Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Lugha—Viunganishi na Vizuizi vya Mawasiliano

Lugha—Viunganishi na Vizuizi vya Mawasiliano

Lugha—Viunganishi na Vizuizi vya Mawasiliano

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO

“Hakuna historia inayoweza kutupa uelewevu kamili juu ya watu, mfumo wao wa kijamii na itikadi na hisia zao, kama tuupatavyo kwa kuchunguza lugha yao.”—MARTÍN ALONSO.

KATIKA historia yote, wasomi wamevutiwa na asili, unamna-namna, na ukuzi wa lugha. Kwa kweli, uvutio wake ungalipo—sawa na rekodi nyingi za kihistoria —kwa sababu ya lugha yenyewe. Bila shaka, lugha ndiyo njia kuu zaidi ya mawasiliano ya wanadamu.

Kwa sasa, wanaisimu fulani wanakadiria kwamba lugha zipatazo 6,000 au zaidi zinazungumzwa ulimwenguni, bila kutia ndani lahaja. Lugha inayozungumzwa na watu wengi zaidi ni Kichina cha Mandarin, inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 800. Lugha nne zinazofuata ambazo huzungumzwa na watu wengi zaidi, bila kufuatia mpangilio, ni Kiingereza, Kihispania, Kihindi, na Kibengali.

Ni nini hutukia tamaduni tofauti-tofauti na bila shaka lugha zao ziunganapo kwa ghafula? Kwa upande mwingine, kikundi kinapotenganishwa, lugha yao huathiriwaje? Acheni tuone jinsi ambavyo viunganishi—na hata pia vizuizi—vya mawasiliano hujengwa.

Pijini, Krioli, na Lugha za Biashara

Ukoloni, biashara kati ya nchi, na hata kufungwa katika kambi za mateso kumefanya watu waone uhitaji wa kuziba pengo la mawasiliano kwa sababu ya kukosa lugha ya pamoja. Kwa hiyo wakaanza kutumia lugha sahili. Waliondoa mambo yenye kutatanisha kisarufi, wakatumia maneno machache zaidi katika mambo yaliyowaunganisha. Pijini zilianzishwa kwa njia hiyo. Hata ingawa pijini ni lugha iliyo sahili sana, ina mfumo wake wa isimu. Lakini sababu iliyofanya lugha hiyo ianzishwe inapokwisha, lugha hiyo yaweza kutoweka.

Watu waanzapo kutumia pijini kama lugha kuu, maneno mapya huongezwa na sarufi hupangwa upya. Hivyo inakuwa krioli. Tofauti na pijini, krioli huonyesha utamaduni wa watu. Leo makumi ya pijini na krioli—kutoka lugha ya Kifaransa, Kiingereza, Kireno, Kiswahili, na lugha nyinginezo—huzungumzwa ulimwenguni. Nyingine hata zimekuwa lugha kuu katika nchi fulani-fulani, kama vile Tok Pisin katika Papua New Guinea na Bislama katika Vanuatu.

Viunganishi vingine vinavyoendeleza mawasiliano ni lugha za biashara. Lugha ya biashara ni lugha ya pamoja inayotumiwa na vikundi vyenye lugha tofauti ya mama. Mathalani, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, watu wanaosema lugha mbalimbali wanaweza kuwasiliana kwa Kisango. Kifaransa na Kiingereza ni lugha za biashara zinazotumiwa na mabalozi. Pijini ni lugha za biashara na hata krioli zaweza kuwa hivyo pia.

Katika mikoa tofauti-tofauti katika nchi fulani, kwaweza kuwa na namna mbalimbali za lugha ya taifa, ambazo huitwa lahaja. Kadiri mikoa hiyo iwavyo mbali na mingine, ndivyo tofauti hiyo huweza kudhihirika zaidi. Baada ya muda, lahaja fulani hutofautiana sana na lugha ya awali ya eneo hilo hivi kwamba huwa lugha nyingine. Katika visa fulani si rahisi kwa wana-isimu kutofautisha kati ya lugha na lahaja. Pia, kwa sababu lugha hubadilika daima, nyakati nyingine lahaja zaweza kukoma kwa kutotumiwa, na hivyo utamaduni unaohusiana nazo hutoweka.

Lugha ni zawadi kutoka kwa Mungu. (Kutoka 4:11) Hatua yenye kuvutia sana ya mabadiliko katika lugha yaonyesha jinsi ambavyo zawadi hiyo hufaa hali za watu. Pia huenda tukajifunza kutokana na lugha kwamba hakuna watu walio bora kuliko wengine, kwa kuwa hakuna lugha duni. Sawa na zawadi nyingine zinazotoka kwa Mungu, watu wote wana lugha, bila kujali utamaduni wao au mahali wanapoishi. Tangu mwanzo kabisa, lugha za watu wote ni kamili vyakutosha kutimiza kusudi lao. Kila moja yastahili kustahiwa, bila kujali inatumiwa na watu wangapi.

Mambo ya Kihistoria na ya Kijamii

Asili ya wanadamu ya kutaka kushirikiana huonekana katika lugha. Hivyo, kunapokuwa na ushirikiano kati ya tamaduni—jambo ambalo hutukia kwa ukawaida—lugha za tamaduni hizo hudumisha ushirikiano huo kwa vizazi vinavyofuata.

Mathalani, lugha ya Kihispania yenye maneno mengi ya asili ya Kiarabu, na inayoonwa kuwa Kilatini kilichorekebishwa, ina rekodi ya ushindi wa Waislamu dhidi ya Wahispania katika karne ya nane. Unaweza kuona jinsi ambavyo Kihispania kimeathiriwa na Kifaransa, Kigiriki, Kiingereza na lugha nyinginezo. Isitoshe, katika Kihispania kinachozungumzwa Amerika, waweza kuona athari za wakazi wa kale wa bara hilo. Kwa mfano, Kihispania cha huko kina maneno mengi yanayotoka kwa lugha ya Nahuatl ya Waazteki wa Amerika ya Kati.

Kama vile lugha ya mama hutambulisha watu kuwa wa taifa au hata wa eneo fulani, lugha yaweza kutambulisha watu wa kikundi fulani, kama vile vikundi vya kazi, ufundi, utamaduni na michezo, au hata magenge ya wahalifu. Orodha hiyo yaweza kuendelea bila kikomo. Wana-isimu huita tofauti hizo za pekee istilahi au simo au wakati mwingine lahaja.

Hata hivyo, kunapokuwa na uhasama kati ya mataifa na vikundi vya kikabila au kijamii, lugha haiwi kiunganishi tena. Yaweza kuwa kizuizi kinachozidisha migawanyiko kati ya watu.

Wakati Ujao wa Lugha

Mawasiliano ni suala tata. Kwa upande mmoja, mwelekeo wa kisasa ni kukomesha vizuizi vya lugha, hasa kupitia vyombo vya habari. Kulingana na Encyclopædia Britannica, Kiingereza sasa huzungumzwa kama lugha ya kwanza au ya pili na mtu 1 kati ya watu 7. Hivyo, Kiingereza ndiyo lugha ya biashara inayotumika zaidi ulimwenguni. Watu wanapoitumia wanaweza kuwasiliana zaidi na kubadilishana habari muhimu.

Kwa upande mwingine, vizuizi vya lugha vimechangia mgawanyiko, chuki na vita. Kichapo The World Book Encyclopedia chasema: “Ikiwa watu wote wangesema lugha moja, . . . nchi mbalimbali zingehangaikiana zaidi.” Bila shaka, hangaiko hilo lingehitaji badiliko kubwa zaidi kuliko kutumia tu lugha ya biashara. Muumba mwenye hekima ndiye pekee awezaye kufanya watu wote waseme lugha moja.

Biblia, njia kuu ya Mungu ya kuwasiliana na wanadamu, yaonyesha waziwazi kwamba hivi karibuni Mungu ataondoa mfumo huu mwovu wa mambo uliopo na kuleta serikali itakayotawala kutoka mbinguni—Ufalme wake. (Danieli 2:44) Serikali hiyo itaunganisha wanadamu wote katika mfumo mpya wa mambo wenye amani na uadilifu hapa duniani.—Mathayo 6:9, 10; 2 Petro 3:10-13.

Hata sasa, lugha safi ya kiroho—kweli kuhusu Yehova Mungu na makusudi yake—inaunganisha mamilioni ya watu kutoka lugha zote, mataifa, na dini zao za awali. (Sefania 3:9) Kwa hiyo, ni jambo la kiakili kwamba katika ulimwengu wake mpya, Mungu ataunganisha wanadamu zaidi kwa kuwapa lugha moja, na kukomesha aliyofanya kule Babeli.

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Asili ya Lugha

Muumba mwenye hekima ya juu zaidi, Yehova Mungu, ametumia lugha katika makao ya kimbingu ya malaika. (Ayubu 1:6-12; 1 Wakorintho 13:1) Alipoumba wanadamu, aliwapa msamiati na uwezo wa kuupanua. Hakuna uthibitisho wa kuwapo kwa lugha ya kibinadamu ya kale yenye miguno na mingurumo. Kinyume cha hilo, fikiria kisemavyo kichapo Encyclopædia Britannica kuhusu lugha ya Kisumeri, lugha ya kale zaidi kuandikwa: “Kitenzi cha Kisumeri, pamoja na . . . viambishi-awali, viambishi-kati, na viambishi-tamati mbalimbali, huonyesha kwamba lugha hiyo ilikuwa tata.”

Yapata karne ya 20 K.W.K., kinyume cha amri ya Mungu ya kutawanyika na ‘kuijaza nchi,’ wanadamu walifanya jitihada ya kusimamia jamii yote kwenye Nyanda za Shinari, huko Mesopotamia, na kuanza kujenga Mnara wa kidini wa Babeli. Unamna-namna wa lugha ulianza wakati Mungu alipotatanisha lugha yao ya pamoja, na kuzuia mipango yao hatari na yenye kudhuru.—Mwanzo 1:28; 11:1-9.

Rekodi ya Biblia haisemi kwamba lugha zote zilitokana na ile lugha ya awali. Huko Shinari, Mungu alianzisha misamiati mipya mingi na namna ya kufikiri, hivyo akatokeza lugha mbalimbali. Hivyo, jitihada ya kutafuta lugha ya asili iliyotokeza lugha nyingine zote haijafua dafu.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Huko Babeli, Mungu alitatanisha lugha ya wanadamu waasi