Kuvuta Tumbaku na Upofu

“Kuvuta tumbaku ni kisababishi kikuu cha upofu,” lasema gazeti la Canberra Times. Wachunguzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia na Chuo Kikuu cha Sydney wakadiria kwamba asilimia 20 ya vipofu Waaustralia wenye miaka zaidi ya 50 wamekuwa vipofu kwa sababu ya kuvuta tumbaku. Wachunguzi hao walitaja uchunguzi mbalimbali wa Australia, Marekani, na Ulaya unaoonyesha kwamba wanaovuta tumbaku wanapozeeka waelekea kupoteza uwezo wa kuona mara mbili hadi tano zaidi kuliko wasiovuta tumbaku. Daktari Wayne Smith wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia alipendekeza kwamba pakiti za sigareti ziwe na onyo hili: “Uvutaji tumbaku ni kisababishi kikuu cha upofu.”

Kutotunza Watoto na Kuwatenda Vibaya

Gazeti la Asahi Evening News latoa habari kwamba kutoka Aprili 1, 1998 hadi Machi 31, 1999 visa vinavyojulikana vya kutenda watoto vibaya nchini Japani viliongezeka kwa asilimia 30. Wataalamu wanadhani kwamba sababu ni “mifadhaiko inayozidi kuongezeka ya akina mama ambao wanalea watoto wao bila wenzi wa ndoa” na vilevile kwamba “umma umezidi kutambua daraka lake” la kupiga ripoti wakijua kuhusu kisa cha kutotunza au kutenda mtoto vibaya. Gazeti la The Daily Yomiuri lasema kwamba nchini Japani vifo vya watoto wachanga walioachwa peke yao, ama nyumbani ama kwa gari, vimeongezeka. Baadhi ya wazazi walioacha watoto hao walikuwa wakicheza kamari. Hadi majuzi ni wazazi wachache sana walioshtakiwa mahakamani kwa mambo kama hayo. Hata hivyo, sasa mamlaka inanuia kushtaki mahakamani wazazi wengi zaidi wasiotunza watoto wao, ikiwa watoto wanaumizwa vibaya.

Watoto Waliozaliwa Karibuni Wenye Virusi vya UKIMWI

“Nusu ya watoto wote wanaozaliwa Afrika huwa wameambukizwa virusi vinavyosababisha UKIMWI,” lasema shirika la habari la United Press International. Dakt. Peter Piot aliye mkurugenzi mtendaji wa Programu ya Pamoja ya Umoja wa Mataifa ya UKIMWI, alitaarifu kwamba UKIMWI na virusi vinavyosababisha UKIMWI vimefupisha matarajio ya muda wa kuishi kwa miaka 25 katika baadhi ya sehemu za Afrika. Ripoti hiyo yaendelea kutaarifu hivi: “Nchi 21 zenye watu wengi zaidi wenye virusi vya UKIMWI zote ziko Afrika, na katika 10 kati ya nchi hizo angalau asilimia 10 ya watu wote wameambukizwa.” Asilimia 80 ya watu wote ambao wamekufa kwa UKIMWI waliishi Afrika.

Nishati ya Baiskeli

“Huenda ikawa kuendesha baiskeli ndiko usafiri unaohifadhi nishati nyingi zaidi kuliko njia nyingine ya kusafiri—si tu kwa sababu hakutumii mafuta lakini kwa sababu muundo wake haupotezi nishati nyingi,” yasema ripoti moja ya shirika la habari la Reuters. Wahandisi wa Chuo Kikuu cha Hopkins, Baltimore walichunguza kwa kamera ya miali mnyororo unaoendeshwa na kompyuta. Walitambua kwamba joto kidogo sana lilifanyizwa mnyororo uliposonga. “Walishangaa kuona kwamba chini ya asilimia 2 tu ya nishati iliyotumiwa kuendesha mnyororo huo ilipotea ikiwa joto,” ilisema ripoti hiyo. “Katika hali mbaya kabisa baiskeli ilipoteza asilimia 19 tu ya nishati.” James Spicer, aliyeongoza uchunguzi huo alisema: “Jambo hili lilinishangaza sana hasa kwa sababu mnyororo huo ulibuniwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.”

“Mvua Yenye Kudhuru”

Jambo la asilia ambalo lajulikana kama mvua yenye kudhuru latukia Turpan, Mkoa Unaojitawala wa Sinkiang Uighur, China. Hata wakati mawingu meusi ya mvua yanapopita juu, chini kuna joto na ukame, lasema gazeti la China Today. Ni kana kwamba mvua inanyesha, na mtu aweza hata kusikia mvua kwa kupunga mkono hewani. Hata hivyo, kwa sababu ya hali ya hewa yenye joto kali ya Turpan, mvua inavukiza kabla haijaanguka ardhini. Kwa hivyo, “mvua yenye kudhuru” haifiki ardhini kamwe.

Chakula Kinachoua

Daktari wa wanyama katika wilaya ya Kutch, sehemu ya magharibi ya India, aliondoa kilogramu 45 za mifuko ya plastiki kutoka katika tumbo la ng’ombe mgonjwa, lasema gazeti la The Week, la Kerala, India. Mbali na mifuko hiyo ya plastiki alipata pia vitambaa, makumbi ya nazi, waya, na skurubu. Nchini India ng’ombe wanaotangatanga hula takataka, na mifuko ya plastiki iliyotupwa ni hatari kwao. Hata ng’ombe za watu binafsi mara nyingi hula takataka barabarani wanapopelekwa malishoni. Daktari wa wanyama aitwaye Jadeja, anasema kwamba ng’ombe hawana matatizo makubwa ila kula mifuko ya plastiki na ugonjwa wa midomo na miguu. Mifuko hiyo isiyomeng’enyeka hufunga tumbo, naye ng’ombe hushindwa kucheua. Mara nyingi ng’ombe kama hao hufa. Dakt. Jadeja alionyeshwa tatizo hilo na washona-viatu waliopata mifuko mingi ya plastiki katika matumbo ya ng’ombe waliokufa, walipokuwa wakiwachuna.