Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ulimwengu Nawashukuru kwa makala zinazotoa habari kuhusu ulimwengu wetu wa ajabu, kama vile “Ni Nini Kilicho Nyuma ya Sayari?” (Julai 22, 1999) na “Kuzuru Tena Sayari Nyekundu.” (Novemba 22, 1999) Zilikuwa zenye kuvutia sana, nazo ziliongeza uthamini wetu wa Muumba wetu.
M.A.T., Italia
Ugonjwa Unaotanua Mboni ya Jicho Nilisoma maelezo yenu ya “Onyo Dhidi ya Upofu” katika sehemu ya “Kuutazama Ulimwengu.” (Novemba 22, 1999) Miaka sita iliyopita nilipata kujua kwamba nina ugonjwa huo unaotanua mboni ya jicho (glaucoma). Huenda ikawa, kama vile makala yenu inavyotaarifu, wengi wenye ugonjwa huo hawahisi maumivu yoyote. Hata hivyo, ijapokuwa ninatumia dawa ya macho kila siku ninahisi maumivu makali ya macho na mara kwa mara maumivu ya kichwa. Je, yawezekana kwamba baadhi ya wasomaji wa makala hiyo watafikiri kwamba ugonjwa huo hauambatani na maumivu kamwe?
H. M., Japani
Taarifa yetu fupi haikukusudiwa kueleza kwa kindani maradhi hayo yenye kudhuru. Makala ya “Glaucoma—Insidious Stealer of Sight!” katika toleo letu la Mei 8, 1988, (la Kiingereza) ilieleza ugonjwa huo kwa kindani zaidi, nayo ikaonyesha kwamba kwa kweli baadhi ya wagonjwa huhisi maumivu.—Mhariri.
Mtoto Aliyezaliwa Kabla ya Wakati Ninawashukuru sana kwa makala ya “Tulijifunza Kumtegemea Mungu Kupitia Majanga.” (Novemba 22, 1999) Makala hiyo ilisimulia habari ya jamaa ya Major na mtoto wao mrembo aitwaye JoAnn. Dada yangu mdogo alipokuwa na miaka miwili tulipata kujua kwamba ana ugonjwa wa akili wa autism. Kushughulikia ugonjwa wa dada yangu ni jambo gumu na lenye kuchosha, lakini yale ambayo jamaa ya Major walipitia yametusaidia kuelewa hata zaidi jinsi ilivyo muhimu kumtegemea Yehova katika hali zote za maisha.
M. C., Marekani
Binti yetu alizaliwa mwaka wa 1992, mwaka uleule alipozaliwa JoAnn. Uzito wake alipozaliwa ulikuwa gramu 700 tu! Madaktari walitaka kumtia damu. Daktari mmoja hata alisema kwamba angekuwa na upungufu wa akili iwapo hangetiwa damu. Hata hivyo, tulitoa sala kwa Yehova nasi tukaweza kusimama imara. Leo anakwenda shule, naye hana dalili yoyote ya upungufu wa akili.
C. H., Japani
Nimeolewa, nami nina watoto watatu. Kwa kuwa mume wangu hana kazi hatuna mapato wala hati ya bima ya kitiba. Lakini, simulizi la JoAnn na jamaa yake limenisaidia kutokuwa na wasiwasi kuhusu wakati ujao, nikishughulikia matatizo ya siku kwa siku. (Mathayo 6:34) Asanteni kwa kunikumbusha kumtegemea Yehova badala ya kujitegemea mwenyewe ili kupata nguvu ya kuvumilia.
K. A., Marekani
Karne ya Ishirini Ninaandika kuhusu mfululizo wa makala wa “Karne ya 20—Miaka Muhimu ya Badiliko.” (Desemba 8, 1999) Nilivutiwa sana na taarifa ya waziwazi juu ya nyakati ngumu tulizoziona katika karne ya 20. Niliweza kuona jinsi jeuri inavyoharibu wanadamu pole kwa pole. Hongera kwa kazi yenu nzuri ajabu.
W. G., Puerto Riko
Maparachichi Sasa hivi nimemaliza kusoma makala ya “Parachichi—Tunda Linalotumiwa kwa Njia Nyingi Sana!” (Desemba 22, 1999) Nafikiri wengi watapendezwa na makala hiyo. Nilianza kula maparachichi nilipokuwa na miezi tisa. Nilipokuwa na miaka mitatu, nilijifunza kutengeneza guacamole. Sasa nina miaka kumi. Maelezo yenu ya upishi ya guacamole yalitia ndani utumizi wa vitunguu, nami nikawafikiria watu wasioweza kula vitunguu hata kidogo. Ninapotengeneza guacamole natumia maparachichi, maji ya limau, chumvi, pilipili, na kitunguu saumu kilichokatwa vipande vidogo.
N. E., Marekani
Asante kwa dokezo lako!—Mhariri.