“Utamaduni wa Mauaji” Huendelezwaje?
“Utamaduni wa Mauaji” Huendelezwaje?
“Licha ya kwamba wakimbizi wachanga wa Kosovo wenye wasiwasi wako mbali sana na watoto Wamarekani wanaokabili jeuri na mambo mengine yenye kuumiza, hali yao ya kihisia-moyo inalingana.” —Marc Kaufman, The Washington Post.
Tupende tusipende, sote tunaathiriwa na kifo kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Hilo ni kweli bila kujali tunakoishi—iwe ni katika nchi inayokumbwa na mapambano ya kikatili au katika ile iliyo na amani ya kadiri.
“UTAMADUNI wa mauaji” wadhihirishwa na visa chungu nzima vya kushuka moyo, maumivu makali ya moyo, uraibu wa dawa za kulevya, utoaji-mimba, mazoea hatari, kujiua, na mauaji ya umati leo. Profesa Michael Kearl, wa Kitengo cha Elimu-jamii na Elimu ya Binadamu katika Chuo Kikuu cha Trinity huko San Antonio, Texas, Marekani, alieleza hivi kuhusu matumizi ya hila ya habari ya kifo: “Tuchunguzapo hali mwishoni mwa karne yetu ya 20 [1999], twaona kwamba . . . kifo kinaonwa kuwa kani muhimu inayotegemeza uhai, afya, na muundo wa utaratibu wa kijamii. Kifo huchochea dini zetu, falsafa, mawazo ya kisiasa, sanaa na tekinolojia ya tiba. Huchochea watu wanunue magazeti na bima, hufanyiza njama zenye kusisimua kwenye vipindi vya televisheni, na . . . hata huimarisha viwanda vyetu.” Acheni tuchunguze mifano kadhaa inayodhihirisha hali hii iitwayo utamaduni wa mauaji katika nyakati zetu.
Uuzaji wa Silaha
“Utamaduni wa mauaji” hudhihirishwa kila siku na uuzaji wa silaha. Silaha hutumiwa kuangamiza askari, lakini hutumiwa hasa kuua raia, kutia ndani wanawake na watoto wasio na hatia. Katika vita, iwe ya wenyewe kwa wenyewe au la, sikuzote uhai hukosa kuthaminiwa. Risasi inayorushwa na mwuaji aliyekodiwa au askari-doria hugharimu fedha ngapi?
Katika nchi fulani uwezo wa umma wa kupata silaha kwa urahisi umesababisha ongezeko kubwa la kuogofya la vifo vya watu mmoja-mmoja na vya vikundi vya watu. Maandamano mengi yalizuka baada ya msiba wa ufyatuaji risasi katika shule ya sekondari huko Littleton, Colorado, kwa sababu ya kuenea kwa uuzaji wa silaha na jinsi ambavyo watoto wanazipata kwa urahisi. Idadi ya vijana wanaouawa kinyama huko Marekani inatisha—gazeti Newsweek, lasema ni wastani wa vijana 40 kila juma. Takriban asilimia 90 kati yao hupigwa risasi. Hiyo ni sawa na visa 150 vya mauaji kila mwaka kama kile kisa cha Littleton!
Ulimwengu wa Vitumbuizo
Sinema hutumia kwa faida habari zinazohusu kifo. Kwa mfano, sinema yaweza kutukuza mno ukosefu wa adili, jeuri, ulanguzi wa dawa za kulevya, au uhalifu uliopangwa na hivyo kupunguza thamani ya uhai na kudunisha kanuni za adili. Hata kuna sinema zinazotilia chumvi kifo—zikikazia hekaya ya uhai baada ya kifo na dhana ya wafu fulani kurudi na kuwatembelea walio hai—hekaya hizo hudunisha kifo.
Ndivyo ilivyo na vipindi fulani vya televisheni na muziki. Kwa mujibu wa ripoti za habari, wale vijana wauaji wa Littleton walikuwa wapenzi shupavu wa mwimbaji mmoja wa roki ambaye amejulikana sana kwa sababu ya “picha zake za wake-dume, na za kishetani,” na nyimbo “zinazokazia uasi na kifo.”
Huko Marekani, njia ya kuainisha vipindi vya televisheni ilirekebishwa ili kuwalinda vijana wasiangalie mambo yanayoweza kuwadhuru. Hata hivyo hali imezidi kuzorota. Jonathan Alter, aeleza kwenye gazeti Newsweek kwamba uainishaji huo wa televisheni “waweza kuwachochea watoto watamani zaidi mambo yasiyo ya adili.” Aliongezea kwamba ili kuwafedhehesha na kuwashurutisha wale wenye wajibu wapunguze jeuri kwenye vyombo vya habari, itambidi Rais Clinton “atangaze hadharani majina ya kampuni zote kubwa (na maofisa wake wakuu)” ambao mbali na kutunga sinema za kudungana visu na kurekodi ‘muziki wa rapu ya magenge,’ pia hubuni programu za michezo ya kompyuta inayowawezesha watoto “waue watu ‘kihalisi’.”
Mauaji Kwenye Michezo ya Kompyuta na Kwenye Internet
Katika kitabu chake The Deathmatch Manifesto, Robert Waring achanganua jinsi ambavyo vijana hupenda ile inayoitwa eti michezo ya misafara ya mauaji. * Bw. Waring anaamini kwamba kikundi kingine cha siri cha wachezaji wa michezo hiyo kimezuka. Kwa kweli michezo hiyo hufunza kuua badala ya kuelimisha. “Mtu huathiriwa sana anapocheza na mpinzani aliye hai kutoka mahali popote ulimwenguni, na kujaribu kuthibitisha kuwa ana uwezo. Ni rahisi mno kutumbukia katika mtego huo,” aeleza Waring. Vijana hunaswa na uvutano wa mandhari kamili zilizobuniwa ili kuremba mapambano yaliyojaa umwagikaji-damu. Wengine hununua programu za michezo ya kompyuta ili wazitumie kwenye televisheni nyumbani wanapokosa Internet. Wengine huzuru kumbi za umma kwa kawaida ambako hukodi mashine za michezo ya kompyuta na kupigana ‘kihalisi’ hadi kifo na wapinzani wengine.
Ijapokuwa michezo ya “misafara ya mauaji” huainishwa kulingana na umri wa mchezaji, ukweli ni kwamba haidhibitiwi vyakutosha. Eddie mwenye umri wa miaka 14 kutoka Marekani alisema hivi: “Kwa kawaida watu hukuambia ungali mtoto, lakini hawakuzuii kununua [mchezo huo].” Yeye hufurahia mchezo
wenye mapambano kabambe ya ufyatulianaji risasi. Ingawa wazazi wake wanajua jambo hilo, nao wanalichukia, wao huchunguza mara chache sana kuona kama anaucheza mchezo huo. Kijana mmoja alifikia mkataa huu: “Kizazi chetu tofauti kabisa na kizazi kingine chochote kimekufa ganzi kabisa kuelekea jeuri. Televisheni huwalea watoto leo badala ya wazazi, na televisheni hutosheleza hamu ya watoto ya kuona jeuri.” John Leland, aliandika hivi kwenye gazeti Newsweek: “Huku vijana milioni 11 sasa wakitumia Internet [huko Marekani], wengi hutumia wakati mwingi zaidi katika mazingira wasiyojua wazazi wengi.”Mitindo ya Maisha Iongozayo Kwenye Kifo
Vipi juu ya utendaji mwingine mbali na ulimwengu wa michezo ya “misafara ya mauaji” na sinema zenye jeuri? Ijapokuwa hatushindani kufa kupona na viumbe wa ajabu maishani, mtindo wa maisha wa watu wengi hutia ndani mazoea hatari. Kwa mfano, licha ya uvutano wa familia, mifumo ya utunzaji wa afya, na watu fulani wenye mamlaka ambao wanaonya juu ya hatari ya kuvuta sigareti na kutumia vibaya dawa za kulevya, mazoea hayo yanazidi kusitawi. Mara nyingi husababisha kifo cha mapema. Ili kuchuma faida zaidi kwa njia haramu, mashirika makubwa ya kibiashara na walanguzi wa dawa za kulevya huendelea kujifaidi kutokana na wasiwasi, kutamauka, na ufukara wa kiroho wa watu.
Ni Nani Chanzo cha Hayo Yote?
Je, Biblia inaeleza mauaji kuwa kitumbuizo? Je, inatetea mitindo ya maisha inayoweza kutufisha? La hasha. Wakristo wa kweli sawa na mtume Paulo huona kifo kuwa “adui” tu. (1 Wakorintho 15:26) Wakristo hawakioni kifo kuwa kitu cha kuvutia na cha kuchezea, badala yake, wanakiona kuwa kitu kinachokiuka asili ya mwanadamu, tokeo la moja kwa moja la dhambi na kumwasi Mungu. (Waroma 5:12; 6:23) Kifo hakikuwa kamwe sehemu ya kusudi la awali la Mungu kwa mwanadamu.
Shetani husemwa kuwa ana “uwezo wa kusababisha kifo.” Anaitwa “muua-binadamu,” si kwa sababu tu anasababisha kifo moja kwa moja, bali kwa sababu anasababisha kifo kwa kutumia udanganyifu, kwa kuwashawishi watu wafanye dhambi, kwa kuendeleza mwenendo unaofisidi na kuleta kifo, na kwa kusitawisha mitazamo ya uuaji-kimakusudi katika akili na mioyo ya wanaume, wanawake, na hata watoto. (Waebrania 2:14, 15; Yohana 8:44; 2 Wakorintho 11:3; Yakobo 4:1, 2) Hata hivyo, kwa nini vijana ndio shabaha yake kuu? Twaweza kuwasaidiaje?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 13 Katika michezo ya “Misafara ya Kifo,” ripoti hiyo yasema, “wachezaji huchochewa kuuana katika michezo yenye mandhari kamili kwenye Internet.”
[Picha katika ukurasa wa 7]
“Kizazi chetu tofauti kabisa na kizazi kingine chochote kimekufa ganzi kabisa kuelekea jeuri”