Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Maradhi ya Cystic Fibrosis Asanteni kwa ajili ya makala “Kuishi na Maradhi ya Cystic Fibrosis.” (Oktoba 22, 1999) Ijapokuwa nina umri wa miaka 17 tu na nina afya nzuri, simulizi la Jimmy Garatziotis lilinistaajabisha. Lilinisaidia nifikirie mambo mengi, pamoja na umuhimu wa kuthamini vitu ulivyo navyo. Licha ya maradhi hayo yenye maumivu makali, Jimmy aendelea kuwa mchangamfu na kuwa na imani thabiti katika ahadi za Yehova. Nasali kwamba Jimmy na Deanne wataendelea kuwa na nguvu za kustahimili majaribu yao.

E. Z., Urusi

Ushirikina Nimekuwa nikisoma vichapo vyenu kwa miaka miwili ijapokuwa mimi si mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Ningependa kuwashukuru kwa ajili ya mfululizo “Je, Maisha Yako Yameamuliwa Kimbele?” (Agosti 8, 1999) na “Ushirikina—Kwa Nini Ni Hatari Sana?” (Oktoba 22, 1999) Hapo awali nilikuwa mshirikina na niliamini maisha yameamuliwa kimbele kwa sababu ya malezi yangu. Lakini sasa nafikiri mwasema ukweli kuhusu Ukristo wa kweli.

N. D., Ufaransa

Makala juu ya ushirikina ziliniudhi. Mimi ni Mkatoliki mwenye bidii, na moja ya makala hizo ilisema kwamba ni ushirikina kwa abiria kufanya “ishara ya msalaba.” Wakatoliki hufanya hivyo kama sala ili wasafiri salama. Jambo hilo ni sehemu muhimu ya ibada yetu na haliwezi kamwe kuitwa ushirikina.

S. W., Marekani

Haiwezi kukanwa kwamba wengi hufanya ishara ya msalaba bila ujitoaji-kidini. Alipoulizwa kwa nini alifanya ishara ya msalaba uwanjani, mchezaji mmoja wa kandanda wa Australia alikiri hivi: “Nafikiri ni ushirikina kwa njia fulani.” Si ajabu kwamba desturi hiyo imekuwa na mambo fulani ya kishirikina tangu awali. Kichapo “The Catholic Encyclopedia” chasema: “Tangu nyakati za kale kufanya ishara ya msalaba kumetumiwa katika upungaji wote na uchawi ili kufukuza roho wa giza.”—Mhariri.

Dawa za Kulevya Nataka kuwashukuru kwa ajili ya ule mfululizo “Je, Dawa za Kulevya Zinaudhibiti Ulimwengu?” (Novemba 8, 1999) Baba yangu amekuwa mtumwa wa dawa za kulevya na vileo kwa sababu ya uvutano wa marafiki. Sipati ulinzi nyumbani bali vitisho mara nyingi. Licha ya hali hizo zote, sitaacha kamwe kuwaalika wazazi wangu waje wapate shangwe ya kumwabudu Mungu.

M. L., Italia

Mara moja kwa juma ofisa mmoja wa polisi huja katika shule yetu na kutuhutubia kuhusu dawa za kulevya na vileo. Niliamua kumpa makala juu ya dawa za kulevya alipozuru darasa letu tena. Alivutiwa sana naye akasomea darasa mafungu kadhaa ya makala hizo. Darasa letu lote lilinufaika na makala hizo!

C. D., Marekani

Mtoto Mlemavu Simulizi la Rosie Major, “Tulijifunza Kumtegemea Mungu Kupitia Majanga” (Novemba 22, 1999), lilinigusa moyo sana. Tuliishi jijini, ila sikufurahia namna ambavyo hali ya jijini ilikuwa ikiathiri binti yangu mkubwa. Kwa hiyo tulihamia mashambani. Mambo yalikuwa shwari hadi nilipofutwa kazi yangu ya mshahara wa dola 56,000 za Marekani kila mwaka. Tulipata mkazo mwingi kwelikweli kwa sababu tuliishi mashambani na watoto wetu watatu huku tukidaiwa rehani. Lakini baada ya kusoma simulizi la Rosie Major, matatizo yangu ya kifedha yalionekana kuwa si kitu kiasi cha kunitia aibu. Kuna watu wengi ambao kwa kweli wanahitaji msaada wa Mungu! Je, naweza kuandikisha Mnara wa Mlinzi na Amkeni!?

M. F., Marekani

Tulifurahi kutimiza ombi la msomaji huyu.—Mhariri.