Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuishi Ili Kuona Milenia

“Imethibitishwa kabisa kwamba wagonjwa mahututi hujitahidi kuishi ili waone matukio muhimu,” asema Richard Suzman wa Taasisi ya Kitaifa ya Uzee, katika Bethesda, Maryland, Marekani. “Japo utaratibu wa kiasili haujulikani, hali hiyo ni halisi sana.” Huku wakiwa wameazimia kuona mwaka wa 2000, watu wengi kuliko ilivyo kawaida walikufa katika juma la kwanza la mwaka huo mpya, laripoti The Guardian la London. Huko Uingereza, asilimia 65 zaidi ya watu walikufa juma hilo, na katika New York City, vifo viliongezeka kupita asilimia 50, ikilinganishwa na juma la kwanza la mwaka wa 1999. Robert Butler, msimamizi wa Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Maisha Marefu, alisema kwamba ongezeko hilo lilikuwapo ulimwenguni pote. Aliongezea: “Azimio la kuishi laweza kuwa na nguvu sana.”

Kuongoza Meli kwa Kompyuta

Huenda meli hazitahitaji kuongozwa tena kwa chati chungu nzima za karatasi kwa sababu ya tekinolojia ya elektroni, lasema The Daily Telegraph la London. Mwezi wa Novemba 1999, Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini, kupitia kwa ofisi ya Ujerumani ya uchoraji wa chati za usafiri wa majini, kwa mara ya kwanza lilitoa ruhusa ya kubuni mfumo wa kuongoza meli unaotumia kompyuta. Badala ya chati za karatasi, kompyuta ina mifumo miwili ya elektroni—kisoma-maandishi ya chati za karatasi na mfumo wa tarakimu unaoitwa chati ya vekta. Faida muhimu ya chati ya kielektroni ni kwamba nyakati zote inaonyesha mahali barabara ilipo meli. Na manahodha wanaweza pia kutambua hatari zilizo njiani kwa kusoma chati za rada kwenye skrini ya kompyuta. Kapteni mmoja wa meli, mwenye furaha tele kwa ajili ya ubuni huo, alisema: “Hutupunguzia kazi . . . kwa hiyo twaweza kukazia uangalifu zaidi uendeshaji, meli nyingine na, uendeshaji wa nahodha tukaribiapo bandari.”

Yaelekea Hakuna Viumbe Kutoka Sayari Nyingine

“Katika miongo michache iliyopita, idadi inayoongezeka ya waastronomia wameeneza maoni ya kwamba yaelekea kuna ustaarabu wa viumbe kutoka sayari nyingine katika nyota mbalimbali,” lasema The New York Times. “Dhana hiyo ya viumbe kutoka sayari nyingine mbali na kuchangia vitabu, sinema na vipindi vya televisheni chungu nzima . . . imetokeza uchunguzi wa kisayansi wa muda mrefu ambao hutumia antena kubwa yenye umbo la pia ili kutafuta angani ishara hafifu za redio kutoka kwa viumbe wenye akili wa sayari nyingine.” Yaelekea kwamba uchunguzi huo hautafua dafu, wasema wanasayansi wawili maarufu, Dakt. Peter D. Ward na Dakt. Donald C. Brownlee, watungaji wa kitabu Rare Earth. Wanasema kwamba uvumbuzi mpya katika elimu ya nyota, visukuku, na jiolojia, huonyesha “kwamba mfanyizo wa Dunia na uthabiti wake ni nadra isivyo kawaida” na kwamba hali za sayari nyinginezo hazifai viumbe tata. “Hatimaye twasema waziwazi jambo ambalo wengi wamefikiria kwa muda mrefu—kwamba viumbe tata, angalau, ni adimu,” akasema Dakt. Ward. Naye Dakt. Brownlee aongezea: “Watu husema Jua ni mfano wa nyota hizo. Hilo si kweli. Mazingira karibu yote katika ulimwengu wote mzima hayawezi kutegemeza viumbe. Ni sehemu zinazofanana na Bustani ya Edeni kama Dunia zinazoweza kutegemeza viumbe.”

Biblia Yatafsiriwa Katika Lugha Zaidi

“Biblia yaendelea kuwa kitabu kilichotafsiriwa zaidi ulimwenguni,” lasema gazeti la Mexico Excelsior. Kwa mujibu wa Chama cha Biblia cha Ujerumani, Biblia ilitafsiriwa katika lugha nyingine 21 mwaka wa 1999, na sasa yaweza kupatikana angalau kwa sehemu katika lugha 2,233. Kati ya lugha hizo, “Agano la Kale na Agano Jipya zimetafsiriwa kikamili katika lugha 371, lugha 5 zaidi ya zilizotafsiriwa mwaka wa 1998.” Lugha zote hizo zapatikana wapi? “Tafsiri nyingi zaidi ziko Afrika, tafsiri 627, ikifuatwa na Asia, 553, Australia/Pasifiki, 396, Amerika ya Latini/Karibea, 384, Ulaya, 197, na Marekani, 73,” lasema gazeti hilo. Na bado, “Biblia haijatafsiriwa hata katika nusu ya lugha zinazozungumzwa duniani.” Kwa nini? Kwa sababu ni watu wachache tu wanaozungumza lugha hizo, na ni kazi ngumu kutafsiri Biblia katika lugha hizo. Pia, watu wengi wanasema lugha mbili, na endapo Biblia haijachapishwa katika mojawapo ya lugha zao, wanaweza kuisoma katika lugha nyingine.

Silaha Zilizotupwa

Hivi karibuni wavuvi Waitalia wamekuwa wakivua vitu ambavyo hawangependa kuvua—silaha za kemikali. Kulingana na Valerio Calzolaio, katibu msaidizi katika Wizara ya Mazingira ya Italia, “kutoka mwaka wa 1946 hadi miaka ya 1970 . . . , lilikuwa zoea la kawaida kutupa silaha zisizofaa baharini.” Inakadiriwa kwamba mabomu 20,000 yamezagaa chini ya bahari ya Adriatiki, karibu na pwani ya mashariki ya Italia. Kufikia mwaka wa 1997, wavuvi 5 Waitalia walikuwa wamekufa na 236 wakalazwa hospitalini kwa sababu ya athari za kemikali hatari mno zilizovuja kutoka kwa silaha zilizooza walizovua kwa nyavu zao. Tatizo baya zaidi ni kwamba idadi isiyojulikana ya mabomu yaliangushwa kwenye bahari hiyo na ndege za kivita wakati wa pambano la Balkani hivi karibuni, na baadhi yake tayari “yamevuliwa” kwa nyavu za samaki. Tatizo hilo halijaathiri bahari za Italia peke yake. Inakadiriwa kwamba tani 100,000 za silaha za kemikali zimezagaa chini ya Bahari ya Baltiki, na yasemekana kwamba kuna silaha pia kwenye maji ya ufuoni huko Japani, Marekani, na Uingereza.

Takwimu Zilizotiliwa Chumvi

“Usiamini sikuzote yale unayosoma magazetini,” lasema The Economist. Waandishi wa habari “wanaweza kukosea pia.” Ndivyo ilivyo hasa takwimu zinapohusika, hususan takwimu za misiba. Kwa nini? “Katika rabsharabsha ya vita, au msiba wa kawaida, bila shaka haiwezekani kujua idadi ya watu ambao wamekufa au kujeruhiwa,” yasema makala hiyo. Ili kutosheleza hamu ya watu ya kutaka kujua, waandishi wa habari hutoa makadirio, mara nyingi huwa ya juu sana, na “ni nadra kwao kupunguza makadirio hayo kadiri muda upitavyo.” Kwa sababu gani? “Waandishi wa habari wanataka watu wavutiwe na masimulizi yao, wahariri wanataka magazeti yao yanunuliwe, watoa-misaada wanataka kuendeleza mashirika yao. Hata maofisa wa serikali huenda wakataka watu wawaonee huruma.” Gazeti hilo lapendekeza kwamba wasomaji “wajihadhari—na usahihi bandia, maneno matamu ambayo kwa wazi hayana maana, na mwelekeo wa waandishi wa habari wa kutilia chumvi daima.” Laongezea: “Bila kujali uvutano wa waandishi wa habari kwa ujumla, habari zinazohusu mauaji huvutia watu kuliko mauaji yenyewe.”

Jihadhari na Wanyama-Vipenzi

Kwa mujibu wa gazeti la Kifaransa linalochapishwa kila siku Le Monde, asilimia 52 ya jamaa zote Ufaransa zina wanyama-vipenzi. Hata hivyo, uchunguzi wa karibuni wa kikundi cha madaktari wa mifugo katika Taasisi ya Elimu-Linganishi ya Kinga Maradhi za Wanyama, huko Maisons-Alfort, Ufaransa, yaonyesha kwamba kuvu na wadudu wanaobebwa na paka milioni 8.4 na mbwa milioni 7.9 walioko Ufaransa ndio wanaowaambukiza magonjwa mbalimbali wamiliki wa wanyama-vipenzi. Magonjwa hayo yatia ndani choa, minyoo, upele, leishmanias, na toxoplasmosis. Ugonjwa wa toxoplasmosis waweza kuharibu mimba au kulemaza mtoto aliye tumboni. Ripoti hiyo yataja pia kuzuka kwa mizio mingi kunakosababishwa na wanyama-vipenzi walio nyumbani na maambukizo yatokanayo na kuumwa na mbwa—takriban 100,000 kila mwaka huko Ufaransa.

Mfumo wa Viumbe Kinywani

“Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Stanford wamegundua viumbe wapya 37 wa pekee katika mojawapo ya mifumo yenye viumbe wengi duniani: kinywa cha mwanadamu,” laripoti The Toronto Star. Hilo laongeza idadi ya jamii za bakteria za kinywani zijulikanazo hadi zaidi ya 500, “nyingi sana kiasi kinachokaribia kile cha bakteria zilizo katika misitu ya kitropiki ya mvua, ambayo huonwa kuwa na viumbe wengi kupindukia.” Je, bakteria hizo zinadhuru? Baada ya kugundua viumbe hao wapya katika ukoga kinywani, mtaalamu wa mikrobiolojia Dakt. David Relman alisema: “Jamii hizo nyingi zinatia moyo sana kwa kuwa hutokeza uthabiti na ulinzi kinywani.” Gazeti Star laongezea kwamba aina nyingi za bakteria “hudhaniwa kuwa zinatokeza starehe, ulinzi na lishe.” Ni chache sana zinazosababisha matatizo kama vile kuoza kwa meno, ugonjwa wa ufizi, na uvundo kinywani.

Vita Vyaongezeka

“Idadi ya vita iliendelea kuongezeka” mnamo 1999, laripoti gazeti la Ujerumani Siegener Zeitung. Kikundi cha Kuchunguza Visababishi vya Vita, katika Chuo Kikuu cha Hamburg, kilihesabu mapambano 35 ya silaha mwaka wa 1999, 3 zaidi ya mwaka uliotangulia. Kati yake, 14 yalikuwa Afrika, 12 yalikuwa Asia, moja huko Ulaya, na mengineyo katika Mashariki ya Kati na Amerika ya Latini. Vita havitakoma karibuni, kikasema kikundi hicho. Kwa kweli, “vita vinane viliorodheshwa kwa mara ya kwanza mwaka huu, miongoni mwake ni mapambano ya kikatili katika Chechnya, Nepal, Kyrgyzstan, na Nigeria.” Sababu moja ni kwamba visababishi fulani vya mapambano vyaweza kupoa kwa muda mrefu kabla ya kuzuka na kuwa mapambano makali ya silaha au vita kamili.