Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mmea Maridadi Wenye Uharibifu

Gugu-maji ni mmea unaokua majini ambao hutokeza ua maridadi la zambarau. Gugu-maji hilo lililopelekwa Ziwa Viktoria la Afrika miongo kadhaa iliyopita, limezaa haraka sana hivi kwamba sasa limefunika kilometa za mraba 2,000 za ziwa hilo, na kuvuruga biashara muhimu ya uvuvi ambayo hulisha mamilioni ya watu katika nchi zinazopakana nalo—Kenya, Tanzania, na Uganda. Limesababisha matatizo makubwa kwa hifadhi ya maji ya Uganda na mitambo ya nguvu za umeme kwa kuziba mifereji inayopeleka maji. Pia unachangia kuzaana kwa mbu, konokono, na nyoka, na kuongeza visa vya kuumwa na nyoka na visa vya malaria na kichocho. Ingawa wadudu ambao hula magugu-maji pekee wamepelekwa huko, kufikia sasa wameshindwa kukabiliana na ukuzi wa haraka sana wa mmea huo. Wavuvi wameamua kung’oa gugu hilo kwa mikono, waking’oa maelfu ya tani. Lakini huo umekuwa utatuzi wa muda tu. Benki ya dunia inadhamini mradi wa kusafisha ziwa hilo utakaogharimu mamilioni ya dola.

Kisukuku Chenye Manyoya Kilikuwa Ni Mzaha

Kisukuku kilichopatikana katika Mkoa wa Liaoning, China, kiliripotiwa na National Geographic kuwa “kiunganishi halisi kilichokosekana katika mfuatano tata unaounganisha dinosau na ndege.” Kisukuku hicho, kilichoitwa Archaeoraptor liaoningensis, kilisemekana kuwa na mkia kama wa dinosau na kidari na mabega kama ya ndege. Hata hivyo, sasa wanasayansi wanaanza kusadiki kwamba “wamedanganywa na kisukuku kidogo bandia,” laripoti Science News. Wataalamu wa elimu ya visukuku waliochunguza kisukuku hicho walianza kukishuku baada ya kugundua kwamba hakikuwa na mifupa inayounganisha mkia na mwili na kwamba bamba la jiwe lilionyesha kuwa kilifanyiwa kazi upya. Philip Currie, wa Jumba la Makumbusho la Elimu ya Visukuku la Royal Tyrrell huko Drumheller, Alberta, Kanada, ashuku kwamba mtu fulani “alijaribu kufanya Archaeoraptor iwe na thamani zaidi kwa kubandika sehemu moja ya mkia wa dinosau kwenye kisukuku cha ndege,” yasema ripoti hiyo.

Wapigaji-Risasi Walio Chini ya Maji

Yaonekana kama sinema ya Magharibi mwa Marekani: Wapambanaji hao wawili wanakabiliana, huku silaha zao zikiwa tayari. Baada ya mpiganaji wa kwanza kufyatua risasi na kurudi nyuma, yule mwingine hulenga shabaha na kufyatua. Lakini uduvi wenye bastola wapiganapo, hakuna anayejeruhiwa, kwa kuwa daima hawakaribiani sana. Hata hivyo, kama ilivyoripotiwa katika gazeti Der Spiegel, michirizo ya maji inayotoka kwenye kucha zao za kulia huwa hatari nyakati nyingine. Pia bastola hiyo ya maji hutumiwa kushtua na kuua mawindo kama vile minyoo, kaa, au samaki wadogo. Mchirizi wa maji, unaotokezwa na kufunga kucha kwa ghafula na kwa nguvu, huwa na nguvu za kutosha kuvunja kioo cha upande cha tangi-samaki. Uduvi mwenye bastola anapopoteza silaha yake, “mpigaji-risasi” huyo mdogo huanza kutumia mkono wa kushoto, akitumia ukucha wa kushoto kama bastola mpya, huku ukucha mpya ukikua kwenye mkono uliokuwa ukirusha risasi hapo kwanza.

Buddha Aliye Hai Atawazwa

“Wenye mamlaka wa China wamesimamia kutawazwa kwa mvulana mwenye umri wa miaka miwili kuwa ‘Buddha anayeishi’ aliye muhimu katika dini ya Tibet,” laripoti The New York Times. Mvulana huyo, Soinam Puncog, alichaguliwa kutoka kwa wavulana 670 kutumikia akiwa Reting Lama wa saba. Yasemekana kuwa watawa wa kiume waliomchagua lama huyo walitumia uaguzi. “Lakini kuna shaka ikiwa watu wengi wa Tibet na watawa wa kiume watakubali kustahili kwa mvulana huyo,” lasema gazeti hilo. Kwa nini? Kwa sababu mapema kidogo Dalai Lama, kiongozi mkubwa zaidi wa kidini wa Tibet, alitangaza chaguo lake mwenyewe la Reting Lama. Katika nyakati za kale, Reting Lama wametumikia wakiwa makaimu wakati Dalai Lama hakuwapo.

Sanamu Zinazosababisha Uchafuzi

Wahindu wana zoea la kutupa sanamu katika maji yaliyo karibu baada ya sherehe. Hakukuwa na tatizo hili la kimazingira wakati sanamu zilikuwa zikipakwa rangi iliyotengenezwa kwa maua au rangi za mboga. Hata hivyo, watengenezaji walipoanza kutumia rangi zilizotengenezwa kwa metali nzito na visababishi vya kansa, sehemu fulani za India zilikumbwa na uchafuzi mkubwa wa maji baada ya maelfu ya sanamu kutupwa ndani ya vijito na maziwa. Ili kupunguza uchafuzi wa maji, wakazi wa mji mmoja walikusanya mamia ya sanamu na kuzipeleka kwenye shamba kubwa ambapo walivunja sanamu hizo vipande-vipande. Gazeti Down to Earth lapendekeza kwamba jambo hilo lifanywe kila mahali India na kwamba watengenezaji-sanamu waanze kutumia rangi za zamani badala ya rangi za sanisia. “Kama sivyo,” lasema gazeti hilo, “mito ambayo Wahindu huabudu yaweza kutiwa sumu na sanamu wanazoabudu.”

Uchunguzi wa Vijana Ulimwenguni

Uchunguzi uliofanyiwa vijana zaidi ya 4,300 walio na umri kati ya miaka 12 hadi 24 waonyesha kwamba vijana huthamini kanuni za zamani, kama vile kutumainika, uungwana, na kufanya kazi kwa bidii, laripoti The Globe and Mail. Kulingana na Kikundi cha Angus Reid, kilichopokea maoni ya vijana kutoka nchi tofauti-tofauti 11, asilimia 95 walisema kwamba kanuni ya maana zaidi ni ‘kutimiza ahadi zako.’ “Kuonyesha wengine uungwana” kulitajwa na asilimia 92 kuwa kanuni inayofuata kwa umuhimu, na “kufanya kazi kwa bidii” kulithaminiwa sana na asilimia 83 ya wale waliotoa maoni. Ingawa “karibu wanane kati ya 10 waliona ni jambo la maana kuwa na mwenzi wa maisha,” ni asilimia 56 tu walioona kufunga ndoa kuwa jambo la maana. Kwa kushangaza, ni asilimia 31 tu waliofikiri kwamba “kuwa tajiri kwelikweli” kulikuwa jambo la maana. Pia uchunguzi huo waonyesha kwamba ni asilimia 45 tu “wanaotazamia mema katika karne ya 21.”

Mambo Hakika Kuhusu Web-Site

Internet ni mfumo mkubwa sana wa kompyuta unaounganisha mamilioni ya kompyuta ulimwenguni pote. Ili kujua ukubwa wake, Inktomi, kampuni inayotayarisha programu za kompyuta, ilitumia muda wa miezi minne kuchunguza na kuainisha Web. Ilipata nini? Idadi ya kurasa zisizo za kawaida ilikuwa zaidi ya bilioni moja! Kiingereza ndicho kilichokuwa lugha inayotumiwa zaidi katika Internet. Hutumiwa zaidi ya mara asilimia 86 ya wakati wote. Zaidi ya asilimia 2 tu ya hati zote zilizo katika Internet ni za Kifaransa, nacho Kiholanzi kilikuwa asilimia 0.5.

Je, Ni Dawa Yenye Sumu?

Makosa yanayofanywa wakati wa matibabu huua kati ya Wamarekani 44,000 hadi 98,000 waliolazwa hospitalini kila mwaka, yaripoti Taasisi ya Tiba. Yasemekana tatizo hilo huchangiwa na makosa ambayo hufanywa hospitalini, kwenye kliniki, na katika maduka ya kuuzia dawa. Kwa mfano, wauzaji-dawa wanaotoa dawa kufuatana na maagizo ya daktari mara nyingi hutatizwa na mwandiko mbaya wa daktari. Je, daktari aliagiza miligramu kumi au mikrogramu kumi? Tatizo hilo huzidishwa na dawa nyingi zenye majina yanayokaribiana, yanayoweza kutatanisha madaktari wengi, wauguzi, wauzaji-dawa, na vilevile wagonjwa. Taasisi ya Tiba imeomba makosa ya kitiba yapunguzwe kwa asilimia 50 katika miaka mitano.

Internet na Wazee

Barua za kompyuta zinathibitika kuwa baraka kwa wazee wanaoishi katika makao ya kutunzia wazee-wazee. “Wataalamu wanasema wakazi wa hospitali ndogo za kibinafsi, hata wale walio dhaifu, hupenda kutumia kompyuta mara moja na wanaweza kuhuisha maisha yao kupitia barua za kompyuta na Internet,” lasema The New York Times. “Wale wanaopata kuwa mahiri wa tekinolojia hiyo hupata uhakika ambao huathiri pande mbalimbali za maisha yao, na wengine hujivunia daraka la kusaidia wakazi wenzao kujifunza stadi hizo.” Si kwamba tu barua za kompyuta huwawezesha wazee-wazee wawasiliane na washiriki wa familia zao walio mbali, watunzaji-afya, na marafiki wa zamani bali pia hufanya wasihisi kuwa hawawezi kujitegemeza, uchoshi, na upweke unaowapata wale waishio kwenye hospitali ndogo za kibinafsi na wanaotumia viti vya magurudumu kwa sababu ya ugonjwa au uzee. Hupata nguvu mpya na kushuka-moyo hupungua. Hata wazee-wazee fulani hushiriki programu za elimu kupitia Internet, na hivyo kuwawezesha wasambaze ujuzi na hekima yao kwa vizazi vijavyo. Hata hivyo, mabadiliko fulani yapasa kufanywa. Yanatia ndani vibao vya herufi vilivyo rahisi zaidi kutumia na njia rahisi ya kuongeza ukubwa wa herufi.

Upungufu wa Chakula Unaosababishwa na Wanadamu

“Misiba inayochochewa na wanadamu kama vile mizozano ya kijamii na matatizo ya kiuchumi huchangia zaidi upungufu wa chakula kuliko matatizo yanayosababishwa na hali za asili,” laripoti Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Dakt. Hartwig de Haen, naibu mkurugenzi-mkuu wa FAO, alisema: “Katika mwaka wa 1984, misiba inayosababishwa na wanadamu ilichangia asilimia kumi tu ya misiba yote. Sasa, ni zaidi ya asilimia 50.” Inakadiriwa kwamba watu milioni 52 kutoka nchi 35 wanakabili upungufu wa chakula. Ripoti hiyo yaongezea hivi: “Hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi ya watu waliopata kukabili upungufu mkubwa wa chakula tangu kuwe na ukame katika sehemu za Afrika zilizo karibu na Sahara mwaka wa 1984.”