Mbona Wengi Wanapendezwa na Uwasiliani-roho?
Mbona Wengi Wanapendezwa na Uwasiliani-roho?
Uwasiliani-roho hufafanuliwa kuwa “itikadi ya kwamba roho ya mwanadamu huendelea kuishi baada ya mwili kufa na yaweza kuwasiliana na walio hai, hasa kupitia kwa mwasiliani-roho.”
ORODHA ya mauzo bora iliyochapishwa na gazeti New York Times yasema kwamba kitabu kimoja kinachoeleza namna ya kuwasiliana na wafu kilipendwa mno huko Marekani na upesi kikawa kimeuzwa kupita vitabu vingine vyote mwaka wa 1998.
Miaka michache iliyopita huko Moscow, wanasiasa na wafanyabiashara waliwahusudu mabingwa wa maono na wawasiliani-roho, hata walilipa fedha nyingi ili kuhudumiwa.
Katika Brazili, watazamaji wengi wa televisheni huvutiwa na mfululizo wa drama za mambo ya kijamii zinazokazia uwasiliani-roho.
Kwa wakazi wengi wa Afrika au Asia, uwasiliani-roho ni jambo la kawaida kama kufanya biashara sokoni.
Sababu Inayofanya Wengi Wageukie Uwasiliani-Roho
Wengi hugeukia uwasiliani-roho ili kupata faraja baada ya kifo cha wapendwa wao. Huenda wakapokea ujumbe wa pekee uonekanao ni kana kwamba umetoka kwa wafu kupitia kwa wawasiliani-roho. Tokeo ni kwamba wafiwa hawa mara nyingi husadiki kwamba wapendwa wao waliokufa wako hai, na kwamba kuwasiliana na wafu kutawasaidia wastahimili msiba wao.
Wengine huvutiwa mno na uwasiliani-roho kwa sababu wanaambiwa kwamba roho zitawasaidia wapate maponyo kwa magonjwa yao, waepuke umaskini, wafanikiwe katika mahaba, watatue matatizo ya ndoa, au kupata kazi ya kuajiriwa. Na wengine wengi hugeukia uwasiliani-roho kwa sababu tu ya udadisi.
Lakini mamilioni ya watu wamegeukia uwasiliani-roho pia kwa sababu wamefundishwa kwamba uwasiliani-roho ni, kama vile mtaalamu mmoja katika uwanja huu alivyoeleza, “dini ya ziada” inayoenda “sambamba na Ukristo.” Mfano mmoja ni hali ya kidini ya Brazili.
Brazili ndiyo nchi yenye Wakatoliki wengi zaidi duniani, lakini kama vile mtungaji Sol Biderman anavyosema, “mamilioni ya waumini huwasha mishumaa katika madhabahu zaidi ya moja nao huona [kwamba] hakuna kosa lolote.” Kwa kweli, gazeti Veja la Brazili linalochapishwa kila juma liliripoti kwamba asilimia 80 ya watu wanaozuru vituo vya uwasiliani-roho kwa kawaida huko Brazili ni Wakatoliki waliobatizwa ambao huhudhuria Misa pia. Ufikiriapo pia kwamba hata makasisi fulani hushiriki katika vikusanyiko vya uwasiliani-roho, waweza kuona kwa nini waumini wengi hufikiri kwamba kuwasiliana na roho ili kupata faraja na mwongozo hukubaliwa na Mungu. Lakini je, ni kweli?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 3]
Namna Mbalimbali za Uwasiliani-Roho
Zoea la uwasiliani-roho laweza kutia ndani kumfikia mwasiliani-roho, kuulizia habari za wafu, au kutafuta ndege. Namna moja ya uwasiliani-roho inayopendwa sana ni uaguzi—kujaribu kutafuta habari za wakati ujao au mambo yasiyojulikana kwa msaada wa roho. Namna fulani ya uaguzi hutia ndani unajimu, kutabiri kwa kutumia tufe la kioo, ufasiri wa ndoto, usomaji wa kiganja cha mkono, na kutabiri kwa kutumia kadi za ubashiri.