Patmosi—Kisiwa cha Apokalipsi
Patmosi—Kisiwa cha Apokalipsi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI
MARA kwa mara, watu wa Patmosi hukodoa macho ng’ambo ya Bahari ya Aegea kuelekea nuru inayowakawaka juu ya miteremko ya mlima iliyo katika kisiwa cha Samosi kilicho karibu. Wengine husema kwamba nuru hiyo ya ajabu ni umeme tuli, lakini wakazi wa kidini wa Patmosi husisitiza kwamba si umeme tuli. Wanakimbia kuwaambia majirani kwamba wamepokea ishara nyingine kutoka kwa mkazi maarufu zaidi wa zamani, aliyehamishwa na kuletwa kwenye kisiwa hiki kidogo cha Ugiriki kilicho kando tu ya pwani ya Asia Ndogo karibu miaka 1,900 iliyopita.
Mtu huyo maarufu alihukumiwa adhabu ya kuishi Patmosi, yaelekea na Maliki wa Roma, Domitian, “kwa ajili ya kusema juu ya Mungu na kutoa ushahidi kuhusu Yesu.” Akiwa huko alisikia sauti ya Mungu, “kama ile ya tarumbeta,” iliyosema: “Mimi ndiye Alfa na Omega . . . Lile ulionalo liandike katika hati-kunjo.”—Ufunuo 1:8-11.
Hati-kunjo hiyo, au kitabu, ni sehemu ya umalizio wa kitabu kinachouzwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Kimetajwa na wengine kuwa kitabu kilicho kigumu sana kueleweka ambacho kimepata kuandikwa—kitabu cha Biblia kiitwacho Ufunuo, au Apokalipsi, kitabu cha mwisho cha Biblia. Mwandikaji alikuwa Yohana, mtume wa Yesu. Maono ambayo Yohana alipokea kuhusu msiba mkubwa wa mwisho wa ulimwengu huu mwovu yamewapendeza wasomaji kwa karne nyingi. *
Patmosi Leo
Wageni wengi watakubali kwamba Patmosi—kisiwa cha kaskazini zaidi kati ya Visiwa vya Dodecanese—ndicho kisiwa kinachofaa zaidi kwa mandhari ya kitabu hiki. Migongo iliyoinuka ya volkeno na mashimo makubwa yenye gizagiza hupakana na vilima vyenye ngazi pana za kijani kibichi na nyasi zenye maua ambazo huunguzwa sana na jua kali la Aegea.
Ili kuona jinsi kisiwa cha Patmosi kilivyo leo, niliabiri kutoka Piraievs, bandari kuu ya Ugiriki. Baada ya usiku wa manane, feri ilipofika katika bandari ya Skála yenye umbo kama la kilangobahari—bandari na mji mkubwa zaidi wa Patmosi—mawingu yaliachana na kisiwa hicho kikaanza kuonekana katika mwangaza wa mwezi mpevu.
Asubuhi iliyofuata, nilipokuwa nikinywa kahawa chungu taratibu, nilijitayarisha kuanza kuchunguza kisiwa hicho. Katika mandhari ya asubuhi na mapema niliona kina nyanya, wakiwa wamevalia mavazi meusi toka utosini hadi miguuni, wakijaribu kutunza watoto wachanga waliokuwa wakikimbia-kimbia. Mvuvi mwenye masharubu aliyeketi karibu alipiga-piga mlo wake wa mchana—pweza aliyetoka tu kumvua kwa mkuki kutoka majini—kwenye gati ya simiti ili kumlainisha.
Badala ya kupanda mashua, niliamua kupanda mlima nyuma ya Skála ili nione kisiwa chote. Kilikuwa chenye kuvutia ajabu. Kisiwa hicho kilienea kama ramani kubwa ya mandhari inayoelea baharini. Kisiwa cha Patmosi ni kama visiwa vitatu katika kimoja—rasi zilizounganishwa na shingo za nchi. Mojawapo ya hivi vipande vyembamba vya nchi kiko katika Skála. Kingine kiko kwenye kile kiitwacho kwa kufaa Diakofti, maana yake “Gawanya,” karibu na ncha ya kusini ya kisiwa hicho isiyokaliwa na watu. Kisiwa cha Patmosi kina urefu wa kilometa 13 hivi, na sehemu nyingine ni fupi sana.
Kimepitia Nyakati Ngumu
Kisiwa cha Patmosi kimeonwa kuwa kitakatifu tangu walowezi wa kwanza walipofika huko karibu miaka 4,000 iliyopita kutoka Asia Ndogo. Wakazi hao wa mapema walichagua sehemu ya pili kwa urefu wa juu kwenye kisiwa hicho iwe mahali pa hekalu lao la Artemisi, mungu wa kike wa uwindaji.
Wapata mwaka wa 96 W.K., wakati ambao yafikiriwa mtume Yohana alipelekwa uhamishoni Patmosi, kisiwa hicho kilikuwa chini ya utawala wa milki ya Roma. Katika karne ya nne, kisiwa hicho kikawa sehemu ya Milki ya Byzantium “iliyofanywa kuwa ya Kikristo.” Kisha, kati ya karne ya saba na ya kumi, ikaja kutawaliwa na Uislamu.
Halafu, kisiwa cha Patmosi kikawa ukiwa na tupu. Kisha, mwishoni mwa karne ya 11, mtawa wa kiume wa Othodoksi ya Kigiriki alianza kujenga ngome ya watawa ya “Mtakatifu” Yohana mahali palipokuwa na hekalu la kipagani la Artemisi. Walowezi walirudi polepole na kujenga nyumba nyingi nyeupe huko Hora, mji ambao ungali unapakana na kuta zenye kulinda nyumba hiyo ya watawa.
Kisiwa hicho kilifurahia kipindi kifupi cha ufanisi mwishoni mwa miaka ya 1800, wakati baadhi ya raia zake walipomiliki mojawapo ya vikundi vyenye kusitawi sana vya meli za kibiashara katika Meditarenia. Kikundi hicho cha meli kilitokeza uvamizi mpya kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Miaka ya 1970, baadhi ya watu matajiri ulimwenguni waligundua uzuri wa ardhi na majengo yasiyo ghali ya kisiwa kilichokuwa kimesahaulika. Walijenga upya nyumba kubwa nyingi za zamani za wafanyabiashara wa baharini, ambazo pamoja na majengo mapya ya bandari yalisaidia kufanya kisiwa cha Patmosi kivutie watalii.
Kisiwa cha Patmosi hakijapata mmiminiko wa watalii ambao karibu umetisha kuharibu visiwa vingine vya Ugiriki. Hasa ni kwa sababu ya kukosekana kwa uwanja wa ndege na kusisitiza kwa watawa wa kiume kwamba kisiwa hicho kibaki tu kikiwa eneo takatifu.
Kuchanganya Historia na Mapokeo
Ili kunisaidia kupanga uchunguzi wangu wa kisiwa hicho, mhudumu wangu alinielekeza kwenye barabara ya miaka 400 iliyotandazwa mawe nyuma ya mji wa Skála, ambayo yapenya msitu wa misonobari yenye manukato hadi lile linaloaminiwa kuwa kaburi la Yohana na pia nyumba ya watawa ya “Mtakatifu” Yohana. Viungani mwa mji, niliona maandishi yenye kuogofya yaliyoandikwa punde kwenye ukuta wa jiwe: “Ohi sto 666” (Jihadhari na 666), mojawapo ya ishara za Ufunuo zinazoeleweka vibaya.
Nyumba ya Watawa ya Apokalipsi, iliyo na kanisa dogo la “Mtakatifu” Anne, ilijengwa mwaka
wa 1090 kuzingira mwingilio wa pango ambapo kulingana na mapokeo, Yohana alipokea maono yake. Nilimtazama mwanamke aliyekuwa peke yake akipiga magoti na kuweka tama (sadaka) kwenye sanamu ya “Mtakatifu” Yohana. Waothodoksi wenye juhudi wanaoamini kwamba sanamu hiyo yaweza kufanya miujiza, huipa tamata—chuma ndogo iliyo mfano wa watu, viungo vya mwili, nyumba, na hata magari na mashua. Nakumbuka nikiona sadaka kama hizo zilizotengenezwa kwa udongo karibu na Korintho katika hekalu la mungu wa kale wa Kigiriki aliye mwanatiba Asclepius. Je, ilikuwa sadfa tu?Masalio na Hati za Kitamaduni
Nilipoingia kwenye ua wa nyumba ya watawa ya “Mtakatifu” Yohana, mtu mwenye urafiki alitokea kwenye vijia vya mzingo vyenye giza. Kwa fahari, “Papa Nikos” (Baba Nick) alinionyesha mimi na watalii wengine kadhaa hazina za nyumba hiyo ya watawa. Nyumba hiyo ya watawa, ambayo inamiliki sehemu kubwa ya Patmosi, ni mojawapo ya nyumba za watawa zilizo na mali nyingi zaidi na mashuhuri zaidi katika Ugiriki.
Tulitembea katika kikanisa kitulivu, kilichofanywa cheusi na moshi wa mishumaa, mlimowekwa mabaki ya mwanzilishi wa nyumba hiyo ya watawa, kisha kupitia Kikanisa cha Bikira, sehemu yake imejengwa kwa mawe kutoka katika hekalu la Artemisi. Katika jumba la makumbusho, tuliona dhahabu nyingi mno na vito vya thamani ambavyo vilikuwa vimetolewa na mazari; hati ya kumiliki kisiwa hicho ya karne ya 11 ya watawa wa kiume, iliyotiwa sahihi na Maliki wa Byzantium Alexius wa Kwanza Comnenus; na kipande maridadi cha Gospeli ya Marko cha karne ya sita, kilichoandikwa kwenye karatasi ya ngozi ya rangi ya zambarau kwa fedha badala ya wino. Pamoja na kipande hiki, nyumba ya watawa ina Biblia nyingi mbalimbali na hati za teolojia.
Mahali Mbalimbali Kisiwani
Kisiwa hicho kina uzuri wa asili pia. Kilometa chache kusini mwa Skála, ufuo wa kale umejipinda kandokando ya ghuba iliyolindwa. Ufuo huo ni bapa na hauna mambo muhimu isipokuwa Kalikatsou, linalomaanisha “Mnandi,” jabali katikati ya ufuo, ambalo lina urefu wa orofa tano au sita na limejaa mapango kama jibini kubwa mno ya Uswisi.
Njia bora zaidi ya kufurahia Patmosi ni kurandaranda kotekote. Huenda ukataka kuota jua lenye kuchoma katikati ya magofu yasiyochimbuliwa ya acropolis la kale huko Kastelli na kusikiliza kengele za kondoo kwa umbali na mbinja kali ya mchungaji. Au alasiri moja ambapo Aegea hueneza ukungu wake kama kitambaa chembamba angani, labda utataka kuketi utazame fuo ambamo mashua zinazoondoka kupitia kwenye ukungu wenye kuvukiza zaonekana kana kwamba zapaa angani.
Siku yangu ya mwisho huko, jua jekundu lenye kupendeza linalotua lilifanya mji ulio chini uonekane mkubwa mno. Kule kwenye ghuba, wavuvi wenye taa walikuwa wakitayarisha mashua zao ndogo zisizo na mota, zijulikanazo kama gri-gri, watoto wa bata, kwa sababu zinavutwa katika mstari na meli kubwa.
Kisiwa chote kilionekana kiking’aa. Upepo baridi na mawimbi yaliyofika juu yalirusha-rusha gri-gri kwa hatari. Baada ya muda wa saa chache, nikiwa sitahani mwa feri nikirudi Piraievs, niliona mashua hizo tena feri hiyo ilipopita kwa wepesi maeneo yao ya kuvulia kilometa chache kutoka ufuoni. Wanaume hao walikuwa wamewasha taa zao zenye mwangaza mkali wanazotumia kuvutia samaki. Usiku huo, wakazi hao na kisiwa kilichokuwa nyuma yao kilipotokomea kisionekane, picha ya Yohana akiwa uhamishoni akiandika maono yake kwenye kisiwa cha Patmosi ilibaki akilini mwangu.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Kwa maelezo ya kinaganaga, ona kitabu Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 27]
Nyumba ya watawa ya “Mtakatifu” Yohana
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
© Miranda 2000